MKRISTO SAFI LAZIMA AWE NA MSIMAMO SAFI WA KIROHO.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu yangu.
Karibu sana nikujuze Neno la MUNGU aliye hai.

◼️Ili Mkristo aifikie hatima njema lazima awe na msimamo.



Msimamo wa kiroho wa Mkristo ni nini?

✓✓Msimamo wa kiroho kwa Mkristo ni hali ya kuishi akilifuata Neno la MUNGU kiasi ambacho hakuna wa kumtoa ili aende kinyume na Neno la MUNGU.

✓✓Mkristo safi lazima awe na msimamo safi wa kiroho akiushika Wokovu halisi wa KRISTO YESU tena bila kumruhusu mtu yeyote au shetani kumtoa katika Wokovu huo.

◼️Kanisa lazima liwe na msimamo safi wa kiroho.

1 Petro 2:5 "Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya ROHO, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na MUNGU, kwa njia ya YESU KRISTO."

Ngoja nikupe mfano hai wa Watu wa MUNGU waliokuwa na msimamo safi wa kiroho.

Danieli 3:17-18 "Kama ni hivyo, MUNGU wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme.
Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha."

✓✓Vijana hawa watatu walikuwa na msimamo safi wa kiroho.

Mfalme wa nchi ile alitaka watu wote waabudu sanamu na kuisujudia lakini vijana hawa watatu wenye msimamo safi wa kiroho walikataa.
Serikali ilitangaza kifo kwa atakayekaidi lakini hadi hapo vijana hao walikataa kusujudia sanamu.

✓✓Hata wewe Mkristo inakupasa kuwa na msimamo thabiti wa kiroho.

◾Kama Kanisani kwenu huwa wanasujudia sanamu, wewe kataa maana ni machukizo kwa MUNGU.

◾Kama Kanisani kwenu huwa wanaabudu sanamu, wewe kataa maana ni machukizo kwa MUNGU.

◾Kama Mchungaji wenu siku hizi anajiita Mungu, wewe kataa na mkimbie huyo ni wakala wa shetani na hayo ni machukizo kwa MUNGU.

2 Wakorintho 4:2 "lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya neno la MUNGU na uongo; bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionyesha kuwa na haki, dhamiri za watu zikitushuhudia mbele za MUNGU."

◾Kama mchungaji wenu ni wakala wa shetani, wewe ondoka huko maana huyo hana neno la kukupeleka uzima wa milele.

◾Kama Kanisani kwenu kuna taratibu viongozi wenu wanaleta na kuwataka washirika kufuata taratibu hizo wakati taratibu hizo Kibiblia ni machukizo, wewe kataa taratibu hizo na hata jitenge na Kanisa hilo kisha jiunge na Kanisa lingine safi la kiroho maana yapo mengi sana makanisa safi ya kiroho.

◾Kama Kanisani kwenu kuna Watu wanafanya ushoga na Kanisa haliwakemei, kuwaonya, kuwakaripia, kuwaweka kwenye marudio, huko hapakufai.

◾Kanisa kwenu siku hizi wanafungisha ndoa za jinsia moja au wanawaabudu Watu na sio MUNGU, huko hapakufai.

◾Kama Kanisani kwenu siku hizi mnaamini mafuta ya upako, maji ya upako, chumvi ya upako au chochote mnakiamini kuliko YESU KRISTO, wewe kataa na usishiriki ujinga huo.

◾Kama Kanisani kwenu mnafundishwa kunywa pombe, wewe kataa maana ni machukizo kwa MUNGU.

◼️◼️Mkristo safi lazima uwe na msimamo sahihi na safi wa kiroho.

Yusufu ni mfano hai mwingine wa Mkristo mwenye msimamo safi, hebu tuangalie faida za kuwa Mkristo mwenye msimamo safi wa kiroho kupitia Yusufu.

Na kabla sijakuambia habari za Yusufu ngoja nikuambie kitu hiki kwanza , ni kwamba ni MUNGU  Tu ndiye  anayetujaalia kukaa salama hivyo usiogope Wala kupunguza Msimamo wako kwa YESU KRISTO.
Ndugu kulala salama na kuamka salama ni MUNGU tu ndiye anakuwezesha.
Imeandikwa katika Zaburi 4:8 Kwamba "Katika Amani nitajilaza na kupata usingizi mara, maana wewe, BWANA, peke yako, ndiwe unijaliaye kukaa salama."

Kwa sababu ni MUNGU tu ndiye anayetujalia kuwa salama basi inatupasa tuzidi kumwabudu katika KRISTO, kuwa na Msimamo thabiti katika Imani na Kumuomba MUNGU na kumshukuru pia. Nakuombea ulinzi wa MUNGU.
Kumbuka Yusufu alikuwa na msimamo safi kiasi kwamba alikataa kufanya dhambi ya Uasherati na akasingiziwa alitaka kubaka hadi akafungwa gerezani.

Faida za Mkristo mwenye msimamo safi.

1. MUNGU atakuwa na wewe, atakupa kibali na kukufadhili.

Mwanzo 39:21 "Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza."

2. MUNGU atakuheshimisha.

Mwanzo 39:22 "Mkuu wa gereza akawatia mkononi mwa Yusufu watu wote waliofungwa, waliomo gerezani; na yote yaliyofanyika humo ndiye aliyeyafanya."

3. MUNGU atakufanikisha katika utakachokifanya.

Mwanzo 39:23 " Wala mkuu wa gereza hakuangalia neno lililoko mkononi mwa Yusufu; kwa kuwa BWANA alikuwa pamoja naye. BWANA akayafanikisha yote aliyoyafanya."

4. MUNGU atakufanya kuwa mtu mkuu.

Mwanzo 41:38-41 " Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya MUNGU ndani yake? Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa MUNGU amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe. Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe. Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri."

MUNGU akubariki sana ukifanyika Mkristo mwenye msimamo safi wa kiroho sawasawa na Neno la MUNGU la injili ya Wokovu wa KRISTO YESU Mwokozi.

2 Petro 1:10 "Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe."
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments