MAISHA YA MTEULE WA KRISTO.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana Yesu Kristo atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Leo namzungumzia Mteule wa MUNGU katika KRISTO YESU.

Mathayo 22:14 "Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache."

✓✓Wateule wa MUNGU katika KRISTO YESU wapo ila Biblia inasema hao ni wachache.

Mteule wa KRISTO yukoje?

Warumi 1:6 "ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa YESU KRISTO;"

1. Mteule wa KRISTO ni yule aliyempokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake.

Yohana 1:12-13 " Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU."

2. Mteule wa KRISTO anaishi maisha ya kujitambua hata abaki kwenye kusudi la MUNGU.

Warumi 8:35-39 " Ni nani atakayetutenga na upendo wa KRISTO? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? ............... Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo,
wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa MUNGU ulio katika KRISTO YESU Bwana wetu."

3. Mteule wa KRISTO anaishi maisha ya uhalisia na sio kuishi maisha ya maigizo.

1 Petro 1:15 "bali kama yeye(YESU) aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;"

4. Mteule wa KRISTO analiishi Neno la MUNGU na analifanyia kazi katika kusudi la MUNGU.

Yohana 8:31-32 " Basi YESU akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru."

5. Mteule wa KRISTO anaenenda katika ROHO MTAKATIFU.

Wagalatia 5:16 "Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili."

6. Mteule wa KRISTO ni muombaji anayeomba kwa imani.

1 Wathesalonike 5:17-18 " ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya MUNGU kwenu katika KRISTO YESU."

7. Mteule wa KRISTO ni yule aliyejitenga na machukizo ya duniani, amejitenga na dhambi ili aambatane na KRISTO Mwokozi.

1 Yohana 2:15-17 " Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba(MUNGU), bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele."

8. Mteule wa KRISTO anaomba maombi yake katika jina la YESU KRISTO.

Yohana 14:13-14 " Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."

9. Mteule wa KRISTO ametakaswa.

1 Petro 1:2 "kama vile MUNGU Baba alivyotangulia kuwajua katika kutakaswa na ROHO, hata mkapata kutii na kununyiziwa damu ya YESU KRISTO. Neema na amani na ziongezwe kwenu."

10. Mteule wa KRISTO hayuko miongoni mwao wapoteao kwa sababu hawamhitaji YESU kama Mwokozi wao.

Waebrania 10:39 "Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu."

◼️Ndugu, hakikisha wewe ni Mteule wa KRISTO.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Sadaka ya kuipeleka Injili,whatsapp, ushauri n.k).
Ubarikiwe 

Comments