HAKIKISHA UKO NDANI YA SAFINA.

Na Mwl Peter Mabula 



Bwana YESU KRISTO asifiwe.!

Karibu tujifunze Neno la MUNGU. 


MUNGU Baba Alimwambia Nuhu Atengeneze Safina Maana Mwisho Wa Viumbe Vyote kwa wakati huo ulikuwa Umekaribia.

Mwanzo 6:13-14 "MUNGU akamwambia Nuhu, Mwisho wa kila mwenye mwili umekuja mbele zangu; kwa sababu wameijaza dunia dhuluma, basi nitawaharibu pamoja na dunia. Ujifanyie safina ya mti wa mvinje; fanya na vyumba ndani ya safina, ukaifunike ndani na nje kwa lami."


●Sababu Ya Mwisho Wa Viumbe Vyote Kukaribia wakati huo  ilikuwa ni maovu ya wanadamu.


Mwanzo 6:5 "BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote."


Maovu ya wanadamu yalisababisha utokee mwisho wa viumbe vyote.


 -Mwanadamu Alimsahau MUUMBA Wake.

 

-Mwanadamu alikuwa Anawaza Ngono Tu Masaa 24.


-Mwanadamu alikuwa  Anamwabudu Shetani Na Sanamu Zake.


 -Mwanadamu alikuwa  Anatoa Mimba Kila Mara Kama Tu Anapenga Kamasi, Yaani kama ilivyo Kila Zikija Kamasi Anazitoa hata mimba kutoa ilikuwa hivyo hivyo.

 

-Mwanadamu alikuwa Akiamka Tu Anakwenda  kulewa pombe Wala Sio Kumwabudu MUNGU.


- Inawezekana Mwanadamu  alikuwa Anawaona Watumishi Wa MUNGU Kama kama akina Nuhu kuwa kama tu watu  Waliokosa Kazi. 


 ●Lakini  Mwisho Ulifika Na Wote Wakafa. 


Mwanzo 7:21-23 " Wakafa wote wenye mwili waendao juu ya nchi, na ndege, na wanyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu, na kila kitambaacho chenye kutambaa juu ya nchi, na kila mwanadamu;  kila kitu chenye pumzi ya roho ya uhai puani mwake kikafa, kila kilichokuwako katika nchi kavu. Kila kilicho hai juu ya uso wa nchi kikafutiliwa mbali tangu mwanadamu hata mnyama wa kufugwa, na kitambaacho, na ndege wa angani; vilifutiliwa mbali katika nchi, akabaki Nuhu tu, na hao walio pamoja naye katika safina.


●Watu wote dunia nzima walikufa wote kwa sababu tu hawakuwa ndani ya Safina.


Kwenye Safina ya Nuhu walipona watu 8 tu yaani Nuhu na mkewe, Yafeti na mkewe, Hamu na mkewe pamoja na Shemu na mkewe.


■Safina ilikuwa ni muhimu sana kwa Nuhu na wanae.


 Inawezekana wapo watu ambao kabla ya hapo hawakuamini kwamba inawezekana watu wote dunia nzima kufa siku moja.


Hawakuamini lakini ndivyo ilivyokuwa, walikufa wote isipokuwa watu 8 walikua ndani ya Safina. 


■Hata leo kuna mamilioni ya watu hawaamini kama kuna jehanamu ya moto. 


Watu hawaamini kama kuna moto wa milele, shetani amewapumbaza na wanajiona wako salama kumbe sio salama.

Biblia inasema hivi Mambo yakatavyokuwa kwa wanaokataa kuingia katika Safina ya sasa.


Ufunuo  21:8 "Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili."


Inawezekana  umejiuliza swali hili "Safina ya sasa ipi hiyo"


 ■Ndugu Hata leo kuna Safina ndugu yangu.

Na safina hiyo iko moja tu kama ilivyokuwa Safina ya Nuhu iliyokuwa moja tu.


Safina ya sasa ni Bwana YESU KRISTO na Wokovu wake, ukikosekana kwenye hii safina hata kama una dini nzuri ujue Jehanamu inakuhusu.


Biblia inasema katika Mathayo 24:37-44 kwamba  ''Kwa maana KAMA VILE ILIVYOKUWA SIKU ZA NUHU, NDIVYO KUTAKAVYOKUWA KUJA KWAKE MWANA WA  ADAMU. Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina, wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu. Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa; wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa. Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja BWANA wenu. Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa. Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja. ''


Ndugu yangu,  ni kwamba Bwana YESU KRISTO siku moja atarudi,   je atakukuta wapi ndugu? 


●Je atakukuta atakukuta ndani ya Safina yake ambayo ni Wokovu wake?


●Je utakuwa sehemu ya walio ndani ya Safina ili gharika iitwayo ziwa la moto isikuhusu?


●Bwana YESU atakukuta unafanya nini? 


Yeye kama mwenye  safina ya mwisho,  siku ya mwisho ikifika je utakutwa ndani ya safina yake hata usiende jehanamu bali uende uzima wa milele? 


●Siku ya kufa kwako ikifika,  Je utakuwa ndani ya safina ili uende mbinguni au utakuwa nje ya safina ili uende Jehanamu?

 

Luka 17:26-27 ''Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. ''


Ndugu,  watakaokosekana kwenye safina hii ya mwisho hawataingia uzima wa milele. 


■Ndugu yangu, MUNGU Ameamua Kuleta Safina Ya Mwisho, Safina Hii Wala Haitabeba Wanyama Na Ndege Bali Wanadamu.


 Safina Yetu Ni Bwana YESU KRISTO  na Wokovu wake.

Imeandikwa 

Yohana 1:12-13 "Bali wote waliompokea(YESU) aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa MUNGU, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU."


●Kumbe ndugu yangu inakupasa umpokee YESU KRISTO kama Mwokozi wako ili uwe sehemu ya watu walio ndani ya safina ya MUNGU kwa ajili ya uzima wa milele.


●Kumbuka watakaokuwa nje ya safina hii mwisho wa dunia ukifika watakuwa pia nje ya uzima wa milele. 


Ufunuo  22:15 "HUKO NJE wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya."


Tena imeandikwa  


Yohana 3:16-18 " Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.  Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.  Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU."


●Kumbe ukiuhitaji uzima wa milele  okoka kwa kumpokea YESU KRISTO kama Mwokozi wako. 


Bwana YESU KRISTO Alikufa Msalabani Ili Atuokoe.

 Ukitaka Leo Kuingia Kwenye Safina Hii Jikane Mwenyewe bila kuangalia ndugu zako au familia yako wanakuonaje, amua kuokoka ndugu yangu na baada ya kuokoka anza kuishi maisha matakatifu usiku na mchana siku zote.


 Luka 9:23-24 '' Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.'' 


■Ukimpokea YESU, Yeye Atakupa Uzima Na Siku Ya Mwisho Atakufufua.


Yohana 6:40 "Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana(YESU) na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho."


■YESU Anaandaa Makazi Ya Watakatifu Mbinguni.


 Yohana 14:2-3 "Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; kama sivyo, ningaliwaambia; maana naenda kuwaandalia mahali. Basi mimi nikienda na kuwaandalia mahali, nitakuja tena niwakaribishe kwangu; ili nilipo mimi, nanyi mwepo. Nami niendako mwaijua njia."


●Ndugu Kimbilia Kwenye Safina Hii Pekee Ya Kukupa Uzima Wa Milele.


 ●Ndugu Mkimbilie KRISTO Mwenye Uzima Wako Wa Milele.

Safina yetu ni Bwana YESU hivyo kila mmoja ahakikishe ameingia kwenye safina hii ya kutupeleka uzima wa milele.


 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine na kama hujampokea Bwana YESU KRISTO muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho Kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO Bwana.

MUNGU akubariki sana .

By Peter Mabula

Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi. 

+255714252292( Kwa lolote na pia kwa whatsapp)

MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Unaweza kuwatumia ndugu zako na  marafiki zako wote unaowapenda ili wawe ndani ya safina kama ambavyo wewe uko ndani ya safina au baada ya kusoma Neno hili la MUNGU umechukua maamuzi ya kuingia katika safina hii kwa ajili ya uzima wa milele. 

Ubarikiwe

Comments