MKRISTO KUHUSU MADHABAHU ZA GIZA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



  Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.

Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU.

Namshukuru ROHO MTAKATIFU kwa ufunuo huu na natamani kila mtu asome somo hili hadi mwisho maana ni muhimu sana.

◼️Leo tunajifunza Neno la MUNGU aliye hai na jinsi MUNGU anatutaka tufanye kuhusu madhabahu za giza  ila hasa katika somo hili nitajielekeza katika nini ufanye juu ya madhabahu za giza.

✓✓Madhabahu za giza zipo na zimejengwa ama na wanadamu wanaompenda shetani au zimejengwa na mawakala wa kuzimu.

✓✓Mfano mmoja wapo ni huu   ''Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; ......... Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, sawasawa na machukizo ya mataifa ......akamjengea Baali(shetani) madhabahu, akafanya Ashera kama alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Akajiinama mbele ya jeshi lote la mbinguni na kulitumikia.-2 Wafalme 21:1-3''

✓Neno madhabahu za giza lina maana zifuatazo;

a. Madhabahu za giza ni mahali ambapo vitu kutoka ulimwengu wa roho wa giza hupitia kabla ya  kuja kwenye ulimwengu wa mwili.

b. Madhabahu za giza ni mahali ambapo vitu vya kishetani hutengenezwa ili viwaletee madhara watu.

c. Madhabahu za giza ni sehemu ambapo mawakala wa shetani hujiimalisha, hupata nguvu zao za kipepo, hufanya vikao na hupanga mipango yao ya kipepo.

d. Madhabahu za giza  ni mahali ambapo shetani au  ujumbe wa shetani hukutana na wanadamu wanaompenda shetani ili lifanyike jambo la kishetani.

e. Madhabahu za giza ni mahali ambapo wakuu wa giza, wanadamu wanaotumika kipepo, majini, mizimu na kila mapepo hukaa kama kituo chao kikuu kabla ya kuwavamia wanadamu. 

f. Madhabahu za giza ni mahali ambapo shetani huabudiwa.

g.  Madhabahu za giza ni eneo linalojengwa na mawakala wa kuzimu  kwa ajili ya kutolea kafara  za kipepo au kufanyia kafara za kipepo. 

Mfano ni huu Zaburi 106:37 '' Naam, walitoa wana wao na binti zao Kuwa dhabihu kwa mashetani. ''

 Madhabahu za giza ziko  katika makundi mengi, baadhi ya makundi hayo ni.

1. Madhabahu za giza za jamii, familia, ukoo au kabila.

✓✓Hivyo kama unatokea katika jamii hiyo inakupasa sana kujitenga na madhabahu za giza za jamii hiyo.

Hizi zinaweza kuhusisha kabila au ukoo n.k.

Mawakala wa shetani wana  mbinu nyingi za kufanya ili  watu wa ukoo huo au jamii hiyo waunganishwe na madhabahu hiyo ya giza, mojawapo ya njia za kuunganishwa na madhbahu za giza ni kupitia vitovu wakati wa kuzaliwa.

Ezekieli 16:3-5 ''.................  Asili yako na kuzaliwa kwako kwatoka katika nchi ya Mkanaani; Mwamori alikuwa baba yako, na mama yako alikuwa Mhiti.   Na katika habari za kuzaliwa kwako, siku ile uliyozaliwa, kitovu chako hakikukatwa, wala hukuoshwa kwa maji usafishwe; hukutiwa chumvi hata kidogo, wala hukutiwa katika nguo kabisa. Hapana jicho lililokuhurumia, ili kukutendea lo lote la mambo hayo kwa kukuhurumia; lakini ulitupwa nje uwandani, kwa kuwa nafsi yako ilichukiwa, katika siku ile uliyozaliwa.''  

✓✓Yako makabila au ukoo au familia mtoto yeyote anapozaliwa kitovu huchukua bibi au babu kwa ajili ya kufanyia ushirikina hata kama hawasemi hilo mbele ya wazazi wa mtoto.

Kuna njia nyingi  zinaweza kuimalisha madhabahu ya giza.

Sio kitovu tu ndio njia hutumika kuwaunganisha watu wa ukoo huo na madhabahu za giza, bali ni zaidi ya njia moja, baadhi ya njia hizo za kipepo za kuwaunganisha watu na madhabahu za giza za ukoo au kabila ni ukeketaji, tohara, kuchukuliwa nywele za kwanza za mtoto, kuchaguliwa wakala wa shetani aliyepakwa madawa mikononi ili awe ndiye mtu wa kwanza kushika mtoto baada ya kuzaliwa na kutoka hospitali, n.k 

 Wakati mwingine imekuwa ni vigumu sana watu wa ukoo fulani kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi, kwa sababu tu ya mungu wa ukoo huo aliye na madhabahu zake za giza katika ukoo huo.

2. Madhabahu za giza za maeneo fulani,mji au taifa.

◼️Hivyo kama unaishi eneo hilo au mji huo, au nchi hiyo inakupasa sana  kujitenga mbali na madhabahu hizo za giza.

Mfano ukisoma 1 Wafalme 11:33 Biblia inasema hivi ''kwa sababu wameniacha mimi wakaabudu Ashtorethi, mungu mke wa Wasidoni, na Kemoshi, mungu wa Wamoabi, na Milkomu, mungu wa wana wa Amoni wala hawakuenda katika njia zangu, kutenda mema machoni pangu, kuzishika sheria zangu na hukumu zangu, kama Daudi baba yake.'' 

Tujanifunza nini?

Ni kwamba nchi ya Sidoni watu wake walikuwa wanatawaliwa na wakala wa shetani kutoka kuzimu aitwaye Ashtorethi ambapo alijulikana kama  mungu mke wa Wasidoni.

Huyu mkuu wa giza alitawala eneo la Nchi ya Sidoni na aliwatawala Kabila la wasidoni. Sasa inawezekana na wewe kuna jini amejigeuza mungu kwa miaka mingi katika nchi yako au kabila lako na wewe sasa umepata neema ya kuokolewa na Bwana YESU hakika unatakiwa ujitenge mbali kimaombi na vitendo na huyo mungu wa taifa au wa mji au kabila unalotoka.

Huyo  Ashtorethi alikuwa amefunga watu wale na alikuwa na madhabahu zake za giza na makuhani wa madhabahu hizo za giza, hivyo wako watu wengi walikuwa wamejiunganisha na madhabahu zile na kumbe ni madhabahu ya mungu mke aitwaye Ashtorethi ambaye ni roho ya kuzimu.

Vipi kama kuna miungu ya kabila lako au familia yako au ukoo wako  au taifa lako au mkoa wako? Hakika unatakiwa ujue namna ya kuharibu madhabahu hizo za giza maana wewe sasa umeokolewa na YESU KRISTO Mwokozi.

Wakati mwingine imekuwa ni vigumu sana watu wa taifa fulani kuokoka, kwa sababu tu ya mungu wa taifa hilo aliye na madhabahu zake za giza katika eneo hilo.
Wakati mwingine imekuwa ni vigumu sana watu wa kabila fulani kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi, kwa sababu tu ya mungu wa kabila hilo aliye na madhabahu zake za giza katika kabila hilo.

 Wakati mwingine imekuwa ni vigumu sana watu wa eneo  fulani kuokoka, kwa sababu tu ya mungu wa eneo  hilo aliye na madhabahu zake za giza katika eneo hilo.

✓✓Unaweza kujikuta katika vita kubwa ya kiroho na kumbe ni madhabahu za giza zinajaribu kukumiliki, ndugu usikubali hata siku moja bali ambatana na YESU KRISTO Mwenye ushindi kwako kila muda ukimuomba MUNGU wa mbinguni kupitia yeye. 

Maandiko hayo  juu  pia yanaonyesha kwamba katika nchi ya Moabu alikuwepo mungu wa wamoabu aitwaye Kemoshi, hivyo mtu wa kutoka eneo hilo au nchi hiyo kama ameokoka anatakiwa kujitenga mbali na madhabahu za giza za Kemoshi ambaye ni roho ya kuzimu.

✓✓Katika eneo la wana wa Amoni kulikuwa na mungu wao aitwaye
Milkomu, Ukiona neno ''mungu'' ujue ni roho ya kuzimu yaani shetani au wasaidizi wa shetani waliojigeuza ili waabudiwe, hao ni maraoho wa kuzimu na siku zote hao wako kinyume na MUNGU wa kweli ambaye ni JEHOVA aliyejifunua tu kupitia YESU KRISTO Mwokozi.

Yohana 1:18 '' Hakuna mtu aliyemwona MUNGU wakati wo wote; MUNGU Mwana pekee aliye katika kifua cha BABA, huyu ndiye aliyemfunua. ''

3. Madhabahu za giza za kidini.

Madhabahu hizi zinaweza kuhusisha dini isiyo na nuru ya KRISTO YESU, au dhehebu ambalo viongozi wake ni mawakala wa shetani, au Kanisa la mahali lakini Mchungaji wa hapo ni wakala wa shetani na anaitumikia madhabahu ya shetani inayotenda kwa siri sana kupitia mgongo wa dini.

 ◼️Wakati mwingine imekuwa ni vigumu sana watu wa dini  fulani kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi, kwa sababu tu ya mungu wa dini hiyo wa kutoka kuzimu aliye na madhabahu zake za giza katika dini hizo.

Watumishi wa madhabahu za kidini za kishetani Biblia inawazungumzia kwa namna tofauti, ona mfano huu ambapo Biblia kwa ukali sana inasema juu ya watendakazi wa madhabahu za kishetani za kidini, Biblia katika maandiko haya inaanza kuwa kuwaita hao kuwa ni kama wanyama tu '' Lakini hao kama wanyama wasio na akili, ambao walizaliwa kama wanyama tu wa kukamatwa na kupotezwa, wakikufuru katika mambo wasiyoyajua, wataangamizwa katika maangamizo yao; Wakipatikana na madhara, ambayo ni ujira wa udhalimu wao, wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa; wamekuwa ni mawaa na aibu wakifuata anasa zisizo kiasi katika karamu zao za upendo, wafanyapo karamu pamoja nanyi; wenye macho yajaayo uzinzi, watu wasiokoma kutenda dhambi, wenye kuhadaa roho zisizo imara, wenye mioyo iliyozoezwa kutamani, wana wa laana; wakiiacha njia iliyonyoka, wakapotea, ..............
  Hawa ni visima visivyo na maji, na mawingu yachukuliwayo na tufani, ambao weusi wa giza ni akiba waliyowekewa. Maana wakinena maneno makuu mno ya kiburi, kwa tamaa za mwili na kwa ufisadi huwahadaa watu walioanza kuwakimbia wale wanaoenenda katika udanganyifu; wakiwaahidia uhuru, nao wenyewe ni watumwa wa uharibifu, maana mtu akishindwa na mtu huwa mtumwa wa mtu yule. Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua Bwana na Mwokozi YESU KRISTO, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza. -2 Petro 12-20 ''

✓✓Ndugu, madhabahu za giza zipo ili kukuondolea haki zako kiroho, kukuzuia kufanikiwa kiroho na kimwili na madhabahu hizo zipo ili kukuzuilia uzima wa milele, hivyo kama umeshaokolewa na YESU KRISTO usikubali kamwe kuzifuata madhabahu za giza wala kuzitii.

◼️Sasa ili uzishinde madhabahu za kishetani ni lazima muunganiko wa kipepo kati yao na hizo madhabahu za giza uvunjike.

✓✓Madhabahu za giza ukiziruhusu maishani mwako zitafuta uhusiano wako na MUNGU aliyeziumba mbingu na nchi.

✓✓Madhabahu za giza zinatakiwa kubomolewa lakini ndugu  huwezi kuzibomoa madhabahu za giza  kama hujajitakasa katika KRISTO YESU, Hivyo mpokee kwanza YESU kama hujampokea, tubu na acha dhambi ndipo utaweza kuzibomoa na kuzivunja madhabahu za giza.

Yohana 8:12 ''Basi YESU akawaambia tena akasema, Mimi ndimi nuru ya ulimwengu, yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe, bali atakuwa na nuru ya uzima.''

✓✓Huwezi kuzibomoa madhabahu za kishetani kama bado na wewe uko ndani ya utawala wa kishetani, inakupasa kuhama kwanza kwa shetani ndipo utaweza kuziharibu madhabahu za giza, ukihama kwa shetani sehemu salama ya kwenda ni kwa YESU KRISTO tu.

◼️Habari njema ni kwamba Bwana YESU anapokuokoa  MUNGU hukuhamisha  kutoka utawala wa shetani na sasa unakuwa katika utawala wa YESU KRISTO.

Wakolosai 1:13 '' Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;''

◼️Habari njema ni kwamba ukikubali YESU KRISTO akuokoe uwe na uhakika kabisa kwamba  utakuwa umehamishwa kutoka ufalme wa giza na sasa utakuwa ufalme wa nuru, na habari njema nyingine ni kwamba ukiokoka unakuwa juu ya falme za giza na madhabahu za giza ili kuzing'oa, kuzibomoa, kuziharibu na kuziangamiza kisha wewe unapanda ufalme wa MUNGU na kuujuenga ufalme wa MUNGU katika maeneo hayo.

Yeremia 1:10 '' angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.''

Ukiokolewa na YESU KRISTO hakikisha unazingatia yafuatayo.

Kumb 18:9-14 '' Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale. Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA; kisha ni kwa sababu ya hayo BWANA, Mungu wako, anawafukuza mbele yako. Uwe mkamilifu kwa BWANA, Mungu wako. Maana mataifa haya utakaowamiliki huwasikiliza wanaoshika nyakati mbaya na kutazama bao; bali wewe, BWANA, Mungu wako, hakukupa ruhusa kutenda hayo. ''

1. Usiende kwa waganga wa kienyeji, usiague, usitambike, usiwe mbashiri wa kipepo wala usiwe msihiri tena jitenge mbali na kila maroho wa kuzimu.

2. Usiroge wala usiwe mpandisha mapepo.

Funguliwa kutoka mapepo na usiwaruhusu kukufuata tena kamwe.

3. Usiwe Mchawi tena usiwaombe wafu lolote lile.

Wanadamu wote ambao walishafariki wakiwemo akina Musa, Eliya, Mariamu, Petro, Yohana n.k huruhusiwi kuwaomba lolote, ukiwaomba ujue wewe ni mwabudu shetani.

Biblia hapo juu inasema ''bali wewe, BWANA, Mungu wako, hakukupa ruhusa kutenda hayo.''

✓✓MUNGU hajakupa kibali cha kushirikiana na makuhani wa kichawi wala watu waliokufa.

 ✓✓MUNGU hajakupa kibali cha kushirikiana na waganga wa kienyeji wala wasoma nyota.

✓✓MUNGU hajakupa kibali cha kuomba wafu wala kuomba wanyama wala sanamu.

Ndugu jitenge mbali na maroho wa kuzimu na jitenge mbali na madhabahu zao.

Kazi za hao maroho wa kuzimu ambao ni majini au mizimu ni kukuchunguza, kukuteka kiroho, kusimamisha maombi yako, kuiba pesa zako au uchumi wako n.k

Majini kazi yake kwako ni kukufanya uwe na tabia za dhambi, kazi zao zingine ni pamoja na kufanya ngono na wewe ndotoni na njia hiyo ni njia yao ya kukufunga maagano na kukuzuilia kuingia katika ndoa halali na kukuzuilia uzao na kukuletea magonjwa.

Watu wanaotumiwa na majini huwa wanapenda sana vita ya kimwili inayoendeshwa na majini katika ulimwengu wa roho yakiwa ndani yao.

◼️Ndugu hakikisha nuru ya KRISTO YESU inaangaza maishani mwako, kwenye familia yako na kwenye ukoo wako bila kusahau kwenye maeneo yako.

Ili ushinde madhabahu za giza lazima umkaribishe YESU KRISTO maishani mwako, utubu dhambi na kuziacha, ujitakase na kujiweka wakfu kwa MUNGU, na takasa kwa damu ya YESU KRISTO maeneo ambayo ziliwahi kutolewa kafara za kishetani.

Nini ufanye juu ya madhabahu za giza?

Andiko hili linakujulisha juu ya mambo manne(4) ya kwanza.

Kumbu 7:5 '' Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga.''

1. Vunja madhabahu za giza kwa maombi ya vita kwa kutumia Damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.

2. Bomoa nguvo zilizobeba madhabahu hizo za giza.

3. Kata maashera ya hiyo madhabahu.

4. Teketeza kwa moto sanamu zao zote.

Mambo matatu mengine yanayofuata katika maombi yako ya kuharibu madhabahu za giza ni haya.

Kumb 12:2-3 ''Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi;  nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo.''

5. Vunja na kupaharibu mahali walipoziweka madhabahu zao za kishetani, iwe madhabahu hizo waliweka kwenye milima au kwenye vilima au kwenye miti au ppote.

6. Futa jina lao mahali hapo au mawakala wa shetani wenye madhabahu za giza.

Iwe wapo kwenye eneo au kwenye kabila lako au eneo lako n.k hakikisha unafuta jina lao hapo

7. Jitenge na madhabahu hizo za giza huku ukifuta maagano yote yaliyofanyika katika madhabahu hizo.

Futa maagano hayo kwa damu ya YESU KRISTO.

Ufunuo  12:11 ''Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao;   ...... ''

 MUNGU akubariki na nitakuandalia kitabu kinachofafanua zaidi juu ya namna ya kuziharibu madhabahu za giza.
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Hadi whatsapp).

Comments