MAMBO YA KUFANYA UKIWA KATIKA DHIKI.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe sana ndugu zangu wote.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU la uzima.

Wakati mwingine wewe mteule wa KRISTO katika maisha yako hapa duniani unaweza ukapitia dhiki na magumu.

Sio lazima kwamba kila mtu lazima apitie dhiki lakini ikitokea magumu hayo yametokea basi jifunze somo la leo na utapata msaada mzuri wa kiroho.

✓✓Jambo la kwanza kujua ni kwamba dhiki zipo tu haijalishi wewe ni nani, maadamu upo duniani basi dhiki zipo tu lakini jipe moyo na tembea kwenye ushindi wa KRISTO.

Yohana 16:33 '' Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu. ''

Dhiki ni nini?

✓✓ Dhiki ni hali ya kutokuwa na raha kwa sababu ya yaliyotokea au yanayotarajiwa kutokea.

✓✓Dhiki ni taabu, mashaka, shida au usumbufu ambao mtu anaupitia katika maisha yake.

✓✓Dhiki ni matokeo ya kukosa kitu ulichokihitaji.

✓✓Dhiki ni jambo linalomuweka mtu katika mashaka makubwa au taabu.

◼️Kwa maana hizo nne za neno dhiki basi kila mtu katika muda fulani wa maisha yake anaweza kupitia dhiki au magumu fulani, na Bwana YESU amekwisha kutuambia mapema kabisa katika andiko hapo juu kwamba duniani kunaweza kutokea dhiki lakini jipe moyo maana yeye Mwokozi wetu YESU KRISTO aliushinda ulimwengu.

Ngoja nikupe mifano hai  yangu Mimi Peter Mabula kabla sijakuambia ufanye nini wakati wa dhiki.

◾Baba yangu mzazi Mzee Marco Mabula alifariki nikiwa mtoto mdogo sana, kabla hata sijafikisha miaka 5 na mama mzazi sikumuona hadi miaka kumi 11 baadae, tena nikamuona akiwa anaumwa na muda mchache baadae akafariki, hizo ndizo dhiki mbaya sana.

 Namshukuru MUNGU nililelewa na ndugu waaminifu walionitunza na kunisomesha na kunisaidia lakini Baba ni Baba tu na Mama ni Mama hivyo ana nafasi yake katika maisha ya mtoto.

◾Kipindi fulani nilipata ajali mbaya sana ya gari, ni MUNGU tu alinihurumia, hizo ndizo dhiki mbaya .

◾Kipindi fulani nikiwa shuleni niliumwa mpaka nikadhani sitamaliza siku moja baadae ila YESU akaniponya kupitia kusikiliza maombezi ya Mwl Mwakasege, hizo ndizo baadhi tu ya dhiki mbaya ambazo nilipitia.

✔️Sasa katika maisha yako wakati mwingine umepitia dhiki au uko katika dhiki au utapitia dhiki mbalimbali maana bado uko Duniani, naomba MUNGU wa Mbinguni akuepushe.

Kuna watu huingia katika dhiki baada ya kuachwa, wengine kuondokewa na wapendwa wao, wengine kufukuzwa kazi, wengine kuumwa, wengine kukosa baraka fulani wanazozihitaji, wengine kuonewa n.k

◼️Katika dhiki zote ndugu inakupasa kujipa moyo na usikubali dhiki yeyote ivunje uhusiano wako na MUNGU katika KRISTO YESU.

Wewe sio wa kwanza kupata dhiki , wapo watu wa MUNGU waaminifu kabisa walipata dhiki kuliko hata dhiki yako lakini wao walisonga mbele na wokovu.

1 Thesalonike 3:3-5 '' mtu asifadhaishwe na dhiki hizi; maana ninyi wenyewe mnajua ya kuwa twawekewa hizo. Kwa kuwa tulipokuwapo kwenu tulitangulia kuwaambia kwamba tutapata dhiki, kama ilivyotukia, nanyi mwajua. Kwa hiyo mimi nami nilipokuwa siwezi kuvumilia tena, nalituma mtu ili niijue imani yenu, asije yule mjaribu akawajaribu, na taabu yetu ikawa haina faida.''

Kuna watu walipopata dhiki kidogo ndio ikawa chanzo chao cha kwenda kwa waganga wa kienyeji na kuingia mikataba ya kishetani iliyowakosesha uzima wa milele, hiyo ni mbaya sana.

Kuna watu walipopata dhiki kidogo ndio waliacha na wokovu wakaacha na ibada, ni mbaya sana hiyo.

◼️Ndugu dhiki zipo lakini katika dhiki ongeza msimamao wako wa YESU na sio kupunguza msimamo.

Na ninaposema dhiki sina maana ya dhiki zile za kujitafutia kwa makosa yako mwenyewe, mfano umezini na kupata mimba au ugonjwa. 
Mfano umeiba kisha ukakatwa mkono au mguu, mimi sizungumzii dhiki za namna hiyo, kama uko katika dhiki ya namna hiyo dawa yake ni kutubu na kuacha dhambi hizo.

✔️✔️Mimi nazungumzia dhiki ambazo zinaweza kumpata mtu kwa sababu ameokoka

Mathayo 24:9 '' Wakati huo watawasaliti ninyi mpate dhiki, nao watawaua; nanyi mtakuwa watu wa kuchukiwa na mataifa yote kwa ajili ya jina langu. ''

✔️✔️Nazungumzia dhiki ambazo zinaweza zikampata mtu kwa sababu ni Mteule wa KRISTO ambaye bado hajatoka duniani, zinampata kwa sababu anamtumikia MUNGU na anatembea kwenye injili ya KRISTO ya uzima wa milele.

2 Kor 6-11 '' Lakini ikiwa sisi tu katika dhiki, ni kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu; au ikiwa twafarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu; ambayo hutenda kazi yake kwa kustahimili mateso yale yale tuteswayo na sisi. Na tumaini letu kwa ajili yenu ni imara, tukijua ya kuwa kama vile mlivyo washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo mmekuwa washiriki wa zile faraja. Maana ndugu, hatupendi, msijue habari ya dhiki ile iliyotupata katika Asia, ya kwamba tulilemewa mno kuliko nguvu zetu, hata tukakata tamaa ya kuishi. Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu, bali tumtumaini MUNGU, awafufuaye wafu, aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna ile; tena atatuokoa; ambaye tumemtumaini kwamba atazidi kutuokoa; ninyi nanyi mkisaidiana nasi kwa ajili yetu katika kuomba, ili, kwa sababu ya ile karama tupewayo sisi kwa msaada wa watu wengi, watu wengi watoe shukrani kwa ajili yetu. ''

✔️✔️Nazungumzia dhiki ambayo unaipata kwa sababu una YESU KRISTO na unaishi maisha matakatifu ya Wokovu.

2 Kor 6:4 ''bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa Mungu; katika saburi nyingi, katika dhiki, katika misiba, katika shida;''

Nini ufanye wakati wa dhiki?

1. Muombe MUNGU ili akutoe katika dhiki hiyo na kukuinua.

Zaburi 20:1 '' BWANA akujibu siku ya dhiki, Jina la Mungu wa Yakobo likuinue.''

✓✓Wewe sio wa kwanza kuingia katika dhiki, jifunze kwa hawa ambao walipoingia katika dhiki walimuomba MUNGU na akawatoa katika dhiki.

Zaburi 107:6 '' Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.''

◼️Hata Bwana YESU alipokuwa duniani katika mwili kama wetu alipitia dhiki kali sana ya kukubali kufa kwa ajili yetu ili tupate ondoleo la dhambi, katika dhiki aliyokuwa nayo Bwana YESU Biblia inasema alizidi sana kuomba.

Luka 22:44 '' Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.] ''

✓✓Hata wewe ukiwa katika dhiki yeyote basi zidi sana kuomba MUNGU.

2. Uwe mwenye haki ili uokolewe wakati wa dhiki.

Mitahli 11:8 '' Mwenye haki huokolewa katika dhiki, Na mtu mwovu ataiingia badala yake.''

✓✓Kama huishi maisha matakatifu na uko katika dhiki tubu haraka sana ili ufanyike mwenye haki na ndipo utauona msaada wa MUNGU.

✓✓Wapo watu hupata dhiki kwa sababu ya uovu wao, hao inawapasa kutubu tu ndipo watafute neema ya MUNGU ya kuwatoa kwenye dhiki.

◼️Uwe mwenye haki katika yote ili MUNGU akuokoe kutoka katika dhiki, mfano kama mnagombea kiwanja na hicho kiwanja ni haki yako kabisa hujamuibia mtu basi huko ndiko kuwa mwenye haki na MUNGU atakuokoa.

Mfano mtu anakuonea katika kitu ambacho ni haki yako kabisa au ni mali yako halali kabisa, ukiwa mwenye haki na ukamwita MUNGU hakika atakuokoa kutoka katika dhiki hiyo.

3. Furahi wakati wa dhiki ili uwe thabiti.

Warumi 5:3-4 '' Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini;''

Kuwa thabiti ni kuwa mtu imara,mwenye tumaini, mwenye nguvu asiyetetereka.

Ukiona mtu baada ya kuingia katika dhiki amezifuata madhabahu za giza ni kwa sababu mtu huyo hajitambui na sio thabiti katika imani ya Wokovu wa KRISTO.

4. Usikubali dhiki yeyote ikutenge na YESU Mwokozi.

Warumi 8:35 '' Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? ''

5. Mngoje MUNGU na atatokea na kukushindia.

Warumi 12:12 ''kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu; ''

✓✓Mngoje MUNGU katika dhiki yako huku ukiomba na kutimiza wajibu wako kwa MUNGU, Mmgoje MUNGU naye atakulipizia kisasi kwa adui zako.

Zaburi 37:34 '' Wewe umngoje BWANA, Uishike njia yake, Naye atakutukuza uirithi nchi, Wasio haki watakapoharibiwa utawaona. ''

6. Kubali kufarijiwa na Watumishi wa MUNGU na Neno la MUNGU.

✓✓Kazi mojawapo ya ROHO MTAKATIFU ni kutufariji sisi wateule wa KRISTO, ndugu kubali kufarijiwa na ROHO MTAKATIFU kupitia watumishi wake.

2 Kor 1:4 '' atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na MUNGU. ''

Hiki ndicho kitu watu wengi hawajui kwamba Neno la MUNGU ni faraja ya ajabu sana na yenye nguvu na iliyo hai, ndugu somo Neno la MUNGU na kulitafakari maana limejaa faraja kubwa sana za kukupa nguvu hata ukajiona kama hauko katika dhiki, pia Neno la MUNGU lina ahadi ya ushindi wako hivyo ukizingatia utatoka salama.

1 Thesalonike 1:6 '' Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, mkiisha kulipokea neno katika dhiki nyingi, pamoja na furaha ya ROHO MTAKATIFU. ''

7. Wakati wa dhiki usikate tamaa.

2 Kor 4:8 '' Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; ''

✓✓Usikubali kukata tamaa hata adui akataka kuchukua nafasi ndani yako, bali songa mbele na YESU bila kukata tamaa.

✓✓Kumbuka pia kwamba hakuna jaribu la kudumu bali kila jaribu ni la muda tu kisha wewe utabaki ukiendelea mbele bila hilo jaribu, ndugu usikate tamaa.

2 Kor 4:17 '' Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana;''

8. Uwe mwaminifu katika KRISTO hata wakati wa dhiki.

Ufunuo 2:10 '' Usiogope mambo yatakayokupata; tazama, huyo Ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima. Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo ROHO ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili. ''

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments