MAOMBI YA KUIFUNGA CHEMCHEMI YA MABAYA NA KUFUNGULIA CHEMCHEMI YA BARAKA.

Na Mwl Peter Mabula


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU la maombi ya ushindi.

✓✓Kuna chemchemi ya mema na kuna chemchemi ya mabaya.

MUNGU ndiye hutupa chemchemi ya mema lakini nguvu za giza ndio hutoa chemchemi ya mabaya, nifuatilie hadi mwisho katika somo hili utanielewe vyema na utapata maarifa ya maombi ya ushindi kwako.

✓✓Ziko chemchemi njema nyingi sana mfano chemchemi ya afya njema, chemchemi ya kibali cha kudumu au ndoa njema.

Mithali 5:18 "Chemchemi yako ibarikiwe; Nawe umfurahie mke wa ujana wako."

✓✓Chemchemi za uchumi.

Isaya 49:10 "Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza."

Lakini pia ziko Chemchemi za mabaya hizo ni pamoja na, Magonjwa yasioisha, Migogoro isiyoisha,Majanga yasioisha,

Tatizo lisiloisha n.k

Nimesema ni nguvu za giza ndio huleta chemichemi za mabaya.

Nguvu za giza zimekuweka chemichemi ya nini?

Tuone mfano huu.

Marko 5:25-29 " Na mwanamke mmoja mwenye kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, na kuteswa mengi kwa mikono ya matabibu wengi, amegharimiwa vitu vyote alivyo navyo, kusimfae hata kidogo, bali hali yake ilizidi kuwa mbaya aliposikia habari za YESU, alipita katika mkutano kwa nyuma, akaligusa vazi lake; maana alisema, Nikiyagusa mavazi yake tu, nitapona. Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, naye akafahamu mwilini mwake kwamba amepona msiba ule."

Tunajifunza nini kwa mama huyu;

Miaka 12 alikuwa anatokwa na damu na kuteswa kwa mikono ya madaktari wengi.

Chemichemi ya damu iliyokuwa inatoka ndani yake iligharimu mali zake na bado hakupona na tatizo likaongezeka.

Alipotambua kwamba YESU yuko eneo hilo alienda kwenye uponyaji kwa staili yake akapona kwa chimichemi ya damu yake kukauka.

Huyu alikuwa na chemchemi ya damu isiyokauka yaani alikuwa anatokwa damu mfululizo miaka kumi na mbili, chemchemi hiyo mbaya ilikoma tu pale ambapo Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu alipoingilia kati, hata wewe kama nguvu za giza wamekufungulia chemchemi ya kuugua mfululizo, kupata hasara mfululizo, kuonewa mfululizo, kuteseka mfululizo n.k unamhitaji YESU KRISTO ili aifunge hiyo chemchemi ya mabaya iliyofunguliwa kwako na nguvu za giza.

YESU hutoa chemchemi ya uzima bure.

Tena wala sio mpango wa MUNGU chemchemi za mapepo zifunguliwe kwako.

YESU anafunga chemchemi za nguvu za giza na atakufungulia chemchemi ya uzima bure, Omba tu ndugu.

Ufunuo 21:6 "Akaniambia, Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Mimi nitampa yeye mwenye kiu, ya chemchemi ya maji ya uzima, bure.''

Nimesema kuna chemchemi ya mabaya na kuna chemichemi mema,

Kazi ya nguvu za giza wanaweza kuikausha chemichemi ya mema na wakafungulia chemichemi ya mabaya.

YESU anaweza kukausha chemichemi ya mabaya na akafungulia chemichemi ya mema na Baraka.

Yohana 4:14 "walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele."

Inawezekana unaumwa, ukimkimbilia YESU atakuponya na kukuelekeza katika chemichemi ya uzima yaani uwe mzima daima bila kuteswa tena na magonjwa au uharibifu wowote wa kipepo.

Ufunuo 7:17 "Kwa maana huyo Mwana-Kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na MUNGU atayafuta machozi yote katika macho yao."

Wakati mwingine chemchemi za baraka zinaweza kufungwa kwa mtu.

Je chemichemi ya Baraka zako zimefungwa? Leo pata nafasi ya kuomba katika jina la YESU KRISTO na chemichemi yako itapona na kufunguliwa na utapata Baraka zote.

chemchemi yako inatakiwa kupona kwa maombi katika jina la YESU KRISTO.

2 Wafalme 2:21 "Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, BWANA asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza."

Lakini pia kumbuka kuna baraka za kipepo yaani mtu asiye na akili anaingia mikataba na shetani ili shetani afungulie chemchemi ya baraka za kipepo za muda mfupi kisha amuue mtu huyo.

Ndugu, Inawezekana wewe unateswa na mtu ambaye chemchemi ya baraka zake ni ya kipepo baada ya mtu huyo kuingia mikataba na shetani.

Sasa kama anakutesa na kukuonea kwa sababu ya utajiri wake unaotokana na chemchemi ya kipepo aliyofunguliwa na nguvu za giza, wewe katika vita ya kiroho ziba chemichemi za Baraka za mawakala wa kishetani maana Baraka zao hutokana na mikataba ya kipepo na kafara.

Kumbuka pia kazi ya Kanisa ni pamoja na kuzivunja na kuziharibu kazi zote za shetani(Yeremia 1:10, 1 Yohana 3:8) hivyo kama watu wanatoa kafara watoto wao au ndugu zao ili shetani awafungulie chemchemi za baraka za kipepo, wewe kwa maombi ziba chemchemi hizo za kipepo nguvu za giza zisienee zaidi hata watu wengi zaidi wakauawa kwa tamaa ya utajiri wa kishetani.

Unaweza kuomba ili kuiziba chemchemi ya baraka za kipepo ili watu wajifunze kumfuata MUNGU aliye hai aliyejifunua tu kupitia YESU KRISTO Mwanaye wa pekee.

Jifunze kwa mfano huu ambapo ili Waisraeli washinde vita MUNGU kupitia Elisha aliwaambia wahakikishe wanaziziba chemchemi za maji zilizoelekea kwa adui zao.

2 Wafalme 3:19 "Nanyi mtapiga kila mji wenye boma, na kila mji ulio mzuri, na kila mti mwema mtaukata, na chemchemi zote za maji mtaziziba, na kila mahali palipo pema mtapaharibu kwa mawe."

Hiyo ndio vita ya kiroho.

Nikiwa mkoa fulani kuhubiri Injili mitaani mwaka 2010 tulienda mtaa fulani ambao una nyumba za kifahari nyingi. Ajabu nyumba kadhaa kati ya nyingi tulizoingia tulikuta kuna zezeta mmoja ambaye ameshatengenezewa chumba nje ya nyumba kubwa. Tuliwaeleza injili wakakataa na tulipoomba tuwaombee hao zezeta ndipo tulifukuzwa kwa vitisho vikali, kwa sababu mimi nilikuwa mgeni huko nilimuuliza mchungaji wangu "Kwanini kila nyumba kuna mtu zezeta? " akaniambia "Watu wengi huku wanawatoa kafara wake zao au watoto au wazazi ili wawe matajiri, ndio maana unaona kila nyumba ya ghorofa nzuri kuna zezeta pia ambaye hulindwa sana dhidi ya wahubiri injili wasije wakamuombea akapona na utajiri ukayeyuka"

Nilisikitika sana jinsi ambavyo baadhi ya watu wanatumia nguvu za giza kupata utajiri, na kwa sababu shetani ni roho ya uharibifu basi hawafungulii chemchemi bure bure lazima walipe gharama na gharama ndio hizo mara mtu kumuua ndugu yake au mzazi wake au mwenzi wake, utasikia mtu fulani kawa kichaa au zezeta ili fulani atajirike, utasikia fulani kambaka mama yake mzazi kisha kumuua ili atajirike, utasikia fulani katolewa kafara na mama yake au baba yake au ndugu yake "

Sasa nini nataka kusema?

Ni wewe ndio uko katika familia au ukoo ambao watu hutoa kafara za watu ili wao watajirike, ndugu usipookoka, usipojua kumcha MUNGU katika KRISTO, kumtegemea na kufanya maombi ujue wanaweza hata wewe kukutoa kafara, hivyo ndugu mkimbilie Bwana YESU KRISTO ili uwe salama, omba ukiziba chemchemi za baraka za kipepo ili watu wajifunze kumtegemea MUNGU na sio shetani.

Kuna ndugu mmoja aliniambia siku Moja jambo la ajabu sana yaani kaka yao mkubwa amewafunga kichawi wadogo zake wote wa tumbo moja ili yeye tu atajirike, na kaka yao huyo ameshawaweka wazi kabisa kwamba amewafunga kichawi maana ndiyo masharti aliyopewa, ni hatari sana.

Sasa wewe mombaji unaweza kuomba maombi kuiziba chemichemi yake ya Baraka za kipepo na unaweza kujifungua kwa maombi kutoka katika vifungo vya giza.

Ona mfano huu baada ya chemichemi ya wakala wa kishetani kuzibwa na Waisraeli Kwa ufunuo wa Elisha.

2 Wafalme 3:25-27 " Wakaibomoa ile miji; wakatupa katika kila mahali palipo pema kila mtu jiwe lake, wakapajaza; wakaziziba chemchemi zote za maji, wakaikata miti yote iliyo mizuri; mpaka katika Kir-haresethi tu wakayasaza mawe yake; ila wenye kombeo wakauzunguka wakaupiga. Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki. Ndipo akamtwaa mwanawe wa kwanza, yeye ambaye angetawala mahali pake, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli; basi wakatoka kwake, wakarudi kwenda nchi yao wenyewe."

Ndugu, usiruhusu chemchemi ya Baraka ya adui anayekuloga, usiruhusu hiyo chemichemi ikabubujika.

2 Nyakati 32:3-4 "akafanya shauri na wakuu wake, na mashujaa wake, kuzuia maji ya chemchemi zilizokuwa nje ya mji; nao wakamsaidia. Wakakusanyika watu wengi, wakazizuia chemchemi zote, na kijito kilichopita kati ya nchi, wakisema, Kwa nini, wakifika wafalme wa Ashuru, waone maji mengi?"

Kuna kuzuia chemichemi ya wakala wa shetani anayekufatilia.

2 Nyakati 32:30 "Naye huyo Hezekia ndiye aliyezuia chemchemi ya juu ya maji ya Gihoni, akayaleta chini moja kwa moja upande wa magharibi wa mji wa Daudi. Akafanikiwa Hezekia katika kazi zake zote."

Sina maana ufunge kila chemichemi ya mtu, usifanye hivyo kamwe bali kama amekufunga kichawi ili afanikiwe, huyo ziba kimaombi chemicemi yake.

MUNGU anaweza kukuletea kwenye ulimwengu wa roho yule aliyoifunga familia yako, amefunga uchumi na kibali chako, amefunga afya yako ili atajirike, amekuzuia kuzaa au mimba yako changa ameitoa kichawi kama kafara ili afanikiwe, mtu wa namna hiyo ziba chemichemi zake za kufanikiwa ili ajue kwamba amevamia pasipomstahili, ili ajue kwamba amevamia kambi ya Waebrania na kinachofuata kwake ni kuabika na kutoweshwa.

Zaburi 40:14-15 " Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu. Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe!"

Kama yuko mtu anakufunga wewe kichawi ili yeye afanikiwe leo ziba chemichemi zake za Baraka na kitakachofuata atanyosha mikono juu na kusalimu amri hata kama alikuwa shujaa.

Hakuna umbali kwenye ulimwengu wa roho hivyo omba ukitaja vitendo vya kichawi alivyokufanyia na utamshinda kwa jina la YESU KRISTO.

Muige Hezekia aliyefunga chemichemi za adui zake mwenye nguvu kisha Hezekia akasema "kwake(adui yetu) upo mkono wa mwili; ila kwetu yupo BWANA, Mungu wetu, kutusaidia, na kutupigania mapigano yetu. Na watu wakayategemea maneno ya Hezekia, mfalme wa Yuda.- 2 Nyakati 32:8"

Nini ufanye kwenye maombi na kwenye maisha yako.

1. Tubu kwa ajili ya makosa yako kwa MUNGU yalichosababisha chemichemi ya Baraka zako kufungwa, ili MUNGU akusaidie anza na toba ya kweli.

Isaya 59:1-2 "Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."

2. Tubu kwa kilichosababisha mawakala wa shetani kufungulia chemchemi za mabaya kwako.

Fanya kama Yeremia alivyokuwa anawaombolezea kwa toba Waisraeli ambao walikuwa wanaenda utumwani Babeli kwa sababu ya makosa yao mbele za MUNGU.

Maombolezo 1:20 "Angalia, Ee BWANA; maana mimi ni katika dhiki; Mtima wangu umetaabika; Moyo wangu umegeuka ndani yangu; Maana nimeasi vibaya sana; Huko nje upanga hufisha watu; Nyumbani mna kama mauti."

3. Fungua chemichemi za Baraka (zitaje hizo Baraka )

Zaburi 36:9 "Maana kwako Wewe(MUNGU) iko chemchemi ya uzima, Katika nuru yako tutaona nuru."

Katika KRISTO tumepewa mamlaka ya kufungua na Kufunga hivyo fungua chemchemi yako ya baraka.

Mathayo 16:19 "Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni."

✓✓Kuna watu kila akianzisha biashara wateja wanakuwa wengi siku chache kisha wanayeyuka, ndugu ifungue chemchemi ya wateja kuja kwenye biashara yako.

✓✓Inawezekana wewe kupata wachumba sio tatizo lakini chemchemi ya kuingia kwenye ndoa ndio imefungwa kipepo ndio Maana ukipiga hesabu ni zaidi ya wachumba kumi umewahi kuwa nao kwa utakatifu kabisa lakini suala la kuingia katika ndoa lilishidikana, ndugu ifungue chemchemi yako ya kukuingiza katika ndoa takatifu kwa ushuhuda na utakatifu safi.

Ziko chemchemi nyingi zinaweza kufungwa kwa mtu, ndugu leo fungulia chemchemi zako njema zilizokuwa zimefungwa, zifungulie kwa maombi katika jina la YESU KRISTO Mwokozi.

4. Funga chemichemi za Baraka wanadamu waliokuloga, kukufanyia uchawi au uganga wa namna yeyote.

Mwite MUNGU mweza yote.

Zaburi 107:33 "Amegeuza mito ikawa jangwa, Na chemchemi za maji zikawa nchi ya kiu."

Katika KRISTO unayo mamlaka ya kufunga na kufungua, wewe leo funga chemichemi za baraka za kipepo za wanadamu waliokuloga, kukufanyia uchawi au uganga wa namna yeyote.

Mathayo 18:18 Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.

5. Mche MUNGU katika KRISTO YESU ili uepukane na tanzi za mauti za nguvu za giza.

Mithali 14:27 "Kumcha BWANA ni chemchemi ya uzima, Ili kuepukana na tanzi za mauti."

Ndugu, omba katika jina la YESU KRISTO na utamuona MUNGU wa Mbinguni.
By Mwl Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai.
+255714252292(Whatsapp, sadaka ya kuipeleka Injili )
Ubarikiwe

Comments