![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU linalotujulisha jinsi ya kuitambua roho ya Yezebeli na kuishinda au kuiepuka au kuizuia ili isifanye kazi.
✓✓Katika maandiko tunakutana na mwanamke anayeitwa Yezebeli ambaye alikuwa wakala wa shetani aliyeleta uharibifu mkubwa kwenye kazi ya MUNGU na kwa watu wa MUNGU.
1 Wafalme 16:31 "Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia."
✓✓Lakini miaka mingi sana baada ya mwanamke huyo kufa tunaona tena maandiko yakimtaja tena Yezebeli lakini Yezebeli huyu hakuwa mtu wa kawaida ila alikuwa ni roho ya kuzimu inayofanya kazi ili kuleta uharibifu kwa watu wengi.
Ufunuo 2:20 "Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu."
✓✓Kwa namna hiyo tunagundua kwamba Yezebeli mwanadamu alikuwa ameibeba roho ya Yezebeli na kwa kupitia kuangalia maandiko tutagundua kazi za hiyo roho ili tuishinde kwa maombi kupitia jina la YESU KRISTO na tuishinde hiyo roho kwa Neno la MUNGU ambalo litatupa kuitambua na kutupa mbinu za kuishinda na kuiepuka.
Mimi Peter Mabula nilipookoka mwaka 2008 nilianza kusikia watu wengi wa makanisani wakiwaambia baadhi ya watu hasa wanawake kwamba wana roho ya Yezebeli, nilitamani kujua hiyo roho ya Yezabeli ndio nini, nilijua kwamba roho ya Yezebeli ni roho ya shetani lakini mbona ni roho ambayo ni maarufu sana?
Nilijifunza maandiko na nikaijua hiyo roho ni roho gani na ikawa rahisi hata kuijua ninapoona ndani ya mtu hasa wanaompinga YESU KRISTO.
Miaka michache iliyopita nikiwa sehemu fulani na baadhi ya watu wengi wa MUNGU nilimsikia mama mchungaji mmoja akimwambia binti fulani kwamba huyo binti ana roho ya Yezebeli, binti yule alikuwa anacheka tu lakini angejua anabebeshwa roho chafu sana angeumia sana.
Dada mmoja pia siku moja alinipigia simu akilia kwa sababu watu Kanisani kwao wanasema ana roho ya Yezebeli wakati yeye anaishi maisha matakatifu wala hausiani kivyovyote na uyezebeli, nilimuombea na kumtia moyo, huyu alikuwa anaijua hiyo roho ya Yezebeli.
Sijui kwa upande wako inawezekana umewahi kusikia watu wakikuita au wakimuita mtu fulani kwamba ana roho ya Yezebeli, kama ni kweli basi ni hatari sana kuwa na roho hiyo ya shetani.
Inawezekana sasa unatamani kujua roho hii ni ipi ili uishinde, ngoja nikujuze machache juu ya hiyo roho kisha nikuonyeshe namna inavyofanya kazi ili upate kuishinda, itakuwa rahisi hata ukigundua kwamba mtumishi fulani ana roho hiyo ya Yezebeli basi hutajiunga naye kwa lolote.
✓✓Roho ya Yezebeli ni roho ya shetani ambayo inaweza kukaa ndani ya baadhi ya wanawake na hata wanaume na ikaleta uharibifu mkuu sana.
Kwanza Yezebeli alikuwa mtoto wa Ethbaali na baba yake alikuwa kuhani wa Baali, Baali ni shetani/miungu.
Sasa maana ya jina ''Yezebeli'' ni ''pamoja na baali'' yaani "pamoja na shetani."
Hivyo ukiambiwa kwamba una roho ya Yezebeli maana yake wewe ni wa shetani na uko pamoja na shetani.
Maana ya pili ya ''Yezebeli'' ni ''mtu asiyeoleka''
✓✓Hii roho ya Yezebeli ni roho ya mpinga Kristo.
✓✓Pia roho ya Yezebeli ni roho ya shetani inayowaingia baadhi ya wanawake ili wawatawale waume zao, ndio maana unaona Ahabu akitawaliwa na mkewe Yezebeli ambaye alimkosesha mbele za MUNGU.
Roho ya yezebeli ni roho ya shetani inayowafunga kiroho baadhi ya watu.
Baada ya utangulizi huo sasa ngoja tuangalie namna ya kuitambua hii roho ya kuzimu.
Tabia za Yezebeli mwanadamu ndizo zinazofunua kazi ya hii roho ya Yezebeli.
Kazi 10 za roho ya Yezebeli, zijue ili uishinde hii roho au ujitengenayo.
1. Roho ya Yezebeli kazi yake ni kuwafanya watu wamwabudu shetani na wajenge madhabahu za giza.
1 Wafalme 16:31-32 " Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia. Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali, aliyoijenga huko Samaria."
✓✓Ndio maana tunaona hapa Ahabu aliyekuwa anamwabudu MUNGU Baba wa mbinguni akigeuka na kuanza kuabudu shetani na kwa sababu roho ya Yezebeli ilimwingia basi roho hiyo ikamfanya kujenga madhabahu ya kumwabudia shetani Tena akaijenga hiyo Madhabahu ikulu.
✓✓Ni roho inayofundisha kumuabudu shetani na kumjengea madhabahu.
✓✓Ni roho inayowalazimisha watu kumwabudu shetani na kujikuta wanamwabudu shetani kwa juhudi kubwa sana.
Mfano hai ni hawa ambao walikuwa wamevamiwa na roho ya Yezebeli.
1 Wafalme 18:26 "Wakamtwaa yule ng'ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya."
Ukimuona mtu anang'ang'ana kumwabudu shetani na kumjengea shetani eneo la kumwabudia tambua kwamba mtu huyo ana roho ya Yezebeli, kama ni wewe nakuomba mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako na jitenge mbali na roho ya Yezebeli.
2. Roho ya Yezebeli ni roho ya kuwaua kiroho watumishi wa MUNGU.
1 Wafalme 18:4 "kwa kuwa ikawa, Yezebeli alipowaua manabii wa BWANA, Obadia akatwaa manabii mia, akawaficha hamsini hamsini katika pango, akawalisha chakula na kuwapa maji)."
Hapa tunamuona Yezebeli akiua watumishi wa MUNGU lakini katika wakati huu roho hiyo ya Yezabeli inawaua watu kiroho kwa dhambi na kuwapofusha macho ya kiroho.
Wako watumishi wamekufa kiroho kwa sababu ya uzinzi, na kufa kiroho huja baada ya uongo wa shetani.
Hivyo kama ni wewe umekufa kiroho basi nakuomba okoka upya na anza kumcha MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.
Kama kuna Mtumishi unaona amekufa kiroho, amebakiza maneno ya uzoefu tu ila ameshakufa kiroho na yuko busy tu na uzinzi , pombe n.k basi kwa njia hii utamgundua na hutakubali akupoteze na roho yake ya Yezebeli.
3. Kazi ya roho ya Yezebeli ni kutengeneza watumishi wa shetani na kuwahudumia.
1 Wafalme 18:19 "Basi sasa upeleke watu, unikusanyie jamii ya Israeli katika mlima wa Karmeli, na wale manabii wa Baali mia nne na hamsini, na wale manabii wa Ashera mia nne, walao chakula mezani pa Yezebeli."
✓✓Katika andiko hili tunaona watumishi 850 wa shetani waliotengenezwa na Yezebeli na hao watumishi 850 hulishwa na huyo Yezebeli, yaani wanahudumiwa na huyo Yezebeli.
Hata leo ni rahisi kusikia kwamba kuna mtumishi amemwacha YESU au mtu fulani amemwacha YESU na kuiingia mikataba ya kishetani ili atajirike, maana yake mtu huyo akiingia maagano na hiyo roho ya kuzimu basi nguvu za giza zitamtajirisha kwa muda kisha kumwangamiza.
Kutajirishwa huko kipepo ndio kuhudumiwa na Yezebeli.
Kuna watumishi wakamwacha YESU leo wanaingia katika mikataba ya kishetani ili wapate utajiri, hiyo ndiyo kazi ya roho ya Yezebeli yaani kuwahudumia kwa muda watumishi wa shetani kisha kuwaua maana wana mikataba na shetani.
Kuna baadhi ya watumishi leo ni mapandikizi ya shetani maana wametengenezwa na shetani ili wampinge YESU KRISTO na kweli yake, ni watoto wa shetani ili kupata kundi kubwa la kwenda jehanamu.
1 Yohana 3:10 "Katika hili watoto wa MUNGU ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. ........"
◼️Je wewe bado uko na YESU KRISTO katika Wokovu wake hata uwe mtoto wa MUNGU?
Au Yezebeli kakuteka hata humtaki YESU KRISTO Mwokozi hivyo wewe ni mtoto wa ibilisi?
Ndugu, kama ni wewe umewekwa na Yezebeli geuka leo, okoka upya na anza upya na YESU KRISTO huku ukijitenga na hila za shetani.
Wasaidie pia watu walioshikiliwa na Yezebeli na wanamwabudu shetani kwa juhudi sana, wasaidie watu hao kwa kuwaambia ukweli na washauri kwamba wamfuate sasa YESU KRISTO Mwokozi na waanze kumwabudu MUNGU Baba katika ROHO MTAKATIFU.
4. Roho ya Yezebeli ni roho ya kuleta vitisho kwa wateule wa MUNGU.
1 Wafalme 19:2 "Ndipo Yezebeli akampelekea Eliya mjumbe, kusema, Miungu wanifanyie hivyo na kuzidi, nisipokufanya roho yako kesho, panapo wakati huu, kama roho ya mmojawapo wa hao."
Ungekutana leo na Nabii Eliya Mtishbi ukamuuliza namna vitisho vya roho ya Yezebeli vilivyo angekueleza vyema sana maana ilifika kipindi kwa sababu ya Yezebeli alianza yeye mwenyewe Eliya kujionbea kwamba afe, yaani vitisho vya Yezebeli na kazi zake zilimfanya Eliya kutamani MUNGU amuue, ni hatari sana.
✓✓Roho ya Yezebelini ni roho ya shetani ya vitisho.
Kuna makanisa leo wanaambiwa ''Msiporuhusu ushoga hatuwapi msaada'' iyo ndio roho ya Yezebeli kuwatisha ili muangukie mikononi mwa shetani.
Mawakala wa shetani wengi wamejaa vitisho kwa wateule wa KRISTO wanaoisimamia kweli ya MUNGU.
Kwanini wawe na vitisho hao wapinga Kristo? Ni kwa sababu ndani yao wana roho ya Yezebeli.
Hata watumishi wa shetani wote wamejaa vitisho kwa wateule wa KRISTO maana hao wapingaKristo wana roho ya Yezebeli ndani yao.
5. Roho ya Yezebeli ni roho ya kutunga hila kwenye mambo ya kiroho ili kupata mali.
1 Wafalme 21:8-13 " Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi. Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana MUNGU na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe. Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. Wakapiga mbiu ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu. Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana MUNGU na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa."
Hapa tunaona Nabothi aliuawa kwa hila za Yezebeli ili Ahabu apate mali isiyo naye.
Unaweza ukajiuliza mfalme Ahabu alikuwa tajiri sana je inaingia akilini mtu tajiri kama Ahabu tena raisi wa Israeli atamani ka ardhi kadogo ka mtu mmoja maskini hata hila zitumike ili kumuua masikini huyo ili tajiri Ahabu amiliki shamba hilo dogo?
Kwa haki ya kawaida sidhani kama inawezekana lakini kwa sababu roho ya Yezebeli ni roho ya kutunga hila ili kujipatia mali basi roho hiyo ya shetani ilifanya kazi hadi Nabothi akauawa kwa hila za Yezebeli.
Hii roho ya Yezebeli ikimwingia mtumishi anaweza kutunga hila nyingi ili ajipatie mali, anaweza kuja na mafunuo ya uongo ili ajipatie mali.
Ndugu, kama ni wewe okoka upya na jitenge mbali na roho ya Yezebeli.
Kama kuna mtumishi utamuona ana hiyo roho ya Yezebeli ya kutunga hila ili apate mali basi jitenge mbali na mtumishi huyo.
Kumbuka hila nyingi za shetani zinatungwa ili kuharibu kanisa hai la MUNGU.
Wako watu wa hii roho ya Yezebeli ya kutunga hila ili kupata mali, watu hao wanaweza hata kumuua mtu ili wapate mali zake, ni mbaya sana.
Zaburi 10:7 "Kinywa chake kimejaa laana, Na hila na dhuluma. Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu,"
6. Roho ya Yezebeli ni roho ya kuchochea maovu na kushawishi uovu.
1 Wafalme 21:25 (Lakini hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa BWANA ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu sawasawa na yote waliyoyafanya Waamori, BWANA aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.)
Ahabu alichochewa na Yezebeli kutenda maovu.
✓✓Roho ya yezebeli ni roho ya kuchochea uzinzi na uasherati na kuwafanya watu kuwa wazinzi na waasherati.
✓✓Ni roho ya kuchochea ushoga na usagaji na kuwafanya watu wawe mashoga au wasagaji.
✓✓Ni roho ya kuchochea maovu ya kila namna, watu wenye hii roho lazima wachochee uovu, mfano ni wasanii wa nyimbo za kidunia wanaochochea ngono na pombe na uvaaji wa kikahaba katika nyimbo zao ili watu wengi waige, hiyo ni kazi ya roho ya yezebeli.
Ndugu kama ni wewe ndio umevamiwa na hii roho ya Yezebeli ya kuchochea maovu nakuomba okoka, tubu na acha dhambi hizo tena.
Ahabu kabla ya kukutana na Yezebeli alikuwa mtu mzuri sana, lakini kwa sababu roho ya Yezebeli Biblia inasema kwamba wakati huo hapakuwa na mtu muovu kama Ahabu "hapakuwa na mtu kama Ahabu, aliyejiuza atende maovu machoni pa BWANA ambaye Yezebeli mkewe alimchochea. Akachukiza mno, kwa kuzifuata sanamu"
7. Roho ya yezebeli ni roho ya uzinzi na uchawi.
2 Wafalme 9:22 "Ikawa, Yoramu alipomwona Yehu, akasema, Je! Ni amani, Yehu? Akajibu, Amani gani, maadamu uzinzi wa mama yako Yezebeli na uchawi wake ni mwingi?"
✓✓Roho ya Yezebeli ni roho inayowafanya watu wawe wachawi au wazinzi.
Yoramu alijulishwa na Yehu kwamba Yezebeli amejaa uzinzi na uchawi, hiyo ndivyo ilivyo roho ya Yezebeli.
✓✓Hii ni roho ya kufanya makubaliano ya kipepo, maagano ya kipepo na dhambi.
Kama ni wewe umenaswa na roho hii hata umekuwa mzinzi, mwasherati au mchawi nakuomba tubu na okoka leo katika KRISTO YESU Mwokozi na MUNGU atakusamehe dhambi hiyo.
Isaya 57:3 "Lakini ninyi karibuni hapa, enyi wana wa mwanamke mchawi, uzao wa mzinzi na kahaba."
◼️Majini mahaba yote ni sehemu ya roho ya Yezebeli, hivyo kama umekamatwa na maroho hayo nakuomba okoka kwa upya, tubu na acha dhambi.
8. Roho ya Yezebeli ni roho ya kujipamba kipepo.
2 Wafalme 9:30 "Hata Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli akapata habari; akatia uwanja machoni mwake, akapamba kichwa chake, akachungulia dirishani."
✓✓Katika Biblia nzima mwanamke mpaka wanja ni Yezebeli tu, sijui wewe mwanamke wa leo unapaka wanja wa Yezebeli au nani?
Ni vyema kuchunguza kila jambo maana sio kila taratibu duniani ni ya ki MUNGU, Taratibu zingine ni za kishetani, kumbuka pia hata Yezebeli leo yuko kazini.
Roho ya Yezebeli ni roho ya shetani inayowafanya watu kujipamba kipepo, kuvaa nguo za kutamanisha ngono, kuvaa mawigi, na vitu vingi vya mapambo ambavyo vinatokana na kazi za Yezebeli.
Ezekieli 16:15 "Lakini uliutumainia uzuri wako, ukafanya mambo ya kikahaba kwa sababu ya sifa zako, ukamwaga mambo yako ya kikahaba juu ya kila mtu aliyepita; ulikuwa wake."
Mfano leo unaweza kumkuta mwanamke amechora tatuu kwenye titi lake, basi mtu kama huyo lazima avae nguo inayoonyesha titi lake ili watu waione tatuu yake, lazima avae nguo za kikahaba, hayo ndio madhara ya kuvamiwa na roho ya Yezebeli.
Mithali 7:10 "Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo;"
Siku moja nilikuwa naangalia video nzuri ya wimbo mzuri sana wa mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili ambaye ni mwanaume, wimbo wake ni mzuri sana na video ni nzuri sana lakini nilishangaa jambo moja. Mwanaume yule nilipomtazama mdomoni niliona midomo yake ina rangi kama nyekundu nikashtuka na kuwauliza waliokuwa jirani na mimi kwamba ''Kwanini huyu mtumishi mwanaume midogo yake ni mwekundu?'' watu wale walinicheka kisha wakasema ''Wewe kumbe hujui kwamba kuna vipodozi vya wanaume vya kupaka midomoni ila huyo kazidisha'' Nilishangaa sana jambo hilo kwamba kuna hadi wanaume leo wanapaka midomo vipodozi kama ambavyo nawaona baadhi ya wanawake, ndugu zangu Yezebeli yuko kazini hivyo wewe unayesoma somo hili nakuomba mche MUNGU katika KRISTO YESU na usikubali kunaswa na Yezebeli.
Wakati mwingine chunguza kwanini vipodozi vingi hutoka katika nchi ambazo sio Wakristo?
Na kwanini baadhi ya watengenezaji wa vipodozi hivyo wao hawavitumii?
✓✓Ndugu, kazi ya roho ya Yezebeli ni kuwafanya watu wajipambe kipepo, yaani unakutana na mtu hadi unajiuliza je huyu ni mtu au jini?
Ndio maana Biblia inalielekeza Kanisa la KRISTO kwamba Kanisa wajipambe rohoni.
1 Petro 3:3 "Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;" bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za MUNGU.
Ndio maana Biblia inaagiza wanawake wacha MUNGU wavae mbele za watu mavazi ya kujisitiri.
1 Timotheo 2:9-10 " Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani; bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa MUNGU."
✓✓Ndugu, inawezekana watu wanasema una roho ya Yezabeli kwa sababu unavaa kikahaba.
Mjue Yezebeli na jitenge naye.
9. Roho ya Yezebeli ni roho ya unabii wa uongo.
Ufunuo 2:20 "Lakini nina neno juu yako, ya kwamba wamridhia yule mwanamke Yezebeli, yeye ajiitaye nabii na kuwafundisha watumishi wangu na kuwapoteza, ili wazini na kula vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu."
Hapa hii ufunuo sura ya pili ndio roho ya Yezebeli imefunuliwa kwa uwazi zaidi.
✓✓Watumishi wenye roho ya Yezebeli hufundisha uongo, hutabiri uongo na kupotosha watu.
✓✓Kazi ya nabii wa uongo ni kuukataa Wokovu wa KRISTO YESU.
✓✓Kazi ya nabii wa uongo ni kupotosha watu ili wasiokoke na kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO YESU Mwokozi.
✓✓Roho ya Yezebeli ni roho ya kuwafanya watu wamfuate shetani na sio kumfuata YESU KRISTO.
Mfano hai ni Ahabu ambaye alimwacha MUNGU na kuwafuata mashetani.
1 Wafalme 18:18 "Naye akajibu, Si mimi niliyewataabisha Israeli; bali ni wewe, na nyumba ya baba yako, kwa kuwa mmeziacha amri za BWANA; nawe umewafuata mabaali."
10. Kazi za roho ya Yezebeli ni kufanya maagano ya kipepo na wanadamu.
Ufunuo 2:22 "Tazama, nitamtupa juu ya kitanda, na hao wazinio pamoja naye, wapate dhiki kubwa wasipotubia matendo yake;"
Wako wamezini na Yezebeli yaani wameingia maagano na Yezebeli,ni hatari sana.
✓✓Lengo la maagano yote ya kishetani ni kuwaweka watu katika vifungo vya giza.
Mithali 23:27 "Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni rima jembamba."
Kahaba ni shimo refu maana yake roho ya ukahaba humfunga mtu kipepo, roho ya Yezebeli ndio hiyo roho ya ukahaba yaani roho ya uzinzi na uasherati, ndio maana kuna wako huota ndoto wako ndani ya mashimo wanajaribu kutoka wanashindwa, unapoona hivyo unakuwa unajulishwa kwako uko katika kifungo cha kishetani.
Ndugu kama una husika na roho ya Yezebeli basi jitenge nayo kuanzia leo.
Mambo hayo kumi juu yanamfunua Yezebeli na kazi zake hivyo hakikisha unajitenga na mambo hayo ambayo ni ya Yezebeli.
Inawezekana miaka yote wewe unajua roho ya Yezebeli ni roho ya uzinzi na uasherati tu, naamini leo umeongeza ufahamu na utajitenga mbali na Yezebeli.
Inawezekana wewe miaka yote ulijua roho ya Yezebeli ni ya kuvaa kihaba tu na kujipamba kipepo, leo naamini umeongeza ufahamu na utajitenga na Yezebeli daima.
Kama kuna mtumishi umegundua ana roho ya Yezebeli kaa mbali naye ili asikupoteze, tafuta kweli ya KRISTO na ungana na watu waliookoka wanaoishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU.
Omba langu ni Bwana YESU KRISTO akusaidie kuishinda roho ya Yezebeli.
1 Petro 2:3-5 " ikiwa mmeonja ya kwamba Bwana(YESU) ni mwenye fadhili. Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa MUNGU ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya ROHO, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na MUNGU, kwa njia ya YESU KRISTO."
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Hadi whatsapp).
Ubarikiwe

Comments