![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Leo nawiwa tu kujibu maswali ambayo baadhi ya marafiki zangu waliniuliza na mimi nawajibu kwa neema ya MUNGU kwa kadiri ninavyojaaliwa.
Najua maswali ni mengi hivyo ukiona swali lako ulilowahi kuniuliza sijakujibu basi inawezekana ipo siku nitakujibu nikipata neema hiyo.
Kwa wewe unayesoma ujumbe huu naamini yamkini kuna kitu utajifunza.
Mbarikiwe sana nyote.
SWALI LA KWANZA.
1. Jambo Mtumishi wa Bwana.
Bwana Yesu asifiwe.
Niko na swali naomba unisaidiye
Hasira ni dhambi au siyo dhambi?
MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.
Kuna aina mbili za hasira.
✓✓Kuna hasira ambayo ni dhambi na kuna hasira ambayo sio dhambi.
◼️Hasira ambayo ni dhambi ni ile hasira ambayo humfanya mtu kutenda dhambi .
Mathayo 5:22 "Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto."
✓✓Yaani Hawezi kuwasamehe waliomkosea, hivyo anaendelea kubaki na hasira, chuki, uchungu na kinyongo.
✓✓Anawaza kulipiza baya kwa baya alilotendewa.
✓✓Anatamani mabaya sana yamfike mtu aliyemkosea.
✓✓Anamuombea kifo au madhara mtu aliyemkosea.
Waefeso 4:31 "Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya;"
✓✓Ukiona hasira inazaa uchungu na ghadhabu ujue hiyo ni hasira ya dhambi.
✓✓Ukiona hasira inazaa makelele na matukano hiyo hasira ya dhambi.
✓✓Ukiona hasira inaleta ubaya na kuchukiana ujue hiyo ni hasira ya dhambi.
Wakolosai 3:8 "Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenu."
✓✓Ukiona hasira inaleta matukano na matusi ujue hiyo ni hasira ya dhambi.
✓✓Hasira ya dhambi ni ya Mtu asiyeachilia wala kusamehe.
Hii ndio hasira ambayo ni dhambi, na hasira ya namna hii hukaa tu vifuani mwa wapumbavu.
Mhubiri 7:9 " Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu."
◼️Hasira ambayo sio dhambi, ni hasira ya kuchukua uovu, kuchukia kinachozuia kusudi la MUNGU n.k
✓✓Ni hasira isiyomnajisi mwenye hiyo hasira.
✓✓Ni hasira isiyomtengenezea chuki kwa mtu yeyote huyo mwenye hiyo hasira.
✓✓Ni hasira inayoukataa ubaya tu na sio kuwachukia watu.
Ngoja nikupe mfano hai.
Bwana YESU hakuwahi kutenda dhambi yeyote ile lakini kuna siku alipata hasira.
Marko 3:5 "Akawakazia macho pande zote kwa hasira, akiona huzuni kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena."
Bwana YESU alipata hasira kali kwa sababu ya ugumu wa mioyo ya wanadamu maana hawakumwamini ili awaokoe na jehanamu.
Hasira ya Bwana YESU haikuwa hasira ya kuwachukia watu ndio maana unaona anahuzunika kwa ajili yao na sio kuwachukia.
✓✓Biblia haitukatazi kuwa na hasira ila inatutaka tuwe na hasira ambayo sio hasira ya dhambi.
Waefeso 4:26 "Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka;"
MUNGU akubariki.
SWALI LA PILI.
"Kuna uwezekano mtu akapokea ROHO MTAKATIFU kabla hajabatizwa ubatizo wa maji?"
MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.
◼️Ndio inawezekana kabisa Mkristo akapokea ROHO MTAKATIFU kabla ya kubatizwa ubatizo wa maji.
Ngoja tupate majibu kutoka ndani ya Biblia kuhusu mtu kupokea ROHO MTAKATIFU kabla ya kubatizwa ubatizo wa maji.
Matendo 10:47-48 " Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea ROHO MTAKATIFU vile vile kama sisi? Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake YESU KRISTO. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha."
Biblia inaonyesha hawa Wakristo walimpokea ROHO MTAKATIFU yaani walibatizwa ubatizo wa ROHO MTAKATIFU kabla hata hawajabatizwa ubatizo wa maji.
Hiyo inatufundisha kwamba kwa neema ya MUNGU Mkristo anaweza kujazwa ROHO MTAKATIFU hata kabla ya kubatizwa ubatizo wa maji, lakini katika maandiko hapo juu tunaona pia kwamba ingawa wakristo wale walikuwa wamebatizwa ROHO MTAKATIFU lakini ni lazima pia wabatizwe na kwa ubatizo wa maji.
✓✓Kumbe ubatizo wa maji nao ni wa muhimu sana, hivyo hata wewe, hata kama imeshajaa ROHO MTAKATIFU au hata kama hadi umeshaanza kumtumikia MUNGU baada ya kujaa ROHO MTAKATIFU lakini bado inakupasa ubatizwe ubatizo wa maji.
Na katika ubatizo wa maji hakikisha unabatizwa ubatizo wa maji mengi au maji ya kuzamishwa maana ndivyo Kanisa la MUNGU la Kwanza walibatizwa ndani ya Biblia na ndio ubatizo ulio na maana ya ubatizo kulingana na maana ya kiroho ya neno "UBATIZO"
Wakolosai 2:12 "Mkazikwa pamoja naye(KRISTO) katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za MUNGU aliyemfufua katika wafu."
Lakini Biblia inaonyesha pia baadhi ya watu walibatizwa kwanza ubatizo wa maji ndipo wakabatizwa ubatizo wa ROHO MTAKATIFU.
Matendo 8:15 "ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee ROHO MTAKATIFU; kwa maana bado hajawashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina lake Bwana YESU. Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea ROHO MTAKATIFU."
Nini nataka niseme zaidi?
✓✓Kwa watumishi usije ukamhubiria mtu akaokoka siku hiyo hiyo na kujazwa nguvu za ROHO MTAKATIFU na kuanza kunena kwa lugha, wewe ukadhani haiwezekani kwa sababu umekariri tu kwamba nilazima abatizwe kwanza ubatizo wa maji kisha afundishwe sana Neno la MUNGU ndipo atampokea ROHO MTAKATIFU, ndugu somo Vizuri Biblia ili usije ukalizuia kusudi la MUNGU mitazamo yako iliyo kinyume na Neno la MUNGU.
Mtumishi mmoja alimkataza mtu kunena kwa lugha kwa sababu ndio tu alikuwa ameokoka.
Mimi binafsi nilibatizwa kwanza ubatizo wa maji mengi ndipo baadae nikapokea ROHO MTAKATIFU lakini hiyo haina maana kwamba niwakataze wanaojaa ROHO MTAKATIFU kabla hawajabatizwa ubatizo wa maji.
Ubatizo wa maji ni wa muhimu sana sanaa ni wa lazima kwa kila aliye kanisa hai la KRISTO lakini ukianza na ubatizo wa ROHO MTAKATIFU usishtuke ila hakikisha unabatizwa kwa batizo zote mbili.
✓✓Muhimu hakikisha unabatizwa ubatizo wa ROHO MTAKATIFU na ubatizo wa maji, haijalishi ni nini kilianza kwanza kati ya hizo batizo mbili muhimu kwa kila mteule wa KRISTO.
Fanya juhudi binafsi ili ubatizwe kwa batizo zote mbili.
Matendo 19:2-6 " akawauliza, Je! Mlipokea ROHO MTAKATIFU mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna ROHO MTAKATIFU hatukusikia. Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana. Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, YESU.
Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana YESU. Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, ROHO MTAKATIFU akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri."
MUNGU akubariki sana.
SWALI LA TATU.
3. Bwana Yesu Atukuzwe, mtumishi Mabula naomba unieleweshwa majina ya malaika wa Mbinguni wanaomkinga mtu au ku mpigania Wakati wowote wa shida na raha anapowaita.
MAJIBU.
✓✓Ni malaika wawili tu waliotajwa kwa majina katika Biblia, ni Mikaeli na Gabrieli,
Malaika Gabrieli ametajwa kwa jina katika maandiko manne katika Biblia, maandiko mawili katika kitabu cha Danieli na maandiko mawili katika kitabu cha Luka, kote huko Gabrieli ametajwa akionekana akipeleka taarifa tunaweza kusema ni Malaika mpeleka taarifa lakini hata kupigana vita anapigana( Danieli 10:20)
Andiko mojawapo linalomtaja Malaika Gabrieli ni pamoja na hili.
Luka 1:26 "Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti,"
Malaika Mikaeli katika Biblia ametajwa kwa jina mara Tano, mara tatu kitabu cha Danieli, mara moja kitabu cha Yuda na mara 1 pia kitabu cha ufunuo.
Ngoja nikuelezee na kazi na sifa za Malaika Mikaeli ili uelewe vyema maana kuna waongo wa dini husema kwamba Malaika Mikaeli ndio Bwana YESU wakati Bwana YESU sio Malaika, yeye aliwaumba Malaika, yeye ni MUNGU anayesujudiwa na Malaika wote mbinguni, yaani hata Mikaeli anamsujudia Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
Waebrania 1:6 "Hata tena, amletapo mzaliwa wa kwanza ulimwenguni, asema, Na wamsujudu malaika wote wa MUNGU."
Maana ya andiko hilo ni kwamba Malaika wote wamsujudie YESU KRISTO, ukiangalia tafsiri ya BHN hilo neno "kusujudi " maana yake Malaika wote wamwabudu YESU KRISTO.
Hapo hata kabla sijaendelea kumzungumzia Mikaeli najua sasa umejua kwamba YESU KRISTO sio Mikaeli maana hata Mikaeli na malaika wengine wote wanamwabudu Bwana YESU KRISTO na kumsujudia.
✓✓Mikaeli ni malaika mkuu lakini YESU KRISTO ni MUNGU mkuu(Isaya 9:6)
Sasa ngoja niseme machache kuhusu Mikaeli
A. Mikaeli ni Malaika aliye mmoja wa wakuu wa mbele.
Danieli 10:13 "Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi."
B. Mikaeli ni Malaika mlinzi wa Wateule wa KRISTO.
Danieli 10:21 "Lakini nitakuambia yaliyoandikwa katika maandiko ya kweli; wala hapana anisaidiaye juu ya hao ila huyo Mikaeli, mkuu wenu."
Neno "Mkuu wenu kwenye tafsiri zingine linamaana ya mlinzi wenu"
angalia mfano BHN, hivyo Mikaeli ni Malaika anayetulinda.
C. Mikaeli ni Malaika aliye jemadari mkuu anayetulinda wateule wa KRISTO YESU, yaani wanaoishi maisha matakatifu ya Wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
Danieli 12:1 "Wakati huo Mikaeli atasimama, jemadari mkuu, asimamaye upande wa wana wa watu wako; na kutakuwa na wakati wa taabu, mfano wake haukuwapo tangu lilipoanza kuwapo taifa hata wakati uo huo; na wakati huo watu wako wataokolewa; kila mmoja atakayeonekana ameandikwa katika kitabu kile."
D. Mikaeli ni Malaika mkuu.
Yuda 1:9 "Lakini Mikaeli, malaika mkuu, aliposhindana na Ibilisi, na kuhojiana naye kwa ajili ya mwili wa Musa, hakuthubutu kumshitaki kwa kumlaumu, bali alisema, BWANA na akukemee."
E. Mikaeli ni Jemadari mkuu katika masuala ya vita, hapa chini tunaona shetani na malaika wake ambao ni majini, mizimu na kila maroho wa kuzimu, hawa walipigwa na Mikaeli na kufukuzwa mbinguni.
Ufunuo 12:7-9 " Kulikuwa na vita mbinguni; Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana nao pamoja na malaika zake;
nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni.
Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye."
Nimesema haya mengi ili mtu ajifunze ukweli wa ki MUNGU ndani ya Neno la MUNGU.
Na hawa Malaika waliotajwa majina yaani Gabrieli na Mikaeli wametajwa kwa majina ili tu kutujulisha kwamba Malaika mbinguni nao wana majina, MUNGU aliwapa majina alipowaumba na majina yao ni mazuri na yanayomtukuza MUNGU.
Hii inatufundisha kwamba Malaika wana majina.
✓✓MUNGU anataka hata sisi tunapowaita majina watoto wetu basi tuwape majina mazuri na yenye maana nzuri inayomtukuza MUNGU wetu.
✓✓Hii inatufundisha pia kwamba watoto wetu kabla hawajazaliwa inatupasa tumuombe MUNGU atupe majina safi ambayo tutawapa watoto wetu.
Kwa hiyo unapoomba kwa MUNGU ili malaika wakusaidie kitu fulani huhitaji kuita malaika jina ila unahitaji kuwaita kwa kazi yao.
Mfano unaweza kuomba kwa MUNGU kwamba "Malaika wapelekao mabaya na wayapeleka mabaya sasa katika madhabahu za giza zinazotesa familia yangu , maisha yangu na ndoa yangu kama Zaburi 78:49 ambayo inasema kwamba kuna kundi la malaika ambao kazi yao ni kupeleka mabaya kwa adui zetu wa kutoka kuzimu "
✓✓Hapo unakuwa umewaita malaika kwa neno la MUNGU kupitia kazi yao kama neno linavyosema na watafanya kazi husika kwa kusudi la MUNGU Baba.
✓✓Unaweza ukawaita malaika wa ulinzi(Zaburi Zaburi 34:7)
✓✓Unaweza ukaita malaika wa kumleta mwenzi wako ili mfunge ndoa katika hali takatifu (Mwanzo 24:40) n.k
Yaani kuna kazi zaidi ya 20 za malaika kimaandiko hivyo kama unajua kumuomba MUNGU kwa kutumia malaika zake ili usaidike basi unaweza ukaomba ukiwataja hao malaika kwa kazi zao kimandiko na utamuona MUNGU.
Kuna somo siku moja nitapost linaloonyesha kazi zaidi ya 20 za malaika hivyo utajua mengi yatakayokusaidia katika maombi na vita ya kiroho ili ushinde katika jina la YESU KRISTO.
MUNGU akubariki.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU Mwenyezi.

Comments