![]()  | 
| Na Mwl Peter Mabula  Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi  | 
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu. 
Karibu tujifunze Neno la MUNGU  la kutupa ushindi dhidi ya nguvu za giza. 
Leo katika maombi yako pambana na kuwashinda wasimamizi wa kipepo. 
Msimamizi ni yule anayeangalia kazi au shughuli fulani kama hiyo kazi imefanyika. 
✓✓Msimamizi wa kipepo ni yule wakala wa shetani aliyepewa jukumu  kipepo  ili kuhakikisha wewe unateseka au mabaya yaliyokusudia kipepo yanakupata.
✓✓Kuna watu wengi wanateseka kwa sababu ulimwengu wa roho wa giza umeweka wasimamizi  ili kuhakikisha watu hao wanaendelea kushikiliwa na vifungo vya giza. 
Ngoja tuanzie hapa,  Farao ni mfano wa shetani au ni Mfano wa mfalme wa kipepo(Ezekieli 29:3).
Sasa huyu farao aliweka wasimamizi ili kuwatesa watu wa MUNGU Waisraeli. 
Kutoka 1:11 "Basi wakaweka wasimamizi juu yao wawatese kwa mizigo yao. Nao wakamjengea Farao miji ya kuwekea akiba, Pithomu na Ramesesi."
Biblia inasema Farao akaweka wasimamizi ili wawatese watu wa MUNGU,  tabia hii ya farao ndio tabia ya wakuu wa giza au falme za giza. 
Kuna watu wanateswa na nguvu za giza kila mara kwa sababu wakuu wa giza wameweka wasimamizi wao juu ya watu hao. 
Inawezekana unawashinda wachawi, majini au maadui zako kiroho lakini ushindi wako unakuwa wa muda tu  kisha matatizo ya kwanza yanakurudia na kuendelea kukutesa. 
Ndugu,  katika vita ya kiroho ya namna hiyo inakupasa uwapige kwa maombi na wasimamizi waliotumwa na kuzimu kuhakikisha unaendelea kuteseka. 
Kuna vita nyingine ya kiroho unaweza kupambana na makundi hata matatu ya maadui katika vita moja. 
Mfano unaweza kuwa unapambana na jini na ukalishida kirahisi lakini baada ya muda linakuja jini lingine kwa sababu yupo mtuma majini,  yeye hujamgusa na anayo majini mengi hivyo ataendelea kuyatumwa kwako, lakini ulishawahi kujiuliza ukimpinga na huyo mtuma majini hayo majini wataendelea kuja kwako? 
Jibu ni hapana. 
Katika pia hizo nguvu za giza unazopambana nazo inawezekana zingine hazipo kukushambulia wewe ila zipo kusimamia zoezi la wewe kupatwa na kilichopangwa kwenye madhabahu ya giza, unaweza kumpiga aliyetumwa na ukamshinda lakini baada ya muda vita inainuka tena kwa sababu msimamizi amepeleka taarifa kwamba bado hujapatwa na madhara yaliyokusudiwa. 
Ndugu, najaribu kuchochea moto wa  maombi ndani yako na kukupa upana kidogo juu ya vita ya kiroho ili kama uko katika vita ya namna hii muda mrefu basi leo kwa maombi katika mamlaka ya jina la YESU KRISTO uombe kwa upana na ushinde,ndugu omba ili upewe ushindi na MUNGU. 
Mathayo 7:8 "kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."
Katika vita ya kiroho usiishie tu kupigana na farasi bali pigana pia na mpanda farasi.
Yeremia 51:20-21 " Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme; na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake;"
Hakikisha farasi na mpanda farasi wote unapambana nao, nazungumza kiroho. 
Usiishie tu kumpiga farasi kwenye vita ya kiroho bali pambana pia na mpanda farasi. 
Unatakiwa kwa maombi umpige na msimamizi aliyetumwa na kuzimu ili kuhakikisha wewe unaendelea kuteseka. 
Wasimamizi wa kipepo wapo hivyo inakupasa kuwapiga kwa jina la YESU KRISTO. 
Waisraeli waliwekewa wasimamizi ili wateswe hadi MUNGU alipoingilia kati kuwaokoa Waisraeli mbele ya wasimamizi waliowekwa na Farao. 
Kutoka 3:7" BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao;"
Hata wewe inawezekana unaendelea kuteswa na nguvu za giza kwa sababu ya wasimamizi wa kipepo,  leo wabadilikie kwa maombi ili wasikuzoee tena wala kukusimamia. 
Msimamizi wa kipepo anaweza kuwa ni yule anayetoa ripoti kuzimu kukuhusu wewe. 
Msimamizi wa kipepo ni yule anayefuatilia mipango yako  mizuri ili akuharibie usifanikiwe kamwe. 
Inawezekana wewe una sifa za kupata kazi lakini hakuna ofisi kwa sababu tu nguvu za giza walio wasimamizi wa kipepo wanafanya kazi yao kuhakikisha hupati kazi. 
Ndugu mmoja mwenye elimu ya digree alitafuta kazi hadi akachoka bila kupata kazi,  lakini kuna ofisi moja ambayo alikataliwa,  lakini ofisi hiyo hiyo alienda kijana mmoja aliyefeli kidato cha nne  akapata kazi. 
Tofauti ya watu hawa wawili ni nini? 
Tofauti ni kwamba mmoja ana kibali na mwingine kwenye ulimwengu wa roho hana kibali,  tofauti ni kwamba mmoja ana wasimamizi wa kipepo wanaomzuia na mwingine hana. 
Dada mmoja alinipigia simu akiniambia kwamba kuna wachumba wacha MUNGU  wanne  wote wanamhitaji afunge nao ndoa ila yeye amewakataa hadi wengine wakatoa machozi ya huzuni. 
Yaani hao vijana wanne   kila mmoja anajaribu kumweleza binti ili  akubaliwe ili atoe mahari wafunge ndoa.  Lakini pia binti mmoja mcha MUNGU safi siku moja alinipigia simu akiniambia kwamba hama tatizo lolote lakini kwa miaka mingi hakuna hata kijana mmoja aliyejitokeza akimhitaji wafunge ndoa. 
Tofauti ya mabinti hawa wawili ni nini? 
Tofauti ni kwamba mmoja amefungwa kwenye ulimwengu wa roho na mwingine hajafungwa.  Aliyefungwa inawezekana yuko vizuri kuliko hata huyo mwingine lakini wasimamizi wa kipepo ndio wanaomzuia. 
Ndugu,  wasimamizi wa kipepo  wanaweza kuwafukuza watu sahihi kwako ili ubaki ulivyo,  wanaweza kuipeperusha  nafasi yako au kazi yako au baraka yako hata ukashangaa siku zote unang'ang'ana bila kufanikiwa. 
leo kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO waponde kwa fimbo ya chuma hao wasimamizi wa kipepo ili wakuachie, waachie familia yako,  waachie baraka zako,  waachie ndoa yako,  waachie uzao wako,  waachie uchumi wako,  waachie fursa zako,  waachie kibali chako na waiachie kila baraka yako, leo waponde wote bila kubakiza hata mmoja. 
Zaburi 2:9 "Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi."
Msimamizi wa kipepo ni yule anayekupeleleza ili apeleke kwenye madhabahu ya giza ripoti kuhusu wewe,  leo kwa maombi katika jina la YESU KRISTO mpige mpeleka ripoti na mpelekewa ripoti kuhusu wewe. 
Msimamizi wa kipepo ni yule anayekutega kichawi ili unase katika mipango yao ya kichawi na kiganga, omba ndugu  ukiomba MUNGU akulinde dhidi ya maadui zako. 
Zaburi 141:9-10 " Unilinde na mtego walionitegea, Na matanzi yao watendao maovu. Wabaya na waanguke katika nyavu zao wenyewe, Pindi mimi ninapopita salama."
Leo usiwahurumie katika maombi bali pambana nao ukimwita MUNGU Baba ili awatoweshe wote. 
Zaburi 71:12-13 " Ee MUNGU, usiwe mbali nami; Ee MUNGU wangu, fanya haraka kunisaidia. Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya."
Mtu mmoja katika ndoa yake alitafuta mtoto muda mrefu, akawa ananipigia simu mara kwa mara namuombea,  neema ya MUNGU ikaja akapata mimba.  Baada ya miezi michache akaona vita ya mwanzo imeinuka ghafula,  akawa anapambana na nguvu za  giza na kuzishinda siku moja nguvu za giza zikawa nyingi akaja hadi na mkuu wa giza,  walimwambia "Hatuwezi kukubali wewe uzae" baada ya muda siku moja walikuja tena  kwenye ulimwengu wa roho ili kupambana naye wakamshinda,  baada ya kumshinda walimchoma sindano moja na tangu muda huo akaanza kutoka damu, mimba ikaharibika.
Katika somo hili nazungumza na watu ambao wanapambana hasa na nguvu za giza,  ndugu fanyia kazi kwa maombi katika jina la YESU KRISTO ili uwe salama. 
Mama mmoja alinipigia simu siku moja nimuombee kwa sababu alikuwa anatokwa damu mfululizo miezi mingi,  wakati namuombea niliona kwenye ulimwengu wa roho nyanya iliyoiva imechomwa sindano inavuja maji kidogo kidogo,  kumbe vile nyanya ile inavuja maji kwa mtego wa mchawi ndivyo huyu mama anateseka kwa kutokwa damu mfululizo karibia mwaka,  amekonda, anaumwa muda wote na alijua anakufa, kumbe kuna mchawi hubadilisha tu nyanya na kuzichoma sindano ili aendelee kuvuja damu. 
Baada ya kumuuliza nini tatizo akasema kuna mama alimtamkia kwamba hayo yatampata kwa sababu ametembea na mume wake. 
Ndugu zangu dhambi ni mbaya,  dhambi inaweza kukuletea mauti.  Ilibidi nimuonye kwanza kisha tuombe toba kisha ndipo tupasue nyanya kwenye ulimwengu wa roho ndipo akapona. 
Katika somo hili nazungumza na wanaoteseka haswa kutokana na nguvu za giza na wamepambana  lakini ushindi ni wa muda tu. 
Ndugu, leo katika jina la YESU KRISTO omba na utamuona MUNGU anayebadilisha historia ya wanaomkimbilia katika wokovu kwa Mwanaye YESU KRISTO. 
Zaburi 7:1 "BWANA, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe, Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye."
Jinsi hali kuwashinda hao wasimamizi wa kipepo na waliowatuma. 
1. Tubu kwa ajili ya dhambi zako na makosa yako, pia kama hujaokoka okoka  ili YESU KRISTO awe Mwokozi wako. 
Isaya 59:1-2 "Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."
2. Mwite MUNGU kwa maombi ili awapige hao wasimamizi wa kipepo. 
2 Samweli 22:4 "Nitamwita BWANA astahiliye kusifiwa; Hivyo nitaokoka na adui zangu."
3. Pambana nao kimaombi hadi watoweke. 
2 Samweli 22:38-39 " Nimewafuatia adui zangu, na kuwaangamiza; Wala sikurudi nyuma hata walipokomeshwa. Nami nimewakomesha na kuwapiga-piga wasiweze kusimama; Naam, wameanguka chini ya miguu yangu."
Katika vita ya kiroho wakati mwingine zingatia kuomba kwa Neno la MUNGU maana Neno la MUNGU lina nguvu kuliko maneno yako.  
Yeremia 5:14 "Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala."
Kwenye vita ya kiroho usizihurumie kamwe nguvu za giza na wanaotumika kipepo maana ukizubaa watakuangamiza wewe, pambana kimaombi ndio maana ya vita vya kiroho. 
Zaburi 18:38 "Nitawapiga-piga wasiweze kusimama, Wataanguka chini ya miguu yangu."
4. Hapo wasimamizi wa kipepo waombee kuabika na kufadhaika. 
Zaburi 6:10 "Adui zangu wote wataaibika na kufadhaika, Watarudi nyuma, kwa ghafula wataaibika."
5. Futa laana zao za kinywa kuhusu wewe, futa maneno ya kukufunga waliyokusemea au kukufunga. 
Zaburi 41:5-10 " Adui zangu wananitaja kwa maneno mabaya, Atakufa lini, jina lake likapotea? Na mmoja wao akija kunitazama asema uongo, Moyo wake hujikusanyia maovu, Naye atokapo nje huyanena. Wote wanaonichukia wananinong'ona, Wananiwazia mabaya.
 Neno la kisirani limemgandama, Na iwapo amelala hatasimama tena. Msiri wangu tena niliyemtumaini, Aliyekula chakula changu, Ameniinulia kisigino chake. Lakini Wewe, BWANA, unifadhili, Uniinue nipate kuwalipa."
6. Wafunge kwa maombi wasimamizi na waliowatuma. 
Mathayo 18:18 "Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni."
7  Hakikisha MUNGU yuko upande wako. 
Zaburi 56:9 "Ndipo adui zangu watarudi nyuma siku ile niitapo. Neno hili najua kuwa MUNGU yu upande wangu;"
8. Kaa ndani ya YESU na katika kusudi la MUNGU. 
Yohana 15:4 "Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu."
Baadhi ya mambo yanayokupasa ukiwa ndani ya kusudi la MUNGU ni  pamoja na  kuwa na muombaji wakati mwingine maombi ya kufunga, kumtumikia MUNGU, kuwaleta watu kwa YESU KRISTO, utoaji na kusonga mbele katika YESU KRISTO bila kutetereka. 
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri. 
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Ni namba hii  kupiga,  kuandika meseji na hadi whatsapp).

Comments