BAADHI YA MAMBO GANI YALITOKEA BAADA YA BWANA YESU KRISTO KUPANDISHWA MSALABANI ?

Na Mtumishi Peter Mabula



■Kwanza, Pazia la hekalu lilipasuka.

Luka 23:45 "jua limepungua nuru yake; PAZIA LA HEKALU LIKAPASUKA KATIKATI."

Hii inamaanisha kuondolewa kizuizi na inamaanisha ushindi mkubwa wa mkristo.

Pazia kupasuka kunamaanisha kuwekwa huru.
Kuondolewa kwa vizuwizi vyote mbele yako.

Ikumbukwe kuwa, pazia, liliwekwa kuwazuwia watu wasiingie wala hata wasiweze kupaona patakatufu pa patakatifu.

Mahali hapa,aliingia kuhani peke yake.
Baada ya pazia kupasuka, kizuwizi kiliondolewa kwa yeyote kufika hapo.

Kifo cha Bwana YESU KRISTO msalabani, kimeondoa dhambi zako, kimekupa kibali cha kunena kwa lugha kwa raha zako n.k.

■Pili, Tetemekeo kubwa.

Mathayo 27:54 "Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda YESU, WALIPOLIONA TETEMEKO LA NCHI na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa MUNGU."

Tetemeko hili,liliambatana na giza nene,ikiwa ni ishara ya nguvu kubwa yenye utisho wa ajabu sana.

Marko 15:33 "Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa."

Tetemeko hili, lilionesha uwezo ulio juu ya uwezo wote,nguvu inayozidi nguvu zote.

Tetemeko hili, lilidhihirisha kuwa kweli YESU KRISTO ni Mwana wa MUNGU, na yule mlinzi alishuhudia kwa kinywa chake.

Mathayo 27:54 "Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda YESU, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, WAKISEMA, HAKIKA HUYU ALIKUWA MWANA wa MUNGU."

Hata leo, maisha ya mtu aliyeokoka, yanapaswa kudhihirika mbele za watu wote kuwa kweli kuna nguvu mpya na uweza wa ziada ndani ya mtu aliyeokoka.

■Tatu, Makaburi yalifunguliwa.

Mathayo 27:52 "makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;"

Baada ya Bwana YESU kukata roho na inawezekana na kushuka kuzimu watu wengi waliokuwa wamekufa wakaamka yaani wakafufuka na wakatangaziwa uzima upya.
Wakawa katika uzima wa milele pamoja na YESU KRISTO.

Baada ya Bwana YESU kumiliki funguo za kuzimu, shetani akawa hana mamlaka tena, uwezo wake wote na mamlaka yote akawa amenyeng’anywa.

Ufunuo 1:18 "na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu."

Nguvu ya msalaba, ni nguvu inayoshinda mauti.

YESU KRISTO ni zaidi ya mateso yote, ni zaidi ya kifo, ni zaidi ya magonjwa, ni zaidi ya kukata tamaa, ni zaidi ya umasikini, nguvu ya msalaba iko juu ya laana na vifungo vyote.

■Nne, Tamko la Ushindi likatolewa.

Yohana 19:30 "Basi YESU alipokwisha kuipokea ile siki, alisema, IMEKWISHA. Akainama kichwa, akaisalimu roho yake."

Tamko la ushindi lilitolewa rasmi YESU KRISTO aliposema (Imekwisha).

Kauli ya YESU KRISTO iliashilia kufikia mwisho kwa mateso yote, uonevu, laana, mikosi na vifungo vyote.

Kauli ya Bwana YESU KRISTO inatufundisha nini aliposema Imekwisha?

Kwa mtazamo wa ndani zaidi, ilimaanisha, kukamiliaka kwa kazi yake iliyomleta duniani ambayo ilikuwa ni ukombozi.

Kumweka huru kila mtu ili asipotee, bali awe na uzima wa milele.

Kwa maelezo mengine tuseme kuwa, Msalaba wa YESUKRISTO, ulibadilisha Historia ya Ulimwengu wote na kuweka utamaduni mpya.

Nyongeza ni kwamba Kupitia mauti ya msalaba wa YESU KRISTO, msamaha wa dunia ulitangazwa kwa wanaoamua kutubu na kuokoka katika yeye Bwana YESUKRISTO.

Kupitia kifo cha msalaba cha Bwana YESU KRISTO toba kwa ulimwengu ilipatikana hivyo yeyote anayehitaji kusamehewa MUNGU katika KRISTO YESU anaweza kusamehewa.

Kifo cha msalabani cha Bwana YESU KRISTO kinatupa maji ya uzima, kinatupa pumziko la kweli, kina tuhesabia haki.
Wakati wayahudi walidhani wanamkomesha, kumbe agano la MUNGU lilikuwa linatimia kwa ulimwengu, kuwa Mtu hatafika mbinguni ila kwa njia ya YESU KRISTO pekee.

Yohana 14:6 "YESU akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa BABA, ila kwa njia ya mimi."

Kupitia kifo cha Bwana YESU KRISTO mlango wa kuiendea mbingu ilifunguliwa wazi kwa wote wampokeao na makao yao yanaanza kuandaliwa tangu hapo.
Hata leo, ukiokoka, makao yako yanaanza kuandaliwa leo Mbinguni.
Ndugu yangu amua kumpokea YESU KRISTO leo ili awe Bwana na Mwokozi wako.
MUNGU akubariki sana.
By Peter Mabula.
Mtenda kazi katika shamba la Bwana YESU KRISTO Mwokozi.
+255714252292.
Ubarikiwe

Comments