MFANYE MTOTO WAKO KUWA MALI YA MUNGU.

Na Mwl Peter Mabula akiwa na Baba yake kiroho Mchungaji Elly Botto(hayati) katika safari za Injili mwaka 2023. Mchungaji Elly Botto alitwaliwa na Bwana YESU KRISTO mwezi February 2024.


Na Mwl Peter Mabula.

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Natamani kila mmoja asome somo hili hadi mwisho na kuzingatia.

✓✓Ni muhimu kujua kwamba roho ya mtoto ni mali ya MUNGU kama ambavyo roho ya mzazi ni mali MUNGU.

Ezekieli 18:4 "Tazama, roho zote ni mali yangu; kama vile roho ya baba ni mali yangu, ndivyo ilivyo roho ya mwana mali yangu; roho ile itendayo dhambi itakufa."

◼️Mtoto wako sio mali yako bali ni mali ya MUNGU hivyo mfundishe kumcha MUNGU katika KRISTO YESU ili mtoto wako alitimize kusudi la MUNGU la kumleta duniani mtoto huyo.

◼️Hakuna mtoto ambaye huzaliwa kwa sababu tu wazazi wake wametaka bali mtoto huzaliwa kwa sababu MUNGU amemleta mtoto huyo duniani kwa kusudi maalumu, hivyo ni jukumu la mzazi kumsaidia mtoto wake alitimize kusudi la MUNGU katika KRISTO YESU.

✓✓Mzazi jifunze kumfanya mtoto wako kuwa mali ya MUNGU, maana ni MUNGU ndie aliyemuumba mtoto wako.

Zekaria 12:1 "Ufunuo wa neno la BWANA juu ya Israeli. Haya ndiyo asemayo BWANA, azitandaye mbingu, auwekaye msingi wa dunia, aiumbaye roho ya mwanadamu ndani yake."

Wazazi wengi wamewaachia watoto wao ili wawe mali ya shetani, ni hatari sana.

✓✓Mzazi ndiye mwalimu wa kwanza wa mtoto, hivyo mfundishe mtoto wako kumtambua YESU KRISTO kama Mwokozi wake.

✓✓Kumbuka Mtoto hujifunza kwanza kwa mzazi wake, mtoto hujifunza zaidi kwa wazazi wake, sasa ni hatari sana kama mzazi husika hamchi MUNGU, kuna hadi wazazi wengine wamewafundisha watoto wao kwenda kwa waganga wa kienyeji na sio kwa YESU.
Mfano hai ni hawa
2 Wafalme 17:17-18 " Wakawapitisha watoto wao, waume na wake, motoni, wakapiga ramli, wakafanya uchawi, wakajiuza nafsi zao wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa BWANA, hata kumkasirisha. Kwa hiyo BWANA akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake; wala hapana aliyesalia ila kabila ya Yuda peke yake."

Kila ambacho mzazi hapendi ni ni rahisi kwa mtoto kuacha.

Mtoto anaweza kujifunza tabia mbaya kutoka kwa mzazi wake.

◼️Ndugu, weka msingi wa kumfundisha mema mtoto wako akiwa mdogo kiumri maana ukitaka umfundishe akiwa mkubwa utashindwa.

Kumbuka msemo huu “mkunje samaki angali mbichi”

NAMNA YA KUMFANYA MTOTO WAKO AWE MALI YA MUNGU;

1. Wafundishe watoto wako kumcha MUNGU.

Kumbu 4:10 " .......... BWANA aliponiambia, Nikusanyieni watu hawa, nami nitawasikizisha maneno yangu, ili wajifunze kunicha mimi siku zote watakazoishi duniani, wakapate na kuwafundisha watoto wao."

✓✓MUNGU anataka sisi tumche yeye na tuwafundishe watoto wetu kumcha yeye.

✓✓Kumcha MUNGU ni kumuogopa MUNGU ili usimkosee.

✓✓Kumcha MUNGU ni kumpenda MUNGU na kufanya akitakacho.

✓✓Kumcha MUNGU ni kujitenga na mabaya huku ukiambatana na KRISTO YESU Mwokozi.

◼️Hakikisha unawafundisha watoto wako kumcha MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.

Mithali 14:26 "Kumcha BWANA ni tumaini imara; Watoto wake watakuwa na kimbilio."

2. Wafanye watoto wako wayaone matendo ya MUNGU.

Zaburi 90:16 "Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, Na adhama yako kwa watoto wao."

◼️Adhama maana yake ni jambo kubwa la heshima na la fahari kubwa, hivyo wafanye watoto wako wayaone matendo ya MUNGU yanayompa MUNGU utukufu.

MUNGU amekutendea nini?

✓✓ Kifunue hicho kwa watoto wako ili na wao wajue ni MUNGU ndiye anaweza kutenda miujiza hiyo.

✓✓Waambie hata kwamba ni MUNGU ndiye amekuumbia watoto wazuri, kama YESU alikuponya usisite kuwaambia watoto wako ili wajue namna ya kujua kazi za MUNGU.

Umeenda safari au kazini na umerudi salama, hiyo ni kazi ya MUNGU na ni muujiza wa MUNGU, wajulishe Watoto wako.

Huumwi, una kazi, familia ina amani, ndugu zenu wako Salama, mna mali fulani n.k hivyo vyote ni kazi ya MUNGU na miujiza ya MUNGU hivyo siku zote wafanye watoto wako wayaone matendo ya MUNGU ili wajifunze kumcha MUNGU, kumtegemea na kumtukuza.

✓✓Onyesha wakati mwingine hata tendo la imani Kanisani kwa kutoa sadaka ya shukrani kwa kile MUNGU ametenda, watoto wako wataona na watajua matendo makuu ya MUNGU.

3. Wafanye kila mtoto wako kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake binafsi wa maisha yake.

Marko 10:14 "Ila YESU alipoona alichukizwa sana, akawaambia, Waacheni watoto wadogo waje kwangu, msiwazuie; kwa maana watoto kama hawa ufalme wa MUNGU ni wao."

◼️Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi ndilo jambo kuu na muhimu kuliko yote kwa kila Mwanadamu aliyeko Duniani.

Habari njema ni kwamba YESU KRISTO anawapenda watoto ndio maana kwenye maandiko anasema kwamba  waachwe watoto wadogo ili waende kwake.

✓✓YESU anawahitaji watoto hivyo wafanye watoto wako kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wao.

✓✓Hata wewe hakikisha YESU KRISTO ni Mwokozi wako binafsi na hiyo itawahamasisha zaidi watoto wako kuhakikisha YESU anakuwa Mwokozi wao pia.

Hiyo itakuwa faida kwao na kwako pia.
Leo kuna watoto baada ya kukua wanatoa kafara wazazi wao ili watajirike, hiyo ni kwa sababu hao watoto hawana YESU na hawakuwa na YESU tangu utotoni mwao.

Kuna kipindi kwenye vyombo vya habari niliona habari ikisema kijana mmoja kambaka mama yake mzazi ili atajirike baada ya kuambiwa na mganga wa kienyeji, siku nyingine nikaona habari kwamba kijana mmoja amemkata ulimi mama yake mzazi ili apeleke kwa mganga awe tajiri. Haya ni baadhi ya madhara ya watu kutokuwa na YESU, inawezekana mtoto wa namna hiyo tangu utotoni mwake anafundishwa kwenda kwa waganga wa kienyeji na sio kwenda Kanisani, hadi mtoto huyo anakuwa mtu mzima anajua msaada ni kwa waganga wa kienyeji, sasa kwa sababu waganga wa kienyeji ni mawakala wa shetani sasa wanampa masharti ya kuua wazazi wake, yaani kosa la mzazi linakuja kumsababishia kifo, ni hatari sana.

◼️Ndugu, hakikisha wewe unawafanya watoto wako kuokoka na kumpokea YESU kama mwokozi wao binafsi.

Nina maana kubwa sana ninaposema kwamba wafanye watoto wako YESU KRISTO awe Mwokozi wao binafsi, maana kuna watoto leo wana YESU wa baba zao tu hivyo baba zao wakiondoka na wao wanamwacha YESU maana hakuwa wao binafsi ila alikuwa wa baba zao tu.

Leo kuna watu wanamwabudu MUNGU wa wazazi wao, hawajamfanya kuwa MUNGU wao ndio maana wazazi wakifariki tu ujue na watoto wanaachana na MUNGU maana alikuwa tu MUNGU wa wazazi wao na sio wao.
Sasa wewe wafanye watoto wako wasiambatane tu na YESU wako bali wamfanye huyo YESU KRISTO awe YESU wao pia.

Leo kuna wachungaji wanamtumikia YESU vizuri sana na watoto wao kila siku wako nao Kanisani lakini watoto hawa MUNGU hajawa MUNGU wao ila wanamwabudu kwa sababu tu ni MUNGU wa baba zao, miaka ya  baadae ya Mchungaji kufariki ukiambiwa kwamba hawa ni watoto wa yule aliyekuwa Mchungaji mwenye upako utakataa maana baada ya Baba yako Kufariki wamekuwa zaidi ya watu wa kidunia yaani kama kungekuwa na tuzo za wazinzi bora au walevi bora au makahaba bora hakuna ambaye angewashinda.

◼️Ndugu hakikisha watoto wako wanampokea YESU kama Mwokozi wao binafsi, Naamini kila Mtu anasema ujumbe huu amenielewa.

4. Wafundishe watoto wako Neno la MUNGU.

Kumbu 6:7 "nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo."

✓✓Biblia inasema uwafundishe watoto wako neno la MUNGU.

✓✓Tena Biblia inasema uwafundishe watoto wako Neno la MUNGU kwa bidii.

Ndugu, hakikisha unawafundisha watoto kwa bidii Neno la MUNGU katika Wokovu wa KRISTO YESU.

Mtoto ni mtoto tu hivyo katika kumfundisha wakati mwingine anaweza kupuuzia au kutokuzingatia ila ili kumwepusha na kuzimu na jehanamu basi hata ukiwa mkali kidogo sio jambo baya.

Mithali 23:13-14 " Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa. Utampiga kwa fimbo, Na kumwokoa nafsi yake na Kuzimu."

◼️Usimlee kama yai asije akakudharau  asizingatie mafundisho yako, bali ikibidi tumia hata fimbo kidogo ili mtoto azingatie Neno la KRISTO litakalomsaidia maisha yake yote.

5. Uwe mwenye haki unayeenenda kwa unyoofu ili watoto wako wabarikiwe badala yako.

Mithali 20:7 "Mwenye haki aendaye katika unyofu wake, Watoto wake wabarikiwa baada yake."

✓✓Hii ni ahadi ya MUNGU ya ajabu sana kwamba wewe mzazi ukiishi maisha matakatifu ya haki huku ukienenda katika unyoofu wa ki MUNGU watoto wako watabarikiwa hata baada ya wewe kuondoka duniani.

Ibrahimu aliishi kanuni hii ndio maana watoto wake walibarikiwa baada yake.

Hii ni ahadi ya MUNGU kuwabariki watoto wako hata baada ya wewe kuondoka duniani.

Sasa kuna wazazi wakiondoka duniani huwaachia matatizo na adhabu za kiroho na kimwili watoto wao, kuna wazazi wakiondoka duniani huwaachia madeni na kesi watoto wao.
Kuna watu leo wanateseka leo na kutafuta maombezi kwa sababu tu wazazi wao walitambika na kuwaachia kufuatiliwa na mizimu,majini, laana na vifungo mbalimbali.

Ndugu, kama ni wewe ndio wewe unatesawa na nguvu za giza kwa sababu ya makosa ya wazazi wako nakuomba mkimbilie YESU KRISTO leo kwa kuokoka na hizo nguvu za giza na laana vitakuachia, havitakufuata tena, baada ya hapo wafundishe Watoto wako haya niliyofundisha Leo, usirudie kosa la wazazi wako hata wakakuachia mizimu ambayo unapambana nayo kimaombi.

1 Yohana 1:7 "bali tukienenda nuruni, kama yeye(MUNGU) alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote."

Lakini pia kwa sababu umeona madhara yaliyokupata wewe hakikisha wewe unaishi maisha matakatifu ya wokovu na haki na unyoofu ili watoto wako wabarikiwe baada yako.

Ishi maisha ya haki na unyoofu ili watoto wako wabarikiwe baada yako.

6. Wafundishe watoto wako tabia njema.

Waefeso 6:4 "Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya BWANA."

✓✓MUNGU anaagiza uwalee watoto wako katika adabu nzuri.
Adabu maana yake ni tabia njema hivyo MUNGU anakutaka uwalee watoto wako katika tabia njema.

MUNGU anataka uwaonye watoto wako ili wawe wenye Adabu kama Neno la MUNGU linavyofundisha.
Tabia njema itawapa vibali na upendeleo hata wakati wakiwa watu wazima.
Mfano hai ni huu;
Mithali 11:16 "Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; ......."

◼️Kama mtoto wako wa kike akiwa hana adabu yaani tabia njema ni nani atamheshimu?

Jibu ni hakuna, hivyo heri mfundishe tabia njema tangu akiwa mdogo ili akiwa mkubwa aheshimiwe na watu hata na mume wake.

7. Nenda na watoto wako wote Kanisani.

Waebrania 10:25 "wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia."

Agizo la MUNGU ni kwamba tusiache kwenda Kanisani, tusiache ibada.
Sasa jitahidi sana uwe mtu wa ibada na wafundishe watoto wako ili wawe watu wa ibada.

✓✓Wafundishe wahudhurie mafundisho Kanisani, wafundishe kuomba, wafundishe kumtumikia Bwana YESU KRISTO.
Hata wewe jitahidi uwe kielelezo chema cha kwenda Kanisani kumwabudu MUNGU.

Usiwe unaenda Kanisani peke yako huku watoto wako umewaacha nyumbani.
Wafundishe watoto wako kumwabudu MUNGU na kumtumikia Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
Nenda ibadani ukiwa na watoto wako.

Jifunze kwa Musa na Waisraeli ambao hawakutana kuwaacha vijana wao na binti zao Misri, bali walikwenda nao kumwabudu MUNGU.
Kutoka 10:9 "Musa akamjibu, Tutakwenda na vijana wetu na wazee wetu, na wana wetu, na binti zetu, tutakwenda na kondoo zetu na ng'ombe zetu; kwa kuwa inatupasa kumfanyia BWANA sikukuu."

Ndugu nakuomba zingatia hayo mambo saba yote ili kumfanya mtoto kuwa kuwa mali ya MUNGU aliyemleta mtoto huyo duniani.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, kuandika meseji na hadi whatsapp).

Comments