MAPEPO HUINGIAJE NDANI YA MTU?


Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 




Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni tujifunze neno la MUNGU.
Ni mara nyingi tumeona watu wakitokwa na mapepo baada ya maombi kupitia jina kuu la YESU KRISTO, lakini hatujui mapepo hayo yaliingiaje ndani ya watu hao.

Siku moja kati ya mwaka 2010 au 2011  nikiwa Zanzibar niliduwaa baada ya rafiki yangu mmoja ambaye tulikuwa tunasali naye, tunaimba naye kwaya, tunaombea watu pamoja na tulishilikiana katika kazi ya MUNGU kwa mambo mengi sana, lakini siku hiyo tukiwa Kanisani aliniambia kwamba tumbo lake linamuuma hivyo nimuombee, nilipomwekea mikono huku nikiomba ili MUNGU amponye ugonjwa ule ghafla mapepo ndani yake yalilipuka na ilichukua karibu nusu saa mtu yule kufunguliwa na akapona na ugonjwa pia.

Baada ya hapo niliwaza sana na kujiuliza sana maana Mtumishi huyo nilipookoka yeye alikuwa wokovuni muda mrefu tu.
Nilibaki Nikijiuliza mapepo huingiaje ndani ya mtu?
 
Tukisoma Marko 9:25-27 Biblia inasema " Naye YESU akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena. Akalia, akamtia kifafa sana, akamtoka; naye akawa kama amekufa; hata wengi wakasema, Amekufa. Lakini YESU akamshika mkono akamwinua naye akasimama."

Hapa tunaona pepo mchafu akimtoka mtu, je tunaweza kujiuliza huyo pepo mchafu aliingiaje ndani ya mtu huyo?

Tunaona mara nyingi mapepo yakiwatoka watu katika maombezi kupitia jina la YESU KRISTO.
 
Ni mara zote tumeona mapepo yakitoka lakini hatujui hao mapepo waliingiaje ndani ya mtu huyo.

Siku moja pia miaka ya karibuni kama sio mwaka 2017 basi ni 2018 nilikuwa naombea watu kwa njia ya simu.
Mama mmoja alinipigia simu akijitambulisha kuwa yeye ni mtumishi wa MUNGU, aliongea kama mtu ambaye analijua vyema neno la MUNGU lakini wakati namuombea ndipo nilishangaa akipiga kelele na kuanguka, neema ya MUNGU ni kwamba simu haikuwa mbali na sikio hivyo mapepo yakaanza kuzungumza vitu vingi sana, nilikemea sana huku nikimwambia MUNGU kwamba malaika wake awepo pale ili kumsaidia huyo mama aliyepagawa na mapepo isije ikawa hatari maana alikuwa amejifungia chumbani peke yake ili nimuombee.
Baada ya kumuombea na mapepo yale kunyamaza nilibaki na simu kama dakika 4 ndipo nikamuita jina akaitika huku akishangaa maana hajawahi kudondoka mapepo, nilimtia moyo na kumweleza nilichokisikia na akakumbuka alivyofungwa kipepo maana huwa anaota hayo hayo yaliyosimuliwa.
Nilibaki nikiwaza mapepo huingiaje ndani ya mtu?

Kuna watu huota aina fulani za ndoto na ni julisho la kuvamiwa na nguvu hizo za giza ambazo ni mapepo.
Biblia pia inaonyesha kwamba mapepo yakitolewa ndani ya mtu huondoka lakini mtu huyo asipokaa vizuri na YESU KRISTO yanaweza kurudi ndani ya mtu huyo na hali yake inayofuata inakuwa mbaya kuliko mwanzo.
Luka 11:24-26 " Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema, Nitairudia nyumba yangu niliyotoka. Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza."

Ndugu usikubali kamwe kuishi na mapepo maana mapepo ni maroho wa kuzimu ili yakufanye ufanye mambo ya kishetani na kukosa uzima wa milele.

Mapepo ni nguvu za giza ambazo zinatakiwa zikae kuzimu na sio ndani yako.
Hivyo hata kama una mke wako jini au mume wako jini na amekuonya kwamba usiende Kanisani kwenye maombezi mimi nakuomba sana nenda Kanisani na huyo nguvu za giza atakuachia, na ndipo baraka zako zilizokuwa zimezuiliwa na hao majini zitakuja sasa ndani yako au ndani ya ndoa yako au uchumba wako au kazi yako au ufahamu wako n.k

Hakikisha unakimbilia maombezi na katika jina la YESU KRISTO utafunguliwa.

Mapepo ni hatari sana.
Rafiki yangu mmoja siku moja aliniambia nimuombee kwa simu msichana wake wa kazi maana msichana huyo husema kwamba kila siku anatokewa na jini na huyo jini hujitambulisha kama mume wake, yaani huyo msichana wa kazi ameshaolewa na jini na huyo jini humpa maelekezo mengi na humjulisha hadi vitu ambavyo hutokea kweli.
Nilipoanza kumuombea huyo dada ghafla akaanza kupiga kelele huku akipigana na bosi wake.
Makelele hayo yakapelekea majirani kujaa pale na wanaume kumshika ili asilete madhara, simu iliwekwa loud speaker na majirani karibu wote hawakuwa wakristo hivyo maombi yale yalikuwa injili hadi kwa ambao hawajaokoka wakatamani waje Kanisani.
Nilimshukuru sana MUNGU maana injili ya KRISTO iliwafikia watu wengi muda huo lakini nilijiuliza inakuwaje mwanadamu anaolewa na jini?

Inakuwaje mtu mapepo wanaishi ndani yake?

Nimekupa mifano hai hii mitatu ili angalau ujiulize mapepo yanamwingiaje mtu?
Ukijua namna mapepo yanapata kibali hadi kuingia ndani ya mtu basi nina hakika utafunga milango hiyo ili mapepo hayo yasiingie ndani yako au ndani ya watu wako wa karibu.

N muhimu sana kujua mapepo huingiaje ndani ya mtu ili umsaidie mtu huyo asijihusishe tena na mambo yanayoleta mapepo ndani yake.

Ndugu ng'ang'ana sana na YESU KRISTO ili uwe huru siku zote.
Mapepo ukiyaruhusu yanaweza hata mapepo maelfu kukaa ndani yako.
Mfano ni huyu ambaye alikuwa na mapepo maelfu ndani yake.
Marko 5:6-9 " Na alipomwona YESU kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, YESU, Mwana wa MUNGU aliye juu? Nakuapisha kwa MUNGU usinitese. Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu. Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi."

Huyu alikuwa na mapepo legioni yaani mapepo yaliyo jeshi zima, yaani mapepo legioni ni kama mapepo elfu 6 ukiangalia maana ya legioni, ni hatari sana.

Nini nataka kusema kwako ndugu yangu?
Usikubali kuwa nyumba ya mapepo, kaa vizuri na YESU KRISTO na hao mapepo hawataingia ndani yako kamwe.
Lakini pia ni vyema tukajua mapepo huingiaje ndani ya mtu ili tupate maarifa ya kumsaidia mtu huyo ili hata yakimtoka basi asifungue tena mlango hata yakarudi ndani yake.

Je mapepo huingiaje ndani ya mtu?

1. Kuwa mchafu wa kiroho yaani kuwa mtu wa dhambi na maovu ni njia ya mapepo kuingia ndani ya mtu.

Mathayo 12:45 "Mara huenda, akachukua pamoja naye pepo wengine saba walio waovu kuliko yeye mwenyewe, nao huingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza. Ndivyo itakavyokuwa kwa kizazi hiki kilicho kibaya."

Pepo wachafu hufanya mambo machafu na huingia ndani ya watu wachafu kiroho hivyo ukiwa mtu wa kufanya mambo machafu yaani dhambi na uovu ujue ni rahisi kuvamiwa na mapepo.
Epuka sana kuishi maisha ya dhambi kama unataka mapepo wasiingie ndani yako.


2. Kuingia maagano ya kipepo/kishetani ni lazima mapepo wawe na wewe na waingie ndani yako.

Kutoka 23:32-33 " Usifanye maagano pamoja nao, wala pamoja na miungu yao. Wasikae katika nchi yako, wasije wakakufanya kunitendea mimi dhambi; kwa sababu ukiitumikia miungu yao, jambo hili halikosi litakuwa ni tanzi kwako."

✓Mapepo ni watoto wa miungu hivyo ukiingia maagano na miungu ujue umeingia agano na mapepo hivyo lazima waingie ndani yako.

✓Lakini baadhi ya mapepo ni miungu kabisa hivyo maagano ndio huwapa uhalali wa kuingia ndani ya mtu, mfano mizimu ni mapepo yaliyo miungu.

✓Maagano ya kipepo yapo kwa waganga wa kienyeji hivyo ukiwaendea ujue umekaribisha mapepo kuwa ndani yako.

✓Kujiunga na dini ya kishetani, mtu aliye wakala wa shetani kukudanganya n.k

✓Kufanya matambiko ni kuingia agano la kishetani.
Kutambika ni kufanya agano la kishetani.

✓Kutoa sadaka katika madhabahu za mawakala wa shetani ni kuingia agano na miungu.
Kutoa kafara kwa mizimu ni agano la kishetani.

Haya ni baadhi ya maagano ya kishetani ambayo mtu anaweza kuingia na kujikuta amegeuka nyumba ya kuishi mapepo, ni hatari sana.

✓Kuna wengine wamenaswa na mapepo kupitia kuiga uvaaji kama mawigi, vikuku, wanja, mikufu, hereni, pete ambazo wanaita pete za bahati n.k

Sasa unaweza kumuona mtu kavaa mapete makubwa kila kidole na wewe unayatafuta mapete hayo na baada ya muda huo unageuka nyumba ya kuishi mapepo.
Ndugu nakuomba vaa pete ya ndoa tu ambayo umevalishwa Kanisani siku unafunga ndoa na pete hiyo iwe imeombewa na watumishi wa MUNGU.

Ndugu ukitaka mapepo wasikuhusu basi okoka na usikubali kuingia katika agano lolote la kishetani.


3. Kurogwa.

Nahumu 3:4 "Kwa sababu ya wingi wa ukahaba wa yule kahaba mzuri, yule bibi wa mambo ya uchawi, auzaye mataifa kwa ukahaba wake, na jamaa za watu kwa uchawi wake."

Wachawi wapo hivyo kaa vizuri na YESU KRISTO ndipo utakuwa mshindi dhidi yao.

Wachawi wote ni mawakala wa shetani hivyo ukiona umelogwa au mtu amelogwa ujue vitendea kazi vya wachawi ni pamoja na mapepo/majini hivyo wakifanikiwa kumloga mtu ujue na mapepo kuambatana na mtu huyo ni rahisi sana.

Sasa inawezekana wewe wala hujaokoka ndio maana unalogwa kila mara, ndugu kulogwa huko ni njia ya mapepo pia kuingia ndani yako na kujigeuza ugonjwa, kukuvuruga akili, kujigeuza maroho ya kuzimu kama roho ya mauti, roho ya kukataliwa n.k

Ukitaka mapepo yasikuhusu Okoka na ishi maisha matakatifu huku ukiwa muombaji unayemsikiliza na kumtii ROHO MTAKATIFU.


4. Kushirikiana na watumishi wa shetani.


Mfano hai ni huyu mfalme ambaye alishirikiana na wenye mapepo ya utambuzi.
2 Nyakati 33:6 "Tena akawapitisha wanawe motoni katika bonde la mwana wa Hinomu; akatazama bao, akabashiri, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa BWANA, hata kumkasirisha."

✓Ukishirikiana na watumishi wa shetani ujue umekaribisha mapepo maana utendaji kazi wa watumishi wa shetani huambatana na mapepo yaani majini.

✓Mfano mtu mwenye pepo la utambuzi ni lazima akudanganye na hivyo mapepo kupata nafasi ndani yako.

✓Mfano kushirikiana na kazi za wanajimu ujue umekaribisha mapepo/majini kujishughulisha na wewe.

✓Kuna watu leo wana nyota zao mfano unaweza ukamkuta mtu anakuambia kwamba nyota yake ni mshale , nge au simba n.k ukifuatilia vyanzo vya nyota hizo ni majini/mapepo hivyo ukitaka uwe nyumba ya mapepo basi shirikiana na watumishi wa shetani na utashangaa umegeuka nyumba ya mapepo.

✓Hata wahubiri pia wapo mawakala wa shetani hivyo uwe makini sana maana unaweza kujikuta umejiunganisha na shetani na sio MUNGU.

Watumishi hao kuwajua ni rahisi mno, hawahubiri Wokovu wa KRISTO na wanalipinga neno la MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi n.k

5. Kufanya ibada ya sanamu.


Biblia iko wazi sana kwamba inampasa kila mwanadamu mwenye akili timamu basi mwanadamu huyo inampasa kuikimbia ibada ya sanamu.
1 Wakorintho 10:14 "Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu."

✓Ibada ya sanamu ni pamoja na kusujudia sanamu au kuiabudu au kuiheshimu.

✓Kumwabudu shetani au mizimu.

✓Kuabudu wanadamu n.k
Ndugu ukitaka mapepo yasikuhusu basi okoka na anza kumwabudu MUNGU Baba katika Roho na kweli huku ukiishi maisha matakatifu ya wokovu wa Bwana YESU KRISTO Mwokozi.


6. Kumwacha YESU KRISTO na Wokovu wake.


2 Petro 2:20 "Kwa maana wale waliokwisha kuyakimbia machafu ya dunia kwa kumjua BWANA na Mwokozi YESU KRISTO, kama wakinaswa tena na kushindwa, hali yao ya mwisho imekuwa mbaya kuliko ile ya kwanza."

✓Kumwacha YESU KRISTO kunaweza kukufanya uvamiwe na mapepo na hali yako ikawa mbaya zaidi.
Hiki ndicho kitu hatari sana na kinachopelekea mtu kuvamiwa na mapepo.
Kumbuka kuna YESU KRISTO na kuna shetani hivyo ukimwacha YESU KRISTO ujue moja kwa moja umemkaribisha shetani.
Ukiwa na YESU KRISTO katika kweli yake ujue hapo unakuwa umemkimbia shetani na wapambe wake.
Ndugu usije ukamwacha YESU KRISTO kwa vyovyote vile.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Peter  Mabula
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(whatsapp).
Nakuomba share kwa marafiki zako ujumbe huu kama ulivyo,usibadili jina la chochote.

Comments