POKEA UTU MPYA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

◼️Mwanadamu ana utu wa nje na utu wa ndani, ana utu wa kimwili na utu wa kiroho.

Warumi 7:22 "Kwa maana naifurahia sheria ya MUNGU kwa utu wa ndani,"

✓✓Biblia inaposema utu wa ndani ujue na utu wa nje upo.

Mwili kiroho ina maana ya mwili wa nyama tuliourithi kutoka kwa Adamu na Eva.

Mwanadamu anaweza kuwa na utu wa kale na utu mpya.

Ninachotaka kuzungumzia hapa ni utu mpya.

Waefeso 4:24 "mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli."

◼️Utu mpya ni matokeo ya mabadiliko ya utu wa kale.

Utu wa kale ni upi?

✔️✔️Utu wa kale ni utu wa asili yaani utu ambayo mtu anaupokea kutokea kwa wazazi wake.

Wakolosai 3:9 "Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake;"

✓✓Utu wa kale pia ni utu wa awali ambao mtu alijifunza au alifundishwa lakini utu huo ukiwa kinyume na wokovu wa MUNGU katika KRISTO YESU.

Unachotakiwa kufanya juu ya utu wa kale ni kuusulubisha ili huo mwili ubatilike

Warumi 6:6 "mkijua neno hili, ya kuwa utu wetu wa kale ulisulibishwa pamoja naye, ili mwili wa dhambi ubatilike, tusitumikie dhambi tena;"

Utu mpya ni upi?

✔️✔️Utu mpya ni ule tulioupokea wakati tunampokea YESU KRISTO kama Mwokozi wetu.

Wakolosai 3:10" mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba."

◼️Utu mpya ni utu unaotengenezwa na Neno la MUNGU kwa kupitia na kulifuata Neno hilo katika KRISTO YESU Mwokozi.

◼️Utu mpya ni mabadiliko ya rohoni yanayofanywa na ROHO MTAKATIFU kwa njia ya Neno la MUNGU ndani ya mtu ambaye anaamua kumpokea YESU kama Mwokozi wake binafsi.

✓✓Ndugu, hakikisha unaishi katika utu mpya ulioumbwa ndani yako na neno la MUNGU la wokovu wa KRISTO.

Hatua za kufanya ili kuupata utu mpya na kuishi katika huo ni

1. Kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako na kutubia dhambi zote.

2 Wakorintho 5:17 "Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya."

2. Kujifunza Neno la MUNGU, kulitafakari na kulifanyia kazi.

Yoshua 1:8 "Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana."

3. Kuwa mtu wa ibada kanisani.

Waebrania 10:25 "wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia."

4. Kukubali kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.

Warumi 8:14 "Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU."

5. Kuacha dhambi zote na kujitenga nazo.

1 Wathesalonike 5:22-24 " jitengeni na ubaya wa kila namna. MUNGU wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu YESU KRISTO. Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya."

Zingatia sana maelekezo hayo ili uwe na utu mpya ulio safi, unaopatikana tu katika KRISTO YESU Mwokozi.

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments