![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU Leo ni kuhusu kutubu na kujitakasa.
●Kutubu ni nini?
▪︎Kutubu ni kuomba msamaha kwa MUNGU katika KRISTO YESU kwa ajili ya makosa, dhambi na uovu ulivyofanya.
Matendo 3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"
▪︎Kutubu ni kujutia dhambi uliyofanya kisha ukaomba msamaha kwa uliyemkosea.
Mathayo 4:17 "Tokea wakati huo YESU alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia."
▪︎Kutubu ni kujutia uovu wako kisha unaomba msamaha na kujitenga na uovu huo.
Moja ya maombi muhimu sana kwa kila Mkristo ni maombi ya kutubu na kujitakasa.
●Kujitakasa ni nini?
▪︎Maana ya kwanza ya neno kujitakasa ni kufanya kitu kinachoifanya roho yako kuwa safi.
Ni kufanya maombi ya toba ya kukusafisha ili uwe safi kiroho.
1 Wathesalonike 4:7 "Maana MUNGU hakutuitia uchafu, bali tuwe katika utakaso."
▪︎Maana ya pili ya kujitakasa ni kuondoa uchafu katika roho yako na mwili kiroho.
Ni muhimu pia kujua kwamba kutakaswa huendana na kuacha dhambi.
Isaya 1:16 "Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;"
●Kinachoweza kutakasa ni nini?
Kinachoweza kumtakasa mtu ni Damu ya YESU KRISTO pekee.
Kwa mtu anayetubu kwa MUNGU katika KRISTO YESU damu ya YESU KRISTO humtakasa mtu huyo, ni damu ya YESU KRISTO tu ndio inayotakasa.
Waebrania 10:10 "Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa YESU KRISTO mara moja tu."
Watu wengi katika maombi yao huwa wanaomba tu msamaha na sio kuomba kutakaswa pia.
Kuomba msamaha kwa MUNGU ni muhimu sana lakini pia katika maombi yako jifunze kuunganisha na kuomba kutakaswa.
MUNGU anataka Watu wajitakase.
Zaburi 18:26 "Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi."
Kuna tofauti kati ya msamaha na kutakaswa.
●Msamaha ni tendo la kumwia mtu radhi kwa makosa aliyoyafanya lakini utakaso ni kumsafisha mtu rohoni na mwilini.
Ndio maana Daudi katika Zaburi 51 hakuomba tu kusamehewa bali aliomba na kutakaswa pia, iga maombi ya namna hiyo katika kutubu, kuachiliwa na kutakaswa.
Zaburi 51:1-2 " Ee MUNGU, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu."
▪︎Anaposema "Ee MUNGU unirehemu " Maana yake Ee MUNGU naomba unisamehe na kuniachilia dhambi zangu.
Lakini hakuishia hivyo tu ndio maana mbele kidogo anamwambia MUNGU amtakase dhambi zake.
Huyu alijua kuomba maombi ya kutubu na kutakaswa pia maana vyote ni muhimu.
Kibiblia hizi ni nyakati za kujitakasa sana.
Danieli 12:10 "Wengi watajitakasa, na kujifanya weupe, na kusafika; bali wabaya watatenda mabaya; wala hataelewa mtu mbaya awaye yote; bali wao walio na hekima ndio watakaoelewa."
Kwa njia hiyo unaweza kujua kwamba unahitaji sana msamaha wa MUNGU lakini pia unahitaji sana MUNGU akutakase dhambi , maovu na makosa.
▪︎Kusamehewa na kutakaswa ni vitu tofauti japokuwa vyote ni vya muhimu sana.
Inawezekana bado hujaelewa, ni hivi unaweza kuwa una mapepo ukatubu na kusamehewa dhambi lakini mapepo yakaendelea kuwa ndani yako lakini ukitakaswa eneo ambalo mapepo wako basi ujue hawawezi kukaa hapo maana damu ya YESU KRISTO itakaa hapo na pepo hawezi kamwe kukaa eneo ambalo lina damu ya YESU KRISTO.
Katika maombi ya utakaso kuna vitu vingi sana vinavyoweza kuhitaji kutakaswa.
Nini cha kutakasa?
■Baadhi ya vitu vya kutakasa ni pamoja na hivi.
1. Nyumba ya ibada.
2 Nyakati 7:16 "Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima."
Ni muhimu kuomba MUNGU aitakase nyumba yenu ya ibada yaani Kanisani kwenu, takaseni hapo kwa damu ya YESU KRISTO na patakuwa safi kiroho hata mpate msaada wa MUNGU sahihi.
Mtu mmoja alisafiri
kwenda mkoa fulani na siku ya Jumapili akaingia kusali Kanisa fulani, wakati wa maombi alipata msukumo wa kuomba utakaso wa damu ya YESU KRISTO eneo hilo, Mchungaji alimfuata haraka kumkataza kuomba akitumia damu ya YESU KRISTO maana kuna vitu anaharibu.
Yule ndugu baada ya ibada alinijulisha juu ya hayo nikamwambia alienda kusali sehemu isiyo sahihi.
Ndugu, ukiona watu hawataki/wanakataza uite damu ya YESU KRISTO ili kutakasa nyumba ya ibada na madhabahu ujue hapo hujaenda Kanisani ila umeeenda tu kwa waganga wa kienyeji.
Ni muhimu kuomba maombi ya kuitakasa nyumba ya ibada.
2. Madhabahu
Kutoka 29:37 "Utafanya upatanisho kwa ajili ya hiyo madhabahu muda wa siku saba, na kuitakasa; ndipo madhabahu itakapokuwa takatifu sana; kila kitu kiigusacho madhabahu kitakuwa kitakatifu."
Madhabahu ndipo mahali ambapo vitu kutoka ulimwengu wa roho hupitia ili kuja katika ulimwengu wa mwili.
Madhabahu ni daraja kati ya ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili.
Madhabahu sahihi lazima iwe imetakaswa kwa damu ya YESU KRISTO.
Ni muhimu sana kuwa na maombi ya kuitakasa madhabahu , ili vipite hapo vitu vya ki MUNGU katika KRISTO YESU.
2 Nyakati 7:9 "Hata siku ya nane wakaita kusanyiko la makini; kwa maana walishika kuitakasa madhabahu siku saba, na sikukuu siku saba."
3. Vyombo/vifaa vinavyotumika ibadani.
Hesabu 7:1 "Ilikuwa siku hiyo Musa alipokwisha kuisimamisha maskani, na kuitia mafuta, na kuitakasa, na vyombo vyake vyote, na hiyo madhabahu na vyombo vyake vyote, na kuvitia mafuta, na kuvitakasa;"
Hivyo ni vifaa vyote vinavyotumika Kanisani kama Mic, Meza, Spika n.k vinatakiwa kutakaswa kwa damu ya YESU KRISTO kwa njia ya maombi.
4. Kutakasa damu ya mtu, familia au ukoo.
Yoeli 3:21 "Nami nitaitakasa damu yao ambayo sijaitakasa; kwa maana BWANA ndiye akaaye Sayuni."
Kutakasa damu ya mtu, familia au ukoo kunahitaji ufafanuzi mkubwa sana, siku moja katika somo lingine nitafafanua hicho tu.
Ila damu ya familia inaweza kuchafuliwa Mfano kama Babu yako alizaliwa baada kufanyika uganga wa kienyeji maana mama yake hakuwa na uzao ujue mtu huyo hata akizaliwa na nyie mnaotoka kwake maana ni yeye alikuja kumzaa Baba yenu au Mama yenu wote na nyie damu yenu ilichafuliwa kiroho maana nguvu za giza zilihusika ndipo akazaliwa Babu yenu mnayetokana naye.
Mama mmoja alikwenda kwa mganga ili apate mimba, mganga akampeleka makaburini usiku na Mama huyu akashangaa kaburi linafunguka likatoka jitu Mfano wa mtu yaani kama li mzimu fulani likamwingilia ndipo likamwambia akalale na Mume wake atapata mimba, uzao wa mama huyo ni damu iliyochafuliwa kiroho.
Kuna Watu wana magonjwa ya ukoo kutokana na kuchafuliwa damu kiroho.
Kuna Watu kuna vitu kama wadudu hutembea ndani ya miili yako n.k
Maombi ya kuitakasa damu yako, ya familia au ukoo ni muhimu sana.
5. Kutakasa mwili kiroho.
Yakobo 4:8 "Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili."
Mwili kiroho unatakiwa kutakaswa kwa damu ya YESU KRISTO kwa njia ya maombi.
Andiko hapo juu linazungumza juu ya kutakasa mikono kiroho, mikono ni sehemu ya mwili hivyo hata viungo vingine vya mwili vinatakiwa kutakaswa.
Kuna Watu huota Ndoto wakijiona ndotoni wamebadilika wamekuwa wa ajabu, takasa mwili wako kiroho.
Kuna Watu wanaota mikono yao au miguu inatoka wadudu, takasa mwili wako.
Mtu mmoja aliota Ndoto amekuwa mweusi sana, takasa mwili wako.
Kwa njia ya Ndoto na maono unaweza kujulishwa juu ya eneo lako la mwili lenye tatizo kiroho hivyo maombi ya kuutakasa mwili kwa damu ya YESU KRISTO ni muhimu sana.
6. Kutakasa vyakula
Marko 7:19 "kwa sababu hakimwingii moyoni, ila tumboni tu; kisha chatoka kwenda chooni? Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote."
Bwana YESU alitakasa vyakula vyote yaani alitoa idhini au ruhusa ya sisi kula vyakula vyovyote hata vilivyokuwa vimekatazwa katika Torati wala hakuna hatia.
Sasa Kabla ya kula vyakula hakikisha unaviombea na kuvitakasa kwa damu ya YESU KRISTO.
1 Timotheo 4:4-5 " Kwa maana kila kiumbe cha MUNGU ni
kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani; kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la MUNGU na kwa kuomba."
7. Kutakasa roho.
Walawi 20:7 "Jitakaseni basi, iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ndimi BWANA, Mungu wenu."
MUNGU anataka tuwe watakatifu hivyo ni muhimu sana kutubu na kujitakasa na kuacha dhambi.
■Baadhi ya faida za Maombi ya kutubu.
1. Unapotubu unasamehewa dhambi zako na kuachiliwa, pia hati za mashitaka zote hufutika.
Luka 24:46-47 '' Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba KRISTO atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu.''
Unapotubu kwa kuamua hakika kutoka moyoni unasamehewa na kuachiliwa. Dhambi yako haibaki kuwa dhambi hata kama ilikuwa kubwa kiasi gani baada ya wewe kutubu katika Bwana YESU hakika dhambi hiyo inafutika na wewe unakuwa huru.
Pia ni muhimu sana kujua kwamba MUNGU husamehe na kuachilia kwa wanaotubu, hivyo na sisi tunapaswa kuwasamehe wale wote waliotukosea kisha wanaotubu kwetu uovu wao huo.
Luka 17:3-4 '' Jilindeni; kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe''
Usipomsamehe aliyekukosea kisha yeye akatubu hakika dhambi ya kutokusamehe itakuwa kwako na yeye kwa kutubu kwake akiwa huru na mwenye haki kwa MUNGU. Hivyo inatubasa pia kuwasamehe wote wanaotuomba msamaha, hata wasioomba msamaha ni muhimu pia kuwasamehe maana wasiosamehe hawataurithi uzima wa milele.
Mathayo 6:14-15 '' Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na BABA yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala BABA yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.''
2. kutubu ni kuipisha ghadhabu ya MUNGU iliyokuwa tayari kuja.
Yona 3:6-10 ''Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie MUNGU kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba MUNGU hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? MUNGU akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi MUNGU akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.''
MUNGU alitaka kuwaangamiza watu wote wa Mji mkubwa wa Ninawi kwa sababu ya uovu wao, lakini walipotubu na kuacha uovu MUNGU alighairi.
Kutubu ni kuibisha adhabu ya MUNGU iliyokuwa ije kwa sababu ya uovu.
Kuna watu Bwana YESU aliwaambia watubu maana wasipotubu wataangamia.
Luka 13:3 ''Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.''
Kwa uovu wako ilikuwa ufe au uharibiwe lakini toba yako ya kweli inaweza kuifuta adhabu ambayo ilikuwa ikupate.
Laana uliyojisababishia inaweza kufutika tu kwa wewe kutubu kwa Bwana YESU kisha unaanza kuishi maisha matakatifu katika Wokovu.
3. Kutubu hutengeneza kukubaliwa na MUNGU.
Isaya 57:15 '' Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.''
Ulikuwa adui wa MUNGU kwa sababu ya dhambi zako na maovu yako lakini toba ya kweli itakufanya ukubaliwe na MUNGU.
Mfano mlifanya uzinzi katika uchumba lakini neema ya MUNGU ikawagusa mkatubu na kuacha uasherati huo hakika mnakubaliwa na MUNGU tena, hivyo jitunzeni kwa kuishi maisha matakatifu hadi ndoa hadi siku ya kuondoka duniani.
Ulikuwa mwizi kazini, ukatubu na kuacha dhambi hiyo hakika unakubaliwa na MUNGU.
Watu wote tulikuwa adui wa MUNGU kwa sababu ya maovu yetu lakini kwa kumpokea YESU na kutubu na kuanza kuishi maisha matak
atifu ya Wokovu hakika tumekubaliwa na MUNGU Muumba wetu.
4. Toba huleta nyakati za kuburudishwa.
Matendo 3:19 ''Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;''
Ulikuwa dhambini uliteswa na mapepo lakini toba ya kweli katika KRISTO iliondoa nguvu za giza hizo ndani yako.
Ndugu mmoja alikuwa hasinzii usiku kwa sababu ya kukabwa na majinamizi na wachawi, alipookoka wale wachawi na majinamizi hakuwaona tena, hizo ndizo nyakati za kuburudishwa.
Kuwa na amani na furaha kwa sababu jina lako limeandikwa katika kitabu cha uzima cha YESU KRISTO, Hizo ni nyakati za kuburudishwa.
Leo kuna watu kwa sababu ya dhambi zao huishi kwa hofu na wanaogopa kifo maana wanajua kabisa wakifa ni motoni.
Dhambi ni utumwa hivyo hivyo ukitubu na kuanza kuishi maisha matakatifu hakika utumwa unaondoka na nyakati za kuburudishwa zinaanza.
Kuburudishwa kukuu zaidi ni uzima wa milele ambao chanzo chake ni kutubu toba ya kweli katika KRISTO kisha kuishi maisha ya wokovu matakatifu yanayoagizwa na Neno la MUNGU.
5. Toba huleta uponyaji.
2 Nyakati 7:14 ''ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.''
MUNGU anasema ataiponya nchi yaani atawaponya wakati pamoja na nchi yao, lakini kwanini MUNGU aseme hivi? Ni kwa sababu kama tu watanyenyekea kwake na kutubu na kuacha dhambi zao.
Uponyaji mwingi sana umetokana na maombi ya toba tu.
■Faida za maombi ya kujitakasa.
1. Mwili wao au nafsi yako au roho yako uliyoitakasa itakuwa safi.
1 Wathesalonike 5:23 "MUNGU wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu YESU KRISTO."
2. Kukufanya uwe safi kiroho.
1 Yohana 3:3 "Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu."
3. Uchafu wa kiroho huondoka.
Ezekieli 36:25 "Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu
wenu wote, na vinyago vyenu vyote."
4. Mtu akitakaswa na damu ya YESU KRISTO ndipo ataweza kumtumikia MUNGU vyema.
Mfano Haruni ilibidi atakaswe kwanza ndipo amtumikie MUNGU kwa viwango.
Kutoka 28:3 "Nawe utawaambia watu wote wenye moyo wa hekima, niliowajaza na roho ya hekima wamfanyie Haruni mavazi ili kumtakasa anitumikie katika kazi ya ukuhani."
5. Kujitakasa hufungua mlango wa MUNGU kutenda muujiza unaouhitaji.
Yoshua 3:5 "Yoshua akawaambia watu, Jitakaseni; maana kesho BWANA atatenda mambo ya ajabu kati yenu."
6. Utakaso hufanya palipobomolewa pajengwe tena.
Ezekieli 36:33 "Bwana MUNGU asema hivi; Siku ile nitakapowatakaseni na maovu yenu yote,
nitaifanya miji ikaliwe na watu, na palipobomolewa pajengwe tena."
7. Kutakaswa ndiko kutakufanya uwe mtii kwa MUNGU maana nguvu za giza zitakuachia.
1 Petro 1:2 "kama vile MUNGU Baba alivyotangulia kuwajua katika kutakaswa na ROHO, hata mkapata kutii na kununyiziwa damu ya YESU KRISTO. Neema na amani na ziongezwe kwenu."
Ni muhimu sana kuomba maombi ya kutubu na kujitakasa.
Na inayotakasa ni damu ya YESU KRISTO hivyo omba kwa MUNGU kwamba damu ya YESU ikutakase na kila aina ya uchafu wa kiroho ndipo utakuwa safi.
Huu ni wakati wa utakaso hivyo ishi maisha matakatifu ya utakaso.
Unaweza ukawa unaishi maisha ya wokovu na kuna mahali hapajatakaswa.
Yoeli 3:21 "Nami nitaitakasa damu yao ambayo sijaitakasa; kwa maana BWANA ndiye akaaye Sayuni."
▪︎Inawezekana ndoa yako haijatakaswa kwa sababu ya misingi mibaya ya ndoa hiyo, yaani mliingia katika ndoa mkitokea katika uasherati.
▪︎Inawezekana mwili wako haujatakaswa kwa habari ya magonjwa ndio maana kila mara unaumwa.
▪︎Inawezekana familia yako haijatakaswa.
▪︎Inawezekana nyumba yako au ardhi yako haijatakaswa.
▪︎Kuna watu kuna vitu huwa vinatembea ndani yao, omba maombi ya kujitakasa katika mwili wako kiroho na kitu hicho kitaondoka maana damu ya YESU itakutakasa.
Kuna watu wana muunganiko na nguvu za giza, jitenge
leo na hizo nguvu za giza kwa maombi ya kujitakasa, takasa nafsi yako, mwili wako na roho yako na huo muunganiko kati yako na nguvu za giza utafutika hivyo wewe utakuwa huru.
Nini ufanye katika maombi ya toba na utakaso?
1. Tubia dhambi zako zote , maovu yako na makosa yako.
Isaya 1:16 "Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;"
2. Tubu kwa ajili ya kilichosababisha kifungo cha kiroho ndani yako.
Yeremia 14:20 "Ee BWANA, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi."
3. Takasa kwa damu ya YESU KRISTO maeneo yako au baraka zako zinazohitaji kutakaswa.
1 Yohana 1:7 "bali tukienenda nuruni, kama yeye(MUNGU) alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote."
4. Takasa mwili wako kiroho, nafsi yako kiroho na roho yako.
Walawi 11:44 "Kwa kuwa mimi ni BWANA, Mungu wenu; takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu; wala msitie uchafu nafsi zenu kwa kitu kitambaacho cha aina yo yote, kiendacho juu ya nchi."
5. Achilia damu ya YESU KRISTO kwenye kila maeneo huku ukiomba utakaso wa MUNGU kupitia damu ya YESU KRISTO.
Waebrania 9:13-14 " Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake KRISTO, ambaye kwamba kwa ROHO wa milele alijitoa nafsi yake kwa MUNGU kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu MUNGU aliye hai?"
Ndugu ukifuata vipengele hivyo vitano na MUNGU atabadilisha historia ya maisha yako.
Pia mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
MUNGU akubariki sana.
Ni mimi ndugu yako Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+ 2 5 5 7 1 4 2 5 2 2 9 2

Comments