NI HERI KUBAKI NA NENO LA MUNGU TU.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

◼️Hii hasa ni kwa wale walioshikilia vitu na sio Neno la MUNGU.

✓✓Inawezekana umedanganywa na mtumishi ambaye wala sio Mtumishi wa Bwana YESU KRISTO na umeshikilia maelekezo yake na sasa humhitaji tena YESU KRISTO maana kitu chako cha upako ulichopewa umeridhika nacho.

Ndugu uwe makini maana waongo katika utumishi nao ni wengi sana.

2 Timotheo 3:6-9 " Kwa maana katika hao wamo wale wajiingizao katika nyumba za watu, na kuchukua mateka wanawake wajinga wenye mizigo ya dhambi, waliochukuliwa na tamaa za namna nyingi; wakijifunza siku zote, ila wasiweze kabisa kuufikia ujuzi wa kweli.
Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani. Lakini hawataendelea sana; maana upumbavu wao utakuwa dhahiri kwa watu wote, kama vile na upumbavu wa hao ulivyokuwa dhahiri."

✓✓Ninaposema haya nina matukio mengi ya watu ambao walishikilia vitu vya upako na kujikuta shetani anawageuza mawindo.

Mtu mmoja alienda sehemu fulani ya ibada na huko akaombewa na kupewa kitu cha upako, wiki iliyofuata alienda Kanisa lingine kuabudu na ajabu akalipuka mapepo yakisema hayatamwacha maana aliyafuata mwenyewe kwenye vitu vya upako, kumbe vile vitu vya upako alivyopewa na mtumishi havikuwa katika MUNGU bali katika shetani.

Mtu mmoja hakuwa na matatizo ila alipoanza tu kutumia vitu vya upako alivyopewa na mtumishi ndipo matatizo yakaanza, kukabwa na majinamizi kukaanza.

◼️Ndugu, unamhitaji YESU KRISTO mwenyewe na sio vitu vya upako ambavyo sehemu kubwa na usanii wa watu.

◼️Sisi tumepewa Neno la MUNGU katika KRISTO YESU.

Mithali 30:5-6 " Kila neno la MUNGU limehakikishwa; Yeye ni ngao yao wamwaminio. Usiongeze neno katika maneno yake; Asije akakulaumu, ukaonekana u mwongo."

Wewe umepewa mafuta ya upako?

Tafuta Neno la MUNGU.

◼️Sisi tumepewa Neno la MUNGU lenye ushindi wetu na neno hilo la MUNGU litasimama milele.

Isaya 40:8 "Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la MUNGU wetu litasimama milele."

Wewe umepewa leso za upako ambazo hazitadumu milele.

◼️Ndugu nakuomba ambatana na Neno la MUNGU katika KRISTO YESU maana Neno hili litasimama milele.

✓✓Sisi tumepewa Neno la MUNGU lililo hai ambalo YESU anasema "Heri wanaolisikia na kulishika"
Luka 11:28 "........ Afadhali, heri walisikiao neno la MUNGU na kulishika."

Wewe umepewa chumvi za upako na hata neno la MUNGU hulizingatii, ila unazingatia matumizi ya chumvi za upako kama ulivyoelekezwa.

Ndugu tafuta neno la MUNGU aliye hai.

◼️Sisi tumepewa Neno la KRISTO la uzima.

1 Petro 1:23 "Kwa kuwa mmezaliwa mara ya pili; si kwa mbegu iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika; kwa neno la MUNGU lenye uzima, lidumulo hata milele."

◼️Sisi tumepewa Neno la KRISTO ambalo hukaa mioyoni mwetu.

Wakolosai 3:16-17 " Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana YESU, mkimshukuru MUNGU Baba kwa yeye."

Wewe umepewa maji ya upako unayopaka ukutani na hakuna msaada
Ndugu zingatia neno la MUNGU na sio vitu.

Ajabu Wewe umepewa vidude vya upako vya kuvaa shingoni au mikononi na neno la MUNGU la uzima hulizingatii.

Ni heri kubaki na Neno la MUNGU tu.

✓✓Watu wanaona na kutendewa miujiza kwa jina la YESU KRISTO tu na sio vinginevyo.

Tafuta Watumishi wa MUNGU wa zamani katika nchi Yako ambao MUNGU aliwatumia kwa Miujiza mikubwa, unadhani kwa Nini MUNGU aliwatumia bila vitu vya upako? Ni kwa sababu ndivyo MUNGU alivyo, anatenda bila visaidizi.
Mfano uliye Tanzania MUNGU zamani sana aliwatumia akina Moses Kulola, Mzee Mabondo, Askofu Lazaro, Askofu Kakobe na wengine wengi sana kwa Miujiza sana.
Mbona Miujiza ilikuwa mingi bila vitu vya upako?
Ni kwa sababu MUNGU ndivyo alivyo.
Ndugu Rudi kwenye msingi wa Miujiza ya MUNGU.

✓✓Watu wanafunguliwa kwa jina la YESU KRISTO na sio kwa kitu kingine chochote.

Mfano ni huu, kama kiwete tangu kuzaliwa anapona kwa jina la YESU KRISTO tu,wewe unakwama wapi hadi umeng'ang'ania vitu vya upako?

Huyu mbona alipona kwa jina la YESU KRISTO tu.

Matendo 3:6-8 " Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la YESU KRISTO wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akiruka-ruka, na kumsifu MUNGU."

Ndugu, ni heri kubaki na YESU KRISTO na neno lake.
MUNGU akubariki sana uliyeelewa.

Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments