![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana Yesu asifiwe sana Mtumishi wa MUNGU Peter Mabula. Ninamtukuza sana MUNGU kwa ajili yako, kupitia masomo ambayo nimekuwa nikiyasoma kutoka kwako. Ni ukweli usiopingika kuwa masomo yako pamoja na maombi unayoniombea yamebadilisha maisha yangu ya kiroho na kimwili kwa kiwango kikubwa mno. Sivyo nilivyo kabla ya haya msomo, ninamuona MUNGU kwa viwango vya juu. Hakika maarifa niliyoyapata na ninayoendelea kupata kupitia masomo yako na maombi yamenivusha sana kwenye dhoruba na misukosuko ya maisha ya kiroho na kimwili. Kazi yako si bure Mtumishi wa MUNGU. MUNGU wa mbinguni akukumbuke kwa hili. Sina cha kukupa Mtumishi wa MUNGU zaidi ya kusema MUNGU wa mbinguni akutunze na kukuinua zaidi na zaidi na kuendelea kukupa mafunuo kwa Utukufu wake katika KRISTO YESU. Ni mambo mengi ninayo ya kushuhudia lakini leo naomba nikueleze kitu ambacho nimekuwa ninasukumwa nikueleze kwa muda wa siku nne sasa, na leo niliambiwa asubuhi nikiwa bafuni kuwa nisiposema leo basi...! Jambo lenyewe ni hivi:
Kama ambavyo nilishakueleza mwanzo kwa kifupi kuwa kwa asili mimi nilizaliwa kwenye familia isiyo ya Kikristo, ndugu zangu na wazazi wangu ni sio wakristo. Nilipofika darasa la Saba mama yangu mzazi alinipeleka kwa baba yake mzazi yaani babu yangu kwa ajili ya kufanyiwa mazindiko ili nifaulu darasa la Saba. Mtumishi wa MUNGU, babu yangu alinichanja chale mwili mzima kwenye kila kiungo cha mwili wangu hadi kwenye ulimi alinichanja. Pia alinizungushia kuku akiwa anasema maneno lugha nisiyoielewa! Pamoja na yote waliyonifanyia darasa la Saba sikuchaguliwa yaani sikufaulu!
▶ Tangu YESU aliponiokoa na kuanza kuijua kweli na kuiona nuru ya KRISTO YESU na ufahamu wangu ukafunguka kujua kuwa nilikuwa gizani nimeomba kila maombi juu ya hizo chale na maagano hayo ya kichawi kufuta na kuvunja kwa Damu ya YESU lakini bado mara nyingi naota ndoto za kijijini nilikozaliwa, na kila nikikumbuka hizi chale nakosa amani pamoja na kuwa nilishaomba sana toba na msamaha kwa YESU KRISTO kwa ajili yangu na kwa huyo babu yangu mwenyewe niliomba toba na rehema lakini bado maisha mambo yanaenda kwa uzito mno. Sasa tangu Jumapili nilipokuwa naomba jioni kabla sijafungua kula nikaambiwa nikuambie hili jambo kuwa babu yangu alikuwa mganga wa kienyeji (mchawi) na mke wake yaani bibi yangu alikuwa ni mkeketaji, alikeketa watoto wa kike hapo kijijini! Kwa sasa babu na bibi yangu ni marehemu, walishafariki.
Siku moja nikiwa naomba nikaona kuwa kumbe ile damu ya kukeketa bibi alikuwa anatoa sadaka kwa madhabahu ya miungu yao!
Nisikuchoshe naomba leo niishie hapo! Unaweza tu kujua sasa kwa nini niko katika vita ya kiroho muda mrefu, hasa katika kusoma Biblia ni shida na mtihani mgumu kwangu, nasoma lakini kwa kutumia nguvu nyingi mno. YESU kwa neema yake ninaishi!
Asante sana Mtumishi wa MUNGU.
Majibu ya Mtumishi Peter Mabula;
MUNGU akubariki sana sana, ninachoweza kusema ni hivi, MUNGU atakuvusha katika haya salama.
Mimi utotoni pia niliwahi kuchanjwa chale na nilipookoka nikapata maelekezo haya na nikafuta hizo kamba za shetani na niko huru.
Mambo ya kufanya.
1. Kutubu kwa kilichosababisha miungu kuwatumia wazazi wako kwa ajili ya kujiunganisha nayo.
Matendo 3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"
2. Kujitenga na miungu ki maombi.
Kutoka 23:13 "Yaangalieni hayo yote niliyowaambia; wala msitaje kabisa majina ya miungu mingine, wala yasisikizwe kutoka kinywani mwako."
3. Kufuta agano la kipepo la damu yangu mwenyewe.
Kutoka 34:15 " Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi, watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, na kuitolea sadaka miungu yao; mtu mmoja akakuita, ukaila sadaka yake."
(Maana damu ya mtu anayechanjwa chale ndio huchanganywa na dawa katika mwili wake baada tu ya kuchajwa).
Agano hilo la damu za chale unalifuta kwa damu yaa YESU KRISTO tu
1 Yohana 1:7" bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote."
4. Kutoa sadaka kwa MUNGU ili hiyo sadaka iwe muhuri wa agano jipya kati yangu na MUNGU.
Zaburi 50:5 "Nikusanyieni wacha MUNGU wangu Waliofanya agano nami kwa dhabihu."
likisimama agano na MUNGU ujue agano na mashetani linakoma.
5. Kuzifuta chale na kilichobebwa na kusudi la aliyekuchanja(Kufuta chale na kazi yake kulingana na aliyekuchanja) unafuta kwa damu ya YESU KRISTO.
Ufunuo 12:11 "Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa."
6. Chale huambatana na roho za kipepo za kufuatilia hivyo zipige hizo roho kwa maombi ya vita.
Waefeso 6:12 "Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."
7. Mtumishi anaweza kuhitimisha kwa kukuombea ili kutangua kila kazi ya shetani iliyokushikilia kupitia chale, madawa uliyopakwa na kupitia ana kupitia damu yako iliyotumika.
2 Wakorintho 5:20 "Basi tu wajumbe kwa ajili ya KRISTO, kana kwamba MUNGU anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na MUNGU."
Mimi nitakuombea katika hilo.
Akikukumbuka YESU KRISTO, shetani anakusahau.
MUNGU akubariki sana.

Comments