![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Leo tunajifunza kutokana na maswali ambayo baadhi ya marafiki zangu waliniuliza na mimi nawajibu kwa neema ya MUNGU kwa kadiri ninavyojaaliwa.
Najua maswali ni mengi sana hivyo ukiona swali lako ulilowahi kuniuliza sijakujibu basi inawezekana ipo siku nitakujibu nikipata neema hiyo.
Kwa wewe unayesoma ujumbe huu naamini yamkini kuna kitu utajifunza.
Mbarikiwa sana nyote.
Maswali ni haya.
1. Bwana Yesu asifiwe mtumishi Mabula. Nina swali naomba unisaidie.
Nnisaidie kitabu ambacho kimeandika YESU alienda kuzimu amemnyanganya shetani ufunguo wa mamlaka ni kitabu gani? Asante.
MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.
Hakuna andiko linalosema kwamba YESU amekwenda kuzimu kumnyang'anya shetani ufunuo wa mamlaka.
Mambo ya kujua ni kwamba
A. YESU KRISTO ana mamlaka yote mbinguni na duniani soma Mathayo 28:18. Na aliyempa YESU Mamlaka yote ni MUNGU Baba soma Yohana 17:2
B. YESU KRISTO ni mfalme wa ufalme wa MUNGU na ufalme wake hauna mwisho soma Luka 1:33. Mfalme lazima awe na mamlaka.
Sasa kama YESU alikwenda kumnyang'anya mamlaka shetani kwanini yeye YESU aseme hivi kwamba shetani hana Nguvu zozote kwake
Yohana 14:30 "Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu."
Andiko hili katika tafsiri ya BHN Biblia inasema
"Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Kwangu mimi hawezi kitu;"
YESU KRISTO anasema haya kipindi hajafa msalabani hata amnyang'anye mamlaka shetani kama baadhi ya watu wanavyosema.
Biblia inaonyesha kwamba YESU KRISTO alikuja duniani akiwa na mamlaka tayari.
Ona mfano wa kile mzee Yakobo alisema kuhusu YESU KRISTO miaka zaidi ya 1500 kabla YESU hajaja duniani katika mwili.
Mwanzo 49:10 ".......... Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii."
Nini nataka niseme?
YESU ana mamlaka yote na funguo zote za mamlaka yote.
Mfano hai ni kwamba YESU ana funguo za mauti na kuzimu.
Ufunuo 1:18 "na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu."
Yaani YESU ana mamlaka yote hata kwa shetani ambaye ndio mkuu wa kuzimu.
Kwa kutumia mamlaka yake yeye YESU KRISTO anaweza kufunga chochote na hayupo wa kufungua, yeye anaweza kumfungua yeyote na asiwepo wa kumfunga.
Ufunuo 3:7 "........ Haya ndiyo anenayo yeye aliye mtakatifu, aliye wa kweli, aliye na ufunguo wa Daudi, yeye mwenye kufungua wala hapana afungaye, naye afunga wala hapana afunguaye."
YESU hakwenda kuzimu kumnyang'anya shetani mamlaka bali yeye alikuwa na Mamlaka kuu tangu kabla hajaja duniani.
2. Bwana Yesu asifiwe Mtumishi wa Bwana Aliye Hai.
Ningeomba kujua tofauti kati ya uzinzi na uasherati tofauti yake iko wapi??
MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.
Hakuna tofauti ya uzinzi na uasherati.
Ila kuna tofauti ya mzinzi na mwasherati.
Uzinzi ni nini?
Uzinzi ni kitendo cha mtu aliye kwenye ndoa kufanya mapenzi na mtu yeyote nje na mwenzi wake wa ndoa.
Wazinzi Ni Wanandoa Wanaotoka kingono nje Ya Ndoa Zao.
Uasherati ni nini?
Uasherati ni kitendo cha kuzini anachokifanya mtu ambaye hajaingia katika ndoa.
Waasherati Ni Wale Ambao Hawajafunga Ndoa Wakifanya Ngono Wao Kwa Wao Au Wakifanya Ngono Na Wale Walio Kwenye Ndoa.
Kama kuna mtu yuko katika ndoa anapozini na mtu ambaye hayuko katika ndoa maana yake mzinzi na mwasherati wanakutana kuzini.
Aliye kwenye ndoa anapotoka nje ya ndoa yake kingono ni mzinzi na mtu ambaye hajaingia kwenye ndoa anapozini huyo ni mwasherati.
Kitendo wanachokifanya wazinzi au waasherati kinaitwa uzinifu au zinaa.
Biblia iko wazi sana kwamba uzinzi na uasherati ni dhambi na dhambi hiyo mtu asipoitubia na kuacha anaweza kuishi jehanamu milele.
1 Kor 6:9-11 '' Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; WAASHERATI hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala WAZINZI, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana YESU KRISTO, na katika ROHO wa MUNGU wetu.''
3. Bwana asifiwe Mtumishi Mabula , Pole na majukumu yako ya kila siku na nikupe hongera kwa kutenga muda wako na kwa kile ulichotunukiwa na Mungu kutupa elimu katika maisha yetu ya ukristo ili kujiweka tayari na ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo.
Nimekuwa nikifwatilia maandiko yako kwa kipindi kirefu kidogo,na mara nyingi kama ninakuwa na swali katika mada unazozijadili kina wakati napata majibu kutokana na comments za members ila leo nimekosa jibu na nimekuwa mzito kidogo kuuliza kutokana na maudhui ya swali lenyewe.
Umezungumzia kuhusu Dhambi ya zinaa,uzinzi na uasherati. Lakini katika maelezo yako ulifafanua zaidi na ukatumia moja ya mstari uliopo katika Biblia,mstari huo ukataja neno uzinzi,uasherati,wafiraji nk;
Hoja/Swali langu linaanzia hapa,umesema dhambi zote ni sawa,ila kuna baadhi ya mafundisho nilipata kuwahi kusikia zamani kuwa wafiraji kamwe hawatauona Ufalme wa Mungu,kwa maana ya kwamba dhambi hii haisameheki.
Tafadhali Mtumishi naomba nisiwe muongo,niliwahi kuitenda iyo dhambi na dhambi hiyo inanihukumu kila nikitafakari uhalali wa kutoingia Mbinguni kwa ajili ya hii dhambi,Dhambi hii inanitafuna hadi wakati mwingine nasema kama hakuna kuingia Mbinguni si bora niendelee na pombe,uzinzi nk kwasababu hata nifanyeje moto ni lazma unichome?!
Tafadhali mtumishi nieleweshe kuhusu hili ili nijue nini la kufanya kabla ghadhabu ya Mungu haijanishukia.
Natumai kupata ufafanuzi na maelekezo.
Asante.
MAJIBU YA MTUMISHI PETER MABULA.
MUNGU akubariki sana kwa kuwa muwazi.
Jibu la swali lako ni rahisi sana, ni kwamba ni dhambi moja tu ambayo wanadamu hawatasamehe, ni kumkufuru ROHO MTAKATIFU
Mathayo 12:31 "Kwa sababu hiyo nawaambia, Kila dhambi na kila neno la kufuru watasamehewa wanadamu, ila kwa kumkufuru Roho hawatasamehewa."
Na kumkufuru ROHO MTAKATIFU sio dhambi ya kawaida, ni kiwango cha juu cha kukufuru.
Kazi yangu leo sio kuzungumzia ilivyo dhambi ya kumkufuru ROHO MTAKATIFU ila nataka tu nikutoe wasiwasi kwamba dhambi yako ya ufiraji inasameheka kama ukitubu na kuiacha.
Hivyo hakuna jana ya kuendelea na dhambi hiyo, hakuna haja ya kunywa pombe, hakuna haja ya kuwa mzinzi au mwasherati bali tubu dhambi zote kwa Bwana YESU KRISTO na utasamehewa.
Hivyo ukiona unasikia sauti ikisema hutasamehewa kwa dhambi ya ufiraji ujue hiyo ni sauti ya shetani ili uende jehanamu kweli.
Dhambi ya ufiraji ni mbaya sana kama zilivyo dhambi zingine hivyo tubu na usirudie tena, mpokee YESU KRISTO kwa upya na ishi maisha matakatifu ya Wokovu kuanzia sasa na hakika uzima wa milele utakuhusu.
Maneno haya ni magumu kuyataja mbele za watu ila ngoja niseme tu kama Biblia inavyosema, nisamehe kama kuna mtu namkwaza kwa kuyataja hadharani maneno haya lakini kila anayehusika na kufira au kufirwa inampasa kutubu haraka na kuiacha mara moja dhambi hiyo chafu sana.
Kufira au kufirwa ni dhambi mbaya sana ila ukitubu na kuiacha unasamehewa.
1 Wakorintho 6:9-11 " Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala WAFIRAJI, wala WALAWITI, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana YESU KRISTO, na katika ROHO wa MUNGU wetu."
Biblia inasema "baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii"
Kumbe baadhi ya waliookoka sasa zamani walikuwa wafiraji au walawiti n.k lakini walipompokea YESU KRISTO na kutubu walioshwa kwa damu ya YESU KRISTO na kutakaswa na kuhesabiwa haki, hivyo ukitubia dhambi hiyo na kuiacha unatakaswa na kuhesabiwa haki na MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.
Asikudanganye mtu kwamba hutasamehewa bali tubu na kuacha hakika MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi atakusamehe.
MUNGU akubariki sana.
*******************************
Sehemu ya pili ya maswali na majibu itaendelea baadae.
***********************************
Naamini kuna kitu umejifunza, nakuomba ishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU na utamuona MUNGU.
MUNGU akubariki sana
By Peter Mabula mtenda kazi katika shamba la MUNGU.

Comments