MAOMBI YA KUACHILIWA

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 




Bwana YESU KRISTO atukukuzwe ndugu zangu wote.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Leo tunajifunza somo kuhusu maombi ya kuachiliwa ili tuombe na kuachiliwa.

✓✓Kuachilia maana yake ni kumsamehe mtu na kumfutia makosa yake na adhabu yake ili visiwepo tena.

✓✓Kwa hiyo ninaposema ''Kuachiliwa'' maana yake ni kuwekwa huru kwa kufutiwa hatia na kuondolewa adhabu.

Biblia inamtaka kila mtu kuwa mtu wa kuwaachilia watu.

Luka 6:37 "Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa."

Maombi ya leo yanakuhusu wewe unayefuatilia somo hili ili kwanza kwa maamuzi yako uwasamehe na kuwaachilia waliokukosea wote kisha omba kwa MUNGU ili uachiliwe na waliokushikilia, waliokufunga kiroho kwa sababu hawajakuachilia.

Hapa Mimi Peter Mabula namanisha watu wa kawaida waliokushikilia Wewe au waliokufunga Wewe kwa maneno yao au viapo vyao.

Lakini kama umeshikiliwa kichawi au kufungwa kichawi omba maombi ya vita ili kuharibu kazi za shetani na utakuwa huru, hapo hakuhitaji kuachiliwa kunahitaji vita ya kiroho kwa maombi ya vita.

Naomba nieleweke kwamba katika maombi ya leo nazungumzia tu watu wa kawaida waliokushikilia au kukufunga na unahitaji kuachiliwa ili uwe huru.

Mfano mke wako au mume wako mlikosana na kukatokea mgogoro kwa sababu ya makosa yako, na hajakuachilia, hajakusamehe na amekufunga kwa maneno mabaya na kifungo hicho kimekupata au kinaendelea kukushikilia.

Wapo watu wamefungwa kiroho na na kushikiliwa kiroho kwa maneno ya wazazi wao au watu wao wa karibu.

Biblia inamtaka kila mtu kuwa mtu wa kuwasamehe watu wengine wa MUNGU na kuwaachilia.

Waefeso 4:32 "tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na MUNGU katika KRISTO alivyowasamehe ninyi."

Kuna watu hawana huruma hata kidogo, hivyo wamewafunga kiroho kwa maneno watu wao wa karibu.

Kuna familia Mama wa familia hiyo watoto wake walimkosea kidogo sana akawatamkia maneno mabaya kiasi kwamba mtoto mmoja akawa kichaa, watoto wengine wakajikuta wanateswa na nguvu za giza kwa kiwango cha ajabu sana yaani ni kama Mama yao kwa maneno yake aliwakabidhi kwa nguvu za giza, mtoto mmoja kati hao wanne ndiye aliyenipigia simu akihitaji maombi na kunielezea yaliyotokea Kutokana na maneno ya Mama yao mzazi.

Wako watu wamefungwa kiroho kwa maneno ya watu waliyotamkiwa utotoni au shuleni au kazini au popote.
Biblia inatutaka tuwe na huruma kwa watu wa MUNGU.

Luka 6:36 "Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma."

✓✓Wako waliofungwa kiroho na wenzi wao.

✓✓Wako watu waliofungwa kiroho na ndugu zao.

✓✓Wako watu waliofungwa kiroho na wachungaji wao au watumishi wa MUNGU.

Kama Kanisa la MUNGU Biblia inatutaka tuchukulianae na kusameheana kama ambavyo MUNGU hutusamehe sisi tunapotubu.

Wakolosai 3:13 "mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama BWANA alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi."

✓✓Wako watu waliofungwa kiroho na walezi wao, vifungo vya kiroho vimewapata na vinawatesa sana na kuwashikilia, sasa wanajaribu kuomba msamaha lakini bado hawajaachiliwa na hawajatoka kifungoni.

Ndugu, ni nani hajakuachilia na ulimuomba msamaha?

Inawezekana ulimkosea mtu na akakutamkia kwamba hutafanikiwa kamwe katika biashara na imekuwa hivyo.

Inawezekana ndugu yako wa karibu au mzazi wako alikulaani umeshikiliwa na laana hiyo ambayo ilitokana na makosa yako.

Inawezekana ulimkosea Mchumba wako au mchungaji wako akakufunga kwa maneno kwamba hata uende wapi hutafanikiwa na imekuwa hivyo.

✓✓✓Ndugu, Nakushauri yeyote aliyekushikilia kwa sababu ulimkosea, nakuomba muombe  msamaha mara moja kama yupo hai  na asikupe masharti ya msamaha kisha kama hajakuachilia au hajakufungua wewe mkimbilie YESU KRISTO na utafunguliwa na kuwa huru.

✓✓Kama uliyemkosea akakufunga kwa maneno yake hayupo Duniani, tubia dhambi Yako kwa MUNGU katika KRISTO YESU Kisha omba kwa MUNGU uachiliwe kifungo hicho utaachiliwa, pia Dawa nyingine kubwa sana ya kuachiliwa vifungo ulivyoshikiliwa ni kuamua Kuokoka yaani Mpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako na vifungo vingi automatically vitaondoka vyenyewe maana Sasa utakuwa Mwana wa ufalme wa MUNGU katika KRISTO YESU.

✓✓Damu ya YESU KRISTO inafuta dhambi, inamtakasa mtu , inamuosha mtu na kumsafisha na kila dhambi na udhalimu uliomshikilia.

1 Yohana 1:7" bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake YESU, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote."

Inawezekana ulimkosea mtu akalulaani na baada ya muda akafariki hivyo huna hata muda wa kumuomba msamaha lakini kiapo cha laana alichokuapia kimekushikilia daima.
Ndugu, tubu kwa MUNGU kisha omba maombi ukitumia damu ya YESU KRISTO ili kukutakasa na laana hiyo uliyojisababishia mwenyewe.

Damu ya YESU KRISTO iko juu ya kila laana, Damu ya YESU KRISTO iko juu ya vifungo vyote vya kiroho.

Hakika katika jina la YESU KRISTO utakuwa huru.

Fuata tu maelekezo kwamba kama mtu huyo uliyemkosea akakulaani yupo muombe msamaha na kama hajakusamehe basi huna hatia mbele zake wewe mkimbilie YESU KRISTO na utakuwa huru hata kama bado ndugu huyo anakuchukia.

Kama mtu uliyemkosea amekataa kukuachilia, wewe kwa maombi mkimbiliee YESU KRISTO na kitakachofanyika amani ya MUNGU kuutengeneza moyo wa aliyekufunga ili akuachilie au MUNGU Mwenyewe kukuachilia na kuifuta hatia yako na adhabu yake.

Kumbuka Bwana YESU alikuja kutuweka huru dhidi ya kila hatia.

Isaya 61:1 "ROHO ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu BWANA amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao."

YESU KRISTO akikukweka huru hakika utakuwa huru kwelikweli.

Yohana 8:36 "Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli."

Kwanini unahitaji sana kuachiliwa?

✓✓Ni kwa sababu kutokuachiliwa kuna madhara mengi na matokeo mengi mabaya.

Baadhi ya madhara anayoweza kuyapata mtu ambaye hajaachiliwa.

1. Kuzuiliwa kuzaa.

Hesabu 5:28 "Na kama mwanamke hakuwa na unajisi lakini yu safi; ndipo ataachiliwa, naye atazaa wana."

Inaposemwa "ataachiliwa" maana kabla alikuwa amefungwa.

2. Unaweza usiachiliwe hadi siku ya kufa kwako, hivyo kifungo kilichotokana na kutokuachiliwa kikakutesa siku zako zote za kuishi duniani.

Ayubu 21:30 "Kwamba mwovu huachiliwa katika siku ya msiba? Na kuongozwa nje katika siku ya ghadhabu?"

Kwanini uteseke mpaka mwisho wa kuishi kwako kwa sababu hujaachiliwa na Mtu? Leo mkimbilie YESU KRISTO Mwokozi utaachiliwa na kuwa huru Kabisa.

✓✓Lakini pia nina neno kwako wewe ambaye umeshindwa kumsamehe mtu na kumwachilia hata anateseka kwa sababu ya neno lako la kumfunga ulilomtamkia.

Wewe usiyewaachilia watu usidhani kwamba wewe uko salama.

Haya yanaweza kumpa mtu asiyesamehe na kuachilia wengine.

1. Na wewe hutasamehewa na MUNGU.

Mathayo 6:15 "Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu."

2. Uzima wa milele hauwezi kukaa ndani yako.

1 Yohana 3:15 "Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji: nanyi mnajua ya kuwa kila mwuaji hana uzima wa milele ukikaa ndani yake."

Ukiona mtu hujamwachilia maana yake bado unamchukia na kama unamchukia wewe ni muuaji na uzima wa milele hauwezi kukaa ndani yako.

3. Mabaya hayataondoka kwako.

Mithali 17:13 "Yeye arudishaye mabaya badala ya mema, Mabaya hayataondoka nyumbani mwake."

4. MUNGU hatakusaidia maana umelipa kisasi wewe mwenyewe,
hata kama una haki haikupasi kulipa kisasi.

Warumi 12:19 "Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya MUNGU; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena BWANA."

Ndugu usiyewaachilia waliokukosea nakuomba samehe na wewe utasamehewa.

Mathayo 5:7 "Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema."

Wewe ambaye hujaachiliwa omba msamaha na omba kwa MUNGU na damu ya YESU KRISTO itakutoa kifungoni.

Nini ufanye katika maombi ili uachiliwe na adhabu yako ifutike?

1. Tubu kwa ajili ya makosa yako.

Matendo 3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"

2. Omba MUNGU kwamba waliokushikilia wakuachilie.

Yohana 14:13 "Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu(YESU KRISTO) , hilo nitalifanya, ili Baba(MUNGU) atukuzwe ndani ya Mwana."

3. Ita damu ya YESU KRISTO ili ikuweke huru(Taja uwekwe huru kwa sababu ya nini)

1 Yohana 1:7 "bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu yake Yesu, Mwana wake, yatusafisha dhambi yote."

4. Futa adhabu na vifungo ulivyofungwa na watu.

Ayubu 5:21 "Utafichwa na mapigo ya ulimi; Wala usiogope maangamizo yatakapokuja."

5. Uliyemkosea akakufunga kwa maneno yake, Muombee awe na roho ya kusamehe na kuachilia na kusahau.

Waefeso 4:32 "tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na MUNGU katika Kristo alivyowasamehe ninyi."
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU.
+255714252292(whatsapp).
Ubarikiwe 

Comments