![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.
◼️Ewe Mkristo, kuhubiri Injili ya KRISTO lifanye kuwa ni jukumu lako.
Hakikisha kila mwanadamu anaipata injili ya KRISTO YESU inayookoa.
Warumi 12:11 "kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia BWANA;"
Hili ni agizo la MUNGU kwa Kanisa lake Duniani.
Kumbuka MUNGU anatumia watu wake hivyo kama wewe una uhakika ni mwana wa MUNGU kupitia YESU KRISTO basi hubiri injili ya KRISTO kwa watu wote wanaokuzunguka.
◼️Hubiri wewe mwenyewe na hubiri kwa pesa zako maana wapo walio tayari kwenda kuhubiri mbali lakini nauli tu hawana, MUNGU anataka wewe uhusike na Injili kuhakikisha hiyo Injili ya KRISTO inaenda kila mahali.
Je maisha yako ya Ukristo unayatumiaje?
✓✓Ndugu nakushauri maisha yako ya Ukristo yatumie kupeleka faida kwa MUNGU.
Wakolosai 1:10 ''mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa Bwana, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya MUNGU;"
✓✓Yatumie maisha yako kumwinua MUNGU.
Yohana 15:8-9 " Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu. Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu."
✓✓Yatumie maisha yako kumhubiri KRISTO tu kwa watu wote.
2 Wakorintho 4:5 "Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali KRISTO YESU ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya YESU."
◼️Ndugu, inakupasa kuifanya kazi ya MUNGU sasa maana kuna kipindi itafika hutaweza, hutakuwa na nguvu na hutakuwa na wakati kama wa sasa.
Siku Moja Mimi Peter Mabula kwenye maono niliona kitu cha ajabu sana, nilisikia sauti ikinielezea ikisema "Kila mwanadamu na wakati wake wa kuishi, akina Daudi na akina Danieli walikuwa na wakati wao, wakati wao ulipoisha waliondoka duniani, hata wewe una wakati wako, hata ukiishi miaka 60 ijayo bado wakati wako duniani utaishi na itakupasa kuondoka duniani, mtumikie KRISTO sana katika wakati wako"
◼️Nillishangaa sana maono hayo, ndugu zangu wakati huu ukiwa hai ndio wakati wa kumtumikia Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu, wakati ukiwa na nguvu mtumikie Bwana YESU, hubiri injili wewe mwenyewe na sapoti wapeleka injili ili injili iende kila eneo.
✓✓Hakikisha injili ya KRISTO inafika kila eneo.
Warumi 1:8 "Kwanza namshukuru MUNGU wangu katika YESU KRISTO kwa ajili yenu nyote, kwa kuwa imani yenu inahubiriwa katika dunia nzima."
Inawezekana Wewe una kiu ya kuipeleka Injili ya KRISTO kwa watu wengi sana ila Kuna Maadui wa rohoni na mwili wanakuzuia, Ndugu usikubali kuzuiliwa kuipeleka Injili ya KRISTO YESU mbele.
Haijalishi una maadui wangapi wanaokupinga, kukuzuia, wanaojaribu kukudhuru, wanaokuwazia mabaya, wanaotumia nguvu za giza, wewe usiwaangalie hao wanaotokana na mipango ya kuzimu bali tafuta nguvu za MUNGU huku ukiendelea kumtumikia Bwana YESU KRISTO Mwokozi maana utayaweza mambo yote kama YESU akikupa nguvu.
Wafilipi 4:13 "Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu."
Utayaweza mambo yote kama ROHO MTAKATIFU akiwa pamoja na wewe.
✓✓Ndugu, kuna maelfu ya watu wanasubiri kuokoka ila hakuna mtenda kazi wa KRISTO wa kuwahubiria na kuwaongoza katika kweli yote ya Neno la MUNGU.
Ngoja nikupe ushuhuda wangu huu, Mwaka mmoja baada ya Kuokoka nilikopa benki milioni 2 kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa, huo ndio ulikuwa mkopo wangu wa kwanza kukopa benki. Namshukuru MUNGU wa Mbinguni tangu wakati huo hakuniacha, alitenda Muujiza kwa Kanisa lile, alinipa Neema nikalipa mkopo ule kwa haraka na Kuna baraka nyingi zimeyafuata Maisha yangu Wala sikupungukiwa.
Furaha yangu moyoni ni kwamba namshukuru MUNGU maana kwa utoaji ule nilimtumikia.
✓✓Kama mteule wa KRISTO, unapotumia muda wako kwa mambo mema kuhusu maisha yako kumbuka pia na kumtumikia MUNGU.
Hata mimi naendelea kumtumikia MUNGU katika KRISTO YESU.
Wakolosai 1:28-29 " ambaye sisi tunamhubiri habari zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika KRISTO. Nami najitaabisha kwa neno lilo hilo, nikijitahidi kwa kadiri ya kutenda kazi kwake atendaye kazi ndani yangu kwa nguvu."
MUNGU akukumbuke na kukubariki.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la MUNGU wa Mbinguni.
+255714252292
Ubarikiwe.

Comments