![]() |
Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni |
Bwana YESU KRISTO asifiwe Rafiki yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU Kisha tuombe Maombi ya ushindi.
Leo nataka tuombe maombi ya kuvunja maagano.
Miaka michache iliyopita Mimi Peter Mabula nikiwa pamoja na wenzangu wachache tukiwa katika maombi ya mkesha Kanisani sauti ilinijia kusema "VUNJA MAAGANO YA GIZA"
Ufafanuzi katika ufunuo huo ulikuwa mkubwa na nikashangaa sana.
◼️Kumbe kuna maagano mabaya mengi ya adui ili kuhakikisha hatusongi mbele lakini ashukuriwe Bwana YESU maana damu yake ya Pasaka inaweza kufuta maagano yote ya kipepo.
Vyanzo vingi vya mateso na taabu za kiroho ni Mtu kuingia kwenye Maagano ya giza kwa kujua au kwa kutokujua, ndio maana MUNGU wa Mbinguni anatukataza Kanisa lake leo kuingia katika Maagano ya giza au Maagano mabaya na walio nje ya Wokovu.
Kutoka 23:32 ''Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao.''
✓✓Waisraeli walikuwa wameokoka kama wewe ambavyo umeokoka katika KRISTO YESU lakini MUNGU aliwaonya juu ya kuingia maagano ya kishetani.
✓✓Agano ni kitu kikubwa sana, agano la kipepo ni mapatano ya kishetani, ni mikataba ya kishetani na MUNGU hataki tuingie agano lolote na shetani wala mawakala wake.
Shetani kwa kulijua hilo kwamba hatumtaki na mipango yake yote basi kuna vitu huwa vimefanyiwa maagano tayari kwa ajili yetu kitu ambacho tusipoomba kuna madhara ya kiroho na hata ya kimwili yanaweza kutokea.
◼️Kuna maagano kwenye baadhi ya vyakula hivyo ni muhimu sana kuombea chakula.
◼️Vitanda vinaweza kuwekewa maagano mabaya na kusababisha vifungo vikubwa vya kiroho.
Ndugu, sio Watu wote ni watumishi wa MUNGU, wengine ni mawakala wa shetani na kazi yao ni kuhakikisha unashikiliwa na agano la kishetani.
Katika Maisha yako ya Wokovu unatakiwa uwe makini sana maana kama ambavyo YESU KRISTO yuko kazini, na shetani naye yuko kazini, majini na mizimu na nguvu zingine za giza wako kazini, hivyo uwe makini ili usiingie katika kamba za kipepo kupitia maagano ya giza.
✓✓Agano la kipepo sio Lazima uingie wewe hata mzazi wako anaweza kuingia agano la kipepo litakalokutesa wewe, hata Kama aliingia agano hilo Kwa kujua au Kwa kutokujua.
✓✓Hata bosi wako anaweza kuingia agano la kipepo Kwa ajili ya eneo la kazi na wewe kuathirika maana unafanya kazi ofisi hiyo.
Kama Watu wa KRISTO ni muhimu sana tuwe Watu wa kumsikiliza ROHO MTAKATIFU na kumtiii sana ili tuwe Salama maana adui zetu mashetani nao wako kazini kujaribu kutudhuru kiroho au kututesa.
Siku moja miaka mingi imepita nilikuwa nasikiliza mahubiri ya Mwalimu Mwakasege, alikuwa anaelezea tukio ambalo lilipangwa kumpata alipokuwa kwenye huduma Marekani, nguvu za giza walitaka kumdhuru kiroho kupitia karamu tu ya kuandikia, ila neema ya MUNGU ni kwamba ROHO MTAKATIFU alimjulisha mapema juu ya hatari hiyo na ilipokuja aliiepuka. Katika Ushuhuda huo nilijua kwamba Watu tukiookoka tuko vitani na tunawindwa hivyo tuwe waombaji sana na tumsikilize na kumtiii sana ROHO MTAKATIFU.
Nguvu za giza na Watu wanaotumika kipepo hufanya mbinu nyingi za Siri ili mtu wa MUNGU uwe katika vifungo vya kipepo, kazi yao Moja ni kuhakikisha unapatwa na maagano ya kipepo.
Kuna maeneo yamejaa maagano mabaya.
Unaweza ukaenda mahali na kumbe mawakala wa shetani wametegeshea kitanda chenye maagano ukilalia tu bila kukiombea unaweza kushangaa umevurugika fahamu, roho ya uzinzi na usaliti imekuvaa, nguvu za giza zinakuvamia n.k
Hata ardhi yako adui anaweza kuifanyia maagano mabaya ili usifanikiwe.
Mambo mengi sana yamewekewa maagano na adui ndio maana tunatakiwa kuomba sana.
Unaweza kujiuliza swali dogo tu kama hili; kwanini wanawake wengi ndio huteswa sana na mapepo?
◼️Jibu ni vitu wanavyotumia maana vingi vina maagano ya kipepo, vingi vina mapando ya shetani mfano vipodozi, mapambo, nywele bandia,wigi n.k.
Mawakala wa kuzimu wanapanda kitu kidogo tu lakini ukizubaa utajikuta mara unavalishwa pete na mwanaume usiyemjua ndotoni kumbe jini maana vitu vyako ndivyo vilivyofungua mlango kwa jini huyo kuingia kwako, na akikuweza anaweza hata kukuzuilia kufunga ndoa, kukuzuilia kuzaa, kwenda Kanisani au kusoma Biblia huku ukitamani lakini umeshindwa.
Adui anaweza kupanda kitu kidogo tu na ukizubaa utajikuta unapenda miziki ya kidunia tu na nyimbo za MUNGU utaona machukizo kumbe adui anakuendesha kipepo.
Adui ukimpa nafasi kidogo tu, ukizubaa unaweza kujikuta kila siku unaota ndoto ukizini kumbe shetani anaongeza maagano mengine zaidi ili hata kupata mtoto baadae iwe tatizo.
◼️Ndugu yangu, maagano ya kipepo lazima yaondoke kwako kwa jina la YESU KRISTO ndio utakuwa huru.
Kuna watu sura zao zimefanyiwa maagano ya kipepo ya kuchukiwa na kila mtu, kuchukiwa kazini, hata unaweza ukakosa mme au mke kwa sababu tu ya tatizo hilo la kishetani la maagano.
Maagano ni mabaya sana.
Kuna maagano kwenye baadhi ya mavazi tunayonunua N.K, hivyo ni muhimu sana kutakasa Tunavyonunua kwa jina la YESU KRISTO.
Hata kuna baadhi ya vitanda vina maagano mabaya, na MUNGU anapokataza uzinzi ni kwa lengo la kukusaidia tu mwanadamu wewe na sio vinginevyo. Maana uzinzi unaweza ukaongeza tatizo zaidi badala ya dhambi tu basi na maagano ya giza juu yake.
Isaya 57:8 '' Na nyuma ya milango na miimo umeweka kumbukumbu lako; kwa maana umejifunua nafsi yako kwa ajili ya mwingine, si kwa ajili yangu, ukakwea juu; umekipanua kitanda chako, nawe umefanya maagano na hao; ulikipenda kitanda chao hapo ulipokiona. ''
Maagano mabaya ni jambo baya sana ndugu.
Kama zamani uliwahi kuingia maagano ya kishetani basi kimbilia Kanisani ukaombewe maana maagano ni mkataba na ukiingia mkataba na shetani mwishowe anaweza kukuangamiza tu na uzima wa milele ukaukosa.
Hosea 10:4 ''Hunena maneno yasiyo na maana; huapa kwa uongo wafanyapo maagano; basi ndipo hukumu huchipuka kama mbaruti katika matuta ya shamba.''
Maagano ya kishetani ni mabaya sana na ni muhimu kujitenga nayo kwa kumkimbilia Bwana YESU na nguvu zake.
1 Nyakati 16:11 "Mtakeni BWANA na nguvu zake; Utafuteni uso wake siku zote."
Wachawi wakati mwingine wanaweza kuifanyia maagano mabaya sauti yako na ndio maana kinywa chako kila siku kinakutendesha dhambi.
Sio kila zawadi unapokea tu bila hata kuiombea.
Sio kila mialiko lazima uende.
omba kwanza na msikilize ROHO MTAKATIFU.
Adui ana mbinu nyingi lakini kama utakuwa mwombaji hakika utashinda siku zote na Miaka yote.
Kuna maagano mengine inahitajika nguvu kubwa sana ili kuyavunja na nguvu kubwa ni mbili tu, Damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO.
Katika utumishi wangu kwa KRISTO Mimi Peter Mabula nimegundua Moja ya maagano ya kipepo mabaya sana ni maagano ya damu na maagano ya pesa.
Ndugu, najua umejifunza kitu na utachukua hatua ya kuomba na kujiunga na Kanisa la kiroho ili uwe kwenye mzunguko wa maombi.
Kuna watu huwa nawaambia wajiunge na Kanisa na wanapofanya hivyo tu mateso yao ya kuteswa na wachawi yanakoma. unajua ni kwanini? ni kwa sababu wanakuwa katika mzunguko wa maombi, mfano mchungaji kama atafunga au ataomba kwa ajili ya huduma yake ni lazima akujumuishe na wewe maana uko katika huduma hiyo, kama viongozi wa wamama au viongozi wa vijana watakuwa wanaombea vijana wao au wamama au wababa lazima na wewe utakuwa unaombewa hivyo ukiongeza na maombi yako mwenyewe na kuhudhuria ibada hakika adui atakimbia hata kama hataki maana atakuwa anapata kipigo kila saa, kama anadhani umelala wewe akisogea tu anapata kipigo maana wakati huo Mchungaji anaomba, wakati huo kundi la maombi linaomba.
Kujiunga na Kanisa na kuanza kuishi maisha matakatifu ya wokovu wa Bwana YESU ni jambo la muhimu sana.
Sina mengi Leo, hapa chini ni maombi ya kumsaidia muombaji mchanga ili kujua kuomba zaidi na kupambana zaidi katika vita ya kiroho ili ashinde.
Wewe muombaji mzoefu naamini uliposoma tu somo uliandika points za kuombea kwenye maisha yako kuhusu maagano ya giza, Omba katika jina la YESU KRISTO na utashinda.
Zingatia tu kugusia maeneo Haya.
1.Ndoa.
Omba na utashangaa ndoa yako imetoka kwenye maagano ya giza.
2. Uzao.
Omba na watoto wako utashangaa wametoka katika maagano ya giza.
3. Pesa zako na uchumi wako.
Omba na pesa zako na uchumi wako utashangaa vimefunguliwa kutoka maagano ya giza.
Uwe pia mwaminifu katika kutoa fungu la kumi na sadaka nzuri kama ukitaka pesa zako na uchumi wako viwe salama na Kwa faida yako.
4. Kibali.
Omba na utashangaa kibali chako kimefunguliwa kutoka maagano ya giza.
5. Mwili na Afya.
Omba na utashangaa mwili wako na Afya yako vimefunguliwa kutoka maagano ya kipepo.
Nina shuhuda nyingi kutoka kwa watu ninaowafanyia Huduma za maombi Mara Kwa Mara.
Kuna Watu vitu vinatembea katika miili yao Kwa sababu ya maagano ya giza ya zamani.
Kuna Watu ni wagonjwa sana Kwa sababu ya maagano ya giza ya zamani.
Kuna Watu baadhi ya viungo vya miili yao havifanyi kazi Kwa sababu ya maagano ya giza ya zamani.
Kuna watu miili yao imekuwa makazi ya nguvu za giza Kwa sababu ya maagano ya giza ya zamani.
Kuna watu afya zao zimeondolewa kichawi
Kwa sababu ya maagano ya giza ya zamani.
Leo Futa kila agano la kipetKwa maombi katika jina kuu la YESU KRISTO.
6. Ardhi yako
futa maagano ya kipepo Katika Ardhi inayokuhusu.
Futa kumbukumbu zote za kipepo zilizotunzwa ardhini kuhusu wewe.
7. Vitu unavyotumia.
Futa maagano ya kipepo katika vitu hivyo.
Vitakase kwa damu ya YESU KRISTO vitu hivyo.
Maombi ya kuvunja maagano ya kishetani.
"BABA yangu uliye mbinguni, jina lako litukuzwe milele, ninakushukuru BWANA kwa kunilinda na kunipa afya njema.
Ninakushukuru kwa kuwalinda ndugu zangu na familia yangu.
Bwana YESU, mimi ni binadamu na yawezekana kabisa kuna sehemu nimekosea, BWANA naomba unisamehe dhambi zangu zote, zile ninazokumbuka na zile ambazo sikumbuki. Neno lako Katika Matendo 3:19 linasema ''Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;''
BWANA ninatubu leo na naomba unisamehe MUNGU wangu. nipe kuishi maisha ya ushindi dhidi ya dhambi na nipe kumtii ROHO MTAKATIFU maana ndiye mwangalizi wa roho yangu.
nakushukuru JEHOVAH BWANA maana naamini umenisamehe MUNGU wa uzima.
BWANA neno lako linasema katika Isaya 41:21 kwamba '' Haya, leteni maneno yenu, asema BWANA; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo.''
Bwana MUNGU hoja yangu yeye nguvu ni maagano ya kipepo yote ambayo ninaomba yafutike leo kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
Maagano ya magonjwa na maagano ya ardhi ninayokaa nanyunyuzia damu ya YESU na Sasa nayafuta kwa jina la YESU KRISTO.
Imeandikwa katika Waebrania 12:24 kwamba " na YESU mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili." Hivyo damu ya YESU KRISTO ya kunyunyizwa naitumia leo ili kuvunja Maagano na kuvuta Maagano ya giza yote.
Maagano ya mavazi na maagano ya vyakula nanyunyuzia damu ya YESU na Sasa nayafuta Maagano hayo kwa jina la YESU KRISTO.
Maishani mwangu ninalifuta leo kwa damu ya YESU na kwa jina la YESU KRISTO Kila agano la giza, haijalishi nililifanya mimi au wazazi wangu nanyunyuzia damu ya YESU na Sasa nafuta agano hilo kwa jina la YESU KRISTO.
Kila agano la kishetani kwenye ardhi yangu au nyumba yangu nanyunyuzia damu ya YESU na Sasa nafuta agano hilo kwa jina la YESU KRISTO.
kila agano la giza kwenye kitanda nilichowahi kulalia au kwenye mashuka niliyowahi kujifunika nanyunyuzia damu ya YESU na Sasa nafuta agano hilo kwa jina la YESU KRISTO.
Kila agano la giza kutoka kwa wote niliowahi kufanya nao mapenzi kimwili au ndotoni nanyunyuzia damu ya YESU na Sasa nafuta agano hilo kwa jina la YESU KRISTO.
Kila agano ambalo yawezekana silijui au nalijua ambalo nila giza nanyunyuzia damu ya YESU na Sasa nafuta agano hilo kwa jina la YESU KRISTO.
Kila agano la giza kuanzia leo limefutika kwa jina la YESU KRISTO, kuanzia sasa niko huru mbali na maagano ya kishetani, kuanzia sasa mimi ni mshindi kwa jina la YESU KRISTO.
Nakushukuru BABA wa mbinguni maana umenishindia, nakushukuru Bwana YESU maana damu imenena mema kwangu kuanzia sasa maana maagano mabaya yote yamefutika kwa jina la YESU.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi.
Amen Amen Ameeeeeeeeeen.
Ndugu hayo ni maombi ya kuanzia tu hivyo endelea zaidi Katika maombi.
Lakini pia nikiwa namalizia somo hili naomba nikueleze hivi.
Ndugu Yangu, Usikubali Kumkana YESU Na Hakikisha Unajikana Ili Umpendeze MUNGU.
Usitende Dhambi Maana Kutenda Dhambi Ni Kumkana Bwana YESU.
Ukidumu katika mema bila kumkana YESU utafanya vyema.
Yeye Bwana YESU anasema '' Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. -Yohana 10:28 ''
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU KRISTO? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU KRISTO Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, Sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na whatsapp pia).
Ubarikiwe
Comments