MUNGU HUTUMIA WATU KWA AJILI YAKO, ISHI VIZURI NA WATU

 




Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote. 
Karibu tujifunze Neno la MUNGU. 

Wakati mwingine MUNGU hutumia watu kufanikisha watu.

●Mfano ni MUNGU alimtumia Musa ili kuwatoa Waisraeli Misri.

Kutoka 3:10 "Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri."

●MUNGU alimtumia Ayubu ili Ayubu awaombee msamaha rafiki zake ndipo MUNGU atawaridhia.

Ayubu 42:7-8 " Basi ikawa, baada ya BWANA kumwambia Ayubu maneno hayo, BWANA akamwambia huyo Elifazi Mtemani, Hasira zangu zinawaka juu yako, na juu ya hao rafiki zako wawili; kwa kuwa ninyi hamkunena yaliyo sawa katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu. Basi sasa, jitwalieni ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba, mkamwendee mtumishi wangu Ayubu, mjisongezee sadaka ya kuteketezwa; na huyo mtumishi wangu Ayubu atawaombea ninyi; kwa kuwa nitamridhia yeye, nisiwatende sawasawa na upumbavu wenu; kwani ninyi hamkunena maneno yaliyonyoka katika habari zangu, kama alivyonena mtumishi wangu Ayubu."

●MUNGU  alimtumia Samweli kumtia mafuta ya ufalme Daudi.

1 Samweli 16:13 "Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya BWANA ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama."

Na tangu siku hiyo Daudi akawa na ROHO MTAKATIFU. 

Ndugu, ni kwamba MUNGU anaweza kumtumia Mtumishi wake yeyote ili watu wengine wafunguliwe vifungo.

Ndugu, nini nataka kusema?

■Hakikisha unaishi vizuri na watu.

Hakuna mtu duniani aliwahi kufanikiwa peke yake, lazima kushirikiana na watu wengine.
Ndugu hakikisha unaishi vizuri na watu wote.

Wagalatia 6:10 "Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio."

Dada mmoja alikuwa anaishi vibaya na wamama wa  Kanisani kwao. Siku moja kijana mmoja  aliyeokolewa na Bwana YESU akaja pale Kanisani na akavutiwa na Dada huyo hivyo akataka afunge naye ndoa. Alichokifanya aliwaendea wamama wa Kanisani hapo ili ajue zaidi kuhusu binti huyo mrembo.
Ndugu yule hakupata habari njema za binti huyo kutoka kwa wamama. Maana Mara mama huyu alisema "Huyo binti juzi kanitukana" Mara mama mwingine anasema "Yule binti hakufai maana hajui kuishi vizuri na watu" n.k

Yaani kijana yule alikosa habari njema za binti yule hivyo akaghairi kumuoa.

Kwanini ikawa hivyo?
Ni kwa sababu hakuna mtu hufanikiwa peke yake, lazima kuna watu watahusika ili afanikiwe hivyo kuishi vizuri na watu wote ni jambo la muhimu sana maana pia hata MUNGU wakati mwingine hutumia watu kufanikisha wengine.
Ukiishi vibaya na watu kuna haki zako au baraka zako unaweza kuzikosa kwa sababu hiyo tu.

Waebrania 12:14 "Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona BWANA asipokuwa nao;"

Ndugu hakikisha unaishi vizuri na watu wote.
MUNGU akubariki Sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika Shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi. 
+255714252292.
UBARIKIWE 

Comments