MAOMBI YA KUKATAA SURA YAKO KUTUMIWA NA ULIMWENGU WA ROHO WA GIZA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Nisikilize itakusaidia.

Kuna aina mbili za ulimwengu.

✓✓Kuna ulimwengu wa roho na kuna ulimwengu wa mwili.

Lakini pia kuna aina mbili za ulimwengu wa roho.

✓✓Kuna ulimwengu wa roho wa nuru na kuna ulimwengu wa roho wa giza.

Ulimwengu wa roho wa nuru yuko MUNGU Baba mwenyewe, YESU KRISTO, ROHO MTAKATIFU, Malaika watakatifu wote na kila Mkristo aliyeokolewa na YESU KRISTO ambaye jina lake liko katika kitabu cha uzima mbinguni.

Katika ulimwengu wa roho wa nuru tunaona Bwana YESU akiwatokea wanadamu katika umbo na sura ya Mfano wa Mwanadamu.

Mfano ni huu.

Danieli 7:13-14 " Nikaona katika njozi za usiku, na tazama, mmoja aliye mfano wa mwanadamu akaja pamoja na mawingu ya mbingu akamkaribia huyo mzee wa siku, wakamleta karibu naye. Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa."

Katika ulimwengu wa roho wa nuru tunaona malaika wakiwatokea wanadamu katika maumbo Mfano wa Mwanadamu.

Luka 24:4 "Ikawa walipokuwa wakifadhaika kwa ajili ya neno hilo, tazama, watu wawili walisimama karibu nao, wamevaa nguo za kumeta-meta;"

Hawa Watu wawili waliokuwa wamevaa nguo za kumetameta walikuwa ni Malaika.

Labda ndio Maana Biblia inasema tumeumbwa kwa Mfano wa MUNGU, tumeumbwa kwa sura za Mfano wa walio mbinguni.

Mwanzo 1:26-27 " MUNGU akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. MUNGU akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa MUNGU alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba."

Lakini pia kuna ulimwengu wa roho wa giza, huko yuko shetani, majini, mizimu na kila maroho wa kuzimu pamoja na wanadamu wote wanaotumika kishetani, Mfano wachawi, waganga wa kienyeji, wanajimu, wasihiri na kila mtu anayetumika kipepo.

Leo Nazungumzia nguvu za giza yaani maroho ya kuzimu kutumia sura za watu, leo ikomboe sura yako kwa damu ya YESU KRISTO ya agano jipya.

Iko hivi, Viumbe wote wa kiroho  hawana maumbo ya Kimwili maana wao ni Viumbe wa kiroho, hivyo ili wafanye kazi katika ulimwengu wa mwili wakati mwingine inabidi wavae sura za Viumbe wa ulimwengu wa mwili, hivyo yapo maroho pia hutumia sura za Watu mbali mbali hata sura yako usipokuwa mtu wa kuiombea inaweza kutumika pia na nguvu za giza.

Ukisoma Walawi 17:7 Biblia inazungumzia Watu ambao hutoa sadaka kwa majini na Biblia inasema pia kuna Watu huzini na majini.

Walawi 17:7 "Wala hawatatoa tena sadaka zao kwa wale majini, ambao huwafuata ili wafanye uasherati nao. Sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao, kizazi baada ya kizazi."

Swali la kujiuliza, je mtu anazini na jini huku jini huyo akiwa na sura yake halisi ya kiroho?

Jibu ni hapana, Ila jini huyo huvaa sura za binadamu au sura za wanyama, Vipi kama ni sura yako jini ameivaa ili akazini na mtu mwingine unayemweshimu sana?

Vipi ikiwa kila mara kuna mtu anakuona ndotoni ukizini naye na kumbe ni jini limevaa sura yako, Kwanini sura yako itumike kipepo?

Kwanini jini mahaba atumie sura yako Katika ushetani wake?

Nakuambia haya ili upate hasira za kiroho za maombi ili uombe katika jina la YESU KRISTO hata kuanzia leo sura yako isitumiwe tena na nguvu za giza.

Ndugu, kuna Watu sura zao zinatumiwa na nguvu za giza hivyo maisha yao huharibiwa kwa kiwango kikubwa sana.

Inawezekana hujanielewa, Ngoja nikupe ushuhuda wa kweli utanielewe.

✓✓Mama mmoja katika ndoa yake walikuwa wanaishi vizuri tu na Mume wake, baadae Mume wake alibadilika ghafla na kununua godoro jipya akawa analala chini huku mke wake akilala kitandani, baadae yule Baba akahama chumba akawa analala chumba cha watoto, kipindi chote hicho mke wake aliuliza kila muda nini tatizo lakini Mume wake alikuwa mkali sana, hakusema chochote, baadae mwanaume huyo akawa analala nje ya nyumba, akawa na mahawara na Mlevi.

Mama huyu ni Mkristo mcha MUNGU mzuri tu na ilibidi kushirikisha watumishi wa MUNGU mbalimbali ili waombee ndoa yake maana kila siku Mume anasema atamwacha Mkewe.

Aliponishirikisha nimuombee niliomba na sikuona chochote lakini siku chache baadae yule Baba akamwambia Mkewe "heri tuachane kwa sababu wewe ni Mchawi " Yule mama alinipigia simu akilia sana maana kaitwa Mchawi wakati sio kweli.

Nilimuombea kisha nikamwambia atafute muda amuulize Mume wake.

Mume alikuwa anamuogopa sana Mkewe lakini siku moja nafasi ikapatikana na alipomuuliza Mume akasema "Kila siku nakuona ndotoni hadi kwenye maono live ukija kichawi kuniloga, nakuona ukiwa unatisha sana. Wakati mwingine nakuona kama unabadilika sura, Jumapili mlipoenda Kanisani na watoto nilishangaa nilipoingia chumbani nikakukuta kitandani lakini ghafla ukapotea, nikaogopa sasa, kuna siku ulikuwa unatembea ghafla nikawaona akina wewe wawili hivyo nikajua wewe sio mtu mzuri " Baada ya hapo mama huyu alinisimulia na nikapata ufunuo kwamba sura yake inatumika na majini ili kuua ndoa yake. Nilimuombea na katika maombi  hayo niliona Mume wake anaishi na nguvu za giza ndani yake, kwenye maombi niliitakasa sura yake kwa damu ya YESU KRISTO na nikakataa sura yake kutumiwa na nguvu za giza, baada ya hapo Mume wake hakumuona tena mke wake kichawi.

Nini nataka kukuambia zaidi?
Viumbe wa kiroho kama mizimu, majini na kila maroho wa kuzimu hutumia sura za Watu au wanyama au wadudu hivyo kataa sura yako kutumika kichawi.

Inakuwaje mtu amekuona ndotoni ukimwibia, na kumbe ni Mchawi tu ametumia sura yako? Si utachukiwa bure.

✓✓Binti mmoja aliota akizini na mwanaume fulani kwa akili yake akadhani yule atakuja kuwa mumewe na kumbe ni majini mahaba yanamtoa kwenye Kusudi.

Kumbuka hawa ni viumbe wa kiroho hivyo ili wafanye kazi katika ulimwengu wa mwili ni lazima wavae sura za Viumbe wa ulimwengu wa mwili.

Yako mabaya ya namna nyingi sana yanaweza kuonekana kwenye ulimwengu wa roho na kumbe ni nguvu za giza zimevaa sura za wanadamu ili kuwagombanisha hao wanadamu au kuwafanya wachukiane.

Maroho wa kuzimu hutenda kazi kwa Siri hivyo ni muhimu tutambue mipango yao ili tuidhibiti kwa maombi.

Mfano Elifazi hapa chini katika kitabu cha Ayubu aliona ndotoni pepo yaani mapepo(Majini/mashetani) na alisikia sauti ya hilo pepo akatetemeka na kupata hofu, nywele zake zikasimama ila hilo pepo hakulitambua sura yake.

Ayubu 4:12-16 " Basi, nililetewa neno kwa siri, Sikio langu likasikia manong'ono yake. Katika mawazo yaliyotoka katika maono ya usiku, Hapo usingizi mzito uwaangukiapo wanadamu. Hofu iliniangukia na kutetema, Iliyoitetemesha mifupa yangu yote. Ndipo pepo ilipita mbele ya uso wangu; Na nywele za mwili wangu zilisimama. Hiyo pepo ilisimama kimya, nisiweze kutambua sura zake, Mfano ulikuwa mbele ya macho yangu; Kulikuwa kimya, nami nilisikia sauti, ikinena,"

Vipi kama hilo pepo limevaa sura yako na mtu akakuona ndotoni akaogopa na kutetemeka? Mtu huyo kama sio mtu wa rohoni anaweza hata kuanza kukutangaza mitaani kwa mabaya.

Kuna hadi Kanisa lilikimbiwa na waumini kwa sababu tu baadhi walimuota mchungaji kwa mabaya wakashawishi na wengine na kazi ya MUNGU ikafa pale, Vipi kama ni majini tu walitumia sura ya Mchungaji?

Ndivyo walivyo viumbe wa kiroho maana hao ni lazima wavae sura za Viumbe wa Kimwili ndio utawaona.

Kumbuka Ndoto na maono ni lango na hilo lango linaweza kutumiwa na MUNGU na linaweza pia kutumiwa na shetani.

Mfano Ukisoma Ezekieli sura ya kwanza unaona Ezekieli katika maono ya MUNGU aliona Viumbe wanne wenye sura ya Mwanadamu

Ezekieli 1:1,5 " Ikawa katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, nilipokuwa pamoja na watu waliohamishwa, karibu na mto Kebari, mbingu zilifunuka, nikaona maono ya MUNGU. ............ Kukatokea katikati yake mfano wa viumbe hai vinne. Kuonekana kwao kulikuwa hivi; walikuwa na sura ya mwanadamu."

Lakini pia kuna Watu huota Ndoto za kishetani ambapo wanaona Watu fulani wanaowajua wakifanya mambo mabaya na kumbe ni maroho tu wa giza wamevaa sura za Watu hao.

✓✓Mama mmoja ambaye anafanya kazi nzuri serikalini, ofisi yao ina wafanyakazi wengi na walikuwa wanaishi vizuri tu.
Baadae kuna mfanyakazi mwenzake alimuota huyu mama akiloga wafanyakazi wenzake pale ofisini Kwao, kesho yake akawahadithia pale ofisini, na mwingine baada ya kuhadithiwa naye akaota vilevile, Hali ili ilipelekea ofisi nzima ya Watu zaidi ya 10 walimchukia huyu mama kwamba ni Mchawi na wakamtangaza sana, kazi kwake ikawa ngumu Sana maana mtu akipata hata mafua tu anasema ni yeye kamloga.
Mama kaokoka na ni muombaji akanishirikisha, nikawa namuombea kwa simu nikikataa sura yake kutumika kipepo kwenye ulimwengu wa roho.

Baadae akafunuliwa ni nani hasa Mchawi pale kazini, akawaeleza baadhi ya Watu na walipofanya mtego walimkamata Mchawi halisi akiweka madawa kwenye vyakula kisha anatemea mate ndipo anawakaribisha wengine kula maana ofisi yao ilikuwa na utaratibu wa wafanyakazi wote kula kazini mchana.
Hapo ndipo ofisi nzima wakagundua mama yule sio Mchawi ila wachawi halisi walitumia sura yake ili kumharibia.

Ndugu yangu, Leo Omba katika jina la YESU KRISTO ukikataa sura yako kutumika na ulimwengu wa roho wa giza.

Yohana 14:14 "Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."

Unaweza ukawa ni binti unahitaji kuolewa lakini hakuna mchumba anayetokea maana mtu akikupenda tu moyoni mwake ghafla anaanza kukuona mzee ndotoni hivyo hawezi kukuoa, ghafla anakuona ndotoni katika hali ya kichawi hivyo anajitenga mbali na wewe.

Inawezekana ndugu zako wanakuchukia sana bila sababu, kumbe huwa wanakuona ndotoni ukiwanga wakati sio wewe ila ni majini yaliyovaaa sura yako.

Inawezekana wewe una roho ya kukataliwa ila hujui inafanyaje kazi, kumbe ni kupitia sura yako.

✓✓Mtu mmoja aliota Ndoto mchungaji wake amelewa akaacha kwenda Kanisani, yaani mashetani wakamuondoa Kanisani huyu ndugu Kwa ujanja tu wa kipepo walipovaa sura ya Mchungaji wake.

Zipo shuhuda nyingi za Watu waliodanganywa na shetani kupitia mashetani kuvaa sura za Watu muhimu kwao hata uhusiano na watu hao ukafa.

Inawezekana kuna Watu umewanunia, huwasalimii ukidhani ndio hukuloga maana huwa unawaona ndotoni na kumbe Mchawi original yuko pembeni anafurahi tu maana hujawahi kumgundua maana yeye hutumia sura za Watu wako wa Karibu.

✓✓Wachawi au majini wanaweza kukuletea hadi sura za marehemu ili kukudanganya umkosee MUNGU.

Ndugu, sio kwamba huwezi kumuona ndotoni adui yako, unaweza kabisa lakini lijue na hili pia kwamba hata nguvu za giza wanaweza kutumia sura ya mtu yeyote ili tu kukuchanganya na kukufanya uangamie. 

Kumbuka vita vyetu ni dhidi ya majeshi ya mashetani, hao wanaweza kuonekana pia katika sura za Watu au wanyama.

Waefeso 6:12 "Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."

✓✓Wako watumishi huzushiwa sana lakini wakati mwingine chanzo ni majini kuvaa sura za watumishi hao kwenye ulimwengu wa roho.

Ndugu uwe makini sana na Msikilize sana ROHO MTAKATIFU ili akusaidie na kukujulisha usahihi.

Kama mashetani wametumia kipepo sura za Watu mbalimbali na wewe unawaona Watu hao ndotoni utapata madhara gani?

Baadhi ni haya

1. Hutawaamini tena Watu hao hivyo unaweza kupishana na baraka zako au kupishana na Kusudi la MUNGU.

2. Unaweza ukawachukia ukidhani wanahusika na matatizo yako na kumbe hawahusiki.

3. Kama umewaona kwa mabaya utadhani hiyo ndio tabia yao hata kama hawahusiki.

Kama nguvu za giza wametumia sura yako na Watu wengine hukuona ndotoni utapata madhara gani.

Baadhi ya madhara ni haya.

1. Watu watadhani wewe una tabia mbaya waliyokuona nayo ndotoni hivyo watakuchukia bure.

2. Watu kukataa kushirikiana na wewe wakidhani wewe ni mtu mbaya wakati sio kweli.

3. Watu kukuogopa na kukutenga wakidhani wewe ni mtu mbaya.

Ndugu, kuna madhara mengi mno sura yako ilitumika na nguvu za giza, leo kwa maombi Katika jina la YESU KRISTO ikomboe sura yako.

Inawezekana wewe hufurahi unapowaona Watu ndotoni na kumbe si Watu hao ila ni majini yaliyovaaa sura zao.

Inawezekana Watu wengi hukuambia wamekuota ndotoni wewe lakini Inawezekana kuna Watu wanakuota kwa mabaya ila hawakuambii tu maana ni mabaya.

Ndugu, sio Ndoto zote unazoota ni kweli zingine ni ulaghai wa shetani.

Najua Ndoto za kweli Zipo na ni nyingi tu lakini Biblia inaonyesha hata Ndoto za uongo Zipo na uongo upo wa aina nyingi.

Yeremia 23:32 "Tazama, mimi ni juu ya hao wanaotabiri ndoto za uongo, asema BWANA, na kuzisema, na kuwakosesha watu wangu kwa uongo wao, na kwa majivuno yao ya upuzi, lakini mimi sikuwatuma, wala sikuwapa amri; wala hawatawafaidia watu hawa hata kidogo, asema BWANA."

Ndugu, Inawezekana wewe huwaona sana wengine kwenye ulimwengu wa roho lakini  hata wewe Inawezekana kuna Watu Wanakuona kwenye ulimwengu wa roho kwa mabaya sana na kumbe ni wachawi wanatumia sura yako.

Nini ufanye Katika maombi.

1. Acha dhambi, maovu na makosa maana huo ni Mlango wa shetani kupata uhalali wa kutumia sura yako kwenye ulimwengu wa roho.

Zaburi 34:14 "Uache mabaya ukatende mema, Utafute amani ukaifuatie."

Kuna faida nyingi Biblia kukuambia uache dhambi(mabaya) faida mojawapo ni ili shetani asipate uhalali hata wa kutumia sura yako.

Hivyo tubia dhambi zako na uziache kuanzia leo.

2. Takasa sura yako kwa damu ya YESU KRISTO na achilia damu ya YESU KRISTO kwenye sura yako hasa uso.

Waebrania 9:14 "basi si zaidi damu yake KRISTO, ambaye kwamba kwa ROHO wa milele alijitoa nafsi yake kwa MUNGU kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu MUNGU aliye hai?"

Sura yako ikiwa na damu ya YESU KRISTO ujue hakuna atakayeitumia kipepo.

3. Kwa maombi kataa sura yako kutumika na ulimwengu wa roho wa giza.

2 Wakorintho 6:14 "Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?"

Wasioamini ni pamoja na nguvu za giza zote, hivyo usikubali kuwa na ushirika wowote na nguvu za giza hata wawe na uhalali wa kutumia sura yako.

4. Kwa maombi mpige  kila adui aliyetoka kuzimu aliyewahi kutumia sura yako kipepo.

Zaburi 2:9 "Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi."

Una mamlaka katika jina la YESU KRISTO hivyo itumie mamlaka hiyo katika maombi. 

5. Futa connection(Muunganiko) kati yako na ulimwengu wa roho wa giza.

1 Wathesalonike 5:22 "jitengeni na ubaya wa kila namna."

Upo ubaya wa namna nyingi hata nguvu za giza kutumia sura yako ni ubaya unaotengeneza ubaya zaidi, Futa connection na hizo nguvu za giza ambazo hutumia sura yako.

6. Omba MUNGU awafunue maadui zako kwa sura zao wenyewe.

Yohana 14:14 "Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."

Umepewa mamlaka katika jina la YESU KRISTO ya kuomba lolote katika Kusudi la MUNGU, leo Omba MUNGU awafunue adui zako kwa sura zao wenyewe.

Inawezekana wachawi hutumia sura za Watu wema kwako ili uwachukie , leo Omba kila adui anayekujia ndotoni aje kwa sura yake mwenyewe na sio sura za Watu wema kwako.

7. Mfungue kwa maombi kila ambaye aliwahi kukuona kwenye ulimwengu wa roho na kumbe ni sura yako ilitumika na nguvu za giza.

Yakobo 5:16 "Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii."

Una kibali cha kumuombea mtu mwingine, leo muombee kila mtu aliyekuona ndotoni au kwenye maono ila alikuwa kwa mabaya ambayo hayakuhusu ila nguvu za giza walitumia sura yako.

Inawezekana mtu huyo sasa anakuchukia bure, muombee ili MUNGU ampe kujua ukweli.

8. Mshukuru MUNGU kwa maombi au hata sadaka ya shukrani kwa imani kwamba sura yako haitatumika tena na nguvu za giza.

Zaburi 52:9 "Nitakushukuru milele kwa maana umetenda; Nitalingojea jina lako kwa kuwa ni jema; Mbele ya wacha MUNGU wako."

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By  Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292
Uki share somo hili nakuomba usibadili chochote.

Comments