![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU.
Ujumbe wa leo unakutaka kuwasaidia watu kulingana na ulichofunuliwa na MUNGU kuhusu wao.
◼️Kama Kanisa tu viungo kila mmoja kiungo cha mwenzake maana yake tunahitajiana kama kundi la watu wa MUNGU waliookolewa na Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu.
Waefeso 4:25" Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake."
◼️Kila mmoja amepewa kipawa chake, karama yake na huduma yake ili kuhudumiana kiroho na wengine.
1 Petro 4:10-11" kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za MUNGU. Mtu akisema, na aseme kama mausia ya MUNGU; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na MUNGU; ili MUNGU atukuzwe katika mambo yote kwa YESU KRISTO. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina."
✓✓Hakuna mtu anayejua yote wala hakuna mtu anayeweza yote.
✓✓Hakuna mtu ambaye anaona vyote au kufunuliwa vyote yeye tu.
Kama Kanisa la KRISTO duniani tunahitajiana sana maana tumepewa karama mbalimbali.
Sasa wakati mwingine MUNGU anaweza kusema na wewe kwa ajili ya wengine.
◼️Tunajua MUNGU husema na watu wake kwa njia ya ndoto au maono au kwa wazo au ufunuo wa ROHO MTAKATIFU wa moja kwa moja, au kwa Neno au kwa andiko au kwa macho ya rohoni au kwa masikio ya rohoni n.k
✓✓Na MUNGU huwa hapangiwi mtu wa kusema naye kitu kwa ajili ya wengine, hivyo anaweza kusema na yeyote yule.
Mfano inawezekana ni wewe umeshajulishwa kwa ndoto hatari zinazowakabili watu wengine hata usio na ukaribu nao.
MUNGU anaweza kukupa ujumbe kwa ajili ya mtu ambaye humpendi sana.
Je ukipewa ujumbe kwa ajili ya wengine huwa unafanyeje?
Wakati mwingine ujumbe huo unaweza kuwa wa hatari kwao,je wewe ndio yule yakitokea madhara unasema "Nilijua haya yatampata huyu maana nikifunuliwa" hiyo ni mbaya sana.
◼️Unajua kwanini MUNGU akufunulie wewe juu ya watu wengine?
1. Ili uwajulishe na kuwasaidia kiroho kulingana na ulichoona.
2. Ili uwaombee, mfano kama ni mabaya yaliyopangwa yasiwapate.
3. MUNGU amekuamini wewe ndio maana akasema na wewe na sio mtu mwingine, hivyo fanyia kazi kwa kuomba na kuwaambia wahusika, kama ni maonyo waonye,kama ni tahadhari waambie haraka.
Unachotakiwa ni kumsaidia mtu kiroho kwa kumwambia ujumbe wa MUNGU uliopewa kwa ajili yake.
Mambo ya MUNGU mengine ni siri hivyo ni baadhi tu hufunuliwa.
1 Wakorintho 4:1" Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa KRISTO, na mawakili wa siri za MUNGU."
◼️Hii maana yake sisi tuliokolewa na Bwana YESU KRISTO tu watumishi wa MUNGU wote na muda wowote kama atakavyo ROHO MTAKATIFU tunaweza kufunuliwa siri yeyote atakayo yeye, na siri hiyo inaweza kuwa msaada kwa mtu aliyekusudiwa, tusipomwambia mtu huyo tunaweza kumfanya apotee au asifanikiwe maana yeye hajui kilichopo mbele yake.
Agizo la MUNGU ni kwamba kama kuna jambo atakuambia usiku au mahali pa siri basi kama ni la kulisema basi liseme nuruni au lihubiri kwa wahusika.
Mathayo 10:27 "Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba."
✓✓Inawezekana ni wewe umeomba sana MUNGU aseme na wewe juu ya jambo fulani lakini MUNGU hajasema na wewe ila kawaambia wengine ili wakujulishe, kama watu hao wakinyamaza ndio hatari.
✓✓MUNGU hapangiwi wa kumfunulia hivyo ujumbe wa wengine uliofunuliwa upeleke haraka sehemu husika na usiache kuomba labda tu kama ROHO MTAKATIFU amekukataza kuupeleka ujumbe huo kwa mhusika ila anakutaka wewe uombe sana kwa ajili ya mtu huyo.
Nimesema MUNGU hapangiwi wa kusema naye hivyo elewe hivyo pia.
Mfano kuna kipindi waisraeli walikuwa na vita na mataifa makubwa waliowazunguka.
Mfalme akaagiza nchi nzima wakutane sehemu moja ili kufunga na kuomba, Katika mkutano huo kulikuwa na watumishi wakubwa wa MUNGU lakini MUNGU hakusema nao bali kwa njia ya wazo MUNGU akasema na mkutano kupitia mtu wa kawaida asiye Mtumishi mkubwa wala maarufu, Biblia inasema
2 Mambo ya Nyakati 20:13-15 " Wakasimama Yuda wote mbele za BWANA, pamoja na wadogo wao, na wake zao, na watoto wao. Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya BWANA, katikati ya kusanyiko; akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; BWANA awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya MUNGU."
✓✓Kwa sababu ni MUNGU alisema hakika Waisraeli walishinda vita bila kupigana vita kama MUNGU alivyosema, kilichofanyika ni kwamba MUNGU aliwachafulia usemi maadui zao wakauana wao kwa wao.
◼️Lakini swali la kujiuliza, kwanini MUNGU asiseme na mfalme. Asiseme na Askofu/Kuhani mkuu, asiseme na nabii mkubwa ila akasema na mtu wa kawaida katika jamii?
✓✓Hapo ndipo tunagundua kwamba MUNGU husema na amtakaye. Ndugu ukiaminiwa na MUNGU hata ukapewa ujumbe wangu, wa kanisa, wa rafiki yako au wa mtu yeyote hakikisha unafuata kile MUNGU atakacho kulingana na ulivyoona.
✓✓Sasa kwenye maandiko hapo juu inawezekana mfalme alidhani MUNGU atasema naye yeye, inawezekana kuhani mkuu alidhani MUNGU atamfunulia yeye lakini MUNGU hapangiwi wa kusema naye, muhimu ni kwamba wewe ndugu ukisemeshwa na MUNGU kwa ajili ya wengine hakikisha unawajulisha na kuwasaidia kiroho kulingana na ulivyofunuliwa.
Ngoja nikupe shuhuda chache juu ya umuhimu wa kuwaambia watu kile ulichosemeshwa na MUNGU kuhusu wao.
Siku moja Mimi Peter Mabula nilikuwa nimelala lakini ilipofika saa saba usiku usingizi ukakata ghafla, nikaamka na nikaanza kuomba, nikiombea maeneo mbalimbali na ilipofika saa Tisa nilisikia sauti ikimtaja jina Dada mmoja ambaye namfahamu, nikashtuka kidogo na nilipewa maonyo juu yake maana alikuwa ni Mtumishi wa Bwana YESU ila akaasi, akaachana na Wokovu, akaanza kunywa pombe na usaliti wa ndoa yake, sasa nilijulishwa live kuhusu yeye na nikaona roho ya mauti juu yake, hivyo nikamuombea lakini roho ya mauti niliendelea kuiona ila nikawa nachelewa kumjulisha maana sikuwa na namba yake.
Yalipita kama masaa 18 nikiwa sina raha na sijamjulisha na naiona roho ya mauti, nikaitafuta namba yake nikaipata kwa neema ya MUNGU, nikamwandikia ujumbe mkali sana, alinipinga na kunidharau na kunisema vibaya. Siku mbili baadae yule Dada akiwa na marafiki zake usiku alipiga kelele ghafla na hali ikawa mbaya akabebwa kupelekwa kutibiwa, kumbe alijifungua kwa operation kama mwaka mzima umepita na alipona lakini ajabu mshono umefumuka, yaani alishapona kidonda cha operation lakini ghafla kovu limefumuka ghafla akaanza kulia na kukosa nguvu.
MUNGU alimpa neema maana alimponya.
Nini nataka kukuambia juu ya hili?
Baada tu ya Mimi kumwambia ndipo nikawa na amani na ndipo nikaacha kuiona roho ya mauti.
Nilishiriki kumuombea ndio maana akapona.
Ningedharau kumuombea na kumjulisha ningekuja kujuta baadae.
Mwishoni mwa mwaka fulani MUNGU hakunipa andiko maalumu la mwaka mpya ila akanipa masomo mengi ya nini cha kufanya katika mwaka huo mpya ki maombi.
Mwanzoni mwa mwaka huo mpya uliofuata kuna Mtumishi wa MUNGU akanitafuta na kuniambia kitu cha ajabu sana juu ya nifanye mwaka huu, aliona vitu vizuri sana(sitavitaja) vingi vikitoka mbinguni kuja kwangu, nilielewa natakiwa nifanye kazi ya MUNGU kwa juhudi sana mwaka huo maana MUNGU ataachikilia Neno lake kwa kiwango kikubwa sana.
Mafunuo hayo kuhusu huduma yangu, huyu Mtumishi aliyaona mwishoni mwa wiki ya mwisho ya kabla ya mwaka mpya kuingia, kipindi hicho nilikuwa nauliza sana kwa MUNGU juu ya mwaka ila sikuona, kumbe yuko aliyejulishwa ila kasahau kuniambia mpaka unavuka mwezi mzima na siku kazaa.
Ndugu hakikisha unafikisha ujumbe wa MUNGU sehemu husika, uwe tu na uhakika kwamba ni MUNGU katika KRISTO YESU amekujulisha.
Wakati mwingine Bwana YESU anaweza kusema na wewe kwa ajili ya wengine, unatakiwa uwajuishe, uwaombee na uwasaidie kama ulivyofunuliwa.
Hata kama ufunuo huo unakuhitaji hata kutoa pesa yako, timiza ndugu.
✓✓Kuna watu wengine unaweza kufunuliwa juu yao ili uwaombee sana na kuwajulisha na kuwasadia na kumbe wana faida kubwa kwako baadae.
Yusufu alisaidia farao kujua ndoto na akawa mkuu wa nchi namba mbili kwa wakati huo.
Unaweza kumjulisha mtu na kumsaidia uliyofunuliwa kuhusu yeye na kumbe mtu huyo miaka 7 ijayo atakuwa Mtumishi wa MUNGU wa kiwango cha juu sana na utamwendea na atakuombea na kupona ugonjwa uliodhani hutapona.
Unaweza kumsaidia mtu kulingana na uliyofunuliwa na MUNGU kuhusu yeye na kumbe miaka michache ijayo atakuja kuwa mtu muhimu sana kwako.
Yako mambo mengi unaweza kufunuliwa na MUNGU juu ya watu wengine, baadhi tu ni haya;
1. Unaweza ukafunuliwa juu ya mipango mibaya ya maadui zao dhidi yao.
2 Wafalme 6:8-10" Basi, mfalme wa Shamu alikuwa akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema, Kituo changu kitakuwapo mahali fulani. Yule mtu wa MUNGU akapeleka habari kwa mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko wanakoshukia Washami. Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale alipoambiwa na yule mtu wa MUNGU, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara moja, wala si mara mbili."
◼️Elisha asingemjulisha Mfalme wa Israeli kile alichofunuliwa kuhusu uvamizi wa washami kwa Israeli wangekufa watu wengi.
✓✓Wewe unaweza kuwa Elisha wa leo unayejulishwa rohoni juu ya mipango ya mawakala wa shetani juu ya mtu fulani, usipomwambia na kumuombea anaweza kupata madhara.
2. Unafunuliwa ili kuwaonya watubu na kutengeneza na MUNGU.
Yona 3:1-10 " Neno la BWANA likamjia Yona mara ya pili, kusema, Ondoka, uende Ninawi, mji ule mkubwa; ukaihubiri habari nitakayokuamuru. Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama BWANA alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu. Yona akaanza kuuingia mji mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki MUNGU; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake; kusema, Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng'ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie MUNGU kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba MUNGU hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili msiangamizwe? MUNGU akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi MUNGU akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende."
◼️Neno la MUNGU lilimjia Yona kama ambavyo linaweza kukujia wewe kwa njia yeyote, Yona asingewahubiri Ninawi wangeangamizwa kama Sodoma na Gomora.
✓✓Ndugu peleka Neno la KRISTO alilokufunulia ROHO MTAKATIFU.
3. Unafunuliwa ili uwajulishe watu kilichoko kwenye ulimwengu wa roho kuhusu wao.
Isaya 38:1-2" Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, BWANA asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba BWANA,"
◼️Ingekuwaje Isaya amefunuliwa kwamba Hezekia asipotengeneza angekufa?
Hakika engekufa, ila Isaya alimweleza kilichoko ulimwengu wa roho kuhusu yeye hivyo akaomba na kutengeneza na MUNGU hata akaongezewa miaka 15 ya kuishi.
✓✓Ndugu kama wewe una roho mbaya kiasi unaambiwa rohoni juu ya madhara yatakayompata fulani unakaa kimya tambua na Neno hili.
Esta 4:14 "Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; ........"
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kuelewa ameelewa.
MUNGU akubariki kwa kujifunza somo hili muhimu na siku moja nitalifafanua zaidi katika kitabu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Sadaka ya kuipeleka Injili,whatsapp, ushauri, Maombi na shuhuda).

Comments