MSHINDE MKUU WA ANGA NDIPO UTASHINDA VITA YA KIROHO .

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu. 
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la maarifa muhimu na maombi ili tuwe washindi katika ulimwengu wa roho na  ulimwengu wa mwili. 
Somo hili ni somo la maombi hivyo fanyia kazi  kwa maombi katika jina la YESU KRISTO na utaona matokeo mazuri katika maisha yako. 

Jambo la kwanza ninataka ujue ni kwamba Mwanadamu alipoumbwa alipewa maeneo matatu (3) kutawala. 

✓✓Maeneo hayo ni Anga, bahari na ardhi ndio maana MUNGU alimwambia Adamu akatawale viumbe wa angani,  viumbe wa baharini na viumbe wa ardhini. 

Mwanzo 1:26-27 " MUNGU akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa MUNGU alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba."

Hayo ndio maeneo matatu ambayo Mwanadamu alipewa kutawala lakini shetani kwa kutumia umbo la nyoka aliondoa utawala wa mwanadamu juu ya anga, Viumbe  baharini na juu ya ardhi(land/nchi) ndio maana shetani anaitwa pia mungu wa dunia hii. 

2 Wakorintho 4:4 "ambao ndani yao mungu(shetaji) wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake KRISTO aliye sura yake MUNGU."

Baada ya mwanadamu kutenda dhambi shetani ndio akawa mtawala lakini neema ya MUNGU ikaja kwa YESU KRISTO kuja kuturudishia utawala wetu  katika ulimwengu wa roho,  tunatawala kwanza kwa sisi kuhakikisha tuna YESU KRISTO kisha tunaitumia kwa maombi mamlaka iliyo ndani ya jina la YESU KRISTO. 

Warumi 8:37 "Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda."

Sasa Moja ya vikwazo vikubwa sana vinavyozuia mafanikio ya Watu wa MUNGU ni wakuu wa giza. 

Wakuu wa giza ni nini?

✓✓Wakuu wa giza ni maroho ya kuzimu wenye vyeo yanayomiliki maeneo kulingana mipango ya kishetani. 

Biblia inasema tuna vita na wakuu wa giza, hivyo wapo na unatakiwa kuwashinda. 

Waefeso 6:12" Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya WAKUU  WA GIZA hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."

Wakuu wa giza wapo wanaotawala aridhi na wengine wanatawala anga.
Wanaotawala anga la eneo hao ndio wakuu wa anga,  inakupasa kuwashinda katika jina la YESU KRISTO. 

Mfano ni huu ambapo Malaika Gabrieli alipokuwa anamletea Majibu Danieli,  huyo Malaika alipambana na Mkuu wa anga la Nchi ile ya Uajemi, na Malaika akasema akitoka hapo kwa Danieli Mtumishi wa MUNGU atakwenda kupigana na Mkuu wa giza wa Uajemi lakini Malaika pia akamwambia kwamba na Mkuu wa anga wa Uyunani atakwenda eneo hilo pia. 

Danieli 10:20 "Ndipo akasema, Je! Unajua sababu hata nikakujia? Na sasa nitarudi ili nipigane na mkuu wa Uajemi; nami nitakapotoka huku, tazama, mkuu wa Uyunani atakuja."

Hapa tunaona wakuu wa anga wawili ambao Lengo kubwa ni kuzuia utumishi wa Danieli. 

Kumbe Inawezekana kabisa waliomfanyia visa Danieli mara kutunga sheria ya dharula ili Danieli anase, Mara kumtupa Danieli katika shimo lenye simba ili afe,  Inawezekana kabisa hao Watu walikuwa wakifanya hayo Kwa kutumiwa na Mkuu wa anga wa Nchi ile. 

Moja ya vikwazo ni wakuu wa giza wanaoshikilia anga.

Wakuu wa giza wapo wanaomiliki anga la eneo, Hawa jina lingine wanaitwa wakuu wa anga,  lengo lao mojawapo ni kuwafanya Watu walio chini ya eneo hilo wajitenge mbali na Wokovu wa KRISTO. 

Waefeso 2:2 "ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;"

Kwa ambaye umewahi kuhubiri injili maeneo mbalimbali unaweza ukanielewa zaidi juu ya mkuu wa anga anavyoweza kufanya vita na ili Watu wa eneo hilo wasihitaji injili ya KRISTO, ndio maana kuna baadhi ya maeneo sehemu kubwa ya wakazi wa eneo hilo ni waabudu shetani maana wamemkataa YESU KRISTO kama Mwokozi wao. 

Unaweza ukaandaa mkutano mkubwa wa injili na ukatangaza sana lakini Watu wasije. 
Mkuu wa anga ni kizuizi kikuu cha injili. 

Mfano ni pale Shetani alimzuia Paulo kufika Thesalonike kuhubiri injili ya KRISTO.
 1 Wathesalonike 2:18 "Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia."

Yaani mkuu wa anga ana eneo lake hivyo Mkuu wa anga katika eneo la Thesalonike aliwazuia akina Paulo kuhubiri huko,  tunajuaje?  Ni Kwa sababu katika maeneo mengine hatuoni Paulo akizuiliwa na nguvu za giza kuhubiri ila Thesalonike.

Madhara ya mkuu wa anga kutawala anga ni kuwa anakuwa na uwezo wa kuzuia kila jambo jema linaloachiliwa kutoka mbinguni na pia anakuwa na uwezo wa kuachilia mabaya juu ya nchi kwa kushirikiana na mawakala wengine wa shetani kama Wachawi, mapepo/majini, waganga wa kienyeji, mizimu n.k
Mkuu wa giza ndio mkuu wao,  mkuu wa giza sio Mchawi wala mganga ila roho ya kuzimu inayotawala eneo kipepo na  hao wachawi na waganga wanakuwa wanatembea katika nguvu zake huyo Mkuu wa giza. 

Ngoja nikupe ushuhuda wangu. 
Nilipochapisha Kitabu changu kiitwacho  Maombi ya  kina kilipokelewa vyema sana na marafiki zangu,  kilifika mikoa 13 Tanzania,  kilifika Kenya na Marekani.  Katika mikoa ya Tanzania kuna mikoa kiliisha nikatuma tena,  sehemu zingine nilituma zaidi ya mara Moja maana vilikuwa vinaisha japokuwa vilikuwa vingi, lakini ajabu  kuna mkoa mmoja hata kitabu kimoja hakikununuliwa,  yaani Watu wengi kutoka mkoa huo walinipigia simu na kuniandikia meseji kwamba wanakihitaji sana kitabu changu lakini nilipokituma tu huko Watu wa huko  wakabaki wakisema tu "nitanunua nitanunua "  Miaka zaidi ya miwili hakuna hata nakala moja ya kitabu ilinunuliwa. 
Nini nataka kusema,  hiyo ni vita ya falme,  Mkuu wa anga alizuia kama hujui unaweza kujikuta unakuwa mtu wa kulaumu tu  kumbe Inakupasa kuongeza maombi 

Kila anga hapa duniani shetani ameweka mfalme wake , ndio huyo aitwaye Mkuu wa anga, ambaye na yeye hutumiwa na watu wa gizani ili kuhakikisha wanaharibu mambo mema ya Watu wa MUNGU. 
Mfano unaweza kukuta mtu ameokoka akatoka katika anga Mfano anga la Dodoma  akaenda anga la Kigoma ,lakini akiwa Kigoma ghafla anajikuta kiu ya kuomba haipo ndani yake tena,  kumbe ameingia kwenye anga la wafalme wa giza wenye mamlaka na anga hilo kazi yao kubwa ni kuzuia asiombe kazi yao nyingine ni kuleta uharibifu kwenye hari  ya kiroho ya Mteule.

Ndugu, Huwezi kufanikiwa sehemu yoyote mpaka umewashinda wakuu wa Giza  wa eneo uliko au ulikohamia, iwe umeingia katika  mji, ukoo au Familia,
usipomwangusha  kwa Maombi mkuu wa Giza huwezi  Kushinda kiroho wala kufanikiwa kiroho na Kimwili.
 Sababu wachawi washirikina waganga wa kienyeji, wasihiri, wasoma nyota, wanajimu,  madhabahu za giza zote, miungu n.k wote wanafanya kazi kwa nguvu za hiyo roho ya kuzimu iitwayo mkuu wa giza. 

Wakuu wa giza wanaweza kuwa  kwenye ukoo, kwenye familia, kwenye mtaa ulioko,  Kwenye eneo la kazi,  katika mji na wapo hadi wakuu wa giza wa taifa.  

Mfano unaweza kuwa na  biashara nzuri ila hauuzi, umepambana Sana Katika maombi ila hujui tatizo ni nini,  ndugu Inawezekana yupo mkuu wa Giza mahali anakupiga vita.

 Ukiwa unapata vita Katika kuolewa au kupata kazi, au kwenye ndoa jua yupo mkuu wa Giza anafanya vita na wewe kwa kuwatumia wachawi, waganga wa kienyeji, washirikina, au anapanda uadui kwa watu waliokuzunguka.
 Sasa bila kumshinda huyu Mkuu wa giza ujue unaweza  Kuzunguka kila eneo la maombezi,  unaweza kuomba sana lakini kama hujamgusa yaani hujampiga  huyo Mkuu wa anga anayekuzuia ujue ataendelea kukuzuia. 

Inawezekana  uko katika vita kubwa ya kiroho ila maadui zako hawaishi, kila siku wanaongezeka tu,  mpige Mkuu wa anga katika eneo hilo ndipo utashinda. 
Wakati mwingine Inawezekana vita kwenye ndoa yako au vita ya uzao wako au vita ya familia zako,  hiyo vita inaratibiwa na Mkuu wa giza,  Leo kwa maombi Katika jina la YESU KRISTO Pambana naye kimaombi na ataiachia ndoa yako,  nyumba yako,  familia yako,  uzao wako na kila baraka yako. 

Inawezekana kabisa uchumi wako una vita Kali, kumbe kuna Mkuu wa anga hataki ufanikiwe ukiwa katika eneo hilo, mji huo au mtaa huo.  
Ndio maana unatakiwa ukifika mahali pamiliki kwanza kwenye ulimwengu wa roho kwa maombi ndipo hazitainuka juu yako kwenye eneo hilo. 

Ndugu,  Biblia haijatuambia kwamba tuwakimbie wakuu wa anga bali inataka tupambane nao na tunayo mamlaka katika KRISTO YESU ya kuwashinda wote,  muhimu tu maombi ndugu. 

Wakati mwingine Inawezekana wewe umeokoka na ni muombaji mzuri na katika maombi yako umewashinda wachawi, mapepo/majini, mizimu au majoka au mamba au ng'ombe au chochote cha kipepo lakini kama hujamshinda  mkuu wa Giza ujue wakuu wa giza  huinua watu wengine au Watenda kazi wengine lakini ukimshinda na yeye huyo Mkuu wa giza wa eneo hilo ujue umeshinda vita hiyo ya kiroho. 

Miaka iliyopita Nimewahi katika somo langu Moja kutoa mifano hai miwili juu ya kuwashinda wakuu wa giza ili umiliki.  Ngoja na  Leo niirudie mifano hai hiyo. 

Mfano hai wa kwanza ni huu. 
David Yonggi Cho wa Korea kusini Ni mhubiri mwenye Kanisa kubwa wanaloabudu pamoja kuliko makanisa yote duniani. Alipoitwa na Bwana YESU ili amtumikie alianza kumtumikia.
 Lakini mwanzo tu wa huduma yake aliona mkuu wa giza anayelimiki eneo la Korea yote. Ilibidi Mchungaji Yonggi Cho
apambane kwa maombi na mkuu yule giza. alipomshinda kwa maombi kupitia jina la YESU ndipo huduma yake ilistawi na huduma hiyo imefikia hatua ya sadaka zinahesabiwa kwa zaidi ya siku 2 na sadaka hiyo kuipeleka bank ni kwa msafara mkubwa wa magari  kukiwa na ulinzi mkubwa wa Polisi wengi.
Ndugu, ukishinda katika ulimwengu wa roho hata katika ulimwengu wa mwili utashinda pia.

Mfano hai wa Pili ni huu. 

Askofu Moses Kulola kabla ya kuanza kuhubiri injili ya mafanikio makubwa katika Tanzania aliingia katika maombi ya kufunga siku 4 mlimani. Katika maombi hayo akiwa katika siku ya mwisho ya maombi aliona jitu kubwa la kutisha likija alipo na lilipokaribia lilimwambia kwanini anataka kulichukua eneo lake huyo mkuu wa giza, yaani
Tanganyika kwenye ulimwengu wa roho  kulikuwa na mtawala wake wa kipepo  ambaye ndiyo huyo roho ya kuzimu, kwa maombi Askofu Moses Kulola alimshinda yule mtoto wa shetani ndio maana akaanza kuhubiri injili ya mafanikio sana. 
Kila Eneo huwa lina utawala wa aina tatu. Kuna utawala wa kibinadamu, kuna utawala kutoka ulimwengu wa roho wa giza na utawala wa MUNGU. Utawala wa MUNGU  hutawala pote na una mamlaka ya mwisho.

Kumbe ili ulipate eneo fulani kwa ajili ya kitu fulani chako chema inabidi kwa maombi umpige mkuu wa giza wa eneo husika.

Ukisoma Biblia utaona baadhi ya kazi za hao wakuu wa  anga ni hizi. 

Kazi ya wakuu wa anga 

1. Kuzuia maombi. 

Danieli 10:13 "Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi."

Majibu ya maombi ya Danieli yalizuiliwa Kwa siku 21. 
Inawezekana na wewe yuko Mkuu wa anga wa ukoo au mji au mtaa au taifa anachelewesha maombi yako kwa siku zaidi ya 21, Leo katika jina la YESU KRISTO Msambaratishe na hatazuia tena maombi yako. 

2. Kuchelewesha majibu yako. 

Danieli 10:10-12 " Na tazama, mkono ukanigusa, ukaniweka juu ya magoti yangu, na vitanga vya mikono yangu.
 Akaniambia, Ee Danielii, mtu upendwaye sana, yafahamu maneno nikuambiayo, ukasimame kiwima-wima; maana kwako nimetumwa sasa. Na aliponiambia neno hili, nalisimama nikitetemeka. Ndipo akaniambia, Usiogope, Danielii; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za MUNGU wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako."

Tunaona hapa Danieli akiguswa na Malaika na kupewa majibu ya maombi yake lakini majibu hayo hayakuzuiliwa tu bali yalicheleweshwa pia. 
Hivyo kazi ya wakuu wa anga ni kuchelewesha majibu yako au kuchelewesha baraka zako. 
Leo kwa maombi Katika jina la YESU KRISTO hakikisha unapambana na kila Mkuu wa giza anayechelewesha  baraka zako na  majibu ya maombi yako. 

3. Kutoa nguvu kwa wanaotumika kipepo. 

Ufunuo 13:1-2 " Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru. Na yule mnyama niliyemwona alikuwa mfano wa chui, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya dubu, na kinywa chake kama kinywa cha simba, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi."

Tunaona mnyama akitoka baharini,  bahari kwenye ulimwengu wa roho ina maana ya mahali wanapoishi Watu yaani duniani,  Kwa hiyo mnyama huyo ni roho ya shetani ambayo itatokea duniani huku Ikiwa na miujiza ya kishetani,  na  katika andiko hilo tunaona  joka akimpa nguvu mnyama ili kuwakamata Watu. 
Huo ni Mfano mmoja wapo wa wafalme wa giza wakiwapa nguvu wadogo zao katika kazi zao za kishetani. 
Kazi ya wakuu wa giza ni kutoa nguvu kwa mawakala wa shetani,  Leo kwa maombi Katika jina la YESU KRISTO  mpige huyo Mkuu wa giza anayetoa nguvu kwa mawakala wa shetani wanaokutesa. 

Nini ufanye Katika maombi yako? 

1. Tubu kwa ajili ya dhambi zako zote ili upate kibali kwa MUNGU. 

2 Petro 3:9 "BWANA hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba."

2. Mpige  Mkuu wa giza ili aachie anga lako. 

Yeremia 5:14 "Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala."

3. Itoe mikono ya Mkuu wa giza  kwenye kila eneo la maisha yako. 

Luka 10:19 "Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru."

4. Wapige wote anaowatumia huyo Mkuu wa anga.

 Zaburi 2:9 "Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi."

5. Haribu madhabahu za giza  kokote zilipo. 

Kumbu 12:2-3 " Vunjeni kabisa mahali pote walipokuwa wakiitumikia miungu yao mataifa mtakayoyamiliki, juu ya milima mirefu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti wenye majani mabichi; nanyi zivunjeni madhabahu zao, zibomoeni nguzo zao, na maashera yao yateketezeni kwa moto, na sanamu za kuchonga za miungu yao zikateni; na jina lao lifutilieni mbali na mahali hapo."

6. Komboa baraka zako zilizokuwa zimeshikiliwa na nguvu za giza. 

2 Wakorintho 9:8 "Na MUNGU aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema;"

7. Omba MUNGU akutoe katika mikono ya falme za giza. 

Kutoka 6:6-7 " Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa; nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri."

8. Mshukuru MUNGU na baki ndani ya Wokovu wa Bwana YESU daima. 

1  Nyakati 16:8-10 " Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake; Wajulisheni watu matendo yake. Mwimbieni, mwimbieni kwa zaburi; Zitafakarini ajabu zake zote. Jisifuni kwa jina lake takatifu; Na ufurahi moyo wao wamtafutao BWANA."

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri. 
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii  kupiga,  kuandika meseji na hadi whatsapp).
Ubarikiwe 

Comments