MAMBO 10 YA KIBIBLIA YA KUFANYA KWA AJILI YA WATOTO WAKO.

Jemimah na Peter Mabula 
Watendakazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu. 
karibu tujifunze Neno la MUNGU. 
Kuna makundi mawili ya watoto ambao unaweza ukahusika nao,  Watoto wako wa kuzaa mwenyewe na  Watoto waliozaliwa na wengine ila wakakulia/Watakulia mikononi mwako.

Watoto wako au watoto wa wenzako ila utaishi nao wewe kuna mambo ya kibiblia ya kuwasaidia ili wawe washindi duniani na ili watimie katika kusudi la MUNGU katika KRISTO YESU. 

■Mtoto ni mfano wa shamba zuri lenye rutuba ila halijapandwa mazao na linastahili kupandwa mazao, aina ya mazao mazuri unayopanda kwenye shamba hilo na kuota ujue yataleta matunda mema yatakayofaa watu wengi. 

■Bwana YESU siku zote anataka mambo mazuri ya ki MUNGU unayofundishwa wewe na wewe inakupasa uwafundishe na watoto wako ili wawe daima katika kusudi la MUNGU katika maisha yao yote. 

Kumbu 12:28 "Maneno haya nikuagizayo yote yatunze na kuyasikiza, ili upate kufanikiwa na watoto wako baada yako milele, hapo uyafanyapo yaliyo mema na kuelekea machoni pa BWANA, Mungu wako."

Mambo haya 10 ya kibiblia ukiwafanyia watoto wako utakuwa umewajengea msingi mzuri wa maisha yao.

1.       MTAMKIE MEMA MTOTO WAKO BAADA YA KUZALIWA KWAKE.

Kwa kuchunguza kwangu Biblia kuna watoto wengi walitamkiwa mema yaliyoishi maishani mwao.

Mtoto anapozaliwa anakuwa ni kiumbe kitupu kisicho na kitu kiroho, maneno yako mema na ya baraka ndio yatakuwa kitu cha kwanza kitakachoingia ndani ya mtoto wako kikiwa hai  mara tu anapozaliwa na kitu hicho cha baraka ulichomtamkia  kitaambatana daima mtoto wako katika maisha yake kuanzia siku hiyo ya kuzaliwa kwake. 

Ngoja nikupe mifano hai ya kibiblia

Baada ya Lameki kumzaa Nuhu alisema ndiye atayewafariji.

Mwanzo 5:28-29 "Lameki akaishi miaka mia na themanini na miwili, akazaa mwana. Akamwita jina lake Nuhu, akinena, Huyu ndiye atakayetufariji kwa kazi yetu na kwa taabu ya mikono yetu katika nchi aliyoilaani BWANA."

 Tunajua Nuhu alikuwa mcha MUNGU hivyo kuwafariji  wazazi wake sidhani kama ilishindikana. 
 Lakini katika uzao wa Lameck ni Nuhu tu alibaki baada ya gharika yaani  baada ya MUNGU kuwaangamiza watu wote ikabaki familia ya Nuhu tu, kama Lameki angeambiwa kwamba Dunia yote watu wote wamekufa isipokuwa mwanao Nuhu na wajukuu zako basi hakika angefurahi maana Nuhu amemfariji, maana  uzao wa wanadamu wote ulikufa isipokuwa uzao wake Lamek kupitia Nuhu hiyo, ndiyo faraja inayotokana na maneno aliyomtamkia mwanae wakati anazaliwa.

Ona mifano hii

Yusufu alipomzaa Manase alisema hivi“MUNGU amenisahaulisha taabu zangu zote”

Mwanzo 41:51 "Yusufu akamwita jina lake yule aliyezaliwa kwanza, Manase, maana alisema, MUNGU amenisahaulisha taabu zangu zote, na nyumba yote ya baba yangu."

■Mtoto unayezaa anaweza kuwa ni ishara ya kukoma kwa mateso na tabu.

Nimejifunza kitu cha ajabu sana ndani ya Biblia yaani kile walichotamkiwa watoto kutoka kwa wazazi wao wakati wanazaliwa ilikuja kuwa kweli kwenye maisha ya watoto husika.

Ndugu mtamkie mema mtoto wako wakati wa kuzaliwa kwake. 

■■Mama unapomshika mtoto wako mikononi mwako kwa mara ya kwanza mtamkie neno jema katika ROHO MTAKATIFU na hicho ulichomtakia mtoto wako kitaambatana naye maishani mwake.

■■Baba na Mama mnalozaa tu mtoto mtamkieni mambo mazuri katika ROHO MTAKATIFU ili mambo hayo mema yaambatane na mtoto wenu. 

Leo kuna watu wanateswa na vifungo vya kipepo,  kuna watu wamewekewa mipaka ya kufanikiwa kwenye ulimwengu wa roho,  kuna watu wanateswa na roho za kukataliwa,  kuna watu wana roho za magonjwa,  kuna wenye roho za mauti n.k hawa wote sio wote vyanzo vyao ni laana za wazazi yaani maneno mabaya ya wazazi wao kipindi wanazaliwa,  lakini hata ambao wana vifungo na matatizo ya kiroho ya kila namna kutokana na kutamkiwa maneno mabaya kipindi wanazaliwa,  watu hao wapo na ni wengi. 
Hivyo wewe jifunze kumuambatanisha mtoto wako na baraka za MUNGU kipindi tu mtoto huyo unamzaa.
Mtamkie jambo jema mtoto wako,  mtamkie wakati anazaliwa au wakati unamuombea baada ya tu kumzaa au wakati unamshukuru MUNGU baada ya kumzaa mtoto huyo. 

Raheli yeye alitapomzaa  Yusufu alisema MUNGU amemuondolea aibu. 

Mwanzo 30:22-23 " MUNGU akamkumbuka Raheli; MUNGU akamsikia, akamfungua tumbo. Akapata mimba, akazaa mwana, akasema, MUNGU ameondoa aibu yangu."

 Na Yusufu aliyaishi maneno hayo ya "kuondoa aibu "
Maana ndiye Yusufu huyo aliwapa vyakula familia yake hata wakati njaa inakaribia kuwaua. 

Mwanzo 42:25 "Yusufu akaamuru kuvijaza vyombo vyao nafaka, na kumrudishia kila mtu fedha yake katika gunia lake, na kuwapa chakula cha njiani."

Hata walipomaliza tena chakula walirudi tena kwa Yusufu muondoa aibu. 

Mwanzo 44:1 "Akamwamuru yule msimamizi wa nyumba yake akisema, Jaza magunia ya watu hawa chakula kwa kadiri wawezavyo kuchukua, utie na fedha ya kila mtu kinywani mwa gunia lake."

Ni Yusufu huyo huyo muondoa aibu maana wakati akiwa hai Waisraeli hawakuteswa kamwe na Wamisri,  hadi alipokufa Yusufu. 

Kutoka 1:8 "Basi akainuka mfalme mpya kutawala Misri, asiyemjua Yusufu."

Alipoondoka Yusufu muondoa aibu ndipo ndugu zake walianza kuteseka kwa miaka zaidi ya mia tatu baada ya Yusufu muondoa aibu kuondoka duniani. 

Maneno ya Raheli kwa mtoto wake Yusufu yaliishi siku zote za maisha ya Yusufu. 

Je wewe watoto wako wanapozaliwa unawaambatanisha na baraka za MUNGU au unawaambatanisha na vifungo vya giza? 

Ndugu kuanzia leo unapozaa mtoto mtamkie mema,  hata kama unamlea mtoto mtamkie mema. 

Kama watoto wako wakati Wanazaliwa  uliwatamkia laana na vifungo leo kwa sababu umetambua hili fanya hivi;

A.  Tubu kwa vyanzo vyote vilivyosababisha watoto wako kutamkiwa mabaya wakati wanazaliwa (mtaje mtoto mmoja mmoja ukitubu kwa ajili ya vyanzo vilivyopelekea kutamkiwa mabaya wakati anazaliwa) 

Kumbuka kuna uzima na mauti katika maneno unayotamka au yanayotamkwa.

Mithali 18:21 "Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake."

 Hiyo ina Maana kuna maneno yanaumba uharibifu na kuna maneno yanaumba baraka na uzima. 
Kama watoto wako waliumbiwa uharibifu tubu 

B.  Kwa maombi katika jina la YESU KRISTO futa maneno yote mabaya waliyotamkiwa watoto wako wakati wanazaliwa (mtaje mtoto mmoja mmoja ukifuta maneno yote mabaya uliyotamka wewe na mwenzi wako au watu wengine) 

Yohana 14:14 "Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."

C.  Kwa maombi katika jina la YESU KRISTO watamkie mema, waumbie mema kwa maombi yako katika ROHO MTAKATIFU. 

Mathayo 7:7-8 " Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;  kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."

D.  Kwa maombi na sadaka wakabidhi watoto wako katika madhabahu ya MUNGU,  ili madhabahu ya MUNGU iwafuatilie watoto wako kuanzia sasa. 

Zaburi 50:5 "Nikusanyieni wacha MUNGU wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu."

Wakristo tuko nyuma sana katika kuwatamkia maneno mazuri watoto wetu wakati wa kuzaliwa kwao, kwa nini nasema hivyo?
 Kuna dini mtoto akizaliwa tu maneno ya kwanza kuambiwa mtoto ni "Fulani ndiye mungu wako na Fulani ndiye nabii wako"

 Sasa wewe Mkristo sijui huwa unamtamkia nini mtoto wako wakati anazaliwa.

Ni heri ukamtamkia mema mtoto wako kisha useme “YESU KRISTO ndiye Mwokozi wako kwa ajili ya uzima wa milele.

2.   MPE MTOTO WAKO JINA JEMA NA LENYE MAANA NJEMA.

Mithali 22:1 "Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi; Na neema kuliko fedha na dhahabu."

■■Jina ni alama ya pekee anayopewa mtu ili kumtofausha na wenzake

■Jina ni kitambulisho cha pekee ambacho mtu anapewa ili awe tofauti na wengine.

Sio kila jina linafaa umpe mtoto wako   jitahidi sana kumpa jina mtoto wako lenye maana nzuri hasa jina la kibiblia

Jina baya linaweza likabeba laana kwa mtoto wako
Jina zuri linaweza likabeba Baraka

Biblia inasema ni heri kuchagua jina jema kuliko hata mali maana jina hubeba vitu vingi vya thamani kuliko mali.
Usimpe mtoto wako jina la kiukoo au usimpe jina lenye vifungo vya giza.

Mfano ni huu ambapo wana ukoo walitaka kumpa jina la kiukoo mtoto Yohana,  ila neema ya KRISTO ni kwamba MUNGU alikuwa ameshawapa ufunuo wazazi ndio maana akaitwa Yohana ambalo halikuwa jina la kiukoo ila ni mapenzi ya MUNGU. 

 Luka 1:59-64 "Ikawa siku ya nane wakaja kumtahiri mtoto; wakataka kumpa jina la babaye, Zakaria. Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana. Wakamwambia, Hapana mtu katika jamaa zako aitwaye jina hilo.
 Wakamwashiria babaye wajue atakavyo kumwita. Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana. Wakastaajabu wote. Papo hapo kinywa chake kikafunguliwa na ulimi wake pia, akaanza kunena akimsifu MUNGU."

Kumbuka ulimi unaumba hivyo uwe makini na jina unalompa mtoto wako,  usije ukampa jina lenye mabaya yanayoumbika kila akiitwa  jina hilo. 

Yakobo 3:8-10 " Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. Kwa huo(Ulimi) twamhimidi MUNGU Baba yetu, na kwa huo twawalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa MUNGU.  Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo."

Haifai kuwa hivyo kwa wateule wa KRISTO. 

Sasa mfano mtoto wako ukimwita Nabali (yaani mpumbavu) ujue atafanya upumbavu mwingi maishani mwake kwa kosa lako ulimpa jina hilo, hivyo watu wanapomwita mpumbavu /Nabali wanakuwa kwa vinywa vyao wanaumba upumbavu,  ataambatana na na upumbavu.

1 Samweli 25:25 "Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma."

Uwe makini sana na jina unalompa mtoto wako, unaweza ukampa jina la jini na usishangae maishani mwake kuteswa na majini. 
Unaweza kumpa mfano jina la Tabu, Shida au Masumbuko na maisha yake akawa wa tabu, Shida au Masumbuko. Mwite mtoto wako jina lenye maana njema mfano.

Mwanzo 29:35 "Akapata mimba tena, akazaa mwana. Akasema, Mara hii nitamsifu BWANA; kwa hiyo akamwita jina lake Yuda; akaacha kuzaa."

Kabila la Yuda ni kabila ambapo lilipitisha ukombozi wetu,  hivyo tunamsifu MUNGU kwa wokovu mkuu. 
Wokovu ulipitia kabila hilo na sio lingine katika makabila 12 ya Waisraeli. 
Bwana YESU Mwokozi ni simba wa kabila la Yuda maana alipitia kabla la Yuda.  

Ufunuo  5:5 "Na mmojawapo wa wale wazee akaniambia, Usilie; tazama, Simba aliye wa kabila ya Yuda, Shina la Daudi, yeye ameshinda apate kukifungua kile kitabu, na zile muhuri zake saba."

Majina yote yana maana ila siyo majina yote yana  maana nzuri, hivyo mpe mtoto wako jina zuri hasa la Kibiblia. 

Mfano; Hana na Elikana alizaliwa mtoto wakamwita jina Samweli (1Samweli.1:20) maana ya Samweli ni aliyesikilizwa na MUNGU hiyo ni dalili ya Samweli kuwa na Kibali kwa MUNGU.

Mwingine alizaa mtoto akamwita jina Leah yaani malkia wa nyumba.

Mwingine  alizaa mtoto akamwita jina   Gabriel yaani mtu wa MUNGU.

  Mtu mwingine  alizaa mtoto akamwita jina  Naomi yaani anayependeza.

  Mtu mwingine  alizaa mtoto akamwita  jina Onesmo maana yake mtu anayesababisha Baraka.

  Mtu mwingine  alizaa mtoto akamwita  jina Nikodemo yaani mshindi wa Taifa

   Mtu mwingine  alizaa mtoto akamwita  jina  Obadia yaani mtumishi wa MUNGU.

Je jina la mtoto wako lina maana gani?

Usimuite mtoto wako kila jina ulilosikia. 

Kuna mtu alizaa mtoto akamuita jina  Delila maana yake mtu wa kujipendekeza.
Je unataka mtoto wako awe mtu wa kujipendekeza?

   Mtu mwingine  alizaa mtoto akamwita  jina  Nabali maana yake mpumbavu.

Somo litaendelea katika kitabu kiitwacho MAMBO 10 YA KIBIBLIA YA KUFANYA KWA AJILI YA WATOTO WAKO ambacho nakiandaa na MUNGU akinipa neema hata mwaka huu au mwakani nitakichapisha.

Asante rafiki yangu kwa kujifunza Neno hili la MUNGU leo.
Kabla sijahitimisha leo ninalo Neno la mwisho kwa ajili yako.
Je umeokoka? 
Kama umeokoka endelea na Wokovu wa Bwana YESU KRISTO hadi mwisho wa maisha yako.
Na wewe ambaye hujaokoka nakuomba okoka leo maana tunaishi siku  za Mwisho. 
Ni YESU tu ndio anayeweza kuliandiika jina lako kwenye kitabu cha uzima hata upate Uzima wa milele, nakuomba sana mpokee YESU KRISTO leo kwa ajili ya Wokovu. 
Huko huko uliko tafuta Kanisa la kiroho wanaohubiri Wokovu Wa KRISTO ukamweleze Mchungaji atakuongoza sala ya toba na utakuwa umeokoka.
Fanya hivyo kwa faida ya roho yako milele
MUNGU akubariki. 
By Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU. 
+255714252292(Sadaka ya kupeleka Injili, Maombi na ushauri)
Ubarikiwe sana

Comments