NATAMANI NDOTO YAKO NJEMA ITIMIE KATIKA JINA LA YESU KRISTO.

Peter na Jemimah Mabula 
Watendakazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.

◼️Ninao marafiki wema wengi sana na wa namna mbalimbali, Kuna marafiki ambao MUNGU amewainua ili kuisapoti huduma yangu, kuna marafiki niliishi nao, kuna marafiki tunaofanya kazi ya MUNGU pamoja, kuna marafiki tunaoshirikiana mambo mema mbalimbali, kuna marafiki ambao ni kama ndugu kwangu n.k.

◼️Lipo pia kundi maalumu sana la marafiki zangu ambao MUNGU Baba amenipa ili wajifunze kwangu Neno la MUNGU, ni marafiki ambao hujifunza Neno la MUNGU ambalo ROHO MTAKATIFU amenipa katika KRISTO YESU, namshukuru MUNGU sana kwa ajili yao.

Wakati mwingine katika maombi yangu huwa ninawaombea na kumsihi Bwana YESU kwamba awalinde na ndoto zao njema MUNGU azitimize.

Filemoni 1:4 "Namshukuru MUNGU wangu sikuzote, nikikukumbuka katika maombi yangu;"

✓✓Ndugu, naomba niwe muwazi mbele za MUNGU leo kwamba wewe ni mtu wa thamani sana kwangu.

Haijalishi Neno la MUNGU nililofundisha nilikukwaza au kukuumiza, kama ni Neno la MUNGU nakuomba fanyia kazi na wewe ni mtu wa thamani sana kwangu Mimi Peter Mabula.

◼️Natamani ndoto zako njema MUNGU Baba azitimize.

3 Yohana 1:2 "Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo."

Pia naomba unielewe kwamba ninaposema ndoto yako ifanikiwe sina maana ya ndoto za kuota ukiwa usingizini bali nazungumzia leo ndoto kama mipango yako unayotamani MUNGU akufanikishe.

Ndoto ni nini?

✓✓Ndoto ni mpango wa kumiliki kitu fulani maishani mwako.

Ndoto ni nini?

✓✓Ndoto ni hali ya kutamani kuwa mtu wa namna fulani baadae.

◼️Katika KRISTO YESU ndoto yako lazima itimie, hayo ndio maombi yangu.

✓✓Inawezekana uko katika ndoa yenye vita na migogoro isiyoisha na ndoto yako ni kwamba ifike mahali ndoa yako iwe ya amani na furaha, MUNGU aifanikishe ndoto yako hiyo.

✓✓Inawezekana ndoto yako ni kufunga ndoa takatifu na kuzaa watoto, MUNGU aifanikishe ndoto yako.

Yeremia 29:6 ''oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue."

✓✓Inawezekana ndoto yako ni kufaulu masomo na kupata kazi nzuri , MUNGU aifanikishe ndoto yako.

✓✓Inawezekana ndoto yako kujenga nyumba na kuishi kwa amani na watu wote, MUNGU aifanikishe ndoto yako.

✓✓Inawezekana ndoto yao kununua gari na kuitegemeza kazi ya MUNGU, MUNGU aifanikishe ndoto yako.

✓✓Inawezekana ndoto yako ndugu zako waokoke, MUNGU aifanikishe ndoto yako.

Wafilipi 1:4 "sikuzote kila niwaombeapo ninyi nyote nikisema sala zangu kwa furaha,"

✓✓Inawezekana ndoto yako upate haki yako na usaidie ndugu zako, MUNGU aifanikishe ndoto yako.

✓✓Inawezekana ndoto yako ununue kiwanja kikubwa cha kujengwa Kanisa, MUNGU aifanikishe ndoto yako.

✓✓Inawezekana una ndoto njema, hata kama hiyo sijaitaja hapa ombi langu MUNGU aifanikishe ndoto yako.
Kila mtu ana ndoto zake, hata mimi  nina ndoto zangu nyingi natamani MUNGU Baba wa mbinguni anifanikishe.

Muhimu tu ndugu yangu ni kwamba Biblia inasema kwamba kwa kila neno jema kwanza tanguliza kusali na kuomba na kumshukuru MUNGU, hivyo hata ndoto yako ili itimie katika KRISTO YESU basi tanguliza maombi na kumshukuru MUNGU, unaweza kumshukuru MUNGU hata kwa sadaka pia kama una msukumo huo rohoni mwako.

Wafilipi 4:6-7 " Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na MUNGU. Na amani ya MUNGU, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika KRISTO YESU."

✓✓Najua wewe una ndoto yako njema, natamani Bwana YESU akufanikishe ndoto yako.

◼️Hana ndoto yake ilikuwa kupata watoto wakati yeye alikuwa tasa, MUNGU akamtimizia ndoto yake kwa kumpa mtoto mzuri Samweli.
Kwa sababu ndoto ya Hana ilikuwa kupata watoto wengi basi siku moja Hana alijitamkia hivi " Naam, huyo aliyekua tasa amezaa watoto saba, "- 1 Samweli 2:5

Kipindi Hana anajitamkia maneno haya alikuwa na mtoto mmoja tu lakini kabla ya hapo alikuwa mtu asiye na uwezo wa kuzaa lakini ndoto yake ni kupata watoto.
MUNGU alimfanikisha Hana kwa kumbariki watoto 6 jumla.
1 Samweli 2:21" Naye BWANA akamwangalia Hana, naye akachukua mimba, akazaa watoto, wa kiume watatu na wa kike wawili. Naye huyo mtoto Samweli akakua mbele za BWANA."

Ndoto ya Hana ikatimia, kutoka kuwa tasa/mgumba na kumzaa nabii Samweli pamoja na watoto wengine watano, MUNGU aifanikishe ndoto yako na wewe.

◼️Ndoto ya Daudi ilikuwa kwamba Adui zake waanguke na yeye Daudi asimame.

Zaburi 20:8 "Wao wameinama na kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama."

Na ni kweli ndoto ya Daudi ilitimia maana hatuoni akishindwa vitani na adui zake.

Tunaona akina Goliathi na wengine wakianguka mbele za Daudi.

Inawezekana ndoto yako wakuu wa giza wote waliokutesa miaka mingi waanguke kwa jina la YESU KRISTO Mwokozi.
Najua una ndoto njema mbalimbali, Mimi Peter Mabula natamani MUNGU Baba akufanikishe.
Hakikisha tu umeokoka na unaishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO YESU Mwokozi.

Ngoja pia nikushauri mambo machache ili ndoto yako itimie.

1. Ishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO YESU.

2. Mtegemee MUNGU kwa maombi na shukrani.

3. Jiepushe na dhambi zote

4. Uwe na malengo juu ya ndoto yako.

5. Vijue vikwazo vinavyoweza kukwamisha ndoto yako kutimia, vishughulikie ili ndoto yako itimie.

6. Itambue ndoto yako na hakikisha iko katika kusudi la MUNGU kisha iombee ndoto hiyo ili itimie.

7. Usiwe na mashaka na kutimia kwa ndoto yako.

8. Jitambue wewe ni nani ili uendane na ndoto yako.

Mfano kama ndoto yako ni uingie katika ndoa njema Jitambue wewe ni mtu wa thamani hivyo kataa uasherati ili uendane na ndoto yako ya kuingia katika ndoa njema.

9. Weka malengo ili ndoto yako itimie.

Mfano kama ndoto yako ni kuwa na kazi nzuri serikali basi weka malengo ya kusoma sana ili ufaulu masomo maana ndoto yako hiyo inaendana na kuwa na elimu nzuri.

10. Weka tumaini kwa MUNGU juu ya kufankiwa kwa ndoto yako.

Isaya 26:3-4 " Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini.
Mtumainini Bwana siku zote Maana Bwana YEHOVA ni mwamba wa milele."

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments