![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu kujifunza neno la MUNGU.
Somo hili linatokana na maswali ambayo rafiki yangu mmoja aliniuliza na mimi nikamjibu hivyo nakuletea hapa maswali hayo ya rafiki yangu na majibu yangu nikiamini unajifunza kitu kizuri cha kiroho.
Maswali ya rafiki yangu yalikuwa ni haya.
1. Kufunga ni nini?
2.Ni nani anatakiwa kufunga?
3. Nini kanuni za mtu aliyefunga/ ni mambo gani ya kuzingatia unapofunga?
4. Kwanini tunafunga?
5. Nini faida za kufunga?
6. Je ni wakati gani unafaa kufunga?
Majibu yangu Mimi Peter Mabula kwa rafiki yangu yalikuwa ni haya
Naomba yakusaidie na wewe katika kujua au kuongeza ufahamu au kukupa msukumo wa kufunga au kukujulisha umuhimu wa maombi ya kufunga n.k
1. Maombi ya Kufunga ni nini?
✓✓Maombi ya kufunga ni hali ya kuutiisha mwili wako kwa muda maalumu kwa kuunyima chakula pamoja na vinywaji kwa makusudi ili upate muda mzuri wa kufanya maombi mbele za MUNGU, katika muda huo maalumu uliojiwekea, muda huo unaanzia siku moja na kuendelea.
Mfano wa watu walioingia katika maombi ya kufunga ni hapa chini.
2 Nyakati 20:3-4" Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute BWANA; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote. Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute BWANA; hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta BWANA."
2. Nani anatakiwa kufunga?
✓✓Kila Mteule wa KRISTO anatakiwa kuingia katika maombi ya kufunga pale inapobidi au unapokuwepo ufunuo wa kufunga au kulingana na utaratibu uliopo Kanisani au utaratibu aliojiwekea mteule huyo wa KRISTO.
Mfano ni hawa waliingia katika maombi ya kufunga siku tatu.
Esta 4:16-17 " Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie. Basi Mordekai akaenda zake, akafanya yote kama vile Esta alivyomwagiza."
3. Nini kanuni za mtu aliyefunga/ ni mambo gani ya kuzingatia unapofunga?
◼️Kanuni ya kufunga ni kutokula chakula na kufanya Maombi.
Zaburi 69:10 "Nilipolia na kuiadhibu roho yangu kwa kufunga, ....."
Mambo ya kuzingatia katika maombi ya kufunga inategemeana na hitaji lako au mahitaji uliyonayo.
✓✓Muhimu zingatia maombi ya toba kwanza kama unahitaji msaada wa MUNGU maana vifungo vingi vinatokana na uzembe wetu au kuruhusu nguvu za giza kuvamia,
yaani mtu hakusimama katika nafasi yake kiroho hadi tatizo kuwepo.
Mfano hai.
Danieli 9:3-6 " Nikamwelekezea BWANA Mungu uso wangu, ili kutaka kwa maombi, na dua, pamoja na kufunga, na kuvaa nguo za magunia na majivu. Nikamwomba BWANA, Mungu wangu, nikaungama, nikasema, Ee BWANA, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano na rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kwa kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi."
4. Kwanini tunafunga?
✓✓Tunafunga kwa sababu kuna vitu hatutavitapatia majibu hadi kwa kufunga na kuomba.
Mathayo 17:21 [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]
✓✓Kuna baraka kuzipata hadi kwa kufunga na kuomba.
✓✓Kuna nguvu zaidi katika maombi ya kufunga kuliko maombi ya kawaida.
✓✓Kuna mambo hayatawezekana kwako hadi kwa kufunga na kuomba.
✓✓Kuna mahitaji yanahitaji kufunga na kuomba ndipo utayapata.
✓✓Kuna vitu havitawezekana kuvishinda hadi kwa kufunga na kuomba.
◼️Kufunga na kuomba ni ufunguo mmojawapo wenye nguvu zaidi kufungua katika ulimwengu wa roho.
5. Nini faida za kufunga?
✓✓Kwanza kufunga ni mojawapo ya kanuni njema ya kiroho ya kupata ushindi kwa maombi, tangu zamani wateule wa KRISTO walikuwa wanafunga na kuomba pale inapohitajika hivyo.
Luka 2:37 ‘’ Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba. ‘’
Sasa faida za kufunga na kuomba ziko nyingi, binafsi Nimeshawahi kuandika masomo kadhaa kuhusu faida za kufunga zaidi ya 10.
Ngoja Nikuambie faida chache tu za maombi ya kufunga kimaandiko.
A. Mwili wako utakuwa umetiishwa.
Wakolosai 3:5 ‘’ Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu;‘’
✓✓Kuutiisha mwili wakati mwingine hauhitaji tu kuishi maisha matakatifu bali ni kuishi maisha matakatifu huku ukiomba na maombi ya kufunga ndio yaliyo na nguvu zaidi za kukusaidia katika hilo.
B. Utapokea kutoka kwa MUNGU katika KRISTO YESU maana ni ahadi ya MUNGU kujibu maombi yako kumtafuta kwa moyo wako wote, maombi ya kufunga ni sehemu mojawapo ya kumtafuta MUNGU kwa moyo wako wote.
Yeremia 29:13 ‘’Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.''
6. Je ni wakati gani unafaa kufunga?
✓✓Wakati wowote unapokuwa unahitaji majibu kutoka kwa MUNGU, huo wakati unafaa kufunga na kuomba.
Zaburi 109:24 "Magoti yangu yamedhoofu kwa kufunga, Na mwili wangu umekonda kwa kukosa mafuta."
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Hadi whatsapp).
Ubarikiwe.

Comments