MUNGU ATAKULINDA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 


Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU.
Leo tunajifunza kwa njia ya swali hili ''BIBLIA INA MAANA GANI INAPOSEMA KWAMBA MUNGU ATAKULINDA?''
Zaburi 121:7-8 " BWANA atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele."
Ni kweli kabisa MUNGU huwa anatulinda lakini Biblia inaposema kwamba MUNGU atakulinda ina maana gani?
Mithali 3:26 "Kwa kuwa BWANA atakuwa tumaini lako, Naye atakulinda mguu wako usinaswe."
Biblia inaposema kwamba MUNGU atakulinda ina maana zifuatazo.
1. MUNGU kukulinda ina maana MUNGU kukuweka salama.
Hii inahusisha kukufanya uwe salama hata kama uko katikati ya adui wengi.
Na wakati MUNGU akikulinda maana yake atahakikisha unakaa salama hata kama umezungukwa na mawakala wa shetani wengi, hata kama umezungukwa na maadui wengi kiasi gani unakaa salama.
Zaburi 4:8 "Katika amani nitajilaza na kupata usingizi mara, Maana Wewe, BWANA, peke yako, Ndiwe unijaliaye kukaa salama."
Ndugu, Msikilize MUNGU na endelea kumtumainia katika KRISTO YESU na atakulinda.
Mithali 18:10 "Jina la BWANA ni ngome imara; Mwenye haki huikimbilia, akawa salama."
2. MUNGU kukulinda ina maana MUNGU kukuepusha na madhara.
Madhara haya haijalishi yapo wakati huo au yamepangwa yaje kwako, MUNGU atakulinda na utakaa bila kudhurika na mabaya hayo kutoka ulimwengu wa giza.
Yeremia 39:18 "Kwa maana ni yakini, nitakuokoa, wala hutaanguka kwa upanga, lakini nafsi yako itakuwa kama nyara kwako; kwa kuwa ulinitumaini mimi, asema BWANA."
Mfano hai wa mtu aliyeepushiwa na madhara ni Danieli aliyeepushiwa tukio la kuuawa na simba wenye njaa.
Danieli 6:22 "MUNGU wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno."
3. MUNGU kukulinda ina maana ya MUNGU kukuepusha na hasara.
Kuna ulinzi wa MUNGU unaoelekezwa katika kukuepusha na hasara.
Ulinzi huu unawahusu hasa watoaji waaminifu mbele za MUNGU kwenye utoaji wa fungu la kumi na dhabihu yaani sadaka za hiari.
Malaki 3:11 "Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi."
Haijalishi wengine wamepata hasara kiasi gani, wewe unaweza kulindwa na MUNGU na hasara zote zilizokusudiwa kwako hazitakupata kamwe maana MUNGU atakulinda ili usipate hasara.
Mithali 3:9-10 " Mheshimu BWANA kwa mali yako, Na kwa malimbuko ya mazao yako yote. Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya."
4. MUNGU kukulinda ina maana ya MUNGU kukuchunga ili usipatwe na mabaya.
Kumbu 31:8 "Naye BWANA, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike."
Ulinzi wa MUNGU unaweza kuhusisha wewe kupata ufunuo au taarifa ya kiroho au maelekezo ya MUNGU ya moja kwa moja na vyote hivyo ili kukuepusha usiingie katika mabaya.
MUNGU akikulinda anaweza kukuchunga kama Mchungaji anavyochunga kondoo ili tu usipatwe na mabaya.
MUNGU anaweza kuweka uangalizii kwako ili usidhurike.
MUNGU anaweza kukutunza ili usidhurike.
5. MUNGU kukuhami wewe dhidi ya maadui.
Zaburi 16:1-2 " MUNGU, unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia Wewe. Nimemwambia BWANA, Ndiwe BWANA wangu; Sina wema ila utokao kwako."
Hii ina maana ya MUNGU kukuhifadhi ili usinaswe na maadui zako wanaokutafuta.
Hii ina maana ya MUNGU kukutetea dhidi ya adui zako.
Hii ina maana ya MUNGU kukusaidia dhidi ya adui zako na kuhakikisha unakaa salama.
6. MUNGU kukulinda ina maana ya MUNGU kuwapiga adui zako ili wasikudhuru.
Kumbu 20:4 "kwa maana BWANA, Mungu wenu, ndiye awaandamaye kwenda kuwapigania juu ya adui zenu, ili kuwaokoa ninyi."
Huo ndio ulinzi wa MUNGU kwako yaani MUNGU kuwapiga maadui zako ili wewe ukae salama.
Hivyo ndugu jifunze kuomba maombi ya ulinzi wa MUNGU na MUNGU katika KRISTO YESU atakulinda na kukuepusha na kila maadui na kila madhara.
7. MUNGU kukulinda ina maana ya MUNGU kumzuia adui yako kukufanya wewe chochote.
Mfano hai ni pale ambapo MUNGU akimzuia Goliathi ili asimdhuru Daudi.
MUNGU pia aliwazuia Simba na Dubu kumdhuru Daudi.
1 Samweli 17:37,50 " Daudi akasema, BWANA aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na BWANA atakuwa pamoja nawe. ...... Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake."
MUNGU akimzuia adui yako kukushambulia na kukufanya lolote hakika utakaa salama maana hakuna atakayekushambulia, huo ndio ulinzi wa MUNGU wa ajabu sana.
8. MUNGU kukulinda ina maana ya MUNGU kukuokoa ukiwa tayari umevamiwa.
Ayubu 5:19-21 "Yeye atakuokoa na mateso sita; Naam, hata katika saba hapana uovu utakaokugusa. Wakati wa njaa atakukomboa na mauti; Na vitani atakukomboa na nguvu za upanga. Utafichwa na mapigo ya ulimi; Wala usiogope maangamizo yatakapokuja."
Inawezekana kuna maadui wengi sana na wanakuchukia sana lakini MUNGU anaweza kukuokoa hata kama wamekuzingira wakidhani wanakumaliza.
Zaburi 18:17 "Akaniokoa na adui yangu mwenye nguvu, Na wale walionichukia, Maana walikuwa na nguvu kuliko mimi."
Haijalishi adui yako anatisha kiasi gani, MUNGU akikulinda utakaa salama mbele ya huyo adui.
Yeremia 15:21 "Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha."
YESU aliwaokoa akina Meshaki anaweza kukuokoa hata wewe ukiwa katikati ya moto wa maadui zako.
Danieli 3:23-25 " Na watu hao watatu, Shadraka, na Meshaki, na Abednego, wakaanguka, hali wamefungwa, katikati ya ile tanuru iliyokuwa inawaka moto.
Ndipo Nebukadreza akastaajabu, akainuka kwa haraka; akanena, akawaambia mawaziri wake, Je! Hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto? Wakajibu, wakamwambia mfalme, Kweli, Ee mfalme. Akajibu, akasema, Tazama, mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu."
Nini nataka kusema zaidi juu ya ujumbe wa leo?.
Ikiwa umemuomba MUNGU akulinde na MUNGU akafanya kipengele hata kimoja tu kati ya hivyo vipengele 8 usidhani MUNGU hajakulinda, hakika amekulinda.
Hi vyema sana tukauelewa ulinzi wa MUNGU ulivyo ndipo tutaongeza juhudi za kuomba.
Inawezekana wewe ulimuomba MUNGU awapige maadui zako lakini MUNGU hakuwapiga maadui zako bali aliwazuia tu kukudhuru, usidhani hapo kwamba MUNGU hajakulinda, bali amekulinda hivyo Mshukuru sana MUNGU.
Inawezekana wewe uliomba MUNGU akuepushe na madhara na MUNGU alichokifanya ni kukuchunga ili usiingie katika mitego ya mabaya, usidhani kwamba hapo MUNGU hajakulinda bali amekulinda, hivyo Mshukuru sana.
Ulinzi wa MUNGU uko katika maeneo hayo manane hivyo katika KRISTO YESU unaweza hata ukaomba ukitumia kipengele kimoja kimoja cha ulinzi wa ,MUNGU na atakulinda hakika.
Kumbuka pia pale ambapo kuna kanuni ya MUNGU ndipo ulinzi utokee basi ifuate hiyo kanuni, mfano kama unataka MUNGU ailinde biashara yako au kazi yako zingatia Kanuni ya kutoa zaka na sadaka.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
0 7 1 4 2 5 2 2 9 2(Ni namba hii kupiga, kuandika meseji na hadi whatsapp).
Uki-share somo hili kwa maandishi naomba share kama lilivyo,usibadili jina wala chochote.

Comments