OMBA MUNGU AKUFUTIE MOYONI MWAKO MAMBO MABAYA YALIYOTOKEA ZAMANI AMBAYO UKIYAKUMBUKA YANAKUUMIZA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote. 
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU kisha tuombe maombi yanayoleta ushindi mkubwa. 

Leo tunajifunza kisha tunaomba ili MUNGU atufutie mioyoni mambo mabaya(kama yapo)  yaliyotokea zamani ambaye tukiyakumbuka tu yanatuumiza mioyoni na kutuvuruga .

✓✓Yapo mambo matukio ambayo yalitokea zamani yanaweza kumtesa mtu kila akiyakumbuka. 

◼️Kuna mambo Biblia inatuambia kwamba inatupasa tusiyakumbuke. 

Isaya 43:18 "Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani."

✓✓Wako watu wanaishi na maumivu makubwa sana kwa sababu ya matukio yaliyotokea zamani. 

Nampenda MUNGU wa Mbinguni Kwa maana ana uwezo wa kuponya hata jeraha za moyoni.

Yeremia 30:17 "Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema BWANA, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye.'

Mimi Peter Mabula katika utumishi wangu kwa KRISTO nimewahi kuwasiliana na watu wengi sana wakinishirikisha mambo yaliyowasibu, baadhi wanasimulia huku wanalia sana na wengine unawasikiliza hadi na Wewe siku nzima unajikuta huna raha maana ni mambo magumu sana.

Wako watu wanasema "asingekufa Baba na Mama nisingekuwa hivi",  kwa sasa wakikumbuka tu namna wazazi wao walivyokufa wanaumia sana na kuvurugika kiroho. 

Wako watu wanasema mioyoni mwao kwamba wasingebakwa wasingepata magonjwa mabaya. 

Yako mambo mengi ambayo kuna watu wakiyakumbuka tu yanawaumiza hata kama yalishatokea miaka mingi iliyopita.
 
Ndugu, kama ni wewe, kwanini uendelee kuumia? 

◼️Leo mwambie YESU KRISTO akuponye katika hayo na ayafute katika ufahamu wako kiasi kwamba hata ikitokea umefikiri hayo hutaumia tena. 

✓✓Inawezekana ulitokea msiba ambao ukiukumbuka tu unakosa raha na amani. 

✓✓Inawezekana uliachwa na mwenzi wako au uliachwa na mchumba wako  ukikumbuka tu unakuwa mtu wa kulia na kukosa amani. 

Wako watu wamewahi kubakwa, ni siri yao inayowaumiza sana, wakikumbuka maumivu ya rohoni mwao yanakuwa mengi sana na hawajui mioyo yao itaponaje. 
Wako watu waliumizwa sana kiroho na hadi Leo wanateswa na maumivu makubwa sana.

Ayubu 6:2" Laiti uchungu wangu ungepimwa, Na msiba wangu kutiwa katika mizani pamoja!"

✓✓Wako watu walifukuzwa kazi bila makosa, wako watu walizushiwa uongo ulioharibu maisha  yao. 

✓✓Wako watu walifanyiwa hila mbaya sana zilizoharibu maisha yao, wako watu walitendwa vibaya sana tena na watu wao wa karibu. 

✓✓Wako watu walipigwa na kuumizwa sana,  wako watu walifungwa bila kosa. 

Matukio hayo mabaya yaliyotokea zamani mtu akiyakumbuka sasa  yanamtesa, mtu kama huyo anahitaji sana kupona majeraha ya moyoni.

◼️Ndugu omba MUNGU akufutie moyoni mwako maumivu yanayotokana na matukio ya zamani mabaya yaliyotokea katika maisha yako. 
Katika Jina la YESU KRISTO Inawezekana hakika.

Inakupasa kuyaona mambo hayo ya zamani kuwa sio kitu, yadharau na hakikisha hayakuumizi tena. 

Wafilipi 3:8 "Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua KRISTO YESU, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate KRISTO;"

✓✓Kuna watu walinyang'anywa mali zao au haki zao kwa uonevu, kwa sababu ya tukio hilo baya lililotokea maishani mwao wamejikuta wanakuwa katika maumivu kiasi ambacho maumivu hayo yamefungulia hadi mlango wa shetani kuwatesa zaidi. 

✓✓Wako wako katika maumivu mengi na yanayowatesa sana, watu hao wanatakiwa kupona leo katika jina la YESU KRISTO Mwokozi. 

✓✓Kuna watu walirogwa zamani kabla hawajaokoka na wako katika maumivu mabaya  sana sasa. 

✓✓Kuna watu walisalitiwa na wanapata uchungu mkubwa sana sasa wakikimbuka na uchungu huo unaendelea kuwatesa sana. 

Inaumiza  sana pale ambapo mtu aliyekufanyia kitu kibaya yupo na anaendelea kukutisha kila mara. 

✓✓Kuna watu maumivu yaliyo mioyoni mwao yamewafanya hata sauti ya MUNGU wasiisikie. 

✓✓Ni kweli maumivu ya moyoni yanaumiza sana lakini katika KRISTO YESU kuna ushindi kupitia maombi. 

Kwanini unahitaji YESU akuponye maumivu hayo ya rohoni  yanayotokana na kile kilitokea zamani? 

1. Ni kwa sababu usipoushinda uchungu  huo unaweza kuwa ni mlango wa shetani kukutesa. 

Waebrania 12:15 "mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya MUNGU; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo."

2. Ni kwa sababu usipoponywa katika maumivu hayo utashindwa kufanya mambo mema yakupasayo,  bali utakuwa unawaza tu mabaya na kulipiza kisasi. 

Warumi 7:15 "Maana sijui nifanyalo, kwa sababu lile nilipendalo, silitendi; bali lile nilichukialo ndilo ninalolitenda."

3. Ni kwa sababu kuna uchungu huleta vifungo vya shetani. 

Matendo  8:23 "Kwa maana nakuona u katika uchungu kama nyongo, na tena u katika kifungo cha uovu."

4.  Ni kwa sababu utakosa upendo hivyo  unaweza kujikuta unabaki tu mtu wa kuhesabu mabaya uliyotendewa au yaliyotokea zamani. 

1 Wakorintho 13:4-5 "Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;"

5. Utakuwa mtu wa hasira ya dhambi kila mara. 

Waefeso 4:26 "Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka;"

6. Ni kwa sababu utaamua vibaya na kujiingiza katika mabaya zaidi. 

Mfano hai ni  Esau  aliyekuwa na maumivu dhidi ya Yakobo kisha akaanza kuwaza mabaya dhidi ya Yakobo. 

Mwanzo 27:41 "Esau akamchukia Yakobo kwa ajili ya ule mbaraka babaye aliombarikia. Esau akasema moyoni mwake, Siku za kumlilia baba yangu zinakaribia, ndipo nitakapomwua ndugu yangu Yakobo."

7. Uchungu ni moja ya chanzo cha kukufanya uwe mtu mwovu. 

Ayubu 15:20 "Mtu mwovu huwa na uchungu siku zake zote, Hata hesabu ya miaka aliyowekewa mwenye kuonea."

8. Maumivu hayo yanaweza kukuletea kifo cha mapema kama hayo maumivu hayataondoka ndani yako. 

Ayubu 21:25 "Mwingine hufa katika uchungu wa roho, Asionje mema kamwe."

9. Maumivu hayo yanaweza kuwa ni mlango wa magonjwa. 

Zaburi 73:21 "Moyo wangu ulipoona uchungu, Viuno vyangu viliponichoma,"

Ndugu,  mimi sijui ni jambo gani ukilikumbuka huwa linakuumiza na kukuondoa katika uwepo wa MUNGU. 
Shetani pia anaweza kuwa anakukumbusha mabaya hayo yaliyotokea ili umkosee MUNGU. 

Na shetani anaweza akawa anakukumbusha mabaya hayo kipindi tu ukiwa katika furaha au amani au ukiwa katika maombi, na akikukumbusha ukiwa katika maombi hata nguvu za kuomba zinaisha unabaki unapiga tu miayo na kulia. 

Nini ufanye katika maombi na  katika mazingira hayo ya kukumbuka maumivu ya zamani? 

1. Tubu kwa ajili ya mabaya yaliyotokea. 

Matendo  3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"

2. Omba MUNGU akupe haki yako na  akutendee mema.

Kama maumivu yako yanatokana na kukosa haki yako omba upewe haki yako. 
Mfano hai ni  Hana ambaye  alikuwa na maumivu ya kukosa mtoto  hivyo katika uchungu wake na maumivu yake aliomba mbele za MUNGU ili apate haki yake ya mtoto na MUNGU akampa watoto sita. 

1 Samweli 1:10 "Naye huyo mwanamke alikuwa na uchungu rohoni mwake, akamwomba BWANA akalia sana."

3. Waeleze bila kuwaficha kitu watumishi sahihi wa MUNGU katika KRISTO YESU ili wakushauri na kukuombea. 

 Ayubu 10:1 "Nafsi yangu inachoka na maisha yangu; Sitajizuia na kuugua kwangu; Nitanena kwa uchungu wa roho yangu."

Ni heri kuuongea huo uchungu mbele za watumishi sahihi wa Bwana YESU ili usaidike. 

4. Omba MUNGU akuponye na kifungo cha uharibifu kilichotokana na jambo baya lililotokea. 

Isaya 38:17 "Tazama; nalikuwa na uchungu mwingi kwa ajili ya amani yangu; Lakini kwa kunipenda umeniokoa na shimo la uharibifu; Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako."

5. Omba MUNGU akulipizie kisasi yeye, kama tukio hilo baya lililotokea linahitaji kisasi,  wewe usilipe kamwe kisasi bali muombe MUNGU akulipizie kisasi. 

Warumi 12:19 "Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya MUNGU; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena BWANA."

6. Usiyakumbuke mabaya ya zamani wala kuyatafakari,  bali yafute kwa  maombi kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO. 

Isaya 43:18 "Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani."

7. Yapuuze mabaya hayo ya zamani na yaone hayana msaada kwako kwa sasa. 

Wafilipi 3:8 "Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua KRISTO YESU, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate KRISTO;"

8. Hakikisha kwa sasa YESU KRISTO ni Bwana na Mwokozi wako. 

 Mathayo 11:28 "Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha."

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments