WATOTO WA SHETANI WALIVYO.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi 



Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU wa Mbinguni.

Kuna Watoto wa MUNGU na kuna Watoto wa shetani.

1 Yohana 3:10 "Katika hili watoto wa MUNGU ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na MUNGU, wala yeye asiyempenda ndugu yake."

◼️Watoto wa MUNGU ni watu wale ambao wamemwamini YESU KRISTO na kisha kumpokea kama Bwana na Mwokozi wao na wanaishi maisha matakatifu ya Wokovu.

Yohana 1:12-13 " Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU."

✓✓Ni heri kila mtu afanyike mtoto wa MUNGU kwa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wake.

Sasa kuna watoto wa shetani, hao ndio nataka niwazungumzie kidogo leo.

Yohana 8:44-47 " Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo. Nami, kwa sababu nasema iliyo kweli, hamnisadiki. Ni nani miongoni mwenu anishuhudiaye ya kuwa nina dhambi? Nami nikisema kweli, mbona ninyi hamnisadiki? Yeye aliye wa MUNGU huyasikia maneno ya MUNGU; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa MUNGU."

Katika hii Yohana 8:44-47 tunaona Bwana YESU KRISTO akiwaambia Watu waliokuwepo pale juu ya kile kilicho ndani yao kinachowatenga na MUNGU.

Kupitia hii Yohana 8:44-47 tunafahamu jinsi watu/watoto wa shetani walivyo.

Sifa za watoto wa shetani ni hizi.

1. Wanafanyia kazi tamaa za shetani.

"Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. "

2. Wana roho ya uuaji na uharibifu.

"Yeye(Shetani) alikuwa mwuaji tangu mwanzo;"

✓✓Kama shetani alivyo na roho ya uuaji na uharibifu basi na watu wake lazima wawe kama baba yao.

3. Hawasimami katika kweli ya MUNGU.

"wala (Shetani) hakusimama katika kweli,"

✓✓Na watoto wake hawawezi kusimama katika kweli ya MUNGU.

4. Hawana kweli ya MUNGU ndani yao, yaani hawana Neno la MUNGU ndani yao.

"kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake(Shetani)"

✓✓Na watoto wake hawana kweli ya MUNGU ndani yao.

5. Husema uongo na udanganyifu.

"(Shetani) Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo. "

✓✓Na watoto wake lazima wawe wanaambatana  na uongo na  udanganyifu.

6. Hawamwamini YESU KRISTO kama Mwokozi wao.

"Nami (YESU KRISTO), kwa sababu nasema iliyo kweli, hamnisadiki."

✓✓Watoto wa shetani hawawezi kumsadiki YESU wala hawawezi kumwamini kama Mwokozi wao, ni hatari sana.

7. Hawasikii Neno la MUNGU wala kulizingatia .

"Yeye aliye wa MUNGU huyasikia maneno ya MUNGU; hivyo ninyi hamsikii kwa sababu ninyi si wa MUNGU."

Ndugu kama bado wewe ni mtoto wa shetani hakikisha leo unahama huko na sasa fanyika mtoto wa MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi.

Kama una sifa za kuwa mtoto wa shetani basi nakushauri leo mkimbie shetani na kazi zake zote, kisha mkimbilie YESU KRISTO Mwokozi.
Okoka Ndugu.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(Ni namba hii kupiga, kuandika meseji na hadi whatsapp).
Share kwa rafiki zako ujumbe huu.

Comments