![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Kibiblia neno "nchi" kwenye baadhi ya maandiko lina maana ya "ardhi".
Mwanzo 1:10" MUNGU akapaita pale pakavu Nchi; na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; MUNGU akaona ya kuwa ni vyema."
Naamini kila mtu anaijua ardhi.
✓✓Kwa kifupi tunaweza kusema kwamba ardhi ni sehemu ya dunia tunayoikanyaga,tunayojenga juu yake, tunayoilima, tunayofanya biashara juu yake n.k
Kuna mambo mengi sana kuhusu ardhi kiroho, leo nadonoa tu kwa sehemu ili tukaombe na kupata ushindi.
Kwa sababu somo letu leo ni la maombi basi ngoja nianze hivi;
Kwanini ufanye maombi juu ya ardhi?
1. Ni kwa sababu ardhi inaweza kutunza kumbukumbu za kifungo cha kiroho kwa mtu husika.
Yeremia 22:29-30 " Ee nchi, nchi, nchi, lisikie neno la BWANA. BWANA asema hivi, Andikeni habari za mtu huyu kwamba hana watoto, kwamba mtu huyu hatafanikiwa siku zake zote; maana hapana mtu katika wazao wake atakayefanikiwa, akiketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kutawala tena katika Yuda."
✓✓Ardhi inaambiwa kwamba iandike juu ya mtu Fulani kwamba hatafanikiwa, ardhi kumbe inaweza kuandika taarifa za Mtu fulani.
✓✓Kwa hiyo ardhi inaweza ikasemeshwa na kutunza kifungo kama Yule aliyeisemesha hiyo ardhi alivyotamka.
Katika somo la leo, ninapozungumzia ardhi iliyobeba vifungo sina maana ya kwamba kila ardhi popote imebeba kifungo kwa ajili yako, nazungumzia ardhi inayokuhusu kama imebeba kifungo kwa ajili yako.
Kuna ardhi moja pia inaweza kubeba kifungo kwa ajili ya mtu mmoja anayeishi hapo lakini kifungo hicho kisimpate mtu mwingine anayeishi katika ardhi hiyo hiyo maana yeye hayuko kwenye maelekezo ya mtoa kifungo hicho.
Je kama ardhi ya kwenu ilisemeshwa na mchawi juu ya kifungo itakuwaje?, usipoomba unaweza kuzaliwa kifungoni, ukaishi kifungoni, ukakulia kifungoni na kuzeekea kifungoni, ndio maana leo tunaomba juu ya ardhi.
2. Ardhi inaweza kupokea laana kwa ajili ya mtu atakayeitumia.
Yoshua 6:26 "Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za BWANA mtu yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo."
Vipi kama ni wewe ndio unaishi katika ardhi ya namna hiyo?
Yaani ukiishi katika ardhi hiyo ujue mtoto wako wa kwanza lazima afe mapema kisha mtoto wa mwisho akiwa ni mwanaume naye afe mapema, lakini hapo hatuoni mtu akitamkiwa mabaya hayo ila imetamkiwa ardhi ya eneo fulani, lakini madhara yakawapata watu.
Ardhi ya Yeriko ilitamkiwa na Mtumishi wa MUNGU na ikawa vile vile kwa sababu ya makosa ya watu.
Vipi kwa habari za wakuu wa giza, unadhani hawajui kwamba ardhi ikisemeshwa inasikia na kutunza kumbukumbu au kusimamia kifungo?
Ukweli wanajua na wameshawafunga watu wengi, leo tunapoomba kuhusu ardhi ujue unaenda kujitoa katika mitego ya siri sana ya mawakala wa shetani, unaenda kujitoa katika kifungo cha siri sana cha wakuu wa giza.
✓✓Ndugu, ardhi ya sehemu fulani inaweza kuwa chanzo cha tatizo lako ndio maana kila muda unaota ndoto za ardhi hiyo na kumbe unajulishwa ni wapi umeshikiliwa kipepo, ni wapi uchumi wako umeshikiliwa, ni wapi uzao wako umeshikiliwa, ni wapi afya yako imeshikiliwa, ni wapi kibali chako kimeshikiliwa n.k
Mimi Mimi Peter Mabula mwenyewe niliwahi kuona ndotoni zamani kule nilikowahi kuishi nikapata Ufunuo namna ya kushughulikia kiroho juu ya ardhi hiyo na kilichokuwa kimesemeshwa juu yangu kwenye ardhi hiyo, namshukuru MUNGU wa Mbinguni maana kwa Nguvu zake nilishinda.
3. Ardhi inaweza kubeba ukiwa hivyo mtu anayekaa katika ardhi ya eneo hilo anakuwa mtu wa ukiwa.
Isaya 62:4 "Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula;kwa kuwa BWANA anakufurahia ,na nchi yako itaolewa."
Ukiwa maana yake kukaukiwa,kuishiwa.
Ukiwa ni upekwe unaotokana na kuondokewa.
✓✓Ukiishi kwenye ardhi yenye ukiwa unaweza kuwa mtu wa kuondokewa na watu muhimu kwako, kuondokewa na baraka zako n.k
Yako mambo mengi sana kuhusu ardhi, siku moja nitafafanua katika somo kamili na katika kitabu.
Nini ufanye katika maombi kuhusu ardhi?
1. Tubu kwa ajili ya ardhi unayokaa ili hiyo ardhi ipone, ikipona hiyo ardhi ni uponyaji na baraka na kwako pia.
2 Nyakati 7:14 "ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao."
MUNGU anaahidi kusamehe na kuiponya ardhi.
2. Haribu kimaombi madhabahu za giza, futa kafara za kipepo na futa maagano ya kipepo kwa sababu hayo mambo matatu yote hufanyika katika ardhi.
Kumbu 12:2-3 "Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo."
Mimi Peter Mabula nina shuhuda nyingi juu ya ardhi, nitakushuhudia siku moja katika somo lingine kuhusu ardhi na namna ya kuiombea.
3. Futa vifungo vya giza vikivyokupata kutokana na kifungo kilichofanyika ardhini.
Yohana 14:14 "Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."
4. Haribu kumbukumbu zote mbaya kukuhusu wewe au unaowaambea zilizotunzwa ardhini na wapige kimaombi watunza kumbukumbu wa kipepo kukuhusu wewe.
Mathayo 7:8 "kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."
5. Kwa sababu ardhi ikisemeshwa inazingatia ilichoambiwa(Yeremia 22:29-30) wewe kwenye maombi leo fanya haya.
A. Futa kwa damu ya YESU KRISTO kila kitu ulichofungwa ardhini.
B. Isemeshe wewe ardhi ili iwakatae wachawi, waganga wa kienyeji na iwakate kila wanadamu walio mawakala wa shetani.
C. Iambie ardhi itoe baraka zako ili uzipate.
Kumbu 28:4 "Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng'ombe wako, na wadogo wa kondoo zako."
Katika maombi ya ardhi unaweza hata ukauchukua udongo wa ardhi husika na kuutakasa kwa damu ya YESU KRISTO na kuuombea kisha unauunganisha na ardhi husika.
Inawezekana ulinunua kiwanja lakini jirani yako na hicho kiwanja chako alisema "atakayejenga hapa nyumba yake haitakamilika kamwe"
Inawezekana mlizaliwa katika ardhi iliyokuwa na Madhabahu za giza zilizofunga eneo hiyo na watakaozaliwa hapo.
Ndugu leo omba katika jina la YESU KRISTO utashinda kiajabu sana.
MUNGU akubariki sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele.
+255714252292
Ubarikiwe sana.

Comments