MUNGU ANAPOKUITA UMTUMIKIE USITOE UDHURU.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu kujifunza Neno la MUNGU.

◼️MUNGU anapokuita umtumikie usitoe udhuru.

Udhuru ni nini?
◾Udhuru ni sababu anayoitoa mtu inayomfanya mtu huyo kusameheka katika kufanya jambo fulani au kufanya kazi fulani ya lazima.

✓✓Tunaweza kutoa udhuru kwa mambo ya kibinadamu lakini sio kutoa udhuru kwa MUNGU.

2 Timotheo 1:8-9 " Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya MUNGU; ambaye ALITUOKOA AKATUITA KWA MWITO  MTAKATIFU, SI KWA KADIRI YA MATENDO YETU SISI, BALI KWA KADIRI YA MAKUSUDI YAKE YEYE NA  NEEMA YAKE. Neema hiyo tulipewa katika KRISTO YESU tangu milele,

Tangu zamani MUNGU hutoa maekezo kwa watu aliowachagua, hivyo ukichaguliwa usitoe udhuru.
Mfano ni huu MUNGU anamwambia Yeremia na Yeremia hakutoa udhuru.

Yeremia 1:17 "Haya basi, wewe jifunge viuno, ukaondoke ukawaambie maneno yote niliyokuamuru; usifadhaike kwa ajili yao, nisije nikakufadhaisha wewe mbele yao."

✓✓YESU KRISTO akisema na wewe ili umtumikie usitoe udhuru.

✓✓Bwana YESU anapokuita umtumikie usitoe udhuru.

◼️MUNGU anapokuita anakuwa anajua wewe utaweza kutimiza kile alichokuitia, usitoe udhuru.

✓✓Ukitoa udhuru wakati mwingine MUNGU anakuacha na ukiachwa na MUNGU ni hatari sana.

Ukitoa udhuru MUNGU anawapa kazi hiyo wengine hata ambao unawaona ni watu wa chini sana, na MUNGU atawatumia hao huku wewe umeachwa.

Mfano ni hawa walioitwa wakatoa udhuru.

Luka 14:18-21 "Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimenunua ng'ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe. Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja. Yule mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete."

✓✓Ndugu ukiitwa na Bwana YESU ili umtumikie usitoe udhuru bali mtumikie kwa uaminifu na utakatifu wote.

◼️Kuna watu wameitwa kumtumikia MUNGU kwa pesa zao, wengine wameitwa kumtumikia MUNGU kwa kuhubiri, wengine kufundisha Neno la MUNGU, wengine kutoa ardhi yao kwa kazi ya MUNGU, wengine kushuhudia mitaani, wengine kutoa mali zao ili kuwahudumia watumishi, wengine kuhubiri kwa njia ya uimbaji, wengine uchungaji, wengine uinjilisti n.k

✓✓Ndugu ukiitwa kumtumikia MUNGU kwa njia yeyote usitoe udhuru.

◼️Unapoitwa kuhubiri hakikisha unahubiri.

◼️Kama umeitwa kufundisha Biblia hakikisha unafundisha.

◼️Kama umeitwa kuhubiri kwa uimbaji basi imba nyimbo zinazohubiri injili ya KRISTO YESU Mwokozi.

◼️Kama umeitwa kuipeleka injili kwa pesa zako basi timiza wito wako kila mara inapowezekana.

Ukiitwa na MUNGU usitoe udhuru katika kazi yeyote.

Wengi wa wanaotoa udhuru kwa MUNGU ni watu hawa.

1. Mtu anayejiona hawezi lakini amesahau kwamba anayewapa watu kuweza ni MUNGU tu.

Mfano hai ni Musa ambaye alitaka kutoa udhuru kwa MUNGU kitu ambacho hakiwezekani.

Kutoka 3:11-12 "Musa akamwambia MUNGU, Mimi ni nani, hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri? Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu MUNGU katika mlima huu."

2. Mtu anayeangalia umri wake, jinsia yake na hali yake ya kiuchumi huku amesahau kwamba MUNGU akikuwezesha hakuna kitakachozuia.

Mfano ni Yeremia aliyetaka kutoa udhuru akijiona hawezi na ni mdogo kiumri.

Yeremia 1:6-8 " Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini BWANA akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema BWANA."

3. Kutokuwa na roho ya kumcha MUNGU katika KRISTO YESU.

Warumi 3:17-18 " Wala njia ya amani hawakuijua. Kumcha MUNGU hakupo machoni pao."

✓✓Mwenye kumcha MUNGU lazima amtii MUNGU wakati wote, hata wakati MUNGU amemuita katika utumishi hawezi kutoa udhuru.

4. Kuipenda dunia kuliko kumpenda MUNGU.

1 Yohana 2:15-17 " Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba(MUNGU) hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele."

5. Kutokujua faida za kumtumikia MUNGU.

Mfano hai ni Petro ambaye alikuwa hana uhakika atapata faida gani kwa kumtumikia YESU KRISTO hadi pale Bwana YESU alipomjibu.

Mathayo 19:27-29 " Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?
 YESU akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.  Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele."

6. Kujidharau huku amesahau kwamba mwezeshaji wa yote ni MUNGU.

Mfano hai ni Musa alidhani hataaminiwa na watu wala hawatamsikiliza sauti yake ya kigugumizi wala hawataamini kama MUNGU amemtokea mtu kama yeye.

Kutoka 4:1 "Musa akajibu akasema, Lakini, tazama, hawataniamini, wala hawataisikia sauti yangu; maana watasema, BWANA hakukutokea."

7. Kuruhusu kupofushwa na shetani.

2 Wakorintho 4:3-4 " Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake KRISTO aliye sura yake MUNGU."

Je umepofushwa na shetani hata hutaki kumtumikia MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi?

◼️Ndugu hakikisha unatimiza kile MUNGU katika KRISTO YESU amekuitia.

Mimi binafsi Kuna pia huniauliza kwamba wana wito na wameshasikia sauti ya MUNGU ikisema na wao ila hawajui waanzie wapi.
Ndugu anza hata leo ukifuata maelekezo uliyopewa na MUNGU.

Wengi sana akiitwa huwaza apewe madhabahu Kanisani ili ahubiri wakati pale Kanisani yupo tayari aliyewekwa pale kwa kazi hiyo.

Ndugu iga mfano wangu huu Mimi Peter Mabula ambapo nilipookoka nikiwa Zanzibar nilipata msukumo wa kufundisha Neno la MUNGU na nikaanza kushuhudia nyumba kwa nyumba, nikawa kila jumamosi saa mbili asubuhi hadi saa tano asubuhi natembelea nyumba kumi nikihubiri wokovu wa KRISTO, nilitukanwa sana maana zaidi ya 90% niliowafuata hawakuwa wakristo.
Niliendelea hadi nilipoanza kuyaona matokeo ya utumishi huo.

✓✓Fuata maelekezo yale yale uliyoambiwa na ROHO MTAKATIFU.

Tatizo la watu wengi wanapoitwa huwafuata watu walio na huduma tofauti na wao hivyo huwashauri vibaya.

Mfano wewe ni muimbaji unanifuata mimi nisiye na mzigo na uimbaji, naweza kukuambia achana na uimbaji na shuhudia mitaani na masokoni, kama nimekupotosha kulingana na wito wako ujue nimekukosesha pakubwa sana.

Ushauri wangu wangu ni kwamba ukiitwa na MUNGU katika KRISTO YESU anza kufanyia kazi wito wako.

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments