WANAOMPENDA MUNGU.

Peter na Jemimah Mabula 
Watendakazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu. Karibu kujifunza Neno la MUNGU kwa ufupi.

◼️MUNGU anawapenda wale wanaompenda.

✓✓Lakini pia ingawa MUNGU anawapenda wanaompenda lakini wanaomtafuta kwa bidii ataonekana kwao.

Mithali 8:17 "Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona."

Nini nataka kusema?

✓✓Usiishie tu katika kumpenda MUNGU bali mpende na mtafute kwa bidii.

Kuna mambo mengi yanayoonyesha kwamba unamtafuta MUNGU.

Baadhi ni haya:

1. Kumtafuta MUNGU kwa maombi.

Luka 18:1 "Akawaambia mfano, ya kwamba imewapasa kumwomba MUNGU sikuzote, wala wasikate tamaa."

2. Kumtafuta MUNGU kwa matoleo.

Malaki 3:10-12 " Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema BWANA wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la. Nami kwa ajili yenu nitamkemea yeye alaye, wala hataharibu mazao ya ardhi yenu; wala mzabibu wenu hautapukutisha matunda yake kabla ya wakati wake katika mashamba, asema BWANA wa majeshi. Na mataifa yote watawaiteni heri; maana mtakuwa nchi ya kupendeza sana, asema BWANA wa majeshi."

3. Kumtafuta MUNGU kwa kumtumikia katika KRISTO YESU.

Yohana 12:26 "Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu."

4. Kufanyia kazi Neno la KRISTO .

Yohana 14:21 "Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake."

✓✓Kuna faida kubwa katika kumpenda MUNGU na kumtafuta kwa bidii.
Biblia inasema "Nawapenda wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona. Utajiri na heshima ziko kwangu, Naam, utajiri udumuo, na haki pia. Matunda yangu hupita dhahabu, naam, dhahabu safi, Na faida yangu hupita fedha iliyo teule. Natembea katika njia ya haki, Katikati ya mapito ya hukumu. Niwarithishe mali wale wanipendao, Tena nipate kuzijaza hazina zao.- Mithali 8:17-21

Utajiri na heshima ziko kwa MUNGU anawangoja wampendao na wamtafutao kwa bidii.

✓✓Kuna faida kubwa sana katika kumpenda MUNGU katika KRISTO YESU maana MUNGU amewaandalia mema wanaompenda.

1 Wakorintho 2:9 "lakini, kama ilivyoandikwa, Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, (Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,) Mambo ambayo MUNGU aliwaandalia wampendao."

Kumpenda MUNGU sio maneno tu bali ni vitendo, ndio maana hata mzinzi au mchawi au mwizi au mwasherati au mlevi ukimuuliza kama anampenda MUNGU atakujibu kwamba anampenda MUNGU sana, lakini matendo yanakataa maana huwezi kumpenda MUNGU huku unafanya kila mara mambo ambayo ni chukizo kwake.

Muhimu kujua ni kwamba MUNGU anatembea katika njia ya haki na anataka mimi na wewe tutembee katika njia ya haki ambayo ni kuishi maisha matakatifu ya wokovu katika KRISTO YESU Mwokozi.

Kumbu 30:16 "kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda BWANA, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; BWANA, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki."

Nakuomba mtafute MUNGU hadi ukutane naye.
Hakuna aliyekutana na MUNGU harafu akabaki kama alivyo.

Ndugu mpende MUNGU katika KRISTO YESU kwa kutii Neno lake.
Waefeso 6:24 "Neema na iwe pamoja na wote wampendao Bwana wetu YESU KRISTO katika hali ya kutokuharibika."

Je unampenda MUNGU?

Kama unampenda MUNGU mtafute kwa bidii.

Kama MUNGU anawapenda wanaaompenda basi wasiompenda wanakosea sana sana maana kuna faida kubwa katika kumpenda MUNGU.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, sadaka ya kuipeleka Injili,kuandika meseji na  whatsapp).
Ubarikiwe sana.

Comments