SADAKA INAWEZA KUWA CHANZO CHA MABAYA KUZUILIWA KWAKO.

N Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele 




Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Neno letu kuu leo linatokea 1 Nyakati 21:1-28, kwa sababu ya kuwa ni  maandiko mengi nitakuwekea machache hapa ila kwa kutaka kujua zaidi unaweza kusoma Biblia yako kuanzia mstari wa 1 hadi 28 ya hiyo Nyakati wa kwanza sura ya 21.

1 Nyakati 21:1 "Tena shetani akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi kuwahesabu Israeli. "

1 Nyakati 21:7-8 "Neno hilo likawa baya machoni pa MUNGU; kwa hiyo akawapiga Israeli. Naye Daudi akamwambia MUNGU, Nimekosa sana, kwa kuwa nimelifanya jambo hili; lakini sasa uuondolee mbali, nakusihi, uovu wa mtumwa wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa."

1 Nyakati 21:13-14 "Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na nianguke katika mkono wa BWANA; kwa kuwa rehema zake ni nyingi sana; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu. Basi BWANA akawaletea Israeli tauni; nao wakaanguka wa Israeli watu sabini elfu."

1 Nyakati 21:22 "Ndipo Daudi akamwambia Arauna, Unipe mahali pa kiwanja hiki, ili kwamba nimjengee BWANA madhabahu hapa; kwa thamani yake kamili utanipa; ili kwamba tauni izuiliwe katika watu."

1 Nyakati 21:26-28 " Kisha Daudi akamjengea BWANA madhabahu huko, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani, akamlingana BWANA; naye akamwitikia kutoka mbinguni kwa moto juu ya madhabahu hiyo ya sadaka ya kuteketezwa. BWANA naye akamwamuru malaika; naye akaurudisha upanga wake alani mwake tena. Wakati huo, Daudi alipoona ya kwamba BWANA amemwitikia katika kiwanja cha Arauna, Myebusi, ndipo hutoa dhabihu huko."

Katika hiyo 1 Nyakati 21:1-28 tunaona Daudi alikosea mbele za MUNGU, kosa lake ilitakiwa kuleta matatizo haya kwa watu wa MUNGU.
1. Miaka mitatu ya njaa.
2. Miezi mitatu ya kupigwa na adui.
3. Siku tatu za upanga wa MUNGU uletao magonjwa ya kuua.

Kwa sababu dhambi aliyoifanya Daudi ilikuwa lazima adhabu itokee basi Daudi alichagua bora kuadhibiwa na MUNGU.

Ndipo MUNGU akaachilia magonjwa na watu sabini elfu wakafa ndani ya hizo siku tatu.

MUNGU akataka kuupiga upya mji mzima lakini kwa neema yake akamzuia Malaika aliyekuwa tayari kuangamiza.

◼️Daudi akaingia kwenye maombi ndipo Malaika ikabidi awasaidie akina Daudi kwa kuwaambia kwamba watengeneze madhabahu ili kutoa sadaka hapo.

◼️Nini kilifuta adhabu ya MUNGU kwa Daudi na mji mzima?

✓✓Biblia inasema katika 1 Nyakati 21:26 kwamba Daudi akajenga madhabahu kisha akatoa sadaka aina mbili, akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani ndipo kupitia tendo hilo tunaona MUNGU akimwambia Malaika kuurudisha upanga wake alani.
Malaika alikuwa tayari kuangamiza kwa upanga lakini baada ya kutengenezwa madhabahu na kutolewa Sadaka njema basi MUNGU alighairi kuwaadhibu ndio maana akamzuia Malaika aliyekuwa tayari kutekeleza amri ya kuwaadhibu.

◼️Watu wengi hawajui nguvu ya sadaka.

Hapa sina maana kila Sadaka bali sadaka zile zinazotolewa kwa kusudi maalumu zikiambatana na maombi maalumu.
Kutoka 35:5 "Katwaeni kati yenu matoleo kwa BWANA; mtu awaye yote aliye na moyo wa kupenda, ayalete matoleo; dhahabu na fedha na shaba;"

Binafsi nimejifunza nguvu ya sadaka, nina shuhuda zangu mwenyewe na za watu wengine nilioshiriki kuomba nao.
Lakini hata ndani ya Biblia kuna mambo ya kushangaza yaliyotokana na sadaka.
Mfano kuna kitu huwa tunakiona kinaitwa upinde wa mvua, kitu hiki kiliumbwa na MUNGU kama ishara ya MUNGU kutokuiangamiza tena dunia yote kwa gharika baada ya sadaka njema ya Nuhu.

◼️Yaani sadaka ya Nuhu ilimfanya MUNGU kusema kwamba halitatokea tena gharika la kuangamiza duniani nzima kama ilivyokuwa gharika la enzi za Nuhu.

Swali kwanini sadaka ndio isababishe neema hii?
Mwanzo 8:20-21 " Nuhu akamjengea BWANA madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. BWANA akasikia harufu ya kumridhisha; BWANA akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya."

◼️Ibrahimu baada ya kuitii sauti ya MUNGU iliyomtaka kutoa sadaka ya kipekee na akatoa basi historia ya maisha yake ilibadilika tangu siku hiyo.

Mambo haya yalitokea kwa Ibrahimu;
✓✓Kubarikiwa na MUNGU, uzao wake kuzidishwa, watoto wa Ibrahimu watakuwa na nguvu daima mbele za maadui zao na mataifa yote duniani watabarikiwa kupitia Ibrahimu.

Swali kwanini ni sadaka tu ndio ifanye mambo haya makubwa na ya ajabu?
Mwanzo 22:15-18 " Malaika wa BWANA akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema BWANA, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee, katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao; na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu."

◼️Kuna nguvu ya ajabu katika sadaka.

Mimi Peter Mabula sitasahau dada mmoja ambaye alikuwa anateswa na nguvu za giza kichwani.
Nguvu hizo za giza alikuwa anaziona kila mara ndotoni na baada ya hapo kichwa kinamuuma, yaani alikuwa anamuona nyoka yupo ndani ya kichwa chake.
Hata aliponishirikisha nimuombee niliomba na kuona nyoka mkubwa akitoka kichwani kwa huyo dada, baada ya siku kadhaa tena Nikamuombea na kuona nyoka akitoka tena kichwani, nilijiuliza ilikiwaje nyoka alitoka harafu amerudi?
Nikimuombea tena kisha zikapita siku nyingi kidogo akaniambia kwamba amepata ufunuo, ni kwamba yule nyoka alikuwa anatoka tukiomba kisha baadae anarudi ni kwa sababu alikuwa na uhalali wa kukaa hapo maana aliingia kwa mtu huyo kwa kafara iliyoelekezwa. Akaniambia anataka atoe sadaka ili kutengeneza agano na MUNGU eneo hilo hilo ambalo nguvu za giza zilikuwa zimeweka agano kwa kafara.

Alituma sadaka yake na niliombea sadaka yake huku nikisimamisha agano na MUNGU sawasawa na Zaburi 50:5 na damu ya YESU KRISTO na zile nguvu za giza ziliondoka na hazikurudi tena kwake.

Nilijifunza kitu kikubwa sana kuhusu nguvu ya sadaka.

Kumbe kuna watu wanateseka kwa sababu ya mikataba ya kishetani iliyofanywa na labda watesi wao au wazazi wao au watu wa karibu wasio wema n.k na kupelekea nguvu za giza zikawa na uhalali kwao, sasa ili kufunguliwa wakati mwingine kama maombi ya kawaida imeshindikana unaweza kuomba ukihusisha sadaka.

Inawezekana kuna familia wako katika adhabu ya MUNGU kwa sababu familia hiyo walishirikiana na miungu, waliua watu wasio na hatia, walienda kwa waganga wa kienyeji n.k
Hapa inahitajika toba na kugeuka na kuziacha njia mbaya.
Isaya 55:7 "Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa."

◼️Ukiwa kwenye maombi au uko kwenye hitaji na ukasikia msukumo wa kutoa sadaka toa maana hilo ndio hitajio la ulimwengu wa roho kuhusu wewe kwa wakati huo ili kupata ushindi wa kudumu.

◼️Wakati mwingine katika maombi husisha na sadaka maalumu inayoambatana na maombi ya Mtumishi wa MUNGU anayejitambua na anajua kuomba kwenye eneo hilo.

✓✓Sio kila maombi lazima uambatanishe na sadaka lakini muhimu sikiliza sauti ndani yako, unapopata ufunuo au unaposikia msukumo wa kufanya hivyo basi fanya haraka maana huo ndio uhitaji kwenye ulimwengu juu ya kufanikiwa kwako.

 ◼️Mkumbuke Daudi ambaye aliambiwa na Malaika juu ya kutengeneza madhabahu na kutoa sadaka ndipo mabaya yakazuiliwa kwake na kwa watu wake.

◼️Ukisimamisha agano na MUNGU kwa sadaka ujue maagano ya nguvu za giza ya kukutesa yatafutika na kwenye eneo hilo hawatakutesa tena.
Zaburi 50:5 "Nikusanyieni wacha MUNGU wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu."

◼️Kuna sadaka huwa zinamfanya MUNGU kuwakemea maadui zako, soma Malaki 3:11, sadaka hizo ni zaka na dhabihu yaani ni fungu la kumi na sadaka ya hiari ya ziada.

Jifunze kitu kutokana tulivyojifunza kuhusu Daudi na jinsi adhabu zilikoma.

◼️Kumbuka pia hili, usitumie sadaka kununua muujiza ila omba au ombewa ukihusisha sadaka ili baraka zilizo ndani ya sadaka ziambatane na wewe.

◼️Kumbuka pia kwamba kiroho sadaka inafanya kazi, kama hutoi ujue hakuna sadaka itafanya kazi kuhusu wewe.

Sasa kama hutii maelekezo ya rohoni ya utoaji unaweza kujikuta pabaya sana maana sadaka za mawakala wa shetani ziitwazo kafara ndio zitakuwa zinafanya kazi kuhusu wewe yaani kukufunga vifungo na kukuzuilia kila jambo jema.

Ndugu zingatia neno la MUNGU na itakusaidia sana.
Kumbuka mambo ya MUNGU hayahitaji mbwembwe bali yanahitaji vitendo tena vitendo vitakatifu.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292( whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments