![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Mimi Peter Mabula binafsi sijawahi kuona wala kusikia mtu yeyote ambaye hajawahi kuona chochote kwenye ulimwengu wa roho kwa maono au ndoto au hata kwa ufunuo .
Ayubu 33:14-15 " Kwa kuwa MUNGU hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani;"
✓✓Kwenye ulimwemgu wa roho watu huona mipango ya MUNGU juu yao, na mipango ya MUNGU ni kukuponya, kukufundisha, kukujulisha nini cha kufanya, kukuelekeza, kukuonya na kukujulisha uko wapi na ufanye nini.
✓✓Kwenye ulimwengu wa roho pia unaweza ukaona mipango mibaya ya wanadamu juu yako au unaweza kuona mipango mibaya ya nguvu za giza dhidi yako au dhidi ya Kanisa au juu ya jamii n.k
✓✓Kwa ujumla watu wengi ukiwemo na wewe huona mambo mbalimbali kwenye ulimwengu wa roho kwa njia ya ndoto na maono.
Mfano ni huu wa kuona kwenye ulimwengu wa roho kwa njia ya ndoto.
Danieli 2:19 "Ndipo Danielii alipofunuliwa siri hiyo katika njozi ya usiku. Basi Danielii akamhimidi MUNGU wa mbinguni."
✓✓Kwenye ulimwengu wa roho unaweza kuona hatari inakufuatilia au inaifuatilia familia yako au watu wako wa karibu au watu unaowafahamu.
✓✓Kwenye ulimwengu wa roho pia unaweza kuona mawakala wa shetani katika maumbo ya wanyama au wadudu wakali na wanaotisha sana.
Mfano kwa maono Mtume Yohana aliona hivi
Ufunuo 12:13-15 " Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume. Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hata mahali pake, hapo alishwapo kwa wakati na nyakati na nusu ya wakati, mbali na nyoka huyo. Nyoka akatoa katika kinywa chake, nyuma ya huyo mwanamke, maji kama mto, amfanye kuchukuliwa na mto ule."
Yohana aliona joka kubwa kwenye ulimwengu wa roho likifanya mikakati ya kumwangamiza mwanamke, tunafahamu maandiko haya yanamzungumzia shetani akijaribu kuliangamiza Kanisa au kuangamiza Israeli lakini hapa ninachotaka kusema ni tukio na kuona kwenye ulimwengu wa roho mambo ya kutisha.
Kwa mfano ndio wewe umeona kwenye maono au ndoto joka kubwa sana ikitaka kukumeza au kumeza watu wako muhimu, nahakika unaweza ukaogopa sana sana.
Labda ni mtoto wako au mtu wako wa karibu anakuambia juu ya kitu cha kutisha sana alichokiona ndotoni, wengine kwa kutokujua nini cha kufanya kimaombi wanaweza hata kujikuta wanaangukia mikononi mwa mawakala wa shetani.
Wengine wameshindwa hata kwenda Kanisani au kusalimiana na baadhi ya watu au wameshindwa kufanya kazi au kusafiri kwa sababu tu ya mambo mabaya ya kutisha waliyoyaona ndotoni.
◼️Ndugu, niko mahali hapa leo kukujulisha kwamba ukishajua kwamba MUNGU wako katika YESU KRISTO ana nguvu hutaogopa.
◼️Kama ukijua kwamba YESU KRISTO ana nguvu kuliko chochote unachokiona kwenye ulimwengu wa roho huwezi kuogopa.
Yeremia 32:27 "Tazama, mimi ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza?"
✓✓Ndugu, katika chochote unachokiona kwenye ulimwengu wa roho kama ukiomba katika jina la YESU KRISTO ujue utashinda na ujue hizo nguvu za giza za kutisha zitakuogopa wewe na kukukimbia.
Siku moja kati ya mwaka 2010 au 2011 nikiwa Zanzibar niliona maono ya kutisha sana, nilikuwa nimelala na ghafla usingizi ukaniondoka usiku wa manane, nikaamka na kukaa, ghafla nikiwa nimekaa nikatazama juu nimezungukwa na sijui kama ni wachawi au majini lakini walikuwa wengi na mkuu wao alikuwa jitu la kutisha akiwa na vichwa zaidi ya 6. Niliogopa maana ilikuwa live nikiwa naona live, na nikasikia mazungumzo yao wakisema wamekuja kuniua, na katika mazungumzo yao nikagundua kwamba nilikuwa napotea mbele yao kisha naonekana ila walitaka wanimalize. Lakini mimi nilikuwa pale pale kitandani nimeweka chandarua nikiwa nimekaa hapo kitandani. Niliogopa sana sana na nikajua kwamba hiyo ni siku yangu ya mwisho kuishi duniani maana ilikuwa ni live, ghafla nikasikia sauti ya mmoja wa hao mawakala wa shetani akisema kwamba kwa sauti kali ya kike kwamba "mkuu yule pale nimemuona, niruhusu nimmalize "
Ghafla nyuma yao akatokea Bwana YESU lakini ni mimi tu ndiye nilimuona, na yeye aliponitazama moyo wangu ukawa na amani ghafla. Baada ya muda kidogo akaondoka na ghafla nikapata ufahamu wa kuomba nikitumia upanga wa MUNGU(Isaya 27:1,Mwanzo 3:24,Ezekieli 21:15) na nikawapiga wote wale mawakala wa shetani.
lakini mwanzo kabla sijamuona Bwana YESU nilikuwa na hofu ya mwisho kabisa, nilijua wananiua lakini siku hiyo akili yangu ilipata ufahamu wa juu hivyo baada ya hapo sikuwa naogopa tena nikiona mambo ya kutisha kwenye ulimwengu wa roho bali muhimu ni kufanya maombi katika jina la YESU KRISTO nikienda kinyume na kila mipango ya shetani niliyoiona.
◼️Ndugu ukishajua kuwa Mwokozi wako YESU KRISTO ana mamlaka juu ya chochote mbinguni na duniani na hata kuzimu basi hutaogopa na kwa maombi utazifuta hizo kalenda za giza ulizoziona kwenye ulimwengu wa roho.
✓✓Ukijua kwamba YESU KRISTO yuko upande wako hakika hutaogopa bali utaomba na kuzishinda hizo nguvu za giza za kutisha ulizoziona.
Isaya 41:10-13 " usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni MUNGU wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu. Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako. Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia."
✓✓Ndugu, hakikisha tu una YESU KRISTO mwenye mamlaka yote mbinguni na duniani.
Mathayo 28:18" YESU akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani."
◼️Ndugu usiwaogope maadui zako katika ulimwengu wa roho bali omba kwa MUNGU katika jina la YESU KRISTO na utawashinda.
✓✓Biblia inasema kwamba hao maadui zako hata kama watakuzonga kama nyuki lakini kwa maombi katika jina la YESU KRISTO watazimika kama moto unavyozimika.
Zaburi 118:12 "Walinizunguka kama nyuki, Walizimika kama moto wa miibani; Kwa jina la BWANA naliwakatilia mbali."
✓✓Ndugu, ukishajua ROHO MTAKATIFU aliye ndani yako ni mkuu kuliko shetani na hata mawakala zake wote huwezi kuogopa.
1 Yohana 4:4 "Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye(ROHO MTAKATIFU) aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye(Shetani) aliye katika dunia."
Wako watu hata hurudi nyuma kiroho pale wanapoona maadui wabaya kwenye ulimwengu wa roho.
Wako watu wanatafuta hata dawa za kiganga au kuwaendea waganga baada ya kuona maadui wabaya ndotoni.
Ndugu usiogope hata kama umeona kitu kibaya kiasi gani.
Unavyoona kwenye ulimwengu wa roho vingine ni mipango ya mawakala wa shetani dhidi yako, kwa kuwa umeona wewe basi inakupasa uharibu mipango hiyo ya kipepo.
Usiogope kwa ajili ya nguvu za giza unanazoziona bali pambana kwa maombi uzishinde na hakika utashinda.
✓✓Katika KRISTO YESU umepewa mamlaka dhidi ya kila nguvu za giza.
Zaburi 91:13 "Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu."
✓✓Usiwape nafasi mawakala wa giza ili wafanikishe jambo lao uliloliona ndotoni bali muite MUNGU katika jina la YESU KRISTO na mipango yao haitafanikiwa kamwe.
Kosa moja watu hufanya baada ya kuona Maadui kwenye ulimwengu wa roho ni kutokuomba.
Ndugu tambua kuwa YESU KRISTO Mwokozi wako ana nguvu kupita wakuu wote wa giza uliowaona ndotoni.
Hivyo basi omba na mipango ya giza haitafanikiwa kamwe.
Omba katika jina la YESU KRISTO na utashinda.
Yohana 14:13 "Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana."
Usiogope ndugu omba na utashinda hata kama kitu hujui maana yake omba.
Omba ndugu na utashinda.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, kuandika meseji na hadi whatsapp).
Ubarikiwe

Comments