![]() |
| Na Mwl Peter Mabula Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi |
Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la kutupa maarifa na ufahamu na msukumo wa kufanya maombi yanayotufanya tuwe salama.
Jambo la kwanza nataka ujue ni kwamba sio watu wote wanakupenda.
Zaburi 37:12 "Asiye haki hunuia mabaya juu ya mwenye haki, Na kumsagia meno yake."
Inawezekana sio kwamba majirani zako wote ni watu wazuri kwako.
Sio kuokoka kwako kunawafurahisha mawakala wa shetani, inawezekana kwa maombi yako unafanya uharibifu kwenye madhabahu za giza, usidhani maajenti wa kuzimu wanafurahia.
Mabaya kuhusu wewe yanaweza kukusudiwa na wanadamu, wachawi au majini.
Unaweza ukacheka na watu na kumbe wako kinyume chako na wamekusudia mabaya dhidi yako.
Ona mfano huu ambapo Sauli alipanga kumuua Daudi bila kosa lolote.
1 Samweli 23:9-10 " Naye Daudi alifahamu ya kuwa Sauli amemkusudia mabaya; akamwambia Abiathari, kuhani, Lete hapa hiyo naivera. Ndipo Daudi akasema, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, mimi mtumwa wako nimesikia hakika ya kuwa Sauli anataka kuja huku Keila, ili kuuharibu mji kwa ajili yangu."
Kuna mialiko mingine iliyobeba mabaya kwako.
Sio kila anayekuambia mkutane mahali ana nia njema na wewe, uwe makini, mche MUNGU na isikilize amani ya KRISTO ndani yako ili ikusaidie katika maamuzi.
Unaweza ukaitwa mahali na kumbe aliyekuita au waliokuita wakawa sio watu wazuri kwako, yaani wamepanga mabaya.
ona mfano huu.
Nehemia 6:2 "Sanbalati na Geshemu wakatuma wajumbe kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono. Walakini wakakusudi kunifanyia mabaya."
Sio kila anayekupa mwaliko ana nia njema na wewe, wapo pia na wapanga mabaya hiyo, uwe makini na uwe muombaji sahihi anayeishi maisha matakatifu sahihi ya Wokovu wa KRISTO YESU Mwokozi.
Sio watu wote ni wema kwako.
Rafiki yangu mmoja alisingiziwa amembaka mtoto mdogo kisha watu wakampiga kidogo wamuue, kisha akashtakiwa na ilimchukua karibia miaka miwili akiwa mahabusu ndipo akaachiwa. Chanzo cha matatizo hayo alikosana na mama wa mtoto huyo kisha huyo mama akamwambia kwamba atamkomesha na kuhakikisha haishi, aliandaliwa mtego huo na kukamatwa akiwa jirani tu na mtoto huyo lakini kwa kuwa kuna watu walikuwa wamepangwa basi walifika tu na kuanza kumpiga huku wakipiga makelele kwamba wamemkuta anambaka mtoto, huyo.
Tulitumia nguvu nyingi sana kwa maombi ili MUNGU aingilie kati ndipo ikaja kuthibitika kwamba alisingiziwa na akaachiwa huru.
Ndugu, sio watu wote wanakupenda.
Zaburi 38:12 "Nao wanaoutafuta uhai wangu hutega mitego; Nao wanaotaka kunidhuru hunena mabaya; Na kufikiri hila mchana kutwa."
Yuko mtu mmoja aliambiwa na mfanyakazi mwenzake kwamba atafanya kila mbinu ili afukuzwe kazi na ikaja ikawa hivyo kweli, leo tunamwita MUNGU wetu katika KRISTO YESU ili atuepushie na kila mabaya yaliyokusudiwa na wanadamu wabaya au nguvu za giza.
Ndugu uwe makini, kuna wakati mwingine unaweza kushangaa ghafula moyoni huna amani, una huzuni kubwa na kumbe hiyo ni taarifa ya rohoni kwamba uombe maana kuna mabaya yanakusudiwa kuhusu wewe wakati huo.
Ndugu hakikisha unaishinda mitego ya wanaokupangia mabaya, shinda kwa maombi katika jina la YESU KRISTO huku ukiishi maisha matakatifu ya Wokovu.
Nini ufanye katika maombi ili mabaya yaliyokusudiwa yazuiliwe na MUNGU?
1. Omba maombi ya toba ili uwe safi na ili maombi yako yanayofuata yakubalike mbele za MUNGU.
Zaburi 51:1-2 " Ee MUNGU, unirehemu, Sawasawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, Uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu, Unitakase dhambi zangu."
2. Omba MUNGU akulinde dhidi ya mabaya yote.
Zaburi 121:7 "BWANA atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako."
3. Kiri ushindi huku ukiomba kwamba mabaya yaliyokusudiwa yasikupate.
Zaburi 91:10 "Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako."
4. Omba MUNGU akuokoe katika mabaya yaliyopo(Kama yapo) na akuokoe katika mabaya yaliyopangwa tayari kwenye ulimwengu wa roho wa giza.
Ayubu 5:19-20 "Yeye atakuoko
a na mateso sita; Naam, hata katika saba hapana uovu utakaokugusa. Wakati wa njaa atakukomboa na mauti; Na vitani atakukomboa na nguvu za upanga."
5. Amuru mabaya waliyoyakusudia kwako yawapate wao.
Zaburi 40:14-15 "Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu. Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe!"
6. Omba MUNGU akulinde dhidi yguvu za giza.
2 Wathesalonike 3:3 "Lakini BWANA ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu."
7. Hakikisha uko ndani ya ufalme wa YESU KRISTO.
1 Yohana 3:8b " Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi."
Ngugu yangu sio watu wote wanakupenda hivyo kaa vizuri ya YESU KRISTO na umwite MUNGU ili akuepushie mabaya yote yaliyopangwa kuhusu wewe.
Inawezekana bado hujaelewa vyema, ngoja nikupe mifano hai hii mitatu;
Kuna mtu mmoja alikuwa anafunga na kuomba ili familia yangu ipatwe na mabaya, ni kitu cha ajabu sana lakini namshukuru MUNGU Baba aliyenipa neema na ufunuo na ushindi.
Sasa kama inafika hatua kuna watu hadi wanaingia kwenye maombi ili wewe usie na hatia upatwe na mabaya, wala hujawakosea ila wivu tu basi ni hatari sana.
Kuna mama mmoja baada ya mume wake kufariki ndugu wa mwanaume walikaa kikao na kutunga uongo ili mama huyo awe hatiani, walipanga kumsingia kwamba yeye ndiye mchawi aliyemloga ndugu yao. Kwa sababu walikuwa ni wengi basi walimzonga kisha wakamhukumu kwa kumfukuza kwenye nyumba yake aliyojenga na mumewe kisha wakajifanya wanagawana watoto wa marehemu ili wapate mgao wa mali na ikawa hivyo kweli yaani akafukuzwa kwa aibu.
Mama yule akawa mtu wa kulia muda wote, akawa anaenda hadi kaburini kwa mumuwe akijaribu labda kumsemesha ili aseme ukweli lakini haikuwezekana maana mtu akifa hawezi kujua lolote linaloendelea duniani.
Mfano hai wa tatu ni huu kuna mama mmoja ambaye alikuwa kwenye ndoa takatifu yenye furaha. Akiwa mimba alienda kijijini kwao na akamchukua binti mdogo tu kiumri wa karibu kifamilia ili aje awe msichana wake wa kazi na akawa anamlipa vizuri, Binti huyo hata miaka 18 alikuwa hajafikisha, mama huyu alimuona binti huyo kuwa ni mdogo lakini ni binti huyo huyo ndiye alikuja kuvunja ndoa ya mama huyo kabla hata hajajifungua. Binti alikuwa alipofika tu baada ya muda mfupi akawa kwenye mahusiano ya kingono na mume wa mama mwenye nyumba na inavyoonekana mume wa mama huyo ni mmoja wa wanaume wasio na akili kabisa duniani ambao Biblia inasema katika Mithali 6:32 kwamba " Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake."
Mama huyo akiwa na mimba ya miezi nane alifukuzwa na mumewe kwa aibu. Mama huyo alinipigia simu akilia sana akiomba nimuombee.
Ndugu, uwe makini sana na wakati mwingine omba MUNGU akuepushe na mabaya yote yaliyopangwa au yanayopangwa sasa au yatakayopangwa baadae kuhusu wewe kutoka kwa nguvu za giza au kutoka kwa watu wabaya.
Leo katika jina la YESU KRISTO omba ukivunja na kufuta kila mabaya yaliyopangwa kuhusu wewe, yaliyopangwa na majirani au ndugu, au wafanya kazi wenzako au wachawi, au waganga wa kienyeji au mizimu au majini n.k, futa mipango hiyo kwa damu ya YESU KRISTO na omba katika jina la YESU KRISTO Mwokozi.
Nini MUNGU atafanya ukimuomba akuepushe na mabaya yaliyokusudiwa?
1. MUNGU hataruhusu mabaya hayo yaliyopangwa yakupate wewe.
Zaburi 21:11-12 " Madhali walinuia kukutenda mabaya, Waliwaza hila wasipate kuitimiza. Kwa maana utawafanya kukupa kisogo, Kwa upote wa uta wako ukiwaelekezea mishale."
2. MUNGU ataliondoa kumbukumbu la waliokusudia mabaya juu yako.
Zaburi 34:16" Uso wa BWANA ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani."
Ukikaa vizuri na YESU KRISTO na ukawa muombaji hakika ipo siku utawatafuta maadui zako na hutawaona.
Isaya 41:11-13 " Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia. Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako.
Kwa maana mimi, BWANA, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia."
3. MUNGU atakuficha mbali na hila za wabaya wako.
Zaburi 64:2 "Utanificha mbali na shauri la siri la watenda mabaya, Mbali na ghasia ya watu wafanyao maovu;"
4. MUNGU atakulinda dhidi ya kila nguvu za giza.
2 Wathesalonike 3:3 "Lakini BWANA ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu."
Ndugu omba na utamuona MUNGU.
Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kueleea naamini ameelewa .
Hapa chini ni MAOMBI YA KUMUOMBA MUNGU AKUEPUSHE NA MABAYA.
Maombi haya ni kwa ajili ya mtu ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba.
Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea.
MAOMBI YA KUMUOMBA MUNGU AKUEPUSHE NA MABAYA.
Baba katika jina la YESU KRISTO, ninakushukuru kwa kunilinda na kunipa afya njema.
Naomba BWANA unisamehe kwa jambo lolote ambalo nimekosea mbele za MUNGU wangu.
Niko mbele zako nikiomba katika jina la YESU KRISTO ili MUNGU wangu uniepushe na mabaya yote yaliyokusudiwa kwa ajili yangu au kwa ajili ya familia yangu au kwa ajili ya ndoa yangu.
Neno lako linasema katika 2 Wathesalonike 3:3 kwamba "Lakini BWANA ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu."
Eee Bwana MUNGU ninaomba unilinde na kila mipango ya kipepo yote.
Nakuomba Eee MUNGU unilinde dhidi ya mipango ya wanadamu wasionipenda na wasionitakia mema.
MUNGU Baba nakuomba pia unilinde dhidi ya mipango mibaya ya kuzimu na kila mipango ya kila nguvu za giza.
Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninatangaza mabaya yote yaliyokusudiwa kwa ajili yangu natangaza hayatanipata kamwe.
Imeandika katika Zaburi 91:10 "Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako."
Hivyo nakataa ajali na nakataa balaa kwa jina la YESU KRISTO.
Nakataa kuonewa wala kufilisika, katika jina la YESU KRISTO nakataa na haitakuwa.
Kwa jina la YESU KRISTO nakataa kuumwa na nakataa magonjwa, katika jina la YESU KRISTO hivyo havitanipata wala havitaipata familia yangu na nyumba yangu.
Kwa jina la YESU KRISTO nakataa ajali na nakataa migogoro, katika jina la YESU KRISTO hivyo havitanipata wala havitaipata familia yangu na nyumba yangu.
Kwa jina la YESU KRISTO nakataa kulogwa na nakataa kunaswa na nguvu za giza, katika jina la YESU KRISTO hivyo havitanipata wala havitaipata familia yangu na nyumba yangu.
Kwa jina la YESU KRISTO nakataa kufukuzwa kazi na nakataa kusingiziwa chochote, katika jina la YESU KRISTO hivyo havitanipata wala havitaipata familia yangu na nyumba yangu.
Kwa jina la YESU KRISTO nakataa kupata ajali na nakataa mikosi, katika jina la YESU KRISTO hivyo havitanipata wala havitaipata familia yangu na nyumba yangu.
Kwa jina la YESU KRISTO nakataa kutembelewa na nguvu za giza na nakataa kuwa mawindo ya majini, katika jina la YESU KRISTO hivyo havitanipata wala havitaipata familia yangu na nyumba yangu.
Sasa kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO naamuru mabaya yote waliyoyakusudia mawakala wa shetani yawapate wao kwa jina la YESU KRISTO.
Imeandikwa katika Zaburi 40:14-15 kwamba "Waaibike, wafedheheke pamoja, Wanaoitafuta nafsi yangu waiangamize. Warudishwe nyuma, watahayarishwe, Wapendezwao na shari yangu. Wakae hali ya ukiwa, na iwe aibu yao, Wanaoniambia, Ewe! Ewe!"
Tena imeandikwa katika Zaburi 71:13 kwamba "Waaibishwe, watoweshwe, adui za nafsi yangu. Wavikwe laumu na aibu wanaonitakia mabaya."
Sasa kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO kila mchawi au mganga aliyekusudia mabaya kwa ajili yangu, huyo wakala wa shetani aabike na afedheheke na huo ubaya alioupanga hautanipata mimi kamwe.
Kwa jina la YESU KRISTO kila jini au mzimu aliyetumwa kwangu aabike, afedheheke na atoweke kwa jina la YESU KRISTO.
Eee MUNGU ninaomba unilinde dhidi ya kila wakala wa kuzimu na kila mipango mibaya dhidi yangu.
Kuanzia leo mabaya hayatanipata mimi, kwa jina la YESU KRISTO hayatanipata.
Kuanzia leo mabaya hayataipata nyumba yangu, kwa jina la YESU KRISTO hayataipata.
Kuanzia leo mabaya hayataipata ndoa yangu kwa jina la YESU KRISTO hayataipata.
Kuanzia leo mabaya hayataupata mwili wangu au kazi yangu, kwa jina la YESU KRISTO hayataupata.
Nakushukuru MUNGU Baba kwa kunipa ushindi dhidi ya adui zangu wote.
Nakushukuru MUNGU Baba maana mabaya yote yaliyokusudiwa kwa ajili yangu au familia yangu au uzao wako au kazi yangu au ndoa yangu, hayo mabaya hayatanipata tena.
Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea ushindi.
Amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen.
MUNGU akubariki hakika wewe u mshindi.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292(Maombi, Ushauri, sadaka ya kuipeleka injili n.k)
Ndugu omba na utamuona MUNGU wa miujiza.

Comments