MAOMBI YA VITA ILI USHINDE DHIDI YA NGUVU ZA GIZA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Hili ni somo lenye ufafanuzi mfupi ila litakusaidia sana na kuwafanya maadui zako kiroho wakuogope.

✓✓Kuna ushindi wa ajabu MUNGU analeta kwako wewe unayeishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO na huwa unafanya Maombi vyema.

Wachawi unaopambana nao hawatakuweza kamwe.

Wanadamu wanaotumika kipepo hawatakuweza kamwe.

Majini wote na kila maroho wa kuzimu hawatakuweza kamwe.

Soma ahadi ya MUNGU kwako na familia yako,
Yeremia 15:20-21 " Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema BWANA. Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha."

 ◼️Kazi yako lifanye Neno la MUNGU katika kinywa wakati wa maombi kuwa moto mbele ya adui zako, yaani omba kwa kutumia Neno la MUNGU.

Yeremia 5:14 "Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala."

✓✓Moto unaoutoa kwa kinywa chako utawadhuru hao mawakala wa shetani unaopambana nao.

Nini kingine ufanye? 

✓✓wahukumu kimaombi wachawi wote na wakuu wa giza wote unaopambana nao. 

Kutoka 22:18 " Usimwache mwanamke mchawi kuishi."

Kwanini uombe hivyo?

✓✓Ni kwa Sababu MUNGU atawafanya kuanzia sasa hao mawakala wa shetani na maroho waliyotuma kwako kukudhuru, MUNGU atawafanya kupigwa mbele yako,
Kumbu 28:7 "BWANA atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba."

Mimi Peter Mabula namshukuru Bwana YESU KRISTO maana hata aliyeandikiwa na wachawi kufa MUNGU anaweza kufuta kifo hicho Zaburi 102:20" Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa, Na kuwafungua walioandikiwa kufa."

◼️Kama wachawi kulikupangia ufe kwa presha au kisukali au ajali au kifo chochote cha kipepo, ukiomba MUNGU Baba anasema atakufungua uliyeandikikiwa kufa, muhimu ishi maisha matakatifu ya Wokovu, okoka na uwe muombaji.

Nini kingine ufanye katika maombi yako ya vita dhidi ya nguvu za giza?

✓✓Ni kwamba watumie malaika waletao mabaya wayapeleke kwa adui zako,

Zaburi 78:49 "Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya."

✓✓Hawa kundi la Malaika waletao mabaya likienda kwa wachawi na majini na mizimu na wakuu wa giza wanaokusumbua ujue watapata mabaya ambayo hawajawahi kupata.

Malaika wako karibu yako muda wote wanasubiri tu uwape kazi kwa Neno la MUNGU na utaona matokeo, Mimi  sikuandikii kitu nilichosikia ila nakufundisha kitu nilichokiona mwenyewe katika maombi, ila tu kumbuka neno hili na usije ukasahau hata siku moja kwamba Malaika hawawajibiki kwako mwanadamu ila wanakusaidia kutokana na Neno la MUNGU unalowaelekeza kwalo katika maombi safi mbele za MUNGU.

✓✓Malaika husikia sauti iliyo ndani ya Neno la MUNGU unalotamka ndipo wanafanya kama Neno la MUNGU linavyoelekeza.

Inawezekana hujanielewa bado kwa sababu ya mila na desturi za dhehebu lenu ulizofundishwa zilizo kinyume na kusudi la MUNGU, Mimi nakufundisha Biblia na sio taratibu za dhehebu, ni kwamba Malaika wapo kukusaidia ila Malaika huisikia sauti iliyo katika Neno la MUNGU na sio maneno yako tu.

Zaburi 103:20 "Mhimidini BWANA, enyi malaika zake, Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake, Mkiisikiliza sauti ya neno lake."

Hivyo ukiwa katika maombi ukitaka msaada wa MUNGU kupitia Malaika basi tambua kwamba Malaika wanaisikia sauti iliyo ndani ya Neno la MUNGU unalotamka, ndugu omba ukitumia Neno la MUNGU katika KRISTO YESU kwa usahihi kabisa.

Wako pia Malaika wenye kazi nyingi, baadhi ni kwamba kuna Malaika wa kupeleka ujumbe, kuna Malaika wa kuwatoa watu kwenye magereza ya kiroho, kuna Malaika wa kuwaangusha chini maadui zako, kuna Malaika wa kupeleka mabaya kwa adui zako n.k

✓✓Mfano katika maombi kama hujawahi kumtumia huyu Malaika wa Isaya 37:36 basi Mtumishi Leo katika maombi yako, kazi ya huyo Malaika ni hivi
Isaya 37:36 "Basi malaika wa BWANA alitoka, akaua watu mia na themanini na tano elfu katika kituo cha Waashuri, na watu walipoamka asubuhi na mapema, kumbe, hao walikuwa maiti wote pia."

huyu Malaika anaweza kuwaua maroho wa kuzimu wote kama mizimu na majini na ukashinda kirahisi sana.

Kama kuna wakala wa shetani hajawahi kukuogopa nakuhakikishia kuanzia leo atakuogopa mno sana.

Nimekupa ufunuo wa ndani sana wa ki maombi na uliyekusudiwa na ROHO MTAKATIFU naamini ukiomba katika jina la YESU KRISTO huku ukifuata maelekezo ya rohoni hakika ipo siku utanipa ushuhuda.

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments