MAOMBI YA KUOMBEA USO KIROHO.

Na Mwl Peter Mabula 
Mtenda kazi katika Shamba la MUNGU wa Mbinguni 




Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni sana tujifunze Neno la MUNGU.
Ninayekuletea ujumbe huu naitwa Mwl Peter Mabula.

✓✓Kuna mambo mengi kwa mtu ambayo yanaweza kuleta kibali kwake, moja ya kiungo muhimu sana kinachoweza kuleta kibali kwa mtu ni uso wake.

Ninaposema uso sina maana kwamba kuna mtu ana uso mbaya na mwingine ana uso mzuri, nifuatilie katika somo hili na utalielewa.

Siku moja nilikuwa katika maombi niliona mtu mmoja uso wake unacheza, sikuelewa maana yake lakini nilijifunza kwamba uso una maana kubwa sana, uso umebeba baraka ya mtu au laana ya mtu.
Biblia inakataza watu kuwapendelea baadhi ya watu kwa sababu tu ya uso.
Kumbu 16:19 "Usipotoe maamuzi; wala usipendelee uso wa mtu; ........"

Lakini katika jamii ya leo uso unaongea sana kiasi kwamba wapo watu hupendelewa kwa sababu ya uso, na wapo baadhi ya watu hunyanyaswa kwa sababu ya nyuso zao.
Sasa kuna uso kimwili na kuna uso kiroho, mimi leo nazungumzia tu uso kiroho maana ndio huonyesha matokeo makubwa sana katika ulimwengu wa mwili.

✓✓Kuna watu wanadharaulika japokuwa wana nyuso nzuri za kimwili, tatizo ni katika ulimwengu wa roho hivyo uso unaweza kuchafuliwa katika ulimwengu wa roho na mtu akayaona matokeo katika ulimwengu wa mwili.

Ayubu 30:10 '' Wao hunichukia, na kujitenga nami, Hawaachi kunitemea mate usoni. ''

✓✓Mtu akifunikwa uso wake huwezi kumtambua, hiyo ni katika hali ya kimwili lakini hata kiroho mtu akifunikwa uso wake kiroho huwezi kumtambua katika ulimwengu wa mwili, huwezi kumtambua hata ukampa heshima yake au ukampa nafasi yake au ukampa haki yake.

Mfano katika hali ya kimwili tu na sio kiroho ukimkuta mfano kiongozi mkubwa katika taifa amefunikwa usoni hutamtambua hata kama amevaa suti nzuri, lakini akifunuliwa uso unaweza hata kujikuta unampigia saluti hata kama wewe sio askari.
Kwanini umpigie saluti?
ni kwa sababu umemuona usoni na ukajua ana hadhi gani au amebeba nini kimamlaka na kiheshima, nakupeleka taratibu ili uanze kuwaza mambo ya rohoni maana inawezekana ukifika mahali tu watu wote pale wananyamaza maana wanakuona wewe sio wa kuwa hapo kama wao, huna kibali, uso wako hauna kibali.

Inawezekana watu hawakuheshimu kwa sababu umechafuliwa uso kiroho.

Inawezekana watu hawakukubali wala kukutambua kama unastahili eneo hilo au nafasi hiyo kwa sababu tu uso wako hauna kibali. Kwanini uso wako ukose kibali mbele za watu? Inawezekana kwenye ulimwengu wa roho uso wako umezibwa hivyo madhara unayaona katika ulimwengu wa mwili.

Inawezekana wewe unaoga mara 4 kwa siku, unabadili nguo mara 5 kwa siku, umetumia kila mafuta ya kujipaka lakini, unaishi maisha ya haki lakini hakuna mtu hata mmoja atahitaji kufunga ndoa na wewe, ndugu inawezekana kabisa tatizo ni katika ulimwengu wa roho na wakati unaweza kuwa umefungwa uso kiroho.

Inawezekana wewe ni mtu wa kukataliwa kila siku, inawezekana kwa sasa mkeo au mumeo anajiuliza ilikuwaje hadi akakubali kufunga ndoa na wewe, akikuangalia anajishangaa na kujilaumu kwamba siku hiyo alipungukiwa labda akili hadi kukubali kuonana na Wewe lakini ukweli ni kwamba kwa sasa wewe huna tu kibali kwake na moja ya vitu ambavyo ulimwengu wa roho wa giza unaweza kuharibu kwa mtu ni uso wake kiroho.

✓✓Kumbuka hii kwamba uso unaweza kuwa mweusi kiroho hivyo mtu husika kuonekana kama ni giza tu mbele za baadhi ya watu muhimu kwake.

Maombolezo 4:8 ''Nyuso zao ni nyeusi kuliko makaa; Hawajulikani katika njia kuu; Ngozi yao yagandamana na mifupa yao Imekauka, imekuwa kama mti."

Nina hakika hakuna mtu hata mmoja duniani ambaye ni mweusi kama mkaa lakini kwenye ulimwengu wa roho inawezekana maana mawakala wa shetani kazi yao ni kuharibu na kuua kiroho na kuiba kiroho.

Kwani hujawahi kumuona mtu ambaye anatumia nguvu nyingi sana kukubalika iwe kwa mchumba, kwa jamii, ofisini, kwenye kundi au taasisi na bado mtu huyo licha ya kutumia nguvu nyingi bado hakubaliki kivyovyote.
Lakini yuko mtu hata hatumii nguvu kukubalika lakini anakubalika kupita kawaida, ndugu uso hubeba baraka za mtu, kibali cha mtu na kukubalika kwa mtu.

Kuna watu nyuso zao zinang'aa kwenye ulimwengu wa roho kiasi kwamba hawatumii nguvu nyingi katika ulimwengu wa mwili ili kukubalika au kupata kibali. Mfano hai wa uso kung'aa ni Musa,
Musa uso wake ulikuwa unang'aa kama jua.
Kutoka 34:29 '' Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na zile mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling'aa kwa sababu amesema naye. ''


✓✓Ndugu hakikisha kwa maombi na utakatifu uso wako unang'aa kwenye ulimwengu wa roho ndipo kuna baadhi ya hasara hutaziona katika ulimwengu wa mwili.

✓✓Mama au Baba omba katika jina la YESU KRISTO ili uso wako ung'ae siku zote kwenye ulimwengu wa roho ndipo kwenye ulimwengu wa mwili utakubalika daima mbele za mwenzi wako wa ndoa, mbele ya watoto wako, ndugu zako, kazini kwako na popote pale.

Wapo watu pia hutumia nguvu za giza ili wakubalike, hao ni mawakala wa shetani usikubali kuwafuata wala kuwaiga hata sekunde moja, hao kung'aa kwao ni kipepo na ni kwa muda mfupi tu kisha wanatoweka.

Hayo wana uso wa wapumbavu usiwafuate wala kuwaiga.

Mithali 14:7 '' Toka mbele ya uso wa mpumbavu, Maana hutaona kwake midomo ya maarifa. ''

Wewe mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na uwe muombaji unayeishi maisha matakatifu ya Wokovu na ombea mwili wako ukiwemo uso wako.
Inawezekana kuna mtu anajifunza ujumbe huu na tatizo lake ni uso kiroho yaani hata afanye jambo jema kiasi gani watu wanamuona kakosea sana kwa sababu tu hana kibali cha uso kinachompa kukubalika, yamkini mtu huyo atajifunza kitu ili awe na nguvu za kuomba na kujikomboa kupitia damu ya YESU KRISTO na jina la YESU KRISTO.
Inawezekana uso wako umeharibika kiroho ndio maana uko katika mateso fulani juu ya baraka fulani.

Ayubu 16:16 '' Uso wangu umeharibika kwa kutoa machozi, Na giza tupu li katika kope zangu; ''

Ndugu mche MUNGU katika KRISTO YESU na atamuona MUNGU atakayebadilisha historia ya maisha yako.
Uso ni muhimu sana.
Unapoombea kibali usiache na kuombea uso wako ili uwe na kibali kama unaona kuna kizuizi kwako kuhusu masuala ya kuwa na kibali.
Kunaweza kuwekwa tatizo la kiroho usoni kiroho na ukajikuta hupati haki yako.
Mimi Peter Mabula niliwahi kumuombea dada mmoja usoni alikuwa amewekewa jini, dada huyo kila mtu alikuwa anamchukua japokuwa alikuwa na tabia nzuri sana na alikuwa mcha MUNGU safi.

Ndugu unapoombea kupata mwenzi wako basi ombea na kibali cha uso wako maana unaweza kukataliwa na hata kutukanwa hata kama unasema umeonyeshwa kwa huyo.

Je hujawahi kusikia binti au kijana anasema amefunuliwa kwa kijana fulani au binti fulani na anapomweleza mhusika anakataa na kumshangaa anayesema ameoneshwa, tatizo ni nini?
Tatizo ni kibali hasa kibali cha uso.

Wako pia watu kwa mitazamo ya kibinadamu wanaonekana wana nyuso mbaya lakini wamefanikiwa kupata kazi, wamefanikiwa kufunga ndoa na watu wenye sura nzuri, wanapendwa sana n.k

Kwanini iwe hivyo?
Ni kwa sababu watu hao wanang'aa kwenye ulimwengu wa roho na matokeo yanaonekana katika ulimwengu wa mwili.
Lakini pia wapo watu wanajiona wana sura nzuri na uso mzuri sana lakini hawajafanikiwa kupata wenzi au kazi n.k kwa sababu tu hawana kibali yaani wamezibwa katika ulimwengu wa roho hivyo hadi washughulikie tatizo hilo kimaombi kupitia jina la YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Unapokuwa katika ndoa basi ombea kibali uso wako ili uendelee kukubalika mbele za mwenzi wako.
Kumbuka pia kwamba mwanaume au mwanamke anaweza kugeuka hafifu mbele ya mchumba wake hivyo akaghairi kufunga naye ndoa.

Mwanzo 29:17-18 " Naye Lea macho yake yalikuwa dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo, na mzuri uso. Yakobo akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo."

✓✓Swali la kujiuliza hapa kwanini Leah alikuwa hafifu machoni pa Yakobo tu lakini Raheli hakuwa hafifu machoni pa Yakobo?
Jibu ni kwamba uso wa Leah haukupata kibali machoni pa Yakobo ndio maana Yakobo hakutaka kumuoa kabisa.

Lakini uso wa Rachel yaani Raheli ulikuwa na kibali machoni pa Yakobo kiasi kwamba kwa Yakobo kufanya kazi miaka 7 ili ampate Raheli haikuwa kazi maana Raheli alikuwa na kibali kikubwa sana machoni mwa Yakobo.

Mwanzo 29:20 "Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile alivyompenda."

Sasa inawezekana wewe mwanamke kwa sasa umekuwa hafifu mbele za mume wako ndio maana nakulazimisha tu kuwa na wewe, kwanini uwe hafifu? Inawezekana uso wako umekosa kibali machoni pake.
Inawezekana Baba kwa sasa umekuwa hafifu machoni kwa mke wako, hivyo anavumilia tu kuishi na wewe.
Inawezekana wewe umekuwa hafifu kwa mchumba wako ndio maana anataka kukuacha na kufunga ndoa na mwingine.

Tatizo ni nini?
Tatizo ni uso wako umekosa kibali mbele zake, inawezekana uso wako wachawi wameufanya uwe mweusi kama mkaa kwenye ulimwengu wa roho ndio maana mambo yamekuwa mabaya kwako.
Wanaweza wakaomba kazi watu mia moja wenye umri sawa na elimu sawa lakini wakaajiriwa 2 kutoka kundi hilo, kwanini iwe hivyo? Ni kwa sababu hao ndio wamepata kibali na wengine hawakupa.
Inawezekana pia waliopata kibali kibinadamu wakaonekana wana sura za kawaida sana lakini kumbe kwenye ulimwengu wa roho wanang'aa kama jua.
Ndugu, leo katika jina la YESU KRISTO hakikisha unaukomboa uso wako kwa damu ya YESU KRISTO.
Pia kuna mambo mengine baadhi ya watu hujulishwa kwa ndoto ili kujulishwa tatizo lao lakini wao wanadharau na kujikuta wako katika matatizo fulani kila wakati.

Nimewahi kukutana na watu walioniambia hivi.

✓Mtu mmoja aliniambia kwamba ameota ndoto amepakwa kinyesi usoni.
Ni kuchafuliwa uso kiroho, roho ya kukataliwa n.k ili tu watu wamchukie kama wanavyochukia mavi.

✓Mtu mwingine aliota ndoto uso wake ukipakwa tope.
Ni kuchafuliwa uso kiroho ili apate madhara katika ulimwengu wa mwili.

✓Mtu mmoja aliota ndoto siafu wanatembea usoni kwake.
Ni kuharibiwa uso kiroho na roho za magonjwa n.k ili tu kuharibu maisha yake.

Ndugu, sio kila kitu unachokiona kwa ndoto au maono unakidharau, mambo mengine kwa neema ya MUNGU unajulishwa kwa ndoto au maono ili ujue nini nguvu za giza wamefanya na sasa kwa maombi kupitia jina la YESU KRISTO uombe na kufunguliwa.
Kuna dada mmoja alkiota ndoto akiona usoni kwake ana alama ya kipepo.
Ni hatari sana kuwekewa alama za kipepo katika mwili wako kiroho, ni kuwekewa alama ili uendelee kuwa mawindo ya wakuu wa giza, ni kufanywa uwe kituko tu katika jamii n.k

Kuna watu wamewahi kuota ndoto wakiona usoni mwao wakibadilika na kuwa wanyama fulani au wadudu fulani, ni hatari sana.
Kuna mtu aliota ndoto akimwagiwa maji usoni.
Kuna mtu mmoja aliota ndoto uso wake ukiwa na mabaka.
Kuna mtu aliota ndoto uso wake una vidonda.
Ndugu yangu pambana na kila nguvu za giza , pambana kimaombi kupitia jina la YESU KRISTO na utashinda.
Wakati mwingine kama jina lako linatajwa katika madhabahu za giza unaweza kuona ishara katika mwili wako hivyo usipuuzie kila jambo bali ingia katika maombi na hawatakuweza kamwe.
Wapo watu pia wamewahi kuota ndoto wakijiona usoni wakiwa na uso mzuri sana, ni taarifa ya kibali na kukubaliwa na ni taarifa ya kutakaswa uso.

Nini ufanye kwenye maombi?

1. Tubu kwa ajili ya dhambi zako, makosa yako na maovu yako yaliyofungulia adui kufanya chochote kwenye mwili wako wote.

Matendo 3:19 "Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA;"

2. Kama uliona uso wako umewekewa alama yeyote kwenye ulimwengu wa roho ifute hiyo alama ya kipepo, ifute kwa damu ya YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.

Yohana 14:14 "Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."

3. Ombea kibali uso wako mbele za watu wote.

Mwanzo 39:21 "Lakini BWANA akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza."

4. Ombea uso wako ung'ae kwenye ulimwengu wa roho na matokeo yake unayone kwenye ulimwengu wa mwili.

Mathayo 17:2 "akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru."

5. Ombea nuru za uso wa MUNGU zikuangazie.

Hesabu 6:25-26 " BWANA akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili; BWANA akuinulie uso wake, na kukupa amani."

Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Mwl Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi wetu aliye hai milele.
+255714252292( whatsapp).
Ubarikiwe 

Comments