UNAPOOKOKA KISHA UKAAONA VITA IMEONGEZEKA TAMBUA HILI.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

Kuna baadhi ya watu wachache walipoamua kuokoka vita ya kiroho ilizidi, mabaya ni kama yaliongezeka, nguvu za giza ni kama ziliinuka zaidi, ndugu kama ni wewe jifunze ujumbe huu.

Kutoka 5:22-23 " Musa akarudi kwa BWANA, akasema, BWANA, mbona umewatenda mabaya watu hawa? Kwani kunituma mimi? Kwa maana tangu nilipokwenda kwa Farao, kusema naye kwa jina lako, amewatenda mabaya watu hawa; wala hukuwaokoa watu wako hata kidogo."

✓✓Waisraeli walipookoka adui yao alionekaana kama ana nguvu kuliko Mwanzo lakini ona kile MUNGU alisema.

Kutoka 6:1 "BWANA akamwambia Musa, Sasa utaona nitakavyomtenda Farao; maana kwa mkono hodari atawapa ruhusa kwenda zao, na kwa mkono hodari atawafukuza katika nchi yake."

✓✓Kwa hiyo japokuwa Farao ambaye ni adui wa Waisraeli waliokoka, huyo Farao alionekana kama ana nguvu lakini MUNGU alisema atampiga huyo adui wa Israeli.

◼️Ndugu, wakati mwingine ni kawaida adui yako kwenye ulimwengu wa roho kuonekana ana nguvu baada ya wewe kuokoka lakini uwe na uhakika MUNGU atamtowesha adui huyo.

✓✓Kumbuka pia walio nje a ufalme wa MUNGU watajaribu kukuchukiza ili umwache YESU KRISTO, ndugu ng'ang'ania kwa YESU KRISTO, usikubali mtu yeyote akuondoe kwa YESU.

Wakala wa shetani anaweza kuonekana ana nguvu kwa muda lakini mwisho wake u karibu na wewe utakuwa mshindi.

Waisraeli walianza kulalamika baada ya MUNGU kuwaokoa maana walimuona adui yao kama ana nguvu kuliko mwanzo lakini siku chache baadae hao hao Waisraeli walijikuta wanaimba wimbo huu wa kumsifu MUNGU baada ya MUNGU kumtowesha Farao na jeshi lake lote.

Kutoka 15:1-5 " Ndipo Musa na wana wa Israeli wakamwimbia BWANA wimbo huu wakanena, na kusema, Nitamwimbia BWANA, kwa maana ametukuka sana; Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini. BWANA ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni MUNGU wangu, nami nitamsifu; Ni MUNGU wa baba yangu, nami nitamtukuza. BWANA ni mtu wa vita, BWANA ndilo jina lake. Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini, Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu. Vilindi vimewafunikiza, Walizama vilindini kama jiwe."

✓✓Hata wewe kama umeokoka kisha ukaona kama vita ya kiroho imekuwa kubwa kuliko vyanzo, ndugu hiyo vita ya muda tu maana MUNGU atawatowesha hao maadui zako katika ulimwengu wa roho.

 Haijalishi hao maadui ni majini au mizimu, haijalishi ni wakuu wa giza au wakuu wa anga, haijalishi ni uchawi au aina nyingine yeyote ya majeshi ya pepo wabaya, hao adui wote watatoweka.

MUNGU anasema Katika Isaya 41:10-13 kwamba "usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni MUNGU wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia."

Mimi Peter Mabula nakusihi na nakuomba sana rafiki yangu unayesoma somo langu hili endelea na YESU kwa utakatifu, utoaji, kutafakari Neno la MUNGU na maombi na ushindi kwako sio hiari bali ni lazima.

Kuna adui wa kiroho wanainuka dhidi Yako ili waangamie.
Adui huyo anainuka Ili MUNGU wako ampige adui huyo kwa ajili Yako.

Kumbu 28:7 "BWANA atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba."

Adui akipigwa amelala wenzake wanaweza kusema amepigwa kwa sababu alikuwa amelala, Sasa kwa sababu MUNGU ana Nguvu kuliko adui wote ndio maana Kuna Maadui anawapiga wakati wameinuka.

Hivyo adui Yako anainuka dhidi Yako ili apigwe na MUNGU hivyo usiogope vinapotokea vita baada ya Wewe Kuokoka.

Isaya 2:12 "Kwa maana kutakuwa siku ya BWANA wa majeshi juu ya watu wote wenye kiburi na majivuno, na juu ya yote yaliyoinuka; nayo yatashushwa chini."

Kuna Maadui wengine wanainuka ili MUNGU aonyeshe Nguvu yake hivyo kazi Yako ni kupigana vita ya kiroho kwa Maombi, kuishi Maisha matakatifu na kutumia mamlaka ya Jina la YESU KRISTO.

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Sadaka ya kuipeleka Injili,whatsapp, ushauri n.k).
Ubarikiwe 

Comments