USHUHUDA WENYE MAJIBU.

USHUHUDA WENYE MAJIBU.
Bwana YESU apewe sifa milele Mtumishi wa MUNGU. Habari ya asubuhi. Ninamshukuru sana MUNGU kwa ajili yako Mwinjilisti Peter Mabula kwa kutushirikisha mfungo wa mwezi mzima ambao bado tunaendelea nao. Binafsi nilipata kibali cha kuungana nanyi kimaombi pamoja na kufunga.
Napenda kushuhudia matendo makuu MUNGU aliyonitendea. MUNGU alinionyesha *Waraka* na *Kalenda* ya *siri* sana iliyokuwa imeandaliwa miaka 36 iliyopita na wachawi juu ya maisha yangu na ndugu zangu. Huo waraka uliandikwa mwaka 1983. Si kitu kirahisi kupata siri hiyo ni kwa sababu MUNGU aliamua nione nikakumbuka Neno la MUNGU Yeremia 33: 3 "Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua".
Ilikuwa hivi: Siku ya 15 ya mfungo tulipanga kukutana na ndugu zangu, mmoja kati yao akatuambia kuna nyaraka alipewa na mama yetu mzazi miaka mingi anataka tuzipitie kwa sababu ameona ni vema tukajua hicho kitu kilichoko katika hizo nyaraka kwa sababu mama alimwambia atushirikishe. Mama alizipata hizo nyaraka mahali zilipokuwa zimefichwa na baba yetu mzazi..... akasema ni vitu vigumu inabidi tuvumilie. Mdogo wangu alikaa na hizo nyaraka zaidi ya miaka kumi, kila akiwaza kutushirikisha alikuwa anasahau...! Au akizitafuta alikuwa hazioni hapo alipoweka. Hiyo siku ya kukutana ilibidi aombe sana na kuzifunga kwa Damu ya YESU kwenye begi lake.. kwa sababu hiyo.. kabla ya kuzifungua kwa ajili ya kusoma nilimwambia anipe niziombee kubatilisha kila hila na nguvu ya kichawi iliyoambatana nazo. Tulianza kupitia moja baada ya nyingine...ukweli ni kwamba kuvumilia kibinadamu ilikuwa ngumu kiasi kwamba tulianza kulia kwa sababu kwenye hiyo Kalenda ya kichawi ndugu zetu wawili walishafariki katika vifo vya kutatanisha na muda waliokufa ni kama Kalenda ilivyokuwa inaonyesha... Nilimuomba sana MUNGU anipe uvumilivu na kusamehe ili niweze kupambana ili MUNGU aweze kuingilia kati atuokoe tuliobaki na ambao tuko ndani ya hiyo Kalenda ya kichawi.
Pia tulijua katika ndugu zetu aliyekabidhiwa li-kitabu likubwa na huyo Mzee ambacho hicho kitabu aliyekabidhiwa alifikiri ni cha dini... alipopeleka msikitini wakakikataa wakasema hiki ni uchawi... huko ndani kuna dua ambazo ukisomea mti au kitu chochote unakauka!
Ninachoendelea kufanya ni toba. Ninatubu kwa ajili yangu binafsi, ndugu zangu, wazazi wangu na wazazi wao yaani babu zetu! Nikitumia Daniel 9: 4-19 Ili tuweze kupata rehema za MUNGU kutukomboa...
Kitu tulichosahau mpaka sasa Mtumishi wa MUNGU ni kwamba hatukukumbuka kabisa mpaka tunaachana kumuuliza huyo ndugu yetu baada ya kitabu kukataliwa alikipeleka wapi? Sielewi hata ni kwa nini tumesahau.
Kwenye hicho kikao tulikuwa ndugu watatu. Huyo aliyekuwa na hizo nyaraka ameokoka anampenda Yesu, ni mkristo mchanga. Huyo mwingine siyo mkristo na ndiye aliyepewa kitabu! Nina mengi ya kusimulia lakini leo naishia hapa.
Mtumishi wa MUNGU Peter Mabula pamoja na ushuhuda huu kwako nakuomba unisaidie maarifa jinsi ya kutoka katika haya.
MUNGU wa mbinguni aendelee kukutunza na kukupa mafunuo zaidi ili watu wengi kupitia wewe waweze kuokolewa na kumtumikia MUNGU aliye hai KRISTO YESU.
ASANTE ROHO MTAKATIFU, ASANTE YESU KWA KUFUNUA HII SIRI KWANGU. ASANTE KWA UPENDO WAKO KWANGU. Hakika kwangu huu ni muujiza mkubwa sana.
(Majibu ya Mtumishi Peter Mabula hii haya chinu.)
Aiseeeee.
Nimeshangaa sana ila MUNGU akubariki sana kwa kutushirikisha ushuhuda huu wa ajabu.
Usijali maana katika KRISTO YESU umeshashinda tayari.
Tutaongea kwa simu na kuomba juu ya hili.
Katika nini cha kufanya juu ya hili ni hiki.
1. Tubu kwa chanzo cha tatizo.
Matendo 3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"
2. Haribu na kuteketeza nguvu za giza zinazotekeleza kalenda hiyo ya kichawi.
Zaburi 2:9 "Utawaponda kwa fimbo ya chuma, Na kuwavunja kama chombo cha mfinyanzi."
3. Wapige wasimamizi wa kipepo, wakuu wa giza waliopangwa kutekeleza kalenda hiyo ya kichawi.
Isaya 41:10-12 " usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni MUNGU wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.
Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako."
4. Bomoa Madhabahu ya giza inayosimamia na kuratibu mipango hiyo ya kipepo.
Kumbu 7:5 "Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga."
5. Mwambie MUNGU akulinde usiku na mchana.
Zaburi 121:7-8 " BWANA atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele."
6. Mshukuru MUNGU kwa kukufunulia hayo.
Zaburi 51:6 "Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni; Nawe utanijulisha hekima kwa siri,"
7. Mshukuru MUNGU kwa kukushindia.
Zaburi 28:7 "BWANA ni nguvu zangu na ngao yangu. Moyo wangu umemtumaini, Nami nimesaidiwa; Basi, moyo wangu unashangilia, Na kwa wimbo wangu nitamshukuru."
MUNGU akubariki sana.

Comments