USIKIPOTEZE KIBALI ULICHOPEWA NA MUNGU .

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU juu ya kibali.

◼️Kibali ni baraka ya MUNGU kwa mtu ili mtu huyo astahili, akubalike, asikilizwe, apendwe, aishi, afanikiwe na apokee kinachomstahili n.k

Mfano ni huu.
Danieli 1:9 "Basi MUNGU alimjalia Danielii kupata kibali na huruma machoni pa huyo mkuu wa matowashi."

Je wewe umepewa kibali kwa akina nani?

Umepewa kibali cha nini?

✓✓Kibali ni kukubaliwa hata kama husitahili.

✓✓Kibali ni kitu cha kiroho unachokipata ili kukufanya ukubalike.

✓✓Kibali ni idhini anayopata mtu ili kupata vitu fulani avitakavyo.

◼️Kibali ni baraka ya MUNGU na Baraka hiyo inapaswa kutunzwa , sio kwa kujipendekeza bali kwa kuishi maisha matakatifu ya Wokovu na haki.

Mithali 28:23 "Amkemeaye mwenzake hatimaye atapata kibali; Zaidi ya mtu ajipendekezaye kwa ulimi wake."

✓✓Sasa inawezekana wewe una kibali kwa mwenzi wako ndio maana anakupenda na kukuheshimu.

✓✓Inawezekana wewe una kibali katika jamii au kazini kwako ndio maana kila mtu anakupenda na unapandishwa cheo kila mara.

✓✓Inawezekana wewe una kibali Kanisani au kwenye mtaa wako au ukoo wao au familia yako.

✓✓Inawezekana biashara yako ina kibali mbele za watu wote ndio maana unauza sana.

✓✓Inawezekana wewe una kibali mbele za watu fulani muhimu.

✓✓Inawezekana wewe una kibali ndio maana watu wamekupa uongozi katika Kanisa, jamii, taasisi au katika ofisi uliyopo.

✓✓Inawezekana wewe una kibali cha kiutumishi katika kazi ya MUNGU katika KRISTO YESU.

1 Wathesalonike 2:4 "bali kama vile tulivyopata kibali kwa MUNGU tuwekewe amana Injili, ndivyo tunenavyo; si kama wapendezao wanadamu, bali wampendezao MUNGU anayetupima mioyo yetu."

◼️Hakuna tatizo la mtu kuwa na kibali ila tatizo la watu wengi wenye vibali ni kuchezea vibali vyao kisha wanavipoteza.

Kuna watumishi wa MUNGU wengi walikuwa na vibali sana kwa watu wengi sana, lakini walivichezea vibali vyao kwa dharau, dhambi, majivuno, majigambo n.k kiasi kwamba kwa sasa hawana vibali tena mbele za watu.

✓✓Dhambi, uovu na makosa vinaweza kufuta kibali cha mtu mbele za watu na hata mbele za MUNGU, ndio maana Biblia ina inakushauri hivi " Rehema na kweli zisifarakane nawe; Zifunge shingoni mwako; Ziandike juu ya kibao cha moyo wako. Ndivyo utakavyopata KIBALI na akili nzuri, Mbele za MUNGU na mbele ya mwanadamu. Mtumaini BWANA kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche BWANA, ukajiepushe na uovu.-Mithali 3:3-7

Kuna wanandoa walikuwa na vibali sana kwa wenzi wao lakini walipovichezea vibali vyao vikaondoka na sasa hawana vibali tena ndio maana mitafaruku imechukua nafasi.

Wengine hawakutembea kwenye kusudi la MUNGU ndio maana shetani akawavamia wenzi wao na sasa watu hawa wamekosa vibali mbele za wenzi wao ambao wameshavamiwa na shetani.

✓✓Ndugu, mimi Peter Mabula sijui wewe una kibali gani cha ki MUNGU mbele za watu, hakikisha hukichezei kibali chako hata kikaondoka machoni pa watu.

Jifunze kwa mifano hii.

1. Kiburi na dharau vilimfanya Vashti apoteze kibali chake cha ndoa na hivyo akafukuzwa na ikulu.

Esta 1:12-21 " Bali Vashti, malkia, alikataa kuja kwa amri ya mfalme kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake. ................ Tumfanyieje Vashti, malkia, kwa sheria, kwa sababu hakufanya kama vile alivyoamriwa na mfalme Ahasuero kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba?
Basi Memukani akajibu mbele ya mfalme na maakida, Huyu Vashti, malkia, hakumkosa mfalme tu peke yake, ila na maakida wote, na watu wote pia walioko katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero. Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja.
Basi mfalme akiona vema, na itoke kwake amri ya kifalme, nayo iandikwe katika sheria za Waajemi na Wamedi isitanguke, ya kwamba Vashti asifike tena mbele ya mfalme Ahasuero; na umalkia wake mfalme ampe mwingine aliye mwema kuliko yeye. .............. Basi neno hili likawapendeza mfalme na maakida; naye mfalme akafanya sawasawa na neno lake Memukani."

◼️Kiburi, tabia mbaya, dharau, ukaidi , kujiona, uongo, tamaa mbaya n.k vinaweza kukuondolea kibali kwa ndoa yako, familia yako, kazini kwako, Kanisani kwenu, kwa wateja n.k

Uwe makini sana na usikubali kibali chako kikafutwa na tabia yako mbaya.

Acha dhambi na tabia mbaya na utakuwa na kibali daima.

2. Sauli alipoteza kibali chake mbele za MUNGU kwa sababu ya dhambi, ndio maana akanyang'anywa ufalme na kupewa Daudi.

✓✓Kulikataa Neno la MUNGU kulimuondolea Sauli kibali cha kuendelea kuwa mfalme wa Israeli.

 ✓✓Kumwasi MUNGU na ukaidi vilimuondolea Sauli kibali cha kuendelea kuwa mfalme wa Israeli.

1 Samweli 15:23 "Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la BWANA, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme."

Kwa sababu kibali kiliondoka kwa sauti kwa sababu ya uovu wake, Kibali hicho kilihamishiwa kwa Daudi.

1 Samweli 16:1 "BWANA akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe."

✓✓Inawezekana wewe kwenye eneo lako la kazi ni kama mfalme au Malkia , inawezekana kwenye familia yako au jamii yako wewe ni kama Malkia au mfalme, inawezekana kwenye ndoa yako au uchumba wako wewe ni kama mfalme au malkia.

✓✓Inawezekana kwenye Kanisa au kundi au taasisi uliko wewe ni kama mfalme au malkia .

◼️Ndugu usikubali dhambi, uasi na kulikataa neno la MUNGU vikuondolee kibali ulichonacho.

✓✓Ukilikataa Neno la MUNGU katika KRISTO YESU ujue umekubali kibali cha ki MUNGU kiondoke kwako.

3. Esau alipoteza kibali cha uzaliwa wa kwanza kwa sababu ya njaa.

Mwanzo 25:33-34 " Yakobo akamwambia, Uniapie kwanza. Naye akamwapia, akamwuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza. Yakobo akampa Esau mkate na chakula cha dengu, naye akala, akanywa, kisha akaondoka, akaenda zake. Hivyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza."

Esau njaa ilimfanya apoteze kibali cha mzaliwa wa kwanza.

Hata katika wakati huu ndugu chunga sana kibali chako kisiondoke kwa sababu ya matendo yako.

Inawezekana uko katika ndoa na umechelewa kupata mtoto, sasa unataka kwenda kwa mganga wa kienyeji, ndugu ukifanya hivyo utapoteza kibali kwa MUNGU na utaanza kuishi kama mfu.

Kuna mtu ameokoka ila ameona amechelewa kuolewa hivyo anafanya uasherati, ndugu ukifanya hivyo utapoteza kibali kwa MUNGU na utaanza kuishi kama mfu.

Kuna mtu amefanya maombi na uvumilivu umemshinda hivyo saa amemfuatta shetani, ndugu ukifanya hivyo utapoteza kibali kwa MUNGU na utaanza kuishi kama mfu.

Njaa ya siku moja isikufanye upoteze kibali chako mbele za MUNGU na mbele za watu wa MUNGU.

Tamaa yako isikufanye upoteze kibali chako mbele za MUNGU na mbele za wanadamu safi.

Usaliti wa ndoa yako unaweza kukufanya usiwe na kibali popote.

◼️Kwa Mtumishi, tamaa ya pesa na maisha ya kuiga inaweza ikakufanya upoteze kibali mbele za MUNGU.

Mapenzi kinyume na maumbile kwa wanandoa na wasio wanandoa vinafuta kibali mbele za MUNGU.

Uzinzi, uasherati, punyeto, kujisaga/usagaji, ulevi na kila dhambi hufuta kibali cha mtu mbele za MUNGU.

◼️Ndugu, jitahidi sana chochote kisiondoe kibali chako mbele za YESU KRISTO.

4. Mke wa Lutu alipoteza kibali cha kuokoka kwa sababu ya ukaidi wake.

Malaika wa MUNGU waliwaambia hivi akina Lutu" Jiponye nafsi yako usitazame nyuma, wala usisimame katika hilo bonde po pote; ujiponye mlimani, usije ukapotea. -Mwanzo 19:17

Mke wa Lutu akafanya ukaidi kwa kugeuka nyuma wakati alikatazwa hivyo akafa na kugeuka nguzo ya chumvi.

Mwanzo 19:26 "Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi."

Inawezekana ndugu ulikuwa umeokoka na YESU alikuwa Bwana na Mwokozi wako lakini baadae umeidharau kazi ya Msalabani hivyo umemwacha YESU KRISTO Mwokozi wako na kuzifuata dini zingine, umemfuata shetani awe Mungu wako, ndugu usipogeuka na kutubu na kuanza kuishi maisha matakatifu hakika usishangae utakapopata madhara kuliko mke wa Lutu aliyeudharau wokovu alioupata.

◼️Ndugu kama ulimwacha YESU KRISTO na wokovu wake nakuomba rejea haraka sana.

5. Herode alipoteza kibali cha kuishi duniani kwa sababu ya kumkufuru MUNGU.

Matendo 12:21-23 " Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao. Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya MUNGU, si sauti ya mwanadamu. Mara malaika wa BWANA akampiga, kwa sababu hakumpa MUNGU utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho."

Ni ni hatari sana sana.

Ndugu usikichezee kibali chako chochote ulichopewa na MUNGU.

Je una kibali gani katika jamii au familia yako?

Je una kibali wa mchumba wako Au mwenzi wako wa ndoa ?

Je huduma yako ina kibali?

Je familia yako ina kibali?

◼️Kitunze sana kibali chako na usikubali kufanya machukizo ambayo yatakifuta Kibali chako.

Mfano ni kwamba ukishavuka kwako wakati wa kupendwa unaweza kujikuta utakutana na wakati wa kuchukiwa hata ukashangaa hakuna mtu wa kutaka kufunga ndoa na wewe.

Mhubiri 3:8 "Wakati wa kupenda, na wakati wa kuchukia; Wakati wa vita, na wakati wa amani."

Sasa kama kwako wakati wa kupendwa umeondoka kwa sababu ya tabia zako ujue hicho ni kibali kimeondoka.

Ndugu tafuta ulipotezaje kibali, kama chanzo ni dhambi tubu na urejee kwa Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Kama pia unatumia Facebook ni follow maana itafika kipindi nitakuwa napost tu katika page yangu na profile yangu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments