MTEULE ALIYE RUNGU LA MUNGU.


Mwl Peter Mabula 

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Biblia inasema kwamba wateule wa MUNGU ni rungu la MUNGU na silaha za vita vyake kwa ajili ya kuharibu kazi za shetani.

Najua kabisa kwenye maombi yako umewahi kuomba hivi ''Mimi ni rungu la BWANA na silaha za vita vyake'' ni sawa kabisa lakini jifunze ujumbe huu itakusaidia.

Yeremia 51:20 "Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme;"

●Kama  mteule wa KRISTO uliyeokoka ukikaa katika nafasi yako kimaombi  utaweza kuharibu na kutowesha falme za giza katika maeneo yako, familia yako au ukoo wako au mji unaoishi n.k

●Wewe mteule wa KRISTO ukijitambua hakika wewe ni silaha kali sana ya kuharibu kazi za shetani zote. 

Isaya 49:2-3 " Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali; katika kivuli cha mkono wake amenisitiri; naye amenifanya kuwa mshale uliosuguliwa; katika podo lake amenificha;  akaniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa."

●MUNGU anaweza kukifanya kinywa cha Mtumishi wake  Kuwa kama upanga,  yaani akitamka Neno linakuwa,  akizitamkia nguvu za giza zitoke kwa mtu hakika zinatoka na kutoweka. 

●MUNGU anaweza kumfanya Mtumishi wake Kuwa kama mshale uliosuguliwa kiasi kwamba huyo mtumishi akizitamkia neno nguvu za giza  zinachomwa kama na mshale kwa sauti yake huyo mtumishi mwaminifu wa Bwana YESU. 

●Wewe mteule wa KRISTO  ukiwa unaomba kwa imani katika KRISTO YESU hakika unaweza kuzifuta nguvu za giza katika eneo lako au katika maisha yako.

■Ukiwa unaishi maisha matakatifu katika KRISTO YESU na ukajua kuomba maombi ya vita  hakika unaweza kuzitowesha nguvu za giza katika maisha yako, ndoa yako, kazini kwako, katika mwili wako, katika eneo lako la biashara n.k

Jifunze tu kupigana vita vya kiroho kwa maombi kupitia jina kuu la YESU KRISTO. 
Yoeli 3:9 "Tangazeni haya kati ya mataifa; takaseni vita; waamsheni mashujaa; watu wa vita na wakaribie; na wapande juu."

■Wewe Mteule  ukiwa mpeleka injili anayejitambua unaweza kuzifuta falme za giza katika eneo unakokwenda kuhubiri.

Ukiwa unajitambua katika maombi unaweza kuwawekea wakuu wa giza ncha ya upanga katika makazi yao ili wasikufanyie chochote maishani mwako, maana upanga huo hautawaruhusu wao kutoka kichawi nyumbani wao.

Ezekieli 21:15 "Nimeweka ncha ya upanga huo juu ya malango yao yote, ili mioyo yao iyeyuke, yakaongezeke makwazo yao; aha! Umefanywa kuwa kama umeme, umenolewa, ili uchinje."

■Ukiwa umeokoka na unajua kuutumia vyema upanga wa ROHO MTAKATIFU ambao ni Neno la  MUNGU hakika utaweza  kuzifuta kazi za shetani zote.

Hakikisha tu unamjua adui yako kwamba ni nguvu za giza, wakuu wa giza,  majini,  mizimu na kila majeshi ya pepo wabaya Katika ulimwengu wa roho. 

Jifunze tu kuomba maombi ya vita na ujue wakati wa kupigana vita ya kiroho na mtegemee MUNGU kwa maombi yako.
 
Kumbu 20:1 "Utokapo kwenda vitani kupigana na adui zako, na kuona farasi, na magari, na watu wengi kuliko wewe, usiwaogope; kwa kuwa BWANA Mungu wako, yu pamoja nawe, aliyekukweza kutoka nchi ya Misri."

●Ukiwa Mteule wa KRISTO uliye rungu la BWANA hakika unaweza  kuangamiza falme za giza, kuvunja kazi za shetani na kuharibu kila nguvu za giza katika maisha yako na ya  unaowaombea.

■Unachohitaji tu ni kuokoka, kisha kuwa mteule  unayeishi maisha matakatifu na unayejua kupigana vita ya kiroho kwa maombi.

●Mteule wa KRISTO anayejitambua kwamba yeye ni rungu la MUNGU na silaha zake za vita ili kuharibu kazi za shetani hakika mtu huyo anaweza kubaki kuwa mshindi wa kiroho siku zote.

■Hakikisha tu uko na YESU KRISTO na unaomba katika kusudi la MUNGU na unaomba kwa imani ukiwa na silaha zote za kiroho. 
Yoeli 3:10 "Yafueni majembe yenu yawe panga, na miundu yenu iwe mikuki; aliye dhaifu na aseme, Mimi ni hodari."

●Nimejaribu kukupitisha maeneo mengi ili ujitambue na ujue kwamba wewe ni rungu la MUNGU kwa ajili ya kuharibu nguvu za giza, Sasa sio Wakristo Wote ni rungu la MUNGU.

Mteule aliye rungu la MUNGU  ni huyu aliye na mambo haya yote 10.

1. Ameokolewa na YESU KRISTO na kuhamishwa kutoka ufalme wa giza.

Wakolosai 1:13 "Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;"

MUNGU anapotuokoa hutuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwanaye wa pekee YESU KRISTO.
Ukiwa ndani ya YESU KRISTO ndipo utaweza kuwa  na uwezo wa kupigana kiroho na nguvu za giza na kuzishinda, huko ndiko kufanyika rungu la MUNGU na silaha za MUNGU za vita.  
Sasa huwezi kupambana na mashetani wakati uko ndani ya shetani,  toka kwanza ndani ya shetani ndipo utaweza kupigana na nguvu za giza. 
Kutoka ndani ya shetani ni kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako. 

2. Ni Muombaji anayemsikiliza na kumfuata ROHO MTAKATIFU.

Warumi 8:26 "Kadhalika ROHO naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini ROHO mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa."

Ukitaka uwe mshindi dhidi ya nguvu za giza lazima uwe umeokoka na uwe na ROHO MTAKATIFU huku ukimtii yeye. 

ROHO MTAKATIFU anajua vyote hivyo hata ukitaka kushinda msikilize yeye na fuata maelekezo yake katika maombi na utashinda dhidi ya kila hila za shetani,  
huko ndiko kufanyika rungu la MUNGU na silaha za MUNGU za vita.  

3. Anajua kutumia upanga wa ROHO MTAKATIFU ambao ni  Neno la MUNGU.

Waefeso 6:17 "Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa ROHO ambao ni neno la MUNGU;"

Kazi ya upanga ni kukata  na Neno la MUNGU ni upanga wa ROHO MTAKATIFU  hivyo omba ukitumia Neno la MUNGU na utashinda kirahisi, huko ndiko kufanyika rungu la MUNGU na silaha za MUNGU za vita. 

4. Zaidi ya yote anaomba kwa imani.

Waefeso 6:16 "zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu."

Huwa najiuliza kwanini Biblia kwenye suala la sisi kushinda vita ya kiroho inasema "Zaidi ya yote mkitwaa ngao ya imani"

Yaani imani ni kiini cha ushindi kwa mteule katika vita ya kiroho. 

Ili uwe rungu la MUNGU na silaha za MUNGU za vita lazima uwe mtu wa imani katika KRISTO YESU na unayeomba kwa imani. 

Kwa nini uombe kwa imani? 

Kwa sababu pasipo imani huwezi kumwona MUNGU akikushindia, hivyo Biblia kuwa na maombi ya imani huwezi kumshinda adui Maana MUNGU haambatani na wenye imani haba. 

Waebrania 11:6 "Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye MUNGU lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao."

5.Anamjua adui anayetakiwa kumpiga.

Waefeso 6:12 "Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho."

Hawa ndio maadui zetu na wamebeba vitu vingi sana vya kipepo lakini ukiwajua  kisha ukafanyika rungu la MUNGU  na silaha za MUNGU za vita hakika utawashinda kirahisi sana. 

6. Anaujua wakati wa kupambana kiroho.

2 Samweli 11:1 "Hata ikawa, mwanzo wa mwaka mpya, wakati watokapo wafalme kwenda vitani, Daudi akampeleka Yoabu, na watumishi wake pamoja naye, na Israeli wote; wakawaangamiza wana wa Amoni, wakauhusuru Raba. Lakini Daudi mwenyewe akakaa Yerusalemu."

Biblia inaonyesha Daudi alikwenda vitani mwanzo.

Tunajifunza nini? 
Watu wengi anaweza kumjua adui lakini anakuja kuchukua hatua za kimaombi kipindi adui ameshamiliki tayari. 

Ngoja nikupe mifano hai. 
Mama mmoja siku moja alinipigia simu akiniambia kwamba nimuombee mume wake ili afufuke maana ana mwezi kaburini sana na akasema kwamba aliota mara nyingi mume wake akipata ajali lakini hawakuzingatia. Mume wake alikosana na ndugu zake katika ukoo na wakamwambia hatamaliza mwaka.  Sasa Mama huyu angeniambia tuingie katika maombi kipindi anaota ndoto hizo mbaya au kipindi mume wake anatamkiwa hayo na ndugu zake basi tungeomba  na mipango ya shetani isingefanikiwa kamwe. Lakini anakuja kuokoka ili aanza kuhitaji msaada wa maombi kipindi ambacho madhara makubwa yameshatokea.  Mimi japo sikumwambia nilianza tu kumuombea yeye na sio mume wake. 
Ndugu inakupasa sana kuujua wakati wa kupigana vita y kiroho. 

Wengine hupewa msukumo wa kuomba au kutoa sadaka au kufunga lakini hawazingatii lakini madhara yanapotokea ndipo wanaamka na kujikuta wanafunga mara kumi zaidi bila mafanikio. 

Ndugu uelewe ulimwengu wa roho na fanyika rungu la MUNGU na silaha za MUNGU za vita ili uwe tayari siku zote kuwakabili wakuu wa giza na giza lao. 

Mama mmoja alinipigia simu nimuombee mume wake arudi kwake baada ya kumwacha ghafla na kuoa mwanamke mwingine anayetumika kichawi,  sasa wakati hata kabla hawajaachana huyu mama alikuwa anaona kwenye ndoto na maono juu ya mipango za shetani za kuivunja ndoa yake lakini hakuzingatia,  sasa anakuja kushtuka kipindi ameachwa na tayari mume wake ameshafunga ndoa ya siri na ameshazaa huko tayari,  ndugu ujue wakati sahihi wa kuingia katika vita ya kiroho ndipo hutatumia nguvu nyingi kushinda. 

Yaani wewe unaota unalogwa lakini unadharau kuingia kwenye maombi ya vita. 
Unaota unafukuzwa kazi,  unaota unaona adui zake wanatoa kafara kwa ajili yako wewe hata kumtolea MUNGU sadaka za fungu la kumi hujawahi,  sasa madhara yanapotokea ndipo unaanza vita ya kiroho,  ndugu unaweza ukajikuta unatumia nguvu nyingi sana na gharama nyingi sana za kiroho na kimwili ndipo ushinde vita hiyo. 
Mimi  Peter Mabula nina shuhuda nyingi sana za watu walioniambia ambao niligundua kwamba hawakuutambua muda sahihi kwa kuanza kupigana na nguvu za giza. 

Kuna watu wanaachwa na wachumba kila siku na ndipo hukumbuka kwamba kabla waliona kwenye ulimwengu wa roho ila hawakuingia katika maombi. 
Ndugu ujue wakati sahihi wa kwenda vitani,  sio mpaka umetekwa ndipo unaanza vita ya kiroho. 

7. Anajua kuzitumia silaha za kiroho  za kimaombi anapokuwa anapambana  na adui.

Kuna silaha nyingi za kimaandiko za kuzitumia katika vita ya kiroho, siku moja nitafafanua kwenye somo lingine ambalo nilishaliandaa, linasubili kuandikwa tu, lakini baadhi ya silaha hizo

A. Giza la MUNGU.

Mfano ni Musa alitumia silaha ya kiroho inayoitwa "Giza "

Kutoka 10:21-23 " BWANA akamwambia Musa, Nyosha mkono wako kuelekea mbinguni, kuwe giza juu ya nchi ya Misri, watu wapapase-papase gizani. Basi Musa akaunyosha mkono wake kuelekea mbinguni; kukawa na giza nene katika nchi yote ya Misri muda wa siku tatu;
 hawakupata kuonana mtu na mwenziwe, wala hakuondoka mtu mahali alipokuwa muda wa siku tatu; lakini wana wa Israeli wote walikuwa na mwanga makaoni mwao."

B. Moto wa MUNGU.

Yeremia 5:14 "Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala."

C. Upanga wa MUNGU.

Isaya 66:16 "Kwa maana BWANA atateta na wote wenye mwili, kwa moto na kwa upanga wake; nao watakaouawa na BWANA watakuwa wengi."

Ukiwa mteule unayejitambua na ni muombaji unaweza kuharibu kazi za shetani na unaweza kupeleka madhara makubwa sana katika ulimwengu wa roho wa giza.

8. Anajua jinsi ya kupigana vita ya kiroho.

Mathayo 7:8 "kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa."

Tunapigana vita ya kiroho kwa maombi huku tufuata kanuni za kiroho zinazoweza kuleta ushindi kwenye kulingana na maandiko. 

9. Anajua kuomba akiwatumia Malaika ili ashinde vita.

Kuna makundi mengi ya Malaika unaoweza kuwatumia katika vita ya kiroho na ukashinda, siku moja nitafafanua kwenye somo lingine kuhusu Malaika lakini kwa ufupi  na kwa uchache sana ni kwamba kuna malaika wapelekao mabaya.
Zaburi 78:49 "Akawapelekea ukali wa hasira yake, Ghadhabu, na uchungu, na taabu, Kundi la malaika waletao mabaya."

Kuna Malaika  wa kukuhudumia wewe mteule wa KRISTO. 
Waebrania 1:14 "Je! Hao wote si roho watumikao, wakitumwa kuwahudumu wale watakaourithi wokovu?"

Kuna Malaika wa kukulinda.  
Zaburi 91:11 "Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote."

Jifunze tu namna ya kuwatumia  Malaika na hakikisha una sifa za hadi Malaika wa MUNGU wakusaidie wewe. 

10.Katika maombi  siku zote anaomba katika jina la YESU KRISTO na anajua kuzitumia mamlaka nne za kiroho.

Mamlaka za  kiroho  za Mteule wa KRISTO aliye rungu la MUNGU ni hizi.

A. Jina la YESU KRISTO.

Yohana 14:14 "Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya."

B. Damu ya YESU KRISTO.

Ufunuo  12:11 "Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa."

C. Nguvu za ROHO MTAKATIFU.

Warumi 15:13 "Basi MUNGU wa tumaini na awajaze ninyi furaha yote na amani katika kuamini, mpate kuzidi sana kuwa na tumaini, katika nguvu za ROHO MTAKATIFU."

Nguvu za ROHO MTAKATIFU humfanya adui kukimbia hata kama hataki, nguvu za giza haziwezi kuhimili kwenye uwepo wa nguvu za ROHO MTAKATIFU. 

Kumbuka pia kwamba nguvu za MUNGU ndizo hizo nguvu za ROHO MTAKATIFU,  Yaani kusema nguvu za MUNGU ni sawa na kusema nguvu za ROHO MTAKATIFU, ni kitu kimoja. 
 ROHO MTAKATIFU akiwa na wewe na nguvu zake ziko hapo na kwa vyovyote vile wewe utakuwa mshindi dhidi ya nguvu za giza zote. 
1 Yohana 4:4 "Ninyi, watoto wadogo, mwatokana na MUNGU nanyi mmewashinda, kwa sababu yeye(ROHO MTAKATIFU)  aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye(shetani) aliye katika dunia."

D. Neno la MUNGU.

Mathayo 8:16 "Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi,"

Bwana YESU alizishinda nguvu za giza zilizokuwa ndani ya watu, alizishinda kwa Neno lake. 
Biblia ndio Neno lake KRISTO hivyo tunazishinda nguvu za giza kwa Neno la MUNGU ndio maana hilo Neno la KRISTO linatakiwa liwe kwa wingi sana ndani yetu ili tuwe washindi. 

Wakolosai 3:16 "Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu."

Wewe mteule wa KRISTO uliye rungu la MUNGU lazima uwe unanitumia mamlaka hizo nne za kiroho ndipo utakuwa mshindi siku zote dhidi ya nguvu za giza. 
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
By Peter  Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTOMwokozi.
+255714252292(whatsapp).
Uki-share kwa marafiki zako ujumbe  huu naomba share  kama ulivyo,usibadili jina wala chochote huo ndio uungwana wa watu wa kweli wa MUNGU. 
Ubarikiwe 

Comments