UTAJUAJE KAMA UPO KATIKA UWEPO WA MUNGU UKIWA KATIKA MAOMBI.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu.

Rafiki yangu mmoja aliniandikia hivi "Bwana Yesu asifiwe mtumishi wa Mungu, nina swali pia naomba ujitaid tu kunijibu huku inbox ili nielewe zaidi, utajuaje kama uko katika uwepo wa Mungu ukiwa katika maombi? nisaidie tafadhali."

Baada ya ndugu huyo kuniuliza swali nilimjibu vile nilivyojaaliwa,  na hapa leo ngoja nifafanue kidogo  kuhusu baadhi ya namna ambazo zinaweza kutujulisha kwamba tuko katika uwepo wa MUNGU tukiwa katika maombi.

Kwa kifupi uwepo wa MUNGU  kwa sehemu muhimu utadhihilika pale ambapo nguvu za MUNGU zitaonekana wakati wa maombi au Wakati wa Neno la MUNGU. 

Wakristo wengi sana huwa hawajui thamani ya uwepo wa MUNGU wakati wa maombi,  wengi wakati wa uwepo wa MUNGU ndio utawaona wanatoka nje ya Kanisa bila sababu,  utawaona wanaenda chooni bila hata kubanwa na haja,  utawaona mfano binti anachukua mtoto wa mama fulani na kutoka naye nje,   utawaona hawaombi n. k. 

Ukweli ni kwamba kama kuna sehemu unatakiwa ung'ang'anie wakati wa ibada ni wakati wa Neno la MUNGU  na pale nguvu za MUNGU  zimeshuka na uwepo wake. 

Bwana YESU KRISTO aliahidi  kujidhihirisha  kwetu na siku zote hujidhihirisha kwetu kupitia nguvu zake zinazoonekana kwetu wakati wa maombi,  mahubiri na katika mambo ya MUNGU mengine. 

Sasa MUNGU katika KRISTO YESU anapojidhihirisha hapo ndipo pa kung'ang'ania maana majibu ya mahitaji yetu hutokea hapo kwenye uwepo wa MUNGU. 

Yohana 14:21" Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake."

MUNGU  hujidhihirisha kwa nguvu zake. 

Utajuaje kama uwepo wa MUNGU umeshuka? 

Utajuaje  kama upo katika uwepo wa nguvu za MUNGU? 

Mambo haya ya kuonyesha uwepo wa MUNGU ni kwa wateule wa KRISTO.

1. Utajua upo katika uwepo wa MUNGU pale unapohisi nguvu zaidi za kuomba.

Mfano ni huu kwamba huwezi kuomba usiku mzima kama hakuna nguvu za MUNGU zinazokupa nguvu za kuomba. 

Luka 6:12 " Ikawa siku zile aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba MUNGU."

Kukesha usiku kucha kunahitaji nguvu za MUNGU, hivyo nguvu za MUNGU zilikuwepo hapo. 

Kwa hiyo uwepo wa MUNGU  utauona  pale unapoona  hakuna ugumu na uchovu wote wa kuomba umeondoka.

2. Utajua upo katika uwepo wa MUNGU  pale ambapo unaisikia sauti ya ROHO MTAKATIFU akizungumza. 

Matendo 13:2 "Basi hawa walipokuwa wakimfanyia BWANA ibada na kufunga, ROHO MTAKATIFU akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia."

Ukisikia ROHO MTAKATIFU anazungumza na wewe au anazungumza mkiwa ibadani au kwenye maombi au kwenye jambo lolote la ki MUNGU huhitaji  ushahidi zaidi kwamba uko kwenye uwepo wa MUNGU. 

ROHO MTAKATIFU mwenyewe ni MUNGU maana huwezi kumtenganisha MUNGU na Roho wake hivyo mahali popote ROHO MTAKATIFU atakuwepo na atazungumza ujue uko katika uwepo wa MUNGU,  tii sauti ya ROHO MTAKATIFU na ifanyie kazi maana hiyo ndiyo sauti ya kweli kupita zote duniani. 

3. Utajua upo katika uwepo wa MUNGU pale unapopewa ufunuo wa rohoni juu ya nini cha kufanya.

1 Wafalme 17:8-9 " Neno la BWANA likamjia, kusema, Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe."

Ufunuo wa MUNGU ni udhihirisho wa uwepo wa MUNGU  hivyo unapotoka  ufunuo ujue uko kwenye uwepo wa nguvu za MUNGU.

4.  Utajua upo katika uwepo wa MUNGU pale unapopata ujasiri mkubwa wa rohoni ambao kabla ya muda huo haukuwepo.

Zaburi 23:4" Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji."

Yaani hata katika vitisho vikubwa vya kiroho kutoka kwa mawakala wa shetani, wewe una ujasiri na huna hofu wala uoga wowote,  hiyo ni taarifa ya uwepo wa MUNGU kukufunika. 

5.Utajua upo katika uwepo wa MUNGU pale unaponena kwa lugha.

Matendo 1:8 "Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu ROHO MTAKATIFU; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi."

Kunena kwa lugha huambatana na nguvu za MUNGU za hali ya juu, 

huo ndio udhihirisho wa uwepo wa MUNGU.

 Utajua upo katika uwepo wa MUNGU

Unapoona wengine ulionao hapo wakinena kwa lugha au wakipata mwamko mpya wa ki MUNGU

6. Utajua upo katika uwepo wa MUNGU pale Unapoweza kutenda  kitu cha kiroho kile ambacho kabla ya hapo usingeweza

Wafilipi 4:13 "Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu."

7. Utajua upo katika uwepo wa MUNGU pale unapoona miujiza ya MUNGU ikitendeka.

Matendo  19:11 "MUNGU akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida;"

Uwepo wa MUNGU huambatana na miujiza ya MUNGU,  hivyo unapoona miujiza ya MUNGU ikitendeka ujue hapo uwepo wa MUNGU upo.  

8. Utajua upo katika uwepo wa MUNGU pale unapoona Neno la MUNGU likibadilisha watu

Matendo  2:37-39 " Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu? Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake YESU KRISTO, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha ROHO MTAKATIFU. Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu, na kwa watoto wenu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na BWANA Mungu wetu wamjie."

Watu hawa walibadilishwa  na neno la MUNGU kwa sababu Neno la MUNGU huambatana na nguvu za MUNGU na uwepo wa MUNGU. 

Hivyo unapokutana na Neno la MUNGU la kweli  ujue kwenye Neno hilo la MUNGU  kuna uwepo wa MUNGU pia. 

9. Utajua upo katika uwepo wa MUNGU pale unapoona kwa kufunuliwa kwamba nguvu za MUNGU ziko pale maana nguvu za MUNGU huambatana na uwepo wa MUNGU

1 Wakorintho 2:10 "Lakini MUNGU ametufunulia sisi kwa ROHO. Maana ROHO huchunguza yote, hata mafumbo ya MUNGU."

10. Utajua upo katika uwepo wa MUNGU pale unapoweza kutumia jina la YESU KRISTO au damu ya YESU KRISTO au Neno la ufunuo na ukaona matokeo ujue hapo kuna uwepo wa MUNGU.

Marko 16:17-18 " Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya."

11. Utajua upo katika uwepo wa MUNGU  pale unapoona Malaika akikutia nguvu au unapoona usalama rohoni mwako hata kama uko katika hatari.

Luka 22:41-43 " Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.  Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu."

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU KRISTO Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU KRISTO? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU KRISTO Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU KRISTO Kwako.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTOMwokozi.
+255714252292(Whatsapp).
Ubarikiwe sana

Comments