![]() |
Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe maombi ya ushindi katika Jina la YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele.
Jambo la kwanza naomba uzingatia hata kabla ya kuomba ni kwamba hakikisha YESU KRISTO ni Mwokozi wako binafsi, yaani mpokee kama Mwokozi wako, tubu dhambi zako na kuziacha ndipo utakuwa na nguvu za kuomba na kupokea kama ulivyoomba.
Yohana 14:23 '' YESU akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na BABA yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. ''
◼️Ndugu, mpende YESU na yeye atakuja kwako na kufanya makao kwako, na kama YESU akifanya makao kwako hakuna namna nguvu za giza zitakushinda ukiomba.
Mpende YESU KRISTO kwa kumpokea kama Mwokozi wako na anza kuliishi Neno la MUNGU kwa utakatifu wote katika Wokovu.
Katika maombi pia hakikisha unaomba kwa imani huku unaomba kwa kuamini kwamba unaenda kupokea na utapokea hakika.
Marko 11:24 '' Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.''
Ikiwa umeshatubu na umempokea YESU KRISTO kama Mwako kwa imani basi omba maombi kwa kufuata mtiririko huu ili uwe huru wewe na familia yako, kazi yako, baraka yako, fursa yako na kila kitu chako.
Maombi ya leo ni haya.
1. Kwa Maombi katika Jina la YESU KRISTO zifunge kazi zote za shetani unazozifahamu katika eneo unalooombea
Mathayo 16:19 '' Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni. ''
✓✓Zifunge kazi zote za shetani katika ndoa yako, katika uchumba, katika mwili wako, katika eneo lako la kazi, katika kibali chako, katika uchumi wako, katika familia yako na kwa watu wako wa karibu(Wataje)
Zifunge kazi hizo za shetani na zitafungwa.
Mathayo 18:18 '' Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. ''
2. Kusudia jambo jema na liombee leo jambo hilo ili litokee.
Ayubu 22:28 '' Nawe utakusudia neno, nalo litathibitika kwako; Na mwanga utaziangazia njia zako. ''
✓✓Kama unakusudia mwaka huu kupata mchumba na mwakani kufunga ndoa basi umba uchumba na umba ndoa kwa maombi yako katika Jina la YESU KRISTO maana utakusudia jambo nalo litakuwa.
✓✓Inawezekana unataka mwenzi wako apate kazi au afunguliwe vifungo vya giza, kwa maombi yako katika Jina la YESU KRISTO umba hicho unachohitaji na kitatokea maana imeandikwa '' Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki -Mathayo 12:37a ''
✓✓Kusudia kupata kazi na umba kazi kwa maombi yako kisha baada ya maombi ukitafuta kazi utapata maana umesahaiumba kwa maombi yako na inatokea.
✓✓Kusudia kupona ugonjwa unaoumwa, hata kama ni ugonjwa ambao madaktari wamesema huwezi kupona, wewe tembea kwenye Neno la MUNGU kwa kuomba katika Jina la YESU KRISTO huku ukiumba afya njema ndani yako na afya itatokea.
◼️Afya ni hali ya kuishi bila magonjwa, unaweza kuiumba afya ndani yako na utashangaa magonjwa yamekimbia bila kufukuzwa, umba uponyaji kwa Maombi na utapona kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
✓✓Kusudia kufaulu, kusudia ndoa yako kuwa na amani, kusudia kupata uzao, kusudia kupata kibali, kusudia kupandishwa cheo na ukiomba bila shaka tena ukiomba huku ukiamini hakika utakachokiumba kwa maombi yako katika Jina la YESU KRISTO kitatokea maana katika maombi kuwa na jawabu lako.
✓✓Umba uharibifu kwenye madhabahu za giza maana ukiomba kwa Jina la YESU KRISTO huku unaamini basi Neno lako katika kinywa chako litakuwa moto na majini au majeshi ya pepo wabaya watakuwa kama kuni kavu na huo moto utakaouumba kwa kinywa chako utawala hao wakuu wa giza.
Yeremia 5:14 '' Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala. ''
✓✓Kusudia jambo kimaombi nalo litatokea, kusudia jambo jema na lenye faida kwako na kwa Kanisa la KRISTO duniani nalo litatokea.
3. Ita nuru ya KRISTO kwa Maombi.
Yahana 1:5 '' Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza. ''
✓✓Ita nuru ya KRISTO katika mwili wako ili nguvu za giza zikimbie hata bila kufukuzwa.
✓✓Ita nuru ya KRISTO katika nyumba unayokaa ili nguvu za giza zikimbie haraka sana.
✓✓Ita nuru ya KRISTO katika ndoa yako ili nguvu za giza ziachie.
✓✓Ita nuru ya KRISTO katika familia yako ili kalenda za kichawi zikome.
✓✓Ita nuru ya KRISTO eneo lako la kazi na majini hawataweka makazi hapo tena.
✓✓Ita nuru ya KRISTO ndani ya kichwa cha mwenzi wako ili asilitumikie kusudi la shetani.
✓✓Ita nuru ya KRISTO katika tumbo lako la uzazi au katika tumbo la uzao la mwenzi wako ili nguvu za giza zimwachie na mpate Watoto.
✓✓Ita nuru ya KRISTO katika viungo vya uzazi vya mume wako au mke wako ili nguvu za giza zimwachie na mpate uzao.
✓✓Ita nuru ya KRISTO katika kila eneo ambalo unadhani limeshikiliwa na nguvu za giza na hizo nguvu za giza zitaachia.
Kumbuka Bwana YESU ndiye nuru ya ulimwengu na anayo nuru ya ajabu, nuru hiyo ikiingia kwako lazima nguvu za giza zikuachie haraka.
Yohana 8:12 '' Basi YESU akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima. ''
4. Kwa Maombi nyunyiza damu ya YESU KRISTO kila palipotolewa kafara na paliposhikiliwa kiroho au kufungwa kiroho na wakuu wa giza.
Jifunze hapa.
Musa alijua matumizi ya damu kiroho ndio maana maandiko yanaoyesha baadhi tu ni haya.
a. Musa alinyunyuzia damu katika madhabahu ili kuitakasa kiroho, kuisafisha n.k
Kutoka 24:6 '' Musa akatwaa nusu ya ile damu, akaitia katika mabakuli; na nusu ya ile damu akainyunyiza juu ya madhabahu.''
Katika Walawi 16:19 Musa alipata ufunuo wa kunyunyiza damu mara saba katika madhabahu, ukipata ufunuo wa namna hiyo wakati wa kuomba ukitumia damu ya YESU KRISTO unaweza kufanya hivyo.
Walawi 16:19 "Tena atanyunyiza baadhi ya damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, na kuitakasa, ili machafu yote ya wana wa Israeli yaitoke."
b. Musa aliwanyunyuzia watu damu.
Kutoka 24:8 '' Musa akaitwaa ile damu, akawanyunyizia watu, akasema, Hii ndiyo damu ya agano alilolifanya BWANA pamoja nanyi katika maneno haya yote. ''
c. Musa alikuwa anainyunyizia Biblia Damu.
Waebrania 9:19 "Maana kila amri ilipokwisha kunenwa na Musa kwa hao watu wote, kama ilivyoamuru sheria, aliitwaa damu ya ndama na ya mbuzi, pamoja na maji na sufu nyekundu na hisopo, akakinyunyizia kitabu chenyewe, na watu wote,"
Inaweza hii ikakuchanganya sana kwamba kitabu cha torati kilikuwa na chenyewe kinanyunyuziwa damu, hilo ni swala la kiroho sana maana damu ya Mwana Kondoo YESU KRISTO ina nguvu za ajabu.
Kwa leo huinyunyuzii Biblia damu ila kwa maombi unaweza kuinyunyuzia damu ya YESU KRISTO ili ukisoma uelewe kama itakavyo.
d. Vyombo vya badani vyote vilinyunyuziwa damu.
Waebrania 9:21 "Na ile hema nayo na vyombo vyote vya ibada alivinyunyizia damu vivyo hivyo."
e. Wengine walikuwa wananyunyuzia damu mara saba na sio mara moja tu.
Walawi 4:17" kisha kuhani atatia kidole chake katika hiyo damu, na kuinyunyiza mbele za BWANA, mbele ya pazia mara saba."
f. Walikuwa wananyunyuzia damu viti.
Walawi 16:14 Kisha atatwaa baadhi ya damu ya yule ng'ombe, na kuinyunyiza kwa kidole chake juu ya kiti cha rehema upande wa mashariki; na mbele ya kiti cha rehema atainyunyiza ile damu kwa kidole chake mara saba."
Sasa unaweza ukaombea kiti chako cha ofisini ukitumia damu ya YESU KRISTO, unaweza kunyunyuzia kiti chako kiroho yaani nafasi yako kiroho, inategemea na ufunuo uliopewa na ROHO wa MUNGU, katika maandiko hapo juu tunaona kiti kikinyunyuziwa damu mara saba, ukipata ufunuo wa namna hiyo fanya na utamuona MUNGU.
Ukipata ufunuo wa kunyunyiza damu ya YESU KRISTO mara saba kwa Maombi basi fanya hivyo, uwe unanyunyizia mwili wako, ndoa yako, kazi yako, afya yako, ukoo wako, madhabahu, ardhi yako n.k
Zamani akina Musa walitumia damu ya Kondoo lakini sisi Kanisa kwa sasa tunatumia damu ya Mwana kondoo wa MUNGU ambaye ni YESU KRISTO pekee.
Ufunuo 12:11 "Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa."
◼️Damu ya YESU KRISTO ina nguvu kupita kawaida.
Ngoja nikupe ushuhuda wangu mwenyewe mimi Peter Mabula.
Ni mwanzoni mwa wiki katika mwezi fulani wa mwaka fulani nilikuwa katika maono ambapo niliona adui mmoja mwanamke akizungumza ili kunifunga kipepo, nilipomshinda nikaona mwanamke na mwanaume ambao maumbo yao ni kama wanadamu lakini huwezi kuwaangalia mara mbili maana ni wabaya sana, meno yametoka nje na niseme ni majitu ya ajabu.
Wakasema wananifuata ili kuniangamiza, nikasema ndani ya maono kwamba ' nifuateni ili mfe''. Baada ya hapo wakaanza kunifuata huku nikijiona naishiwa nguvu za kuomba na kukemea, wakati wananikaribia nikajikuta nasema hivi ''Naachilia damu ya YESU KRISTO ya agano jipya katika ardhi mliyopokanyaga'' ile namaliza tu kusema nikaiona ardhi ya eneo hilo imechanganyika na makaa ya moto madogo madogo yaliyo sambaa yanayowaka yaani ni kama taa ndogo ndogo zimewekwa ardhini, au kama taa ambazo huwa zinawashwa wakati wa Christmas zikiwa katika majengo au miti, sasa hiyo ilikuwa ardhini. Dakika ile ile wale wakuu wa giza wakaanza kuungua na kukimbia kwa spidi kali na wakatoweka kabisa.
Baada ya hapo nikawa natembea na nikasema ''Hata ninapoishi ntaachilia damu ya YESU KRISTO ya agano jipya'' ni kweli nilipofika nyumbani nikaachilia damu ya YESU katika ardhi na sekunde ile ile ardhi ya pale ikawa ni kama imechanganyikana na moto unaowaka lakini haumuunguzi mwanadamu wa kawaida.
Baada ya maono hayo imani yangu iliongezeka sana juu ya damu ya YESU KRISTO katika maombi.
◼️Ndugu, Damu ya YESU KRISTO ni halisi kabisa na ina nguvu ambazo hakuna wakala wa shetani anaweza kushindana nayo.
Tumia damu ya YESU KRISRO leo katika maombi yako, nyunyuzia kila maeneo yako au maeneo ambayo unahisi yamefungwa, omba katika jina la YESU KRISTO huku ukitumia damu ya YESU KRISTO na utapata ushindi wa ajabu sana sana sana.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(whatsapp, Maombezi na Sadaka ya kuipeleka mbele Injili).
Ubarikiwe sana
Comments