![]() |
Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU.
Lengo la somo hili ni kutupa ufahamu ili tujitenge mbali na wafanyakazi wa shetani ambao hujaribu kuwaondoa kwa YESU KRISTO Mwokozi.
Biblia inasema kwamba nyakati hizi ni za hatari sana ambapo watu wengi wanamwacha YESU KRISTO Mwokozi pekee na kuzifuata roho zidanganyazo ambazo ni roho za kuzimu.
1 Timotheo 4:1-2 " Basi ROHO anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;"
✓✓Ziko roho zidanganyazo na maana ya neno "uongo" ni tabia ya kudanganya hivyo yako makundi kadhaa yanayoongoza kuwadanganya Watu na kuwatoa kwenye kweli ya MUNGU.
Makundi ya waongo wanaoongoza kwa kusababisha madhara.
1. Manabii wa uongo.
Mathayo 7:15 "Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali."
✓✓Manabii wa uongo wote hutumwa na shetani.
Kazi ya hawa manabii wa uongo ni kutabiri uongo.
Kufanya miujiza ya kishetani.
Kuwaaminisha watu uongo hadi wanamwacha YESU KRISTO Mwokozi.
Kuleta mafunuo ya uongo.
Kwa nje hawa manabii wa uongo ni kama watu wa MUNGU lakini ukweli ni kwamba hawa ni mbwa mwitu na sio kondoo.
✓✓Kazi nyingine ya manabii wa uongo ni kuwadanganya watu.
✓✓Kazi nyingine ya manabii wa uongo ni kuwafanya watu wasimwamini YESU KRISTO kama Mwokozi wao pekee, Kumbuka YESU KRISTO ndiye njia pekee ya uzima wa milele(Matendo 4:12,Yohana 14:6) lakini manabii wa uongo wao kazi yao ni kuwafanya watu wajitenge na YESU KRISTO.
✓✓Wapo pia manabii wa uongo ambao hujaribu kumtaja YESU lakini ni mawakala wa shetani wa siri sana hivyo Mteule wa KRISTO uwe macho sana.
Mathayo 24:11 "Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi."
Ndugu uwe makini sana na ukimjua nabii wa uongo yeyote kaa naye mbali sana maana huyo atakupoteza ukimpa nafasi hadi utamwacha YESU KRISTO.
Manabii wa uongo wengi wameanzisha dini mbalimbali zilizo kinyume na YESU KRISTO na wengine wameanzisha madhehebu mbalimbali huku wakipinga wokovu wa Bwana YESU KRISTO.
Na ninapokufundisha somo hili ni muhimu kujua kwamba nabii wa uongo sio lazima ajiite nabii au aitwe na watu kwamba ni nabii, bali Biblia inasema tutawatambua kwa matendo yao.
Mathayo 7:15-16 " Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali. Mtawatambua kwa matunda yao. Je! Watu huchuma zabibu katika miiba, au tini katika mibaruti?"
Hivyo matendo ya mtumishi huyo hata kama haitwi nabii , hayo matendo ndiyo yanamfunua kwamba yeye ni nabii wa uongo.
2. Makristo wa uongo.
Marko 13:22 "kwa maana wataondoka Makristo wa uongo, na manabii wa uongo, watatoa ishara na maajabu, wapate kuwadanganya, kama yamkini, hata hao wateule."
✓✓Hawa makristo wa uongo wametumwa na shetani kujaribu kuchukua nafasi ya YESU halisi ili kuwahamishia watu upande wa shetani na sio wa MUNGU.
✓✓Hawa kazi yao ni kudanganya watu kwamba wao wametumwa na MUNGU kuchukua nafasi ya YESU KRISTO, Hawa hujiweka daraja sawa na YESU KRISTO mbele za watu hivyo huwanasa baadhi ya watu.
Biblia iko wazi sana sana kwamba YESU KRISTO ni yeye yule miaka yote iliyopita, miaka hii na miaka ijayo yote.
Waebrania 13:8-9 " YESU KRISTO ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; ............."
Hivyo wako makristo wa uongo wengi na wengine hadi hujiita Kristo, wengine hujiita Mungu, wengine hujiita wafalme wa wafalme n.k ili tu wawatoe watu kwa YESU KRISTO wa kweli.
Mfalme wa wafalme ni mmoja tu ambaye ni YESU KRISTO hivyo ukimuona au kumsikia mwanadamu yeyote akijiita mfalme wa wafalme ujue huyo ni mwendawazimu kutoka kuzimu.
Makristo wa uongo watafanya miujiza ya kishetani, watatoa ishara na ajabu nyingi lakini za kishetani.
Lengo la Makristo wa uongo ni kuwatenga watu na YESU KRISTO wa kweli.
Mathayo 24:24 "Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule."
Na ninapokufundisha somo hili ni muhimu kujua kwamba makristo wa uongo sio lazima ajiite Kristo au aitwe na watu kwamba ni Mungu, bali Biblia inasema tutawatambua kwa matendo yao, hivyo matendo ya mtumishi huyo hata kama haitwi nabii , hayo matendo ndiyo yanamfunua kwamba yeye ni nabii wa uongo.
Wengine ni kweli kabisa wanajiita Yesu au Mungu, ndugu uwe makini sana.
3. Mashahidi wa uongo juu ya kweli ya MUNGU katika KRISTO YESU.
Matendo 6:13 "Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati;"
✓✓Mashahidi wa uongo wametumwa na shetani ili walete madhara kwa watu wa MUNGU.
✓✓Mashahidi wa uongo wengine ni wale walioasi Wokovu wa Bwana YESU na kuanza kutumika upande wa shetani.
Kazi yao hawa ni kusema uongo dhidi ya watumishi wa MUNGU wa kweli ili kuua huduma au kuwarudisha nyuma watu ili waache Wokovu.
Mathayo 26:59-60 "Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya YESU, wapate kumwua; wasiuone wangawa walitokea mashahidi wa uongo wengi."
✓✓Kazi yao nyingine ni kutoa ushuhuda wa uongo.
Mashahidi wa uongo wamebeba hila.
Mithali 12:17 "Atamkaye maneno ya kweli hufunua haki; Bali shahidi wa uongo hutamka hila."
✓✓Mashahidi wa uongo wanaweza hata kuapa uongo, wamebeba hila ili kuifanya kazi ya MUNGU isiendelee.
Ndugu Omba kwa MUNGU ili uwashinde Mashahidi wa uongo.
Zaburi 27:12 "Usinitie katika nia ya watesi wangu; Maana mashahidi wa uongo wameniondokea, Nao watoao jeuri kama pumzi."
Mfano wa mashahidi wa uongo ni kama huu; Mtumishi mmoja alimzushia Mtumishi fulani wa MUNGU kwamba ana chumba pembeni ya madhabahu kina joka kubwa sana hivyo miujiza yake hutokana na joka hilo lakini ukweli ni kwamba hata hakuna chumba pembeni ya madhabahu, Na Mhubiri huyu huzunguka kuhubiri maeneo mengi sana je nyoka humweka wapi? Kama ndio hivyo, Mtumishi huyu huenda mataifa mbalimbali kuhubiri je airport hakuna ukaguzi? Huu ni uongo tu na watu wengi bila kutafakari walimwacha YESU kwa sababu ya shahidi wa uongo.
Mchungaji mmoja alikuwa anakemea pepo kanisani kwake sasa lile pepo nikasema kwamba watulie litoe siri, kwa karibia saa nzima lile pepo lilianza kusema kuwa watumishi karibia wote wakubwa Tanzania wa makanisa karibia yote eti ni mawakala wa shetani maana huenda kuzimu, pepo lile lilianza hadi kuigiza sauti ya kila Mtumishi, Baada ya ibada Mtumishi huyo alianza kuuza cd ya mazungumzo ya huyo pepo mchafu na hadi kuna rafiki yangu mmoja alinunua hiyo cd wakati mtumishi huyo yuko mkoa wa mbali sana na Dar es salaam, niliposikiliza niligundua ule ni uongo wa shetani ili kuwaondoa watu kwa YESU, nilisikitika sana sana, mashahidi wa uongo baadhi yao ni watumishi ndio maana ni rahisi kumsikiliza Mtumishi wakati akihubiri anamsema vibaya Mtumishi mwingine ambaye ameinuliwa sana na MUNGU kuliko yeye, ni heri kazi zijionyeshe maana ziko kinyume na Biblia ndipo uziseme kwa ujasiri kabisa maana ni kweli, lakini sio umesikia tu kwa akikuambia "yule mtumishi ni freemason " na wewe unatangazia maelfu ya Watu na kumbe ni uongo tu.
Najua kabisa kwamba mawakala wa shetani wapo na ni wengi sana lakini Biblia inasema tutawatambua kwa kazi zao, ni rahisi sana kumjua wakala wa shetani lakini wengi wamenaswa kwenye ushahidi wa uongo.
Mathayo 7:20 "Ndiposa kwa matunda yao mtawatambua."
Mtumishi mmoja mkoa fulani nilimsikia anasema juu ya mtumishi mwingine kwamba huyo mtumishi ili awe na upako mkubwa ibadani lazima atoke kuzini na mke wa mtu, nilimuuliza ulimuona akasema kwamba aliambiwa na rafiki yake na huyo rafiki yake aliambiwa na mtu mwingine, hakuna ushahidi ila ni uzushi tu wa kuwafanya watu watoke kwa YESU.
Shetani kupitia mashahidi wa uongo huitumia sana kanuni ya kumpiga Mchungaji ili kondoo watawanyike ndio maana kuna baadhi ya maeneo makanisa yalifungwa baada ya mchungaji kuzushiwa uongo.
Natambua kabisa wapo hadi mawakala wa shetani huwapa baadhi ya wanawake pesa ili watangaze kwamba walilala na Mtumishi fulani, hiyo ni kazi ya shetani kuwatoa watu kwa YESU.
Ndugu kama ni ukweli ambao una uhakika nao na mbingu zinathibitisha basi huo ukweli useme bila hofu lakini kama unazusha vitu vinavyotokana na shahidi wa uongo basi tambua kwamba unatumika pia kama shahidi wa uongo ili kupunguza watu kwa YESU.
✓✓Mashahidi wa uongo wengine hadi husema kwamba YESU KRISTO hakufufuka hivyo Watu wasimfuate lakini ukweli ni kwamba YESU KRISTO alifufuka na yuko hai milele, ndiye Mwokozi pekee wa kila mtu ulimwengu anayeutaka uzima wa milele.
1 Wakorintho 15:20 "Lakini sasa Kristo amefufuka katika wafu, limbuko lao waliolala."
4. Washitaki wa uongo.
Luka 3:14 "Askari nao wakamwuliza, wakisema, Sisi nasi tufanye nini? Akawaambia, Msidhulumu mtu, WALA MSISHITAKI KWA UONGO; tena mtoshewe na mshahara wenu."
✓✓Washitaki wa uongo wako katika makundi mengi, ninaowazungumzia leo ni Wale ambao huwashitaki kwa uongo watumishi wa MUNGU au Wateule wa KRISTO ili kupunguza Watu katika Wokovu.
Hawa kazi yao ni kuwashitaki kwa uongo watumishi wa MUNGU katika KRISTO YESU.
Kazi zingine za mashahidi wa uongo ni kutoa ushahidi wa uongo ili kuwazuilia watu wengi kuokoka.
Kazi zingine za mashahidi wa uongo ni kuwashitaki watu wema kwa uongo.
Kazi za mashahidi wa uongo ni kuwabambikizia kesi za uongo watu wema.
Marko 3:2 "wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato; wapate kumshitaki."
Kazi zingine za mashahaidi wa uongo ni kuwanyang'anya watu wema haki zao.
✓✓Mashahidi wa uongo hutafuta visingizio vya uongo kuwaweka hatiani wateule wa KRISTO.
Mashahidi wa uongo kazi yao nyingine ni kuwakosanisha watu wema na serikali yao au Kanisa lao au kikundi chao au idara yao Kanisani.
Ndugu usikubali kumsapoti shahidi wa uongo maana huyo ni wakala wa shetani.
Ndugu, jihadhari sana na washtaki wa uongo.
Luka 23:2 "Wakaanza kumshitaki, wakisema, Tumemwona huyu akipotosha taifa letu, na kuwazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema kwamba yeye mwenyewe ni KRISTO, mfalme."
5. Mitume wa uongo.
2 Wakorintho 11:13-14 " Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa KRISTO. Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru."
✓✓Mitume wa uongo wametumwa na shetani ili kuanzisha uongo dhidi ya Wokovu na kutangaza uongo juu ya YESU KRISTO.
Na katika masikio ya watu siku zote uongo ukitangazwa sana hugeuka ukweli machaoni pao hivyo mitume wa uongo hutangaza uongo hadi kuna baadhi ya watu huuamini huo uongo wakidhani ni ukweli.
Mitume wa uongo wameanzisha dini nyingi na madhehebu mengi na lengo lao kuu ni watu wajitenge mbali na YESU KRISTO Mwokozi.
Mitume wa uongo hujifanya kuwa watumishi wa MUNGU kumbe wao ni watumishi wa shetani, wamejaa hila.
Mitume wa uongo hufundisha elimu ya dini ya uongo.
Warumi 16:17-18 " Ndugu zangu, nawasihi, waangalieni wale wafanyao fitina na mambo ya kukwaza kinyume cha mafundisho mliyojifunza; mkajiepushe nao. Kwa sababu walio hivyo hawamtumikii Bwana wetu KRISTO, bali matumbo yao wenyewe; na kwa maneno laini na ya kujipendekeza waidanganya mioyo ya watu wanyofu."
Mitume wa uongo huanzisha dini za uongo na madhehebu ya uongo, ili tu kwenda kinyume na YESU KRISTO aliye Mwokozi pekee.
Mitume wa uongo siku zote wako kinyume na wokovu wa Bwana YESU KRISTO.
Na ninapokufundisha somo hili ni muhimu kujua kwamba mitume wa uongo sio lazima ajiite Mtume au aitwe na watu kwamba ni mtume, bali Biblia inasema tutawatambua kwa matendo yao, hivyo matendo ya mtumishi huyo hata kama haitwi nabii , hayo matendo ndiyo yanamfunua kwamba yeye ni nabii wa uongo.
6. Walimu wa uongo.
2 Petro 2:1 "Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata Bwana(YESU) aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia."
✓✓Walimu wa uongo wametumwa na shetani na kazi yao kuu ni kufundisha uongo ili kuwapotosha watu.
✓✓Walimu wa uongo wametumwa na shetani ili kuwaondoa watu katika Wokovu wa Bwana YESU KRISTO.
✓✓Walimu wa uongo wana maarifa mengi ila ni ya uongo.
✓✓Walimu wa uongo wana majini ndani yao ambayo ndiyo huwafundisha ili kupotosha na kuwatoa watu kwa YESU KRISTO Mwokozi.
Walimu wa uongo wanafundisha uzushi wa kupoteza watu, mafundisho yao ni ya kumkana YESU KRISTO au kumkataa.
✓✓Walimu wa uongo huipotosha injili ya wokovu wa YESU KRISTO.
✓✓Walimu wa uongo hukataza watu kuokolewa na YESU KRISTO Mwokozi.
✓✓Walimu wa uongo huruhusu baadhi ya dhambi kwa watu wao, Mfano Huruhusu pombe, sigara, kuvaa kikahaba n.k
Na ninapokufundisha somo hili ni muhimu kujua kwamba walimu wa uongo sio lazima ajiite mwalimu au mchungaji au aitwe na watu kwamba ni mwinjilisti au askofu, bali Biblia inasema tutawatambua kwa matendo yao, hivyo matendo ya mtumishi huyo hata kama haitwi nabii , hayo matendo ndiyo yanamfunua kwamba yeye ni mwalimu wa uongo.
Mwalimu wa uongo anaweza kuwa na cheo chochote cha kihuduma, anaweza kuwa na Karama yeyote au huduma yeyote inayompa kufundisha au kuhubiria Watu, na katika mahubiri yake ya uongo ndipo hujifunua kuwa yeye ni Mwalimu wa uongo.
7. Wanaoapa kwa uongo.
Hosea 4:2 "Hapana neno ila kuapa kwa uongo, na kuvunja ahadi, na kuua, na kuiba, na kuzini; huruka mpaka, na damu hugusana na damu."
✓✓Hili ni kundi lingine hatari sana linalosababisha madhara makubwa.
Hawa huapa uongo ili huo uongo uaminiwe na kisha wawapoteze watu wema.
Hawa husingizia watu wema kupitia kuapa kwao.
Hawa hujitenga mbali na mafundisho ya uzima ya injili ya Bwana YESU KRISTO.
Hawa hutoa ushahidi wa uongo ili maamuzi yapindishwe na wao wapate faida.
Ndugu, nimekuelezea haya makundi saba yanayoongoza kwa kusababisha madhara makubwa kiroho na kuwapoteza watu, hakikisha wewe huwi katika kundi hata moja kati ya haya makundi saba.
Hakikisha unajitenga mbali na mtu yeyote anayehusika na kundi hata moja kati ya haya saba.
Hakikisha unaifuata Biblia katika kusudi la MUNGU la wakati huu ambapo kusudi hilo la MUNGU sasa ni Wokovu wa YESU KRISTO.
Yohana 3:16-18 " Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU."
Na kumbuka kuwa YESU KRISTO ndiye kiini na msingi wa imani yetu sisi waenda mbinguni wote.
1 Wakorintho 3:11" Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, YESU KRISTO."
Hivyo msingi wa imani yako hakikisha msingi huo unauweka kwa YESU KRISTO tu na sio kwa wanadamu wanaojiita watumishi.
Mpime kila mtu anayekufundisha Neno la MUNGU yaani mpime kila mtu anayekufundisha mambo ya kidini ili ujue kama anatokana na MUNGU , asiyetokana na YESU KRISTO jitenge naye mbali.
1 Yohana 4:1-3 " Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na MUNGU; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani. Katika hili mwamjua ROHO wa MUNGU; kila roho ikiriyo kwamba YESU KRISTO amekuja katika mwili yatokana na MUNGU. Na kila roho isiyomkiri YESU haitokani na MUNGU. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; na sasa imekwisha kuwako duniani."
Kila roho isiyomkiri YESU KRISTO Mwokozi haitokani na MUNGU hiyo roho.
Kumbe watumishi wasiotokana na MUNGU ni rahisi kuwajua, maana kila roho isiyomkiri YESU KRISTO Mwokozi haitokani na MUNGU hiyo roho.
Narudia tena kumbe kila roho isiyomkiri YESU KRISTO Mwokozi haitokani na MUNGU hiyo roho.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, kuandika meseji na hadi whatsapp).
Uki-share kwa marafiki zako ujumbe huu naomba share kama ulivyo,usibadili jina wala chochote.
Comments