![]() |
Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU.
◼️Leo nazungumzia vijana wanaompenda YESU KRISTO na wako tayari kwa ajili ya ndoa takatifu.
Ngoja nianze hivi;
Kijana ni nani?
✓✓ Kijana ni Mwanadamu yeyote ambaye sio Mtoto Wala sio mzee.
Ukijiona Wewe sio Mtoto Wala sio Mzee basi Wewe ni Kijana wa Kiume au wa Kike.
Kijana ana thamani mbele za MUNGU katika KRISTO YESU.
1 Yohana 2:14 "Nimewaandikia ninyi, akina baba, kwa sababu mmemjua yeye aliye tangu mwanzo. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la MUNGU linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu."
✓✓Kijana ni mwanadamu yeyote mwenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 45(hii ni kwa mujibu wa taratibu za baadhi ya makanisa)
✓✓Kijana ni mtu mwenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 35(Hii ni kwa mujibu wa kamusi ya kiswahili sanifu)
✓✓Kwa ujumla ni kwamba kijana ni mwanadamu yeyote ambaye sio mzee wala mtoto.
Kuna vijana wa kiume na kuna vijana wa kike, wote hao ni vijana.
Kuna vijana walio katika ndoa takatifu, kuna vijana walio katika uchumba na kuna vijana ambao hawako katika ndoa wala uchumba.
Mimi leo nazungumzia kijana ambaye hajaingia katika ndoa takatifu, anaweza kuwa na mchumba au hana.
Mpango wa MUNGU kila mmoja siku Moja awe katika Ndoa yake mwenyewe.
Mathayo 19:5-6" akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja? Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha MUNGU, mwanadamu asiwatenganishe."
Vijana wengi wanatamani au wanapanga kuingia katika ndoa.
Vijana hao wa kiume na wa kike baadhi wako katika makundi haya kwa uzoefu wangu Mimi Peter Mabula kutokana na kumtumikia Bwana YESU KRISTO kwa Miaka zaidi ya 15 huku nikiwasiliana na vijana mbalimbali.
✓✓ Wapo vijana ambao hawajaingia katika ndoa kwa sababu muda wa MUNGU kwao bado.
Mhubiri 3:1 "Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.''
✓✓Lakini wapo pia vijana ambao wameshindwa kuingia katika ndoa kwa sababu wamekosa wa kuwaelewa hata waingie nao katika ndoa.
✓✓Vijana wengine wamefungwa vifungo vya giza.
✓✓Vijana wengine wana tabia mbaya ndio maana imeshindikana kuingia katika Ndoa.
Mithali 11:16 "Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; ......"
✓✓Vijana wengine hawajitambui au hawatambui majira ya MUNGU kwao.
✓✓Vijana wengine tamaa za kidunia zimewashikilia hata wamekosa watu wa kufunga nao ndoa.
✓✓Vijana wengine bado wanasoma
✓✓Vijana wengine dhambi inawazuilia
✓✓Vijana wengine hawamchi MUNGU hivyo hakuna anayewahitaji.
✓✓Vijana wengine kwa sababu ya kuumizwa kulikotokana na dhambi zao za zamani hivyo wameathirika kiakili.
✓✓Vijana Wengine wako katika uchumba sugu unaowapotezea muda tu kisha waachwe ila wao kwa Sasa hawajui.
✓✓Vijana wengine wanaufanyia kazi uongo walioelekezwa hivyo wapo wapo tu.
✓✓Vijana wengine wamefundishwa uongo hivyo wanaishi katika uongo.
✓✓Vijana wengine wameshindwa kuizingatia sauti ya MUNGU.
✓✓Vijana wengine kwa mujibu wa wao wamekosa wachumba wenye sifa sahihi ingawa Mimi Naamini wachumba sahihi wapo na ni wengi sana.
✓✓Vijana wengine wanajiona muda wao bado hata kama muda umevuka
✓✓Vijana wengine wana washauri wabaya ingawa wakati Mwingine unakuta mshauri Yuko katika Ndoa ila anamshauri Kijana asiingie katika Ndoa.
◼️Ni jambo jema kuingia katika ndoa lakini jitahidi uwe na sifa safi unapoingia katika ndoa.
Yeremia 29:6 "oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue."
✓✓Sasa ni mambo gani yampasayo kijana anayempenda YESU aliye tayari kuingia katika ndoa takatifu?
◼️Mambo haya 12 yazingatie wewe kijana unayempenda YESU KRISTO na uko tayari kwa ndoa takatifu.
1. Hakikisha umeokolewa na YESU KRISTO na umefunguliwa vifungo vyote vya giza.
Maombolezo 3:27 "Ni vema mwanadamu aichukue nira Wakati wa ujana wake."
✓✓Nira inayozungumzwa hapa ni ya kuifuata njia ya MUNGU na hiyo njia ni moja tu kukubali kuokolewa na YESU KRISTO Mwokozi.
✓✓Ukiokoka hakikisha umefunguliwa vifungo vya giza vyote.
Mfano kijana huyu alifunguliwa na Bwana YESU.
Mathayo 17:18 "YESU akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile."
Hata wewe kwa maombi tafuta kufunguliwa kama umefungwa kipepo.
2. Hakikisha unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO siku zote.
1 Petro 1:15 "bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;"
✓✓YESU aliyekuita katika Wokovu wake anataka uishi maisha matakatifu kwa sababu ukiishi maisha ya dhambi kuna hukumu na jehanamu.
Mhubiri 11:9 "Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote MUNGU atakuleta hukumuni."
◼️Hivyo heri kuishi maisha matakatifu siku zote.
3. Hakikisha siku zote wewe unakuwa kielelezo chema katika mema tu.
1 Timotheo 4:12 "Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi."
✓✓Kijana aliye kielelezo cha mema ni kijana anayetenda mema hata anakuwa mfano mzuri wa mema.
4. Hakikisha unakuwa Mkristo muombaji.
✓✓Jifunze kwa mfano huu ambapo Kijana Ishmaeli ambapo Biblia inasema MUNGU aliisikia sauti ya kijana huyu akiyekuwa anaomba,
Mwanzo 21:17 "MUNGU akasikia sauti ya kijana. Malaika wa MUNGU akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana MUNGU amesikia sauti ya kijana huko aliko."
◼️Hata wewe hakikisha unakuwa kijana muombaji, na katika jina la YESU KRISTO utajibiwa Maombi yako.
5. Hakikisha unamtumikia MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi .
Mhubiri 12:1 "Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo."
✓✓Biblia inamtaka kijana kumtumikia MUNGU tangu ujana wake.
✓✓Hakikisha YESU KRISTO ni Mwokozi wako na mtumikie katika ujana wako.
Muige Samweli ambaye alianza kumtumikia MUNGU tangu akiwa kijana mdogo.
1 Samweli 2:18 "Lakini Samweli alikuwa akitumika mbele za BWANA, naye alikuwa kijana, mwenye kuvaa naivera ya kitani."
6. Hakikisha MUNGU yuko pamoja na wewe daima.
✓✓Jifunze kwa kijana huyu ambaye MUNGU alikuwa pamoja na yeye.
Mwanzo 21:20 "MUNGU akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde."
◼️Hakikisha humwachi MUNGU kwa ajili ya chochote.
7. Usiwe mtu wa kukata tamaa unapokuwa katika vita ya kiroho bali mtumaini MUNGU.
✓✓Jifunze kwa kijana Daudi ambaye alipokuwa katika vita ya kiroho na kimwili alimtumaini MUNGU na kwa ujasiri akashinda vita ile.
Hata kama wanadamu walimkatisha tamaa yeye alimtumaini MUNGU na kushinda.
1 Samweli 17:33 "Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake."
◼️Hakikisha hukatishwi tamaa na wanadamu bali mtumainie Bwana YESU KRISTO.
Zaburi 71:5 "Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana MUNGU, Tumaini langu tokea ujana wangu."
8. Mche MUNGU siku zote kwa kulifanyia kazi Neno lake.
Zaburi 119:9 "Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako."
✓✓Safari yako ya duniani itakuwa safi na salama kama tu utakuwa ni Mkristo anayemtii MUNGU na kulifuata Neno lake.
9. Uwe mwenye hekima katika kila usemi na maamuzi .
Hekima ni nini?
✓✓Hekima ni akili inayomwezesha mtu kufikiri na kuweza kutoa uamuzi unaofaa.
Mhubiri 4:13 "Heri kijana maskini mwenye hekima Kuliko mfalme mzee mpumbavu."
✓✓Ukikosa hekima unaweza kukosa hata baadhi ya baraka zako.
✓✓Hakikisha una hekima na hekima kuu ni matokeo ya kujifunza Neno la MUNGU na kulitii.
✓✓Hivyo enenda na wenye hekima ya ki MUNGU itakuwa faida kwako.
Mithali 13:20 "Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia."
10. Jiwekee malengo mazuri ukiwa kijana ili uzeeni yakusaidie ili usiwe mtumwa wa wanadamu.
Yohana 21:18 "Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka."
✓✓Ukiwa mzee kuna majukumu hutaweza kuyafanya hivyo jishughulishe ukiwa kijana ili ije iwe faida kwako uzeeni.
11. Hakikisha unazikimbia tamaa za ujanani.
2 Timotheo 2:22 "Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao BWANA kwa moyo safi."
✓✓Tamaa za ujanani ni pamoja na kuipenda dunia na machukizo yake, Biblia inakukataza.
1 Yohana 2:15 "Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake."
◼️Hakikisha Neno la MUNGU liko ndani yako daima na mshinde shetani na kazi zake zote.
1 Yohana 2:14 " ....... Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu."
12. Uwe na utii wa ki MUNGU kwa wakubwa zako.
1 Petro 5:5 "Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu MUNGU huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema."
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na whatsapp).
Ubarikiwe sana.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na whatsapp).
Ubarikiwe sana.
Comments