MASWALI MAZURI NA MAJIBU YAKE.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



1. Bwana asifiwe Mtumishi,Pole na majukumu yako ya kila siku na nikupe hongera kwa kutenga muda wako na kwa kile ulichotunukiwa na Mungu kutupa elimu katika maisha yetu ya ukristo ili kujiweka tayari na ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Nimekuwa nikifwatilia mafundisho yako kwa kipindi kirefu kidogo,na mara nyingi kama ninakuwa na swali katika mada unazozijadili kila wakati napata majibu kutokana na comments za members ila leo nimekosa jibu na nimekuwa mzito kidogo kuuliza kutokana na maudhui ya swali lenyewe.
Umezungumzia kuhusu Dhambi ya zinaa,uzinzi na uasherati.Lakini katika maelezo yako ulifafanua zaidi na ukatumia moja ya mstari uliopo katika Biblia,mstari huo ukataja neno uzinzi,uasherati,wafiraji nk; Hoja/Swali langu linaanzia hapa,umesema dhambi zote ni sawa,ila kuna baadhi ya mafundisho nilipata kuwahi kusikia kuwa wafiraji kamwe hawatauona Ufalme wa Mungu,kwa maana ya kwamba dhambi hii haisameheki.
Tafadhali Mtumishi naomba nisiwe muongo,niliwahi kuitenda hiyo dhambi na dhambi hiyo inanihukumu kila nikitafakari uhalali wa kutoingia Mbinguni kwa ajili ya hii dhambi,Dhambi hii inanitafuna hadi wakati mwingine nasema kama hakuna kuingia Mbinguni si bora niendelee na pombe,uzinzi nk kwasababu hata nifanyeje moto ni lazma unichome?!
Tafadhali mtumishi nieleweshe kuhusu hili ili nijue nini la kufanya kabla ghadhabu ya Mungu haijanishukia.
Natumai kupata ufafanuzi na maelekezo.
Asante.

MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA:

MUNGU akubariki sana kwa kuwa muwazi.
Jibu la swali lako ni rahisi sana, ni kwamba ni dhambi moja tu ambayo wanadamu hawatasamehe, ni kumkufuru ROHO MTAKATIFU
Mathayo 12:31 "Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa."

Na kumkufuru ROHO MTAKATIFU sio dhambi ya kawaida, ni kiwango cha juu cha kukufuru, mfano wake mmoja  ni kama Mtu alikuwa Mchungaji au Askofu na ROHO MTAKATIFU alimtumia sana kwa Miujiza mikubwa ya MUNGU mwenyewe, watu wengi wakaokoka kupitia yeye lakini baadae kwa tamaa zake akaacha Wokovu na kujiunga na dini ya mpinga KRISTO Kisha akaanza kusema huo aliokuwa ansufanya zamani ni usanii tu hakuna Cha ROHO MTAKATIFU Wala Nini, hapa anasema ili awafurahishe dini yake mpya wansomlipa lakini moyoni anajua ni kweli ni MUNGU kupitia ROHO MTAKATIFU alimtumia, huko ni kumkufuru ROHO MTAKATIFU na hawezi kuifikia Neema Mtu huyo maana atawafanya wengi kuona ROHO MTAKATIFU sio chochote na YESU haokoi, ni hatari sana kwa Mtu anayefikia kiwango Cha kumkufuru ROHO MTAKATIFU.

Kazi yangu leo sio kuzungumzia ilivyo dhambi ya kumkufuru ROHO MTAKATIFU ila nataka tu nikutoe wasiwasi kwamba dhambi yako ya ufiraji inasameheka kama ukitubu na kuiacha.

Hivyo hakuna haja ya kuendelea na dhambi hiyo, hakuna haja ya kunywa pombe, hakuna haja ya kuwa mzinzi au mwasherati bali tubu dhambi zote kwa Bwana YESU KRISTO na utasamehewa.

Kuna msamaha wa uhakika kwa MUNGU katika KRISTO YESU kama kutubu na kuacha dhambi.

Wakolosai 2:13 "Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote;"

Hivyo ukiona unasikia sauti ikisema hutasamehewa kwa dhambi ya ufiraji ujue hiyo ni sauti ya shetani ili uende jehanamu kweli.

Dhambi ya ufiraji ni mbaya sana kama zilivyo dhambi zingine hivyo tubu na usirudie tena, mpokee YESU KRISTO kwa upya na ishi maisha matakatifu ya Wokovu kuanzia sasa na hakika uzima wa milele utakuhusu.

1 Yohana 2:12 "Nawaandikia ninyi, watoto wadogo, kwa sababu mmesamehewa dhambi zenu, kwa ajili ya jina lake."

Asikudanganye mtu kwamba hutasamehewa bali tubu na kuacha hakika MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi atakusamehe, dhambi yako itafutwa kwa damu ya YESU KRISTO na haitakumbukwa tena mbinguni, kama utaikumbuka wewe hiyo dhambi ni kupoteza muda ila ukitubu katika KRISTO YESU unasamehewa kabisa na inafutwa kabisa hiyo dhambi maana ni MUNGU wetu aliaahidi kusamehe dhambi kwa wanaotubu na hatazikumbuka.

Waebrania 8:12 Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, Na dhambi zao sitazikumbuka tena.
MUNGU akubariki sana.

2. Bwana Yesu asifiwe Mtumishi wa Bwana Aliye Hai.
Ningeomba kujua tofauti kati ya uzinzi na uasherati, tofauti yake iko wapi??

MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA:

Hakuna tofauti ya uzinzi na uasherati ila kuna tofauti ya mzinzi na mwasherati.

Uzinzi ni nini?

Uzinzi ni kitendo cha mtu aliye kwenye ndoa kufanya mapenzi na mtu yeyote nje na mwenzi wake wa ndoa.

Wazinzi Ni Wanandoa Wanaotoka kingono nje Ya Ndoa Zao.

Uasherati ni nini?

Uasherati ni kitendo cha kuzini anachokifanya mtu ambaye hajaingia katika ndoa.

Waasherati Ni Wale Ambao Hawajafunga Ndoa Wakifanya Ngono Wao Kwa Wao Au Wakifanya Ngono Na Wale Walio Kwenye Ndoa.

Kama kuna mtu yuko katika ndoa anapozini na mtu ambaye hayuko katika ndoa maana yake mzinzi na mwasherati wanakutana kuzini.
Aliye kwenye ndoa anapotoka nje ya ndoa yake kingono ni mzinzi na mtu ambaye hajaingia kwenye ndoa anapozini huyo ni mwasherati.
Kitendo wanachokifanya wazinzi au waasherati kinaitwa uzinifu au zinaa.

Biblia iko wazi sana kwamba uzinzi na uasherati ni dhambi na dhambi hiyo mtu asipoitubia na kuiacha anaweza kuishia jehanamu milele.

1 Kor 6:9-11 '' Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; WAASHERATI hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala WAZINZI, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana YESU KRISTO, na katika ROHO wa MUNGU wetu.''

3. Mtumishi Mabula ubarikiwe sana, naomba unisaidie tofauti ya DHAMBI, UOVU na MAKOSA.

MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA:

Dhambi ni nini?

Dhambi ni uasi kwa MUNGU.
Ni matendo yote yaliyo chukizo kwa MUNGU.

1 Yohana 3:4 " Kila mtu afanyaye dhambi,afanya uasi maana dhambi ni uasi."

Uovu ni nini?

Uovu ni dhambi iliyokomaa na kuwa ya kujirudiarudia kwa mhusika.

Uovu pia ni tabia sugu ya kishetani inayoambatana na mtu kutokana na miungu, madhabahu za giza, kufundishwa, kujifunza au kuiga.

Isaya 59:2 " lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na MUNGU wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia."

Makosa ni nini?

Makosa ni kutenda mabaya/Dhambi kwa kukusudia au kutokukusudia,kwa kutokujua au kwa kutokujua.

Lakini habari njema ni kwamba mtu akitubu kwa MUNGU katika KRISTO YESU na kuacha anasamehewa.
Mtu akitubia dhambi zake anasamehewa.

Mtu akitubia uovu wake na kuuacha anasamehewa.
Mtu akitubia makosa yake anasamehewa.

Kutoka 34:6-7 "BWANA akapita mbele yake, akatangaza, BWANA, BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe UOVU na MAKOSA na DHAMBI; wala si mwenye kumhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; mwenye kuwapatiliza watoto uovu wa baba zao, na wana wa wana wao pia, hata kizazi cha tatu na cha nne."

MUNGU akubariki sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU Baba wa mbinguni.

Comments