MAOMBI YA UPONYAJI MAGONJWA.

Mwl Peter Mabula,  Mtenda kazi katika shamba la MUNGU 

Bwana YESU KRISTO Mwokozi atukuzwe ndugu yangu.
Namshukuru MUNGU kwa neema hii na  tunaendelea na maombi yetu, na muda huu  tunaombea uponyaji magonjwa.

■Jambo la kwanza kabisa nataka nikujulishe ni kwamba kila kitu unachokiona katika ulimwengu wa mwili, hicho kitu kina chanzo chake katika ulimwengu wa roho.

Mfano kuna siku moja niliota ndoto naumwa yaani ndotoni nilijiona naumwa na mwili hauna nguvu kabisa.
Nilipoamka nilishangaa na kucheka maana nilikuwa mzima kabisa wakati huo.
Yaani ingawa nilijiona katika ulimwengu wa roho ninaumwa lakini katika hali halisi ya ulimwengu wa mwili nilikuwa mzima sana, niliendelea na majukumu yangu kama kawaida lakini baada siku kama nne au tano mwili wangu ulianza kuuma, kichwa kilianza kuniumwa sana nikiwa Kanisani, baadae nikaenda Hospitali kucheki nikakutwa nina typhoid na Malaria, nilikuwa sijawahi kuumwa typhoid katika maisha yangu hivyo hali Ikawa mbaya na ilinichukua karibia wiki mbili kupona na kurudi katika hali ya kawaida.

Nini nataka kusema?
Kutoka ulimwengu wa roho kama amekufunulia  MUNGU, ulimwengu wa roho huwa haudanganyi.
 Mimi angeota ndoto hiyo mtu mwingine inawezekana ningemkatalia au hata kumwambia  "labda wewe ndio unaumwa" 

Nini nataka kusema?
Kila ugonjwa huwa una chanzo chake katika ulimwengu wa roho, hata kabla ugonjwa huo haujaonekana katika ulimwengu wa mwili.

Mfano ni Sasa ambapo ugonjwa wa corona ni tishio kubwa duniani, ebola, homa ya ini, ukimwi n.k ni magonjwa hatari sana, lakini ukweli ni kwamba  kila mtu anayeumwa huo ugonjwa kwake una chanzo katika ulimwengu wa roho, ni muhimu kushughulika na chanzo katika ulimwengu wa roho kwa maombi.

Yuko mtu aliota ndoto ameugua akakonda sana na kweli baada ya miezi kadhaa akaugua na kukonda Sana.

Baba mmoja aliota anaumwa na ugonjwa ule ukamwondoa duniani na kweli ilikuja kuwa hivyo hivyo, kilichomsaidia yeye ni kuandika tu urithi kwa familia yake ili awaache bila migogoro maana alipoanza tu kuumwa na migogoro ikaanza kuamka.
Ndugu zangu, ingawa kuna magonjwa lakini yuko MUNGU Baba wa mbinguni anaponya magonjwa yote.

Kumbu 7:15" Na BWANA atakuondolea ugonjwa wote; wala hatatia juu yako maradhi yo yote mabaya uyajuayo ya Misri, lakini atayaweka juu ya wote wakuchukiao."

 Siku moja nilipata ufunuo nilipokuwa namuombea mtu uponyaji, nilisikia sauti ikisema hivi "Ili mtu apone ugonjwa kwa maombi yanahitaji mambo manne(4). Mambo hayo ni Imani ya muombaji, imani ya anayeombewa, kutafuta Mapenzi ya MUNGU na Ufunuo wa ROHO MTAKATIFU, siku moja nitafafanua juu ya haya manne(4) tu kwenye somo lingine.

●Hivyo kwa maombi kupona ugonjwa wowote ni jambo rahisi sana katika KRISTO YESU.
Ona mfano huu.
Mathayo 8:2-3 " Na tazama, akaja mtu mwenye ukoma akamsujudia, akisema, Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.
 YESU akanyosha mkono, akamgusa, akisema Nataka; takasika. Na mara ukoma wake ukatakasika."

Kazi ya watumishi wa MUNGU katika KRISTO YESU ni pamoja kuombea wagonjwa na wanapona.
Luka 10:9" waponyeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa MUNGU umewakaribia."

Mmoja wa watumishi wa MUNGU ni wewe Mkristo muombaji, hivyo kama unaumwa jiombee ili upone na kama ni mtu wa karibu yako muombee ili apone, katika jina la YESU KRISTO atapona.

Kama huna ndugu wala rafiki anayeumwa basi ombea wagonjwa walio katika hospitali karibu na wewe na kwa maombi yako Bwana YESU KRISTO mponyaji atawaponya kwa imani yako.

 ●Lakini pia kumbuka sana kufanya Maombi ya kukataa roho za magonjwa kwako na kwa watu wako wa karibu.

Mambo ya kujua kuhusu kumuombea mgonjwa.

1. Mamlaka ya uponyaji iko ndani ya YESU KRISTO, hivyo omba Maombi yako katika jina la YESU KRISTO.

Marko 16:17 Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; KWA JINA LANGU watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya."

2. Kuna magonjwa hutokana na mapepo, ukiyatoa mapepo na mgonjwa anapona.

Luka 13:11-13 " Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. YESU alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako. Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza MUNGU."

●Uking'ang'ana kutoa ugonjwa bila kuyatoa ndani mapepo yaliyosababisha ugonjwa huo ujue mgonjwa hatapona au atapata nafuu tu ila ugonjwa wake utaendelea kumsumbua.

Ng'oa nguvu za giza zilizoweka ugonjwa ndani ya mtu ndipo atapona. 

Mfano ni huu kwamba mapepo yalipoondolewa mgonjwa alipona.

Mathayo 9:32-33 "Hata hao walipokuwa wakitoka, tazama, walimletea mtu bubu mwenye pepo. Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wakastajabu, wakasema, Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wo wote."

3. Kuna magonjwa mengine  kupona kwake anza na Maombi ya toba kwanza maana dhambi ndio chanzo cha ugonjwa huo, tubu kwa ajili ya chanzo cha ugonjwa na MUNGU atamsamehe na kumponya.

Mathayo 9:2 "Na tazama, wakamletea mtu mwenye kupooza, amelala kitandani; naye YESU, alipoiona imani yao, alimwambia yule mwenye kupooza, Jipe moyo mkuu, mwanangu, umesamehewa dhambi zako."

4. Kama unaumwa na umeomba hujapona ndio maana tuko kwenye maombi haya ya kufunga, uponyaji utatokea hakika.

Yakobo 5:14-16 " Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa. Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii."

Kumpaka mafuta kwa jina la YESU KRISTO maana yake kumuombea nguvu za ROHO MTAKATIFU.

Kuna nguvu za uponyaji katika nguvu za ROHO MTAKATIFU.

Ni kusudi la MUNGU kila anayeumwa apone katika jina la YESU KRISTO Mwokozi.

Luka 10:9 "waponyeni wagonjwa waliomo, waambieni, Ufalme wa MUNGU umewakaribia."

Nini ufanye leo katika maombi.

1. Tubu kwa ajili ya chanzo cha ugonjwa.

Danieli 9:13 "Kama ilivyoandikwa katika sheria ya Musa, mabaya haya yote yametupata lakini hata hivyo hatukumwomba BWANA, Mungu wetu, atupe fadhili zake, ili tugeuke na kuyaacha maovu yetu, na kuitambua kweli yake."

2.  Kwa maombi mwambie Bwana YESU KRISTO akuponye ugonjwa huo maana yeye ni mponyaji.

Mathayo 8:16-17 " Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi,
 ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu."

3. Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO amuru nguvu za giza zilizoleta ugonjwa zitoke na mgonjwa atapona.

Marko 9:25-27 " Naye YESU akiona ya kuwa mkutano unakusanyika mbio, akamkemea yule pepo mchafu, akamwambia, Ewe pepo bubu na kiziwi, mimi nakuamuru, mtoke huyu, wala usimwingie tena. Akalia, akamtia kifafa sana, akamtoka; naye akawa kama amekufa; hata wengi wakasema, Amekufa. Lakini YESU akamshika mkono akamwinua naye akasimama."

4. Kwa maombi katika jina la YESU KRISTO amuru ugonjwa utoke na utatoka.

Yohana 14:13-14 "Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."

5.  Kwa maombi ita afya  ya ki MUNGU ndani ya mgonjwa atapona.

Yeremia 30:17 "Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema BWANA, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye."

6. Haribu Madhabahu za giza zilizotengeneza magonjwa.

Kumbu 7:5 "Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga."

7. Tumia jina la YESU KRISTO katika maombi yako, tumia damu ya YESU KRISTO, tumia Neno la ufunuo wa ROHO MTAKATIFU na omba kwa imani.

✓✓Jina la YESU KRISTO.
Wafilipi 2:10 "ili kwa jina la YESU kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;"

✓✓Damu ya YESU KRISTO.
Ufunuo  12:11 "Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa."

✓✓Neno la MUNGU la ufunuo wa ROHO MTAKATIFU.
Waebrania 4:12 "Maana Neno la MUNGU li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo."

✓✓Nguvu za ROHO MTAKATIFU.
Zekaria 4:6 "Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la BWANA kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, BALI NI KWA ROHO YANGU, asema BWANA wa majeshi."

Natamani niseme mengi mno lakini naamini mwenye kueleea naamini  ameelewa .

Hapa chini ni MAOMBI YA UPONYAJI MAGONJWA.
Maombi haya ni kwa ajili ya mtu ambaye hajui kuomba ili katika kuomba kwa kutumia hayo basi atakumbuka mahitaji yake na kuyataja katika maombi yake. Haya hapa chini ni maombi ya kuanzia tu katika maombi yako ili uendelee zaidi kuomba.

Kwa waombaji wazoefu naamini baada tu ya kulisoma somo na kulielewa basi anajua aombee nini maana alikuwa anaandika points za kuombea.

MAOMBI YA UPONYAJI MAGONJWA.


Baba katika jina la YESU KRISTO. 
Niko mbele zako MUNGU wa uzima na uponyaji nikiita uponyaji wako.

Ninaanza kwa kutubu kwa ajili ya dhambi zangu zote naomba unisamehe Eee BWANA na unipe neema yako.

Nakuomba takasa maisha yangu na mwili wangu.

Ninakushukuru kwa sababu wewe ni MUNGU  mponyaji na unaweza kuirudisha afya  iliyokuwa imechukuliwa na magonjwa. 
Neno lako linasema katika Yeremia 30:17  kwamba "Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema BWANA, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye."

Kumbe wewe MUNGU Baba unaweza kunirudishia afya yangu na kuniponya, nakushukuru sana na ninaomba BWANA uniponye na kunipa afya.

Bwana YESU KRISTO ninakushukuru maana wagonjwa wote waliokuja kwako uliwaponya.
Neno lako linasema katika Mathayo 8:16-17 kwamba " Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi,
 ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu."

Wewe Bwana YESU KRISTO uliwaponya wagonjwa wote na kila mwenye udhaifu, nami naungana leo na wote uliowaponya wewe nikiomba uniponye ugonjwa huu(utaje), niponye udhaifu katika mwili wangu na nipe uzima utokao kwako Bwana YESU KRISTO. 

Neno lako Bwana YESU KRISTO linasema katika Yohana 14:13-14 kwamba  "Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."

Hivyo leo mimi ninaomba uponyaji katika jina la YESU KRISTO. 

Kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO ninaamuru uponyaji katika mwili wangu, nafsi yangu na roho yangu.

Naamuru ugonjwa huu(utaje) utoke kwangu katika jina la YESU KRISTO. 

Naachilia damu ya YESU KRISTO katika eneo lenye maumivu mwilini wangu, naamuru uponyaji katika jina la YESU KRISTO. 

Neno la MUNGU linanitaka niombe lolote katika jina la YESU KRISTO litatendeka, kwa mamlaka ya jina la YESU KRISTO naita uponyaji ndani ya mwili wangu  na ndani ya miili ya watu wa familia yangu.

Eee ugonjwa(utaje) nakuamuru toka katika mwili wangu, kwa jina la YESU KRISTO toka.

Eee Bwana YESU ninakushukuru maana wewe unaponya ugonjwa wa kila namna.
Neno lako linasema kwamba hakuna ugonjwa unaoweza kukataa kupona mbele zako.
Neno lako linasema unaponya magonjwa yote na madhaifu yote. 
Ni katika Mathayo 9:35  ambapo Biblia  inasema "Naye YESU alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina."

Bwana YESU nami naomba usinipite,  naomba uniponye leo nami niwe huru mbali na magonjwa.
Ni katika jina la YESU KRISTO ninaomba na kushukuru.
Amen amen Ameeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeeen. 

Ndugu, endelea kuomba sana, wewe ni mzima na utapona.
Hata unaowaombea uponyaji  wote hakika watapona.
MUNGU akubariki sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+ 2 5 5 7 1 4 2 5 2 2 9 2.
Endelea kuomba na utamuona MUNGU mponyaji.

Comments