RUDI KWENYE ASILI YAKO NJEMA

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Kama wateule wa MUNGU katika KRISTO kuna asili njema ambayo MUNGU alituumba nayo, asili hiyo inatupasa kuiishi, asili hiyo ni matendo mema ambayo MUNGU aliyaumba ili sisi tuyaishi.

Waefeso 4:22-24 " mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya MUNGU katika haki na utakatifu wa kweli."

✓✓Kuna utu mpya ulioumbwa na MUNGU, hiyo ndio asili yetu tunayotakiwa kuiishi daima kama wateule wa KRISTO.

◼️Ni MUNGU ndio alituita, ni KRISTO ndio alituchagua, na katika mwito wenu ni lazima tuiishi asili yetu njema iliyoumbwa na MUNGU iwapasayo wateule wa KRISTO kuiishi.

Warumi 8:29-30 " Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza."

✓✓Ndugu, hakikisha unaiishi asili yako njema inayowapasa wateule wa KRISTO.

✓✓Kama umeacha asili yako iwapasao walio ndani ya wokovu basi rudi haraka katika asili yako hiyo njema iwapasayo wateule wa MUNGU katika KRISTO YESU.

Asili njema ni nini?

✓✓Asili njema ni sababu ya MUNGU hata sisi tuokoke, ni sababu ya MUNGU kutupa Wokovu wa KRISTO.

Asili ni kitu cha kimaumbile ambacho mtu anazaliwa nacho, sisi tuliompokea YESU KRISTO kama Mwokozi wetu tunayo asili yetu pia ambayo ni utakatifu.

Sasa nasikitika sana kwa sababu baadhi ya watu wameiacha asili yao njema na kufuata mashetani, wengine wamefuata roho zidanganyazo, wengine wamefuata miungu, wengine wamewafuata waganga wa kienyeji, wengine wamefuata dunia na anasa zake, wengine wamefuata dhambi na maovu, wengine wamewafuata manabii wa uongo, wengine wamefuata mawakala wa shetani mbalimbali wa kila namna n.k

Inawezekana ni wewe ndio umeiacha asili yako njema na kufuata uzushi.

Inawezekana ni wewe umemwacha YESU na kufuata dhambi, ndugu nakuomba rudi leo katika asili yako iwapasayo wateule wa MUNGU katika KRISTO YESU.

Kuna Wakristo wameziacha asili njema ziwapasao wateule wa KRISTO walio tayari kwa uzima wa milele, inawezekana ni wewe ndugu ndio umeiacha asili yako iwapasao wateule wa MUNGU.

Ulikuwa muombaji lakini kwa sasa umeacha maombi, umeiacha asili yako njema.

Umesahau ndugu kwamba Biblia uwe mtu wa maombi siku zote?

Luka 18:1 "....... imewapasa kumwomba MUNGU sikuzote, wala wasikate tamaa."

Ulikuwa unaiheshimu ndoa yako lakini sasa huiheshimu ndoa yako kwa sababu ya uzinzi na ukorofi.

Ndugu Umesahau kwamba Biblia inasema " Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi MUNGU atawahukumia adhabu-Waebrania 13:4."

Ndugu rudi haraka kwenye asili njema, anza kuiheshimu ndoa yako, acha dhambi za usaliti wa ndoa.

Ulikuwa unasoma Biblia na kuitafakari lakini kwa sasa umeacha.

Ndugu kwa nini umeiacha asili njema ya kulisoma Neno la MUNGU na kulitafakari?

Umesahau kwamba Biblia inakutaka uhakikishe Neno la MUNGU haliondoki kinywani mwako.

Yoshua 1:8 "Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana."

Ulikuwa unachukia dhambi lakini sasa unapenda dhambi na unatenda dhambi.

Umesahau kwamba Biblia inakutaka ujitenge mbali na dhambi za kila namna.

1 Wathesalonike 5:22" jitengeni na ubaya wa kila namna."

Ndugu, hakikisha unarudi kwenye asili njema ya kujitenga mbali na dhambi zote.

Ulikuwa mpatanishi lakini sasa umekuwa mfarakanishi, ndugu rudi kwenye asili yako njema iwapasayo wateule wa MUNGU, rudi kuwa mpatanishi na sio mfarakanishi.
Kumbuka wateule wa MUNGU tumepewa huduma ya upatanisho na sio ufarakanisho.

2 Wakorintho 5:18 "Lakini vyote pia vyatokana na MUNGU, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa KRISTO, naye alitupa huduma ya upatanisho;"

Ulikuwa unatoa fungu la kumi, sadaka na dhabihu lakini kwa sasa hutoi, ndugu rudi kwenye asili yako hiyo njema na ya kumpendeza MUNGU.

Biblia inawataka watu wa MUNGU Kuwa watoaji tena wanaotoa kwa upendo.

Kutoka 25:2-3 "Waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka; kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu. Sadaka utakayopokea mikononi mwao ni hii; dhahabu, na fedha, na shaba,"

Ulikuwa unatoa matoleo kwa moyo lakini siku hizi hutoi kwa moyo, ndugu rudi kwenye asili yako njema katika KRISTO YESU.
Kumbuka Biblia inakushauri hivi "

 Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana MUNGU humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.- 2 Kor 9:7"

Ulikuwa unawaheshimu wazazi wako na wazazi wako wa kiroho yaani watumishi wa MUNGU lakini sasa huwaheshimu tena, ndugu rudi kwenye asili yako njema haraka sana.

Ndugu Umesahau ahadi ya MUNGU ni nzuri mno kwako juu ya hilo?
Biblia inasema "Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia.-Waefeso 6:2-3"

Ulikuwa mtu wa ibada na mikesha na maombi lakini kwa sasa huna moyo wa ibada tena, ndugu rudi kwenye asili njema ya kuwa mtu wa ibada.

Biblia inatushauri kama Kanisa la KRISTO ikisema "wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.-Waebrania 10:25"

Ndugu kwanini wewe umeacha ibada na mikesha? Nakuomba ndugu rudi kwenye asili yako njema.

Ulikuwa unajifunza Neno la MUNGU kwa bidii lakini kwa sasa umeacha, ndugu rudi kwenye asili yako njema.
Biblia inakushauri kudumu katika neno la MUNGU ili ujiokoe nafsi yako.

1 Timotheo 4:16 " Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia."

Ulikuwa Umeokoka lakini kwa sasa umeacha wokovu na kuamua kuwa mpagani, ndugu rudi kwenye Wokovu haraka sana kama kweli unautaka uzima wa milele.

Ndugu, Biblia inakushangaa sana kwanini unamwacha YESU.
Wagalatia 1:6 "Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya KRISTO, na kugeukia injili ya namna nyingine."

Ulikuwa una YESU KRISTO lakini kwa sasa umemwacha YESU na umeamua kwa sasa uwe na shetani.

Ni hatari sana kufanyika mtoto wa Shetani, ndugu nakushauri rudi kwa YESU ili ufanyike mtoto wa MUNGU.

1 Yohana 3:10 "Katika hili watoto wa MUNGU ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na MUNGU, wala yeye asiyempenda ndugu yake."

Ulikuwa mtu mkweli na msema kweli lakini kwa sasa umegeuka na kuwa muongo gwiji, ndugu rudi kwenye asili njema ya kusema ukweli.
Biblia inakushauri hivi "Msiambiane uongo, kwa kuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeuumba.- Wakolosai 3:9-10"

Ulikuwa mtumishi wa MUNGU lakini kwa sasa umekuwa mtumishi wa shetani, Ndugu rudi kwenye asili njema na kumtumikia MUNGU katika KRISTO YESU.

◼️Biblia inakutaka umtumikie Bwana YESU na sio vinginevyo.

1 Wakorintho 15:58 "Basi, ndugu zangu wapendwa, mwimarike, msitikisike, mkazidi sana kutenda kazi ya Bwana sikuzote, kwa kuwa mwajua ya kwamba taabu yenu siyo bure katika Bwana."

Ulikuwa unavaa vizuri sana lakini siku hiyo unavaa kikahaba.

Mithali 7:10 "Na tazama, mwanamke akamkuta, Ana mavazi ya kikahaba, mwerevu wa moyo;"

Ndugu acha kuvaa kikahaba, rudi kwenye asili njema ya kuvaa kiheshima kama iwapasavyo wateule wa MUNGU.
Acha kuvaa kikahaba.

Ulikuwa mnyenyekevu lakini kwa sasa umeota kiburi na umekuwa na kiburi hadi kwa MUNGU.

Ulikuwa ukielezwa mambo ya ki MUNGU unaelewa lakini kwa sasa umeshupaza shingo.

Ulikuwa unasikiliza ushauri mzuri lakini kwa sasa hutaki ushauri wowote wa kiroho wa kukusaidia.
Ndugu katika yote niliyokueleza hakikisha unarudi kwenye asili njema iwapasayo wateule wa MUNGU katika KRISTO YESU.

Ulikuwa unawahesabu wengine kuwa ni bora lakini kwa sasa unajiona wewe ndio bora kuliko watu wote.

Umekwama wapi ndugu?
Umesahau Biblia inakushauri hivi "Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.-Wafilipi 2:3"

Ulikuwa hukata tamaa ukiwa ndani ya Wokovu lakini kwa sasa umekuwa mtu wa kukataa tamaa kwenye kila jambo jema la kiroho, ndugu kwa namna hiyo unajichelewesha mwenyewe kupokea muujiza wa MUNGU.

Ulikuwa na hofu ya MUNGU lakini kwa sasa mzinzi, mwasherati, tapeli, mwizi yaani umegeula wakala wa shetani kabisa.

Asili yako njema umeisahau, asili yako njema ambayo ndio iwapasayo wateule wa KRISTO hiyo asili njema umeisahau na umeiacha.

Ndugu nakushauri tubu na urejee kwenye asili yako njema ambayo ni kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO ulio wa thamani sana.

Matendo 3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"

Ndugu ulikuwa unalitii Neno la MUNGU lakini kwa sasa hulitaki tena Neno la MUNGU.
Kwa sasa kuanzia asubuhi hadi usiku huna muda na Neno la MUNGU, ndugu rudi kwenye asili yako njema iwapasayo wateule wa MUNGU katika KRISTO YESU.

✓✓Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, kuandika meseji na hadi whatsapp).
Share kwa rafiki zako ujumbe huu.

Comments