SIKU YA KUINULIWA.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu. 

Karibu tujifunze Neno la MUNGU.  

Katika dunia wako watu wameinuliwa, wako watu wameinuliwa kiasi, na wako watu wameinuliwa sana na pia wapo watu hawajainuliwa kabisa. 

Nazungumzia tu wale walioinuliwa na MUNGU au watakaoinuliwa na MUNGU na si vinginevyo.  

■Kuinuliwa ni kupandishwa juu na kupewa mahitaji yako uliyoomba.

■Kuinuliwa na MUNGU ni kutoshelezwa na MUNGU hata unakuwa mtu usiyedharaulika. 

Usitafute kuheshimiwa na watu lakini sio mpango wa MUNGU uwe masikini siku zote, sio mpango wa MUNGU uwe mhitaji tu  siku zote.

Biblia inazungumza mengi juu ya umaskini na mhitaji, baadhi ni haya;

1. Tajiri humtawala maskini. 

Mithali 22:7 "Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye."

Inawezekana ni wewe kwa sababu ya umaskini  umekuwa mtu wa kutawaliwa tu na ndugu zako, jirani zako, au wafanyakazi wenzako n.k. 

Je ni mpango wa MUNGU uwe unatawaliwa kila siku?

Sio kweli,  sio mpango wa MUNGU huo. 

2. Maskini huchukiwa hata na jirani yake. 

Mithali 14:20 "Maskini huchukiwa hata na jirani yake; Bali tajiri ana rafiki wengi."

Je unadhani ni mpango wa MUNGU wewe udharaulike na kuchukiwa kwa sababu ya hali yako mbaya ya kiuchumi na kimaisha? 

Sio mpango wa MUNGU kamwe. 

4. Maskini hutengwa na marafiki zake. 

Mithali 19:4 "Utajiri huongeza rafiki wengi; Bali maskini hutengwa na rafiki yake."

Sio mpango wa MUNGU uwe masikini.

Unaweza ukaonekana kama kitu cha kutisha kwa watu wako wa karibu kwa sababu ya umaskini, taabu na matatizo yanayokuandama.

 Zaburi 31:11 "Kwa sababu ya watesi wangu nimekuwa laumu, Naam, hasa kwa jirani zangu; Na kitu cha kutisha kwa rafiki zangu; Walioniona njiani walinikimbia.

Ndugu na marafiki wanaweza wakasimama mbali na wewe wakati wa jambo baya au wakati wa taabu zako. 

Zaburi 38:11 "Wanipendao na rafiki zangu wanasimama mbali na pigo langu; Naam, karibu zangu wamesimama mbali."

Kama ni hivyo ndugu yangu unahitaji kuinuliwa na MUNGU. 

Inawezekana huna kazi ndio maana hakuna anayesimama na wewe karibu. 

Inawezekana ulipofukuzwa kazi hakuna anayesimama na wewe karibu. 

Inawezekana kwa sababu ya hali ya familia yako au ukoo wako hakuna anayetamani kupata mchumba huko.

Ndugu inawezekana hata leo hujui utakula nini kwa sababu huna pesa. 

Ndugu hakikisha tu unaishi maisha matakatifu ya kumpendeza MUNGU, tafuta kazi na uwe mtu wa maombi maana  siku moja MUNGU  ataleta siku ya kuinuliwa kwako.

Dawa ni kufanya kazi na kuomba. 

Fuata kanuni za kibiblia ziletazo mafanikio. 

Zingatia utakatifu, kufanya kazi halali,  kutoa zaka na sadaka na maombi. 

Mweleze Bwana YESU  kwa uwazi juu ya hali yako ukihitaji kutoka katika matatizo uliyopo. 

Zaburi 70:5 "Nami ni maskini na mhitaji, Ee MUNGU, unijilie kwa haraka. Ndiwe msaada wangu na mwokozi wangu, Ee BWANA, usikawie."

Mtegemee MUNGU na huku ukifanya kazi njema ipo siku ya kuinuliwa na MUNGU itafika kwako. 

Umaskini sio wa pesa tu,  uko umaskini wa aina nyingi tu. 

Kuna wenye umasikini wa pesa au mali. 

Kuna maskini wa afya yaani wao kila siku ni magonjwa. 

Kuna maskini wa kukosa kibali n.k

Inawezekana wewe wala hauna umasikini wa pesa ila una umaskini wa furaha katika ndoa yako, MUNGU anaweza kukuinua kwa kuiponya ndoa yako hata amani na furaha vikarejea. 

Inawezekana wewe una kazi lakini huna afya njema, MUNGU anaweza kukuinua kwa kukuponya. 

Inawezekana wewe upo katika ndoa lakini hauna uzao, MUNGU atakuinia na kuponya uzao wa tumbo lako.

Ona mfano huu wa Mwanamke aitwaye Hana. 

 Hana   alikuwa na vitu vingi lakini kwa kukosa mtoto kulimfanya aonekane wa chini sana.

 Lakini Hana tegemeo lake ni lilikuwa kwa JEHOVAH muumbaji, hivyo aliomba na kuiniliwa katika uzao. 

Hakika MUNGU humwinua mnyonge.  

1 Samweli 2:8 "Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina BWANA, Naye ameuweka ulimwengu juu yake."

Baada ya MUNGU kumwinua Hana akazaa watoto, na Hana  alipata sio bora uzao lakini bali alipata uzao bora.

Ndugu unapohitaji mafanikio basi yahitaji kwa MUNGU. 

Ukihitaji mafanikio kipepo utakufa hata kabla hujafaidi hayo mafanikio ya kipepo,  ni hatari sana. 

Ukitafuta mafanikio kipepo utaishia kuibiwa na kudhalilika na kufungwa vifungo vya giza.  

Ndugu husika na YESU KRISTO maana ana ushindi wako.

Zaburi 72:13 "Atamhurumia aliye dhaifu na maskini, Na nafsi za wahitaji ataziokoa."

 Na kama ulikuwa hujui ni kwamba mtu kwa kumwamini MUNGU na kumtegemea basi MUNGU anaweza kumwinua mtu huyo kutoka katika hali ya chini na kumpandisha juu sana. 

Zaburi 113:7-9 " Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, Na kumpandisha maskini kutoka jaani. Amketishe pamoja na wakuu, Pamoja na wakuu wa watu wake. Huweka nyumbani mwanamke aliye tasa, Awe mama ya watoto mwenye furaha."

Inawezekana huduma yako imefungwa. 

Inawezekana familia, ukoo, uchumba, kazi au uchumi wako umefungwa, ndugu ng’ang’ana na YESU kwa maombi na utakatifu maana vifungo vitakuachia na utainuliwa sasa. 

Isaya 10:27 "Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta."

Achana na hirizi, achana na udi wala uvumba, achana na kwenda kwa waganga,  achana na wizi,  achana tunguli, achana na kila kazi ya shetani uliyodanganywa na mawakala wa shetani. 

Ndugu sasa mkimbilie YESU KRISTO Mwokozi anayeokoa  na utaokoka,  uchumi wako utaokoka,  ndoa yako itaokoka,  kibali chako kitaokoka.

 

Inawezekana ndoa yako ina dhoruba kali. 

Inawezekana unapokaa kuna shida.

Inawezekana watu wanakuchukia bila kosa.

Inawezekana mke au mme amekukimbia  

Inawezekana ndugu zako wamekikimbia wote.

Ndugu mkimbilie YESU Mwokozi maana yeye ndio rafiki wa kweli na asiyebadilika. 

Tubu dhambi zako na anza kumtegemea MUNGU katika KRISTO YESU, fanya kazi na maombi  na muda wako wa kuinuliwa utafika. 

Waliomwambia YESU awaokoe aliwaokoa. 

Mathayo 8:25 "Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwamsha, wakisema, Bwana, tuokoe, tunaangamia."

 Ipo siku ya kuinuliwa na itafika siku moja.

Itarajie hiyo huku ukifanya kazi,  ukiishi maisha matakatifu,  ukiwa mwaminifu katika utoaji na ukiwa mtu wa maombi na siku ya kuinuliwa kwako itafika kwa jina la YESU KRISTO. 

Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri. 
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Whatsapp, Sadaka, Maombi na ushauri)

Comments